UISLAMU CHANGUO LANGU (61)
  • Kichwa: UISLAMU CHANGUO LANGU (61)
  • mwandishi: Iran Swahili Radio
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 17:24:5 2-11-1403

Uislamu Chaguo Langu

Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Hamjambo wapenzi wasomaji, na karibuni kujiunga  nami katika makala hii, ambayo huangazia watu ambao baada ya kufanya utafiti wa kina huamua kufuata njia iliyojaa nuru maishani, yaani Uislamu. Karibuni kujiunga nami hadi mwisho.

Ni jambo la kusikitisha kuona kuwa utamaduni uliokita mizizi katika nchi za magharibi ni ule wa kuridhia na kufadhilisha matamanio ya kinafsi na kuyataja kuwa ni fanaka na saada ya mwanaadamu. Hali kama hiyo bila shaka itampelekea mwanaadamu katika maangamizi. Katika jamii kama hizo za kimagharibi umaanawi na dini ni vitu ambavyo vimepuuzwa kwa kiasi kikubwa . Pamoja na kuwa mwanaadamu wa Kimagharibi anapata anasa zote za kidunia atakazo, lakini bado angali anajihisi kuwa mtupu na daima anasumbuliwa na masuala ya kiroho. Kinyume na hilo, mwanaadamu ambaye ana fikra za kidini na kimaanawi huwa anafahamu kuwa kila kitu duniani kina mahesabu maalumu na kwamba kuna maisha baada ya haya ya dunia. Kwa hivyo mtu mwenye imani daima huwa ana tafakari kuhusu kifo chake na hujitahidi kutenda amali njema kwa ajili ya kesho akhera. Yeye huamini kuwa Mwenyezi Mungu ndie Mwenye kumiliki mbingu na ardhi, na kwamba yeye ni mwenye uadilifu na huruma. Ni kwa sababu hii ndio anayemuamini Mwenyezi Mungu na siku ya kiyama hapotezi imani na matumaini hata kama atakumbwa na masaibu maishani kwani yeyey hujua kuwa masaibu na matatizo maishani hayaji ila kuna hekima nyuma yake. Mwanaadamu muumini hata wakati ambao ana maisha mazuri na yenye utulivu hujitahidi kuendeleza maadili mema na kuchunga mipaka ya Mwenyezi Mungu. Yeye daima hulenga kumridhisha Mwenyezi Mungu katika hali zote za shida na masaibu na furaha na maisha bora. Fikra na mtazamo kama huu humpa mtu mwenye imani matumaini ambayo huleta utulivu wa kina moyoni. Kwa hakika matatizo mengi ya kinafsi au kisaikolojia huondoka iwapo tu kutakuwepo na dini maishani. Wanasaikolojia wengi wanaamini kuwa magonjwa mengi ya kinafsi au kiakili huonekana zaidi katika watu wasio kuwa na dini huku watu wanaomuamini Mungu, kadiri imani yao ilivyo imara, hawapati magonjwa ya kinasi na yakiwepo hutibika haraka zaidi. Msomi Mfaransa Ernest Renan katika kitabu chake kuhusu 'Historia ya Dini' anasema: "Yamkini siku moja, kila kitu nikipendacho kikaangamia na kile ambacho kinanifurahisha zaidi maishani kikaondoka. Lakini ni nadra kuona mvuto katika dini ukiondoka au kuangamia. Bali hisia ya kupenda dini daima itabakia." Karibuni kujiunga nami katika makala yetu ya leo ya 'Uislamu Chaguo Langu' ambapo leo tutamuangazia mwanamke mjerumani aliyesilimu.

'Kwa muda wa miaka 20 katika umri wangu niliishi bila lengo lolote na kwa uhuru usiokuwa na maana. nilipotea hadi pale Mwenyezi Mungu alipouchukua mkono wangu na kuniondoa katika kiza tororo kisha akanifikisha katika kilele cha nuru."

Haya ni maneneo ya Tania Poling, Mjerumani aliyezaliwa mjini Hamburg. Ingawa hapendagi sana kuzungumzia yaliyopita, lakini kufuatia ombi letu amezungumzia namna alivyopata taufiki ya kusilimu ifuatavyo:

"Kisa changu kinaanzia hapa; siku moja nilikutana na mwanamke Mwislamu aliyevaa Hijabu katika soko la mji wa Hamburg. Mimi nikiwa na marafiki zangu, tulijaribu kumfanyia masikhara mwanamke huyo kutokana na hijabu yake. Nilimwambia hivi, 'mbona una vaa vazi kama hili, kwani wewe ni mwendawazimu? Alinijibu moja kwa moja kwa kusema. 'mbona wewe umeuacha mwili wako wazi ili kila mtu auone atakavyo'. Maneno hayo yalinishtua sana kwani alijitahidi kuthibitisha kuwa kuvaa vazi la stara la hijabu kunamhifadhi na kumtakasa, na ni ishara ya afya ya kiroho na mlingano wa kisaikolojia ambao unampa mwanamke uhuru wa kimaanawi na usalama wa kijamii. Kwa vyovyote vile baada ya mazungumzo marefu kidogo tuliachana na kila moja wetu akaenda zake. Lakini mantiki na yakini aliyokuwa nayo mwanamke huyo Mwislamu ni jambo ambalo lililinishughulisha kwa muda mrefu."

