SHARTI ZA KUFIKIA MJA KATIKA UKAMILIFU NO.2
  • Kichwa: SHARTI ZA KUFIKIA MJA KATIKA UKAMILIFU NO.2
  • mwandishi: NDUGU ZETU WA KIISLAMU
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 20:9:1 19-8-1403

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
SHARTI ZA KUFIKIA MJA KATIKA UKAMILIFU NO.2
Tukiendelea na mada yetu inayohusiana na masharti na vizuizi vinavyompelekea mwanaadamu asiweze kufikia katika ukamilifu, katika makala hii tutaelezea masharti sharti jengine linalomfanya mwanaadamu asifikie katika ukamilifu. Sharti hilo ni:-
3) Chuki na kukalidi matendo ya wengine.
Sharti ya tatu miongoni mwa masharti yanayomfanya mwanaadamu amfahamu Mola wake ni kujiepusha na chuki, kukalidi au kuiga matendo ya wengine bila ya kuwa na dalili au elimu nayo.
Kutafuta na kujua uhakika wa mambo, ni siri kubwa inayomfanya mwanaadamu afanikiwe katika maisha yake ya kila siku, na akili na fitra ya wanaadamu ndio nyenzo bora zinazomsaidia mwanaadamu huyo kufikia katika mafanikio,na kwa sababu hiyo basi aya nyingi ndani ya Qur-ani zinawataka wanaadamu wafikiri na wakumbuke. Kiasi ya kwamba ikiwa mwanaadamu atafikiri na kuzingatia kwa makini anaweza kufahamu utukufu mkubwa wa Mwenyeezi Mungu katika uumbaji wake, na ataelewa kuwa madai ya mungu asiyekuwa Mola wa haki hayana uwezo wa kufaya lolote katika dunia hii, na hii itamfanya mwanaadamu huyo aamini Mola mmoja wa haki anayepaswa kuabudiwa, kama tunavyosoma ndani ya Qur-ani:-

وَسَخَّرَ لَكُمُ اللَّيْلَ وَالْنَّهَارَ وَالشَّمْسَ وَالْقَمَرَ وَالْنُّجُومُ مُسَخَّرَاتٌ بِاَمْرِهِ إِنَّ فِى ذٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يَعْقِلُونَ[1]

Na amefanya ukutumikieni usiku na mchana, na jua na mwezi, na nyota zikutumikieni kwa amri yake. Hakika katika hayo zipo ishara kwa watu wenye akili.
Na kwa upande mwengine, kuwa na chuki au kuiga matendo ya watu – ikiwa jamii fulani, au watu waliopita, - bila ya kuwa na dalili yoyote, - yaani kuwa zumbukuku, eti kwa sababu fulani kafanya hivi basi na mimi nafanya –
ni kizuizi kikubwa kinachowazuilia wanaadamu kutofikia katika saada, kama anavyosema Mwenyeezi Mungu Mtukufu kuwaambia wale waliokufuru:-

وَإِذَا قِيلَ لَهُمْ تَعَالَوْاْ إِلَي مَا اَنزَلَ اللّهُ وَإِلَي الرَّسُولِ قَالُواْ حَسْبُنَا مَا وَجَدْنَا عَلَيْهِ آبَاءنَا اَوَلَوْ كَانَ آبَاؤُهُمْ لاَ يَعْلَمُونَ شَيْئاً وَلاَ يَهْتَدُونَ[2]
Na wanapo ambiwa: Njooni kwenye yale aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu, na kwa Mtume, husema: Yanatutosha tuliyo wakuta nayo baba zetu. Je, hata ikiwa baba zao walikuwa hawajui kitu wala hawakuongoka?
4)Kumkumbuka na kuwa pamoja na Mwenyeezi Mungu kila wakati.
Sharti ya nne miongoni mwa masharti yanayomfanya mwanaadamu aamfahamu Mola wake, ni kuwa karibu na Mwenyeezi Mungu kila wakati, kumtukuza na kumsabihi (kumtakasa) kwa sifa zake njema, hii ndio njia bora kabisa itakayomfanya mwanaadamu amfahamu Mola wake, kama tunavyosoma ndani ya Qur-ani:-
يَا اَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اذْكُرُوا اللهَ ذِكْراً كَثِيراً .  وَسَبِّحُوهُ بُكْرَةً وَاَصِيلاً .  هُوَ الَّذِى يُصَلِّى عَلَيْكُمْ وَمَلاَئِكَتُهُ لِيُخْرِجَكُم مِّنَ الظُّلُمَاتِ إِلَي النُّورِ وَكَانَ بِالْمُؤْمِنِينَ رَحِيماً[3]

Enyi mlio amini! Mdhukuruni Mwenyezi Mungu kwa wingi wa kumdhukuru. Na mtakaseni asubuhi na jioni. Yeye na Malaika wake ndio wanakurehemuni ili kukutoeni gizani mwende kwenye nuru. Naye ni Mwenye kuwarehemu Waumini.
Kwa hiyo mtu yoyote yule atakayezingatia na kutafakari katika aya za Mwenyeezi Mungu, na akawa anamtakasa Mola wake kwa sifa zake njema, Mwenyeezi Mungu humfungulia njia mtu huyo, ili aweze kumfahamu Mwenyeezi Mungu kwa wingi zaidi, na humnufaisha kwa yale ambayo yanaweza kumsaidia siku ya Kiama. Kama anavyosema:-
وَالَّذِينَ اهْتَدَوْا زَادَهُمْ هُدًى وَآتَاهُمْ تَقْواهُمْ[4]

 Na wale walio ongoka anawazidishia uongofu na anawapa uchamngu wao.

*Haya ndiyo hayo yanayosemwa kila siku kuwa wanaokubali kuongoka ndio anaowaongoa Mwenyeezi  Mungu.

[1] Surat Nahli aya ya 12
[2] Surat Al-Maidah Aya ya 104
[3] Surat Ahzaab Aya ya 41-43
[4] Surat Muhammad aya ya 17

MWISHO