BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI
KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
MALENGO YA MITUME YA MWENYEEZI MUNGU NO.7
* Mitume Mitukufu ya Mwenyeezi Mungu imekuja kuwalingania wanaadamu katika kitu gani?.
katika makala iliyopita tulielezea kuhusu malengo ya Mitume ya Mwenyeezi Mungu, katika makala hii tutaendelea na mada yetu ile ile inayohusiana na malengo ya Mitume.
5. KUWALINGANIA WATU KUHUSU SIKU YA KIAMA
Mitume, baada ya kuwalingania watu tawhiyd, na kuwataka wamuabudu Mola mmoja, ujumbe mwengine muhimu waliokuja nao ni kuwafunza na kuilea jamii, kuwapa wanaadamu habari kuhusu siku ya Kiama, na kuwataka wajiepushe na anasa za dunia, kwani zinaweza zikawapeleka pabaya, vile vile Mtume Muhammad (s.a.w.w) aliwatia mori na shauku watu ili wapigane jihadi, na wawe madhubuti katika hukumu za dini yao, angalia Qur-ani inavyosema:-
اَلَمْ تَرَ إِلَي الَّذِينَ قِيلَ لَهُمْ كُفُّواْ اَيْدِيَكُمْ وَاَقِيمُواْ الصَّلاَةَ وَآتُواْ الزَّكَاةَ فَلَمَّا كُتِبَ عَلَيْهِمُ الْقِتَالُ إِذَا فَرِيقٌ مِّنْهُمْ يَخْشَوْنَ النَّاسَ كَخَشْيَةِ اللهِ اَوْ اَشَدَّ خَشْيَةً وَقَالُواْ رَبَّنَا لِمَ كَتَبْتَ عَلَيْنَا الْقِتَالَ لَوْلا اَخَّرْتَنَا إِلَي اَجَلٍ قَرِيبٍ قُلْ مَتَاعُ الدَّنْيَا قَلِيلٌ وَالآخِرَةُ خَيْرٌ لِّمَنِ اتَّقَي وَلاَ تُظْلَمُونَ فَتِيلاً[1]
Je, huwaoni wale walio ambiwa: Izuieni mikono yenu, na mshike Sala na mtoe Zaka. Na walipo amrishwa kupigana, mara kundi moja kati yao liliwaogopa watu kama kumwogopa Mwenyezi Mungu, au kwa khofu kubwa zaidi. Na wakasema: Mola Mlezi wetu! Kwa nini umetuamrisha kupigana? Laiti unge tuakhirishia kiasi ya muda kidogo hivi! Sema: Starehe ya dunia ni ndogo, na Akhera ni bora zaidi kwa mwenye kuchamngu. Wala hamtadhulumiwa hata uzi wa kokwa ya tende.
Kuwa na itikadi na siku ya Kiama kunaleta athari kubwa kwa Waumini na Wacha Mungu, kama inavyosema Qur-ani:-
والَّذِينَ يُؤْمِنُونَ بِمَا اُنزِلَ إِلَيْكَ وَمَا اُنزِلَ مِن قَبْلِكَ وَبِالآخِرَةِ هُمْ يُوقِنُونَ[2]
Na ambao wanayaamini yaliyo teremshwa kwako, na yaliyo teremshwa kabla yako; na Akhera wana yakini nayo.
Na kwa upande mwengine, kughafilika au kusahau na siku ya Kiama, ni kwao wao Makafiri na wapendao anasa za dunia, na Mwenyeezi Mungu anawambia watu hao:-
كَلاَّ بَلْ تُحِبُّونَ الْعَاجِلَةَ. وَتَذَرُونَ الآخِرَةَ[3]
Hasha! Bali nyinyi mnapenda maisha ya duniani,Na mnaacha maisha ya Akhera.
Na kwa sababu hiyo basi Mtume Muhammad (s.a.w.w) anatahadharisha wale wasiokuwa na itikadi ya Siku ya Kiama, kuwa kutokuwa na itikadi na siku ya Kiama ndio chanzo cha kufuru, na kutenda maasi. Kama anavyosema ndani ya Kitabu chake kitakatifu.
إِلَهُكُمْ إِلَهٌ وَاحِدٌ فَالَّذِينَ لاَ يُؤْمِنُونَ بِالآخِرَةِ قُلُوبُهُم مُّنكِرَةٌ وَهُم مُّسْتَكْبِرُونَ[4]
Mungu wenu ni Mungu Mmoja. Lakini wasio iamini Akhera nyoyo zao zinakataa, nao wanajivuna.
[1] Suratun Nisaa Aya ya 77
[2] suratulBaqarah Aya ya 4
[3] Suratul Qiyamah Aya ya 20-21
[4] Suratun Nahli Aya ya 22
MWISHO