BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
UMUHIMU WA KUVAA HIJABU KATIKA JAMII. NO.1
Katika makala zilizopita tulielezea umuhimu wa kuvaa hijabu katika jamii, na tukaashiria baadhi ya masuala ambayo yanahusiana na umuhimu wa kuvaa hijabu, tunamshukuru Mola kwa kutupa nguvu za kuweza kuyajibu masula hayo, katika makala hii tutaendelea na mada yetu hiyo hiyo, tunategemea mtafaidika na tutakayoyaeleza yanayohusiana na umuhimu wa kuvaa hijabu.
Miongoni mwa masuala yaliyoulizwa ni haya yafuatayo:-
KWA NINI HAMUWAAMBII WANAUME WASIWAANGALIE WANAWAKE? KWANI JAMBO HILO LITAWAFANYA WANAWAKE WASIVAE HIJABU
Naelewa kwamba kwa kutokana na hatua nilizozielezea hadi kufikia hapa utakuwa huna haja ya kuuliza suala kama hili, kwa sababu wewe mwenyewe umeshaona kwamba sio kwamba wanaume tuwameambiwa wasiwaangalie wanawake tu, bali kuna msisitizo mkubwa zaidi ya huo, kwani wao ndio wa mwanzo kukatazwa kabla ya wanawake kuamrishwa kuvaa hijabu, kama ilivyo katika Suratun-Nuur, pale Mola alipowataka wanawake kuvaa hijabu, kwanza aliwaanza wanaume kuwaambia wasiwaangalie wanawake, na amemwambia Mtume (s.a.w.w) akisema “waambie waumini wa kiume wainamishe macho yao.
Ama ni jambo lililowazi kwamba haitoshi kuwaambia tu wanaume wasiwaangalie wanawake mpaka kupatikane matayarisho yatakayowafanya wanaume wasiwaangalie wanawake (yaani kuvaa hijabu), kama ilivyokuwa kuihifadhi mali ya jamii haitoshelezi kuwaambia watu tu kwamba wasiikodolee macho mali ya wengine, na wasiitumie mali ya wengine, bali inahitajika vile vile kuusia watu wasiziweke ovyo ovyo mali zao na wazihifadhi mali hizo, basi ndiyo hivyo hivyo katika sheria za Mola zenye kuihifadhi jamii, pande zote mbili zimeamrishwa kutekeleza wajibu wake, wanaume wasiwaangalie wanawake kwa matamanio, na wanawake nao wasijitangaze kwa wanaume kwa kujipamba na kujiweka uchi.
KWA NINI WANAUME WANA RUHUSA YA KUFANYA WALITAKALO NA KUVAA NGUO WAZIKATAZO? NA WANAWAKE WANALAZIMISHWA KUJIHIFADHI.
Katika kujibu suala hili kunalazimika kusema kwamba, sio kwamba wanaume hawawajibikiwi au hawana wadhifa wowote na dini inawaruhusu kuvaa nguo wazitakazo, lakini kwa sababu lengo la amri zote hizi ni kuhifadhi heshima ya jamii na kuleta amani ya kimwili na ya kiroho katika jamii, na kuzuia shetani na fikra zakezisipenye katika safu za watu, ikiwa mwanamme ataelewa kwamba kuhudhuria kwake katika jamii katika hali maalum, kama vile kuvaa nguo ya mikono mifupi au kujipamba, kutawafanya wengine waingie katika makosa basi atajiepusha kufanya hivyo.
Ama sababu ya kwamba wanaume sheria haiwabani zaidi katika sheria za kivazi ni kwamba Mola uzuri na kuvutia amekuweka katika kiwiliwili cha mwanamke na wanaume kwa ujumla hawavutii, kiasi ya kwamba wao walazimike kujifunika,basi sheria ya kivazi inaendana na suala la kuvutia na uzuri, ushahidi kuhusiana na maelezo haya ni huu, sisi tumeona katika tarehe aghalabu wanawake ndio wenye kuindwa, na wanaume ndio wawindaji, na mashairi pamoja na visa vya waandishi mara nyingi vinazungumzia uzuri na mvutio wa wanawake, lakini hakujatokea hata mara moja mwanashairi kumsifu mwanamme kwa uzuri wa mwili wake, basi wewe mwenyewe umeona kwamba suala la kutofautisha mwanamme na mwanamke na ubaguzi halipo,bali Mola kwa kutokana na ukweli ulivyo na mambo ya kimwili ya mwanamke na mwanamme pamoja na mambo ya kiroho, ndiyo ambayo yamemfanya Mola azipange sheria kama uzionavyo.
MWISHO