BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI
KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
MALENGO YA MITUME YA MWENYEEZI MUNGU NO.4
* Mitume Mitukufu ya Mwenyeezi Mungu imekuja kuwalingania wanaadamu katika kitu gani?.
katika makala iliyopita tulielezea kuhusu malengo ya Mitume ya Mwenyeezi Mungu, na tukafikia sehemu ambayo ilitulazimu kuelezea maana ya neno Tawhiyd, katika makala hii tutendelea kufafanua kuhusu neno hilo na kuthibitisha hayo kwa mujibu wa Aya za Qur-ani takatifu.
Maana nyengine ya neno Tawhiyd :
Ni kuwa, maisha na rizki zote za wanaadamu zinakuja kutokana na mapendeleo yake Mwenyeezi Mungu, kama alivyosema Nabii Ibrahimu (a.s) kuwaambia kaumu yake:-
إِنَّمَا تَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللهِ اَوْثَاناً وَتَخْلُقُونَ إِفْكاً إِنَّ الَّذِينَ تَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللهِ لاَ يَمْلِكُونَ لَكُمْ رِزْقاً فَابْتَغُوا عِندَ اللهِ الرِّزْقَ وَاعْبُدُوهُ وَاشْكُرُوا لَهُ إِلَيْهِ تُرْجَعُونَ[1]
Hakika nyinyi mnaabudu masanamu badala ya Mwenyezi Mungu, na mnazua uzushi. Hakika hao mnao waabudu badala ya Mwenyezi Mungu hawakumilikiini riziki yoyote. Takeni riziki kwa Mwenyezi Mungu, na mumuabudu Yeye, na mumshukuru Yeye. Kwake Yeye ndio mtarudishwa. Lakini kwa upande mwengine kuikubali serikali ya kitaghuti hakuna maana ya kukubali hukumu za wanaadamu madhalimu wakidai kuwa ni kanuni kutoka kwa Mwenyeezi Mungu. Kama anavyosema Allah (s.w) kuwaambia wanafiki:-
اَلَمْ تَرَ إِلَي الَّذِينَ يَزْعُمُونَ اَنَّهُمْ آمَنُواْ بِمَا اُنزِلَ إِلَيْكَ وَمَا اُنزِلَ مِن قَبْلِكَ يُرِيدُونَ اَن يَتَحَاكَمُواْ إِلَي الطَّاغُوتِ وَقَدْ اُمِرُواْ اَن يَكْفُرُواْ بِهِ وَيُرِيدُ الشَّيْطَانُ اَن يُضِلَّهُمْ ضَلاَلاً بَعِيداً[2]
Huwaoni wale wanao dai kwamba wameamini yale yaliyo teremshwa kwako na yaliyo teremshwa kabla yako? Wanataka wakahukumiwe kwa njia ya upotofu, na hali wameamrishwa wakatae hayo! Na Shet'ani anataka kuwapotezelea mbali.
Kukubali hukumu za kitaghuti yaani ni kuporomoka kwa nguzo za kidini katika jamii, na kuwafanya makafiri na wapendao dunia ni bora kuliko wengine, kama inavyosema Qur-ani kuwaambia baadhi ya watu wa Ahlul-kitaab:-
اَلَمْ تَرَ إِلَي الَّذِينَ اُوتُواْ نَصِيباً مِّنَ الْكِتَابِ يُؤْمِنُونَ بِالْجِبْتِ وَالطَّاغُوتِ وَيَقُولُونَ لِلَّذِينَ كَفَرُواْ هَؤُلاء اَهْدَي مِنَ الَّذِينَ آمَنُواْ سَبِيلاً[3]
Huwaoni wale walio pewa sehemu ya Kitabu? Wanaamini masanamu na Shet'ani! Na wanawasema walio kufuru, kuwa hao wameongoka zaidi katika njia kuliko Walio amini.
*Tamko la jibti na Taghuti linatumika katika Uislamu kama tamko la shetani, hutumika katika kila ibada isiyokuwa ya haki, (ya Mwenyeezi Mungu) na katika kila jambo lisilowafiki sharia ya haki.
