MIPAKA KATIKA UHAKIKI WA DINI
  • Kichwa: MIPAKA KATIKA UHAKIKI WA DINI
  • mwandishi: NDUGU ZETU WA KIISLAMU
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 17:22:31 2-11-1403

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

MIPAKA KATIKA UHAKIKI WA DINI

Msingi wa kuwepo mipaka katika uhakiki wa dini.

Huo ni msingi mwengine miongoni mwa misingi ya uhakiki wa dini.

Vitengo vya uhakiki wa dini vinavyowadhamini na kuwaletea faida wahakiki wa dini ni vile vitengo ambavyo vinabainisha na kuelezea mipaka yote ya dini katika Nyanja mbali mbali, kifikra na kimatendo, kwa sababu pindi itakapokuwa uhakiki wa dini haukubainisha mipaka ya dini katika Nyanja mbali mbali, muhakiki hataweza kupata yale mahitajio yake anayoyahitajia, katika kutatua matatizo yanayomkabili au katika kuhukumu kulingana na uhakiki alioufanya. Msingi wa kutoa natija iliyopatikana katika uhakiki wa dini.
Muhakiki wa dini baada ya kukamilisha hatua za tahakiki zake na uhakiki wake inampasa kutoa nadharia na mabainisho yake katika jamii, nadharia hizo ni kulingana na mahitajio yake au matatizo yaliyokuwa yakimkabili, matatizo au mahitajio ambayo ndiyo yaliyomfanya kuingia katika uwanja huo wa uhakiki, nadharia hizo ndizo zitakazomfanya muhakiki huyo kukua kifikra, na anaweza kutoa mabainisho yake katika mtindo wa maandiko. Siasa hiyo ya mabainisho ya wahakiki inaweza ikasaidia katika kukuza kiwango cha fikra cha wanajamii kwa kuandikwa makala tofauti au hata vitabu, kwa hiyo, itakapokuwa wahakiki watafanya tahakiki zao kupitia mfumo huo hapana shaka kutaleta mafanikio ndani ya jamii na hata muhakiki mwenyewe binafsi. Kutokuwepo kwa dini nyingi tofauti. Licha ya kuwepo tofauti msingi za dini na madhehebu, vile vile kuna mashirikiano baina yao, suala lipo hapa. Hivi mashirikiano hayo yaliyopo baina ya dini inawezekana pakawepo na idhini ya kukubali misingi ya dini hizo? Ikiwa kuna uwezekano wa kupatikana natija zilizo sahihi zinazotokana na itikadi au imani ya dini kwa kutumia misingi isiyokuwa ya kidini, hivi misingi hiyo ina nguvu za kidini zitakazoweza kuthibitisha kuwa uhakika wa misingi hiyo (isiyokuwa ya kidini) inaweza kukubalika kama ni itikadi au imani ya dini hiyo? Au dini ni mfumo maalumu uliojengwa katika nidhamu maalumu, nidhamu ambayo imekusanya ndani yake itikadi, imani, mwenendo, matendo n.k. hiyo ni nidhamu inayoweza kuarifishwa na kukubalika katika msingi mmoja tu, na misingi mengine haziwezi kuingia katika nidhamu hiyo, kwa sababu mbali ya kuwa misingi hiyo haitambuliki kama ni misingi ya dini, vile vile ni vikwazo vikuu vinavyowaweka na kuwazuia watu kuwa mbali na dini.

Natija inayopatikana kutokana na maelezo hayo ni kwamba; dini ya haki ni moja tu, na dini hiyo imeteremshwa kulingana na mahitajio ya dhati yaliyomo ndani ya nafsi ya kila mwanaadamu, dini hiyo alibainishiwa mwanaadamu pale alipoumbwa na Mola wake, kidogo kidogo ikalinganiwa na wajumbe wa Mwenyeezi Mungu kabla hata ya kuja Mtume Muhammad (s.a.w.w) kulingana na mahitajio ya wanaadamu, na alipokuja Mtume Muhammad (s.a.w.w) aliipa ustawi na kuinawirisha dini hiyo katika nyoyo za watu ili kuwaongoza watu hao katika njia ya saada itakayowafikisha wao katika ukamilifu, kwa hiyo, dini ya haki ni ile dini ambayo inaendana sawa na mahitajio ya mwanaadamu, kwa sababu, kama ikiwa dini ya haki ni ile dini ambayo itamfikisha mwanaadamu katika ukamilifu, na ikiwa ukamilifu huo utapatikana kutokana na muongozo wake Mtume Muhammad (s.a.w.w) na Ahlulbayt wake (a.s), basi hakuna njia nyengine zozote zile zitakazoweza kumfikisha mwanaadamu katika ukamilifu huo anaotakiwa kuufikia, (ijapokuwa njia hizo zinaweza kumpa mwanaadamu kiasi cha taaluma ndogo tu, taaluma ambayo inaweza kuwa na chembe maarifa ya dini), basi njia hizo hazikubaliki, na ni njia moja tu inayoridhiwa na Yeye Mola Mtakatifu itakayomfikisha mwanaadamu katika ukamilifu, na kumpatia saada ya duniani na akhera, na ni Mtume Muhammad (s.a.w.w) na Ahlulbayt wake ndio waliopewa taufiki hiyo ya kuwaongoza na kuwalingania watu katika njia hiyo ya ukamilifu.


MWISHO