YENYE KUHATARISHA NYUMBA
  • Kichwa: YENYE KUHATARISHA NYUMBA
  • mwandishi: Ummu Nassra
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 15:25:32 1-9-1403

BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

MAMBO YA KUZINGATIA HASA KWA KINA MAMA
Miongoni mwa mambo yenye kuporomoa Uislamu katika majumba ya Waislamu ni udhaifu wa baadhi ya kinamama kuupuuza au kutoyatambua mafunzo muhimu yanayowahusu ambayo dini yetu yameyaweka wazi. Miongoni mwa hayo ni haya yafuatayo:

i. Kudhihirisha Mapambo:
Kawaida, wanawake huwa na mvuto wa kimaumbile. Hivyo Uislamu umeweka sheria maalum juu ya kuhifadhi maumbile hayo, heshima, staha pamoja na hadhi zao. Suurat Al-Ahzab: 59 Allaah Subhaanahu Wata'ala Anatueleza:
Ewe Mtume! Waambie wake zako na binti zako na wanawake wa Kiislamu wajiteremshie uzuri shungi zao, kufanya hivyo kutapelekea wepesi wajuulikane (kuwa ni watu wa heshima) ili wasiudhiwe. Ni mazoea ya wanawake wengi wanapotaka kutoka au kupata wageni majumbani mwao hudhihirisha mapambo yao yakiwemo maumbile yao kwa nguo za wazi au za kubana, manukato pamoja na mapambo mengine. Hali hii inaweza kusababisha vishawishi vingi, fitina na mtafaruku katika familia. Ni lazima tuwe waangalifu ni nani waliotuzunguka hasa wale wasiotakikana kuona mapambo hayo (wasiokuwa mahrim). Suuratu Nnuur: 31 Allaah Subhaanahu Wata'ala Anatuhimiza:
Na waambie waumini wanawake wainamishe macho yao na wazilinde tupu zao, wala wasidhihirishe viungo vyao isipokuwa vinavyodhihirika. Kujistiri kwa hijabu ya ki shari'ah kunapelekea kupata ridhaa ya Allaah Subhaanahu Wata'ala na kutii amri Yake, kujitakasa pamoja na kuheshimika na wengine.
ii. Kutoka toka bila ya sababu maalumu
Wanawake wa Kiislamu hawajakatazwa kutoka nje ima kwa, kufanya kazi, kutembelea wazee, marafiki au katika shughuli za kijamii, ikiwa hakuna kipingamizi chochote cha shari'ah kitachowazuia. Muhimu ni kuchunga na kuielewa mipaka iliyowekwa katika dini. Hata hivyo kutulia majumbani ni bora zaidi kwao na kutawaepusha na mambo mengi. Ulimwengu tulionao, kina mama wengi imekuwa ni adimu kutulia majumbani mwao, hii hupelekea familia kukosa utulivu, kizazi kukosa malezi na maadili mema kutokana na wazazi huwa hawana muda wa kutosha na watoto wao. Allaah Subhaanahu Wata'ala Anatufahamisha katika Suuratul Ahzaab: 33
Na kaeni majumbani mwenu, wala msionyeshe mapambo yenu kama walivyokuwa wakionyesha wanawake wa zama za ujahili (ujinga)
Hivyo ni lazima kwa kinamama kuzingatia ni sababu gani zitakazowatoa ndani ya majumba yao, kuwe na mtizamo na upeo wa hali ya juu kabla ya kuamua kutoka. Na ikibidi kutoka basi azingatie mipaka ya Allaah Subhaanahu Wata'ala, kusiwe na aina yoyote ya mapambo kama vipodozi, manukato, udi na mengineyo. Awe amejihifadhi vizuri kwa mujibu wa shari'ah. Kufanya hivyo kutahifadhi utu wao, dini yao pamoja na kizazi chao kwa ujumla.
HITIMISHO
Ni wajibu wa Waislamu kudumisha mafunzo mazuri tuliyoekewa wazi katika dini yetu. Jamii bora huanza majumbani. Ni vyema kwa wasimamizi wa majumba kusaidiana na kushirikiana pamoja katika kulinda na kuhifadhi mazingira mazuri kwa kumuogopa Allaah Subhaanahu Wata'al. Ni juu yetu kuwa waangalifu wa kile tunachokikuza - watoto, kwani wao husoma kutoka kwetu. Ni jukumu la kila mmoja wetu kusoma na kujifunza kitu gani Allaah Subhaanahu Wata'ala Anapendezeshwa nacho na kipi Amekikataza hasa ndani ya majumba yetu ili tuishi hali ya kuwa Allaah Subhaanahu Wata'ala Ameturidhia. Tuzipambe nyumba zetu kwa misingi ya Kiislamu ili zitofautike na zile zisizo za Kiislamu. Huu ni ukumbusho kwa wenye kukumbuka. Tumuombe Allaah Atuongoze katika haki na kuifuata, tuijuwe batili na kuiacha, Atupe tawfiyq, Atulinde na Kutuweka katika msimamo ulio sawa. Aamiyn
MWISHO