Mayahudi bughudha yao ilipozidi juu ya Uislamu walikwenda kufanya uitifaki na Makureishi na Waarabu wengine ili wamshambulie pamoja, Mtume na watu wake – wawasagesage, asisalie yoyote. Basi hao wakubwa wa Kiyahudi walipofika huko kwenda kufunga huo uitifaki waliwasujudia masanamu waliokuwa wakiabudiwa na Waarabu – na hali wao ni Ahlul-kitaab, wanajua kuwa ni ukafiri kufanya hivyo, na wakawatilia nguvu katika mambo mengine (hao Makureishi), na wakawaambia kuwa mwendo wao wa dini yao ni bora kuliko mwendo wa dini aliyokuja nayo Nabii Muhammad – na hali ya kuwa wanajua kuwa hivyo sivyo hata chembe lakini basi tu, wanataka wapate huo msaada wa Makureishi na Waarabu wengine ili wawasagesage Waislamu kwa hasadi na husuda yao tu, basi na kuona uchungu, kwa nini Nabii Muhammad kupata neema hiyo ya Utume, kama kwamba ufalme wa Mwenyeezi Mungu ni wao, wamehamaki kwa nini akapewa mtu kitu pasi na amri yao, Ndiyo Mungu anawasimanga kwa namna hiyo katika Aya ya 53.
اَمْ لَهُمْ نَصِيبٌ مِّنَ الْمُلْكِ فَإِذاً لاَّ يُؤْتُونَ النَّاسَ نَقِيراً[4]
Au wanayo sehemu ya ufalme (wa Mwenyeezi Mungu; basi wanahamaki kwa nini kapewa mtu kitu pasi na amri yao), basi hapo wasingeliwapa watu hata tundu ya kokwa ya tende.
*Aya hii inaonyesha kuwa yote hayo waliyokuwa wakiyafanya Mayahudi ni kwa ajili ya husuda tu; wanaona kwa nini Waislamu wapate hayo waliyoyapata. Hapana kitu kinachowatia tabuni watu, kikawazuilia kufuata ya haki kama uhasidi, ukimhusudu mtu basi hukubali kufuata lake, japo hilo ndilo la haki, na lenye manufaa dhahiri duniani na akhera, basi natutahadhari na sifa hii ili tufuate yaliyo ndiyo, tustarehe huku na huko.
Na hii hasadi ni kitiba (sifa) ya zamani sana, kama ilivyotajwa hapa katika Aya ya 54 , na ndicho kilichompelekea Iblisi kuwa Shaitaniy Rajiim na qatilun Athiym; na chungu ya wengineo tunaowasikia katika tarehe.
اَمْ يَحْسُدُونَ النَّاسَ عَلـٰي مَا آتَاهُمُ اللّهُ مِن فَضْلِهِ فَقَدْ آتَيْنَا آلَ إِبْرَاهِيمَ الْكِتَابَ وَالْحِكْمَةَ وَآتَيْنَاهُم مُّلْكاً عَظِيماً[5]
Au wanawahusudu watu kwa yale aliyo wapa Mwenyezi Mungu kwa fadhila yake? Basi tuliwapa ukoo wa Ibrahim Kitabu na hikima na tukawapa utawala mkubwa.
Tukiendelea na mada yetu, tunapata natija kuwa Mitume yote imekuja kuwalingania wanaadamu kumuabudu Mola mmoja, na kuwatahadharisha kufuata au kuikubali hukuma ya kitaghuti, kama anavyosema Allah (s.w):-
وَلَقَدْ بَعَثْنَا فِى كُلِّ اُمَّةٍ رَّسُولاً اَنِ اعْبُدُواْ اللّهَ وَاجْتَنِبُواْ الطَّاغُوتَ فَمِنْهُم مَّنْ هَدَي اللّهُ وَمِنْهُم مَّنْ حَقَّتْ عَلَيْهِ الضَّلالَةُ فَسِيرُواْ فِى الاَرْضِ فَانظُرُواْ كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الْمُكَذِّبِينَ[6]
Na kwa hakika kwa kila umma tuliutumia Mtume kwamba: Muabuduni Mwenyezi Mungu, na muepukeni Shetani. Basi kati yao wapo alio waongoa Mwenyezi Mungu. Na kati yao wapo ambao ulio wathibitikia upotovu. Basi tembeeni katika ardhi, muangalie ulikuwaje mwisho wa wanao kanusha.
[1] Surat Ankabuut Aya ya 17
[2] Surat Nisaa Aya ya 60
[3] Suratun Nisaa Aya ya 51
[4] Surat Nisaa Aya ya 53
[5] Suratun Nisaa Aya ya 54
[6] Surat Nahli aya ya 36
MWISHO