Tania anaendelea kwa kusema: "Suala la Hijabu na maneno ya huyo mwanamke Mwislamu ni mambo ambayo yalinipelekea katika kina cha fikra hadi siku moja nikaamua kuenda katika Msikiti wa Imam Ali AS mjini Hambruge na hapo niliweza kukutana na Waislamu kutoka mataifa mbali mbali ambapo tulibadilishana mawazo. Hapo ilinibainikia kuwa si tu kuwa Hijabu si kizingiti kwa mwanamke bali hata humuandalia mazingira ya kuwa na harakati zaidi katika jamii huku vazi hilo likiwa limemdhaminia usalama wake. Kwa hakika Hijabu humpa mwanamke uwezo mkubwa sana. Ni kama ishara ambayo huwajulisha wengine kuwa: 'mimi sitaku kujiweka wazi niwe chombo cha kimaonyesho kwa wengine.' Mwanamke huyu mjerumani aliyesilimu anaendelea kusema kuwa: "Ilinibainikia kuwa Uislamu umempa hadhi ya juu mwanamke . Hijabu mbali na kuwa na faida nyingi za kiroho na kisaikolojia kwa mwanamke pia huweza kuwa na nafasi muhimu katika kuleta maadili  bora na mazingira salama katika jamii. Kwa mtazamo wangu Hijabu pia hupelekea kuimarika uhusiano wa kifamilia na kulinda misingi ya kijamii.  Uhusiano wangu na Waislamu kabla ya kusilimu pia ni jambo ambalo lilipelekea niwezi kujua kuhusu uhusiano wa kimaanawi baina ya Waislamu na Mwenyezi Mungu. Uhusiano huu ni wa karibu na jambo hili kwa kweli lilinivutia sana. Nilitambua kuwa Waislamu ni watu wenye malengo maalumu na kwamba baina yao hakuna mipaka ya kirangi, kitaifa au kijiografia. Kadiri nilivyozidi kujikurubisha na Waislamu nilihisi kuwa mimi pia ni Mwislamu," anasema Bi. Tania.

Mjerumani huyo aliyesilimu anafafanua kuhusu masuala ambayo yanaashiria udhaifu katika jamii ya Kimagharibi kwa kusema: "Uhusiano wa kibinaadamu na kiroho miongoni mwa watu wa nchi za Maghairbi ni dhaifu sana. Hata wakiwa na jamaa na familia hufadhilisha kuishi maisha ya upweke.  Binafsi pamoja na kuwa nilikumbwa na matatizo mengi baada ya kuamua kuwa Mwislamu lakini ningali nafadhilisha kuishi na wazazi wangu wawili. Imani yangu kwa Uislamu ni imara kabisa na wazazi wangu sasa wameukubali ukweli huu na hatuna mgogoro nao tena kuhusu hili. Hata naweza kusema kuwa wazazi wangu wanapenda tabia zangu sasa zaidi ya kabla nilivyokuwa kabla sijasilimu. Mimi hutumia wakati wangu wa mapumziko kusoma Qur'ani na vitabu vya kidini kwa lugha ya Kijerumani.

Katika sehemu nyingine ya maneno yake, Mjerumani aliyesilimu Bi. Tania Poling  anazungumza kuhusu Ayatullah Sayyed Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Iran kwa kusema:

"Kwa mtazamo wangu yeye ndie kiongozi pekee msomi, muumini na anayependa wanaadamu katika zama zetu hizi. Mimi namuona kama shakhsia iliyojaa ukarimu kwa kweli. Kwa mtazamo wangu Ayatullah Khamenei anadiriki ipasavyo matatizo ya kale ya watu duniani hasa ya Waislamu. Maneno yake ni yaliyojaa mema na huruma. Yeye ni shakhsia mtakatifu na wa kirho na daima mimi humuomba Allah SWT ampe afya na salama."

Kwa kumalizia, Mjerumani aliyesilimu Bi.Tania Poling  anasema: "Iwapo kwa kusilimu nilipoteza kila nilichokuwa nacho lakini mahapa pake nimejipata. Kabla ya kusilimu nilikuwa na kila kitu isipokuwa Allah SWT na nilikuwa nahisi utupu lakini leo nimempata na Uislamu umenipa kila kitu nilichotaka. Nimepata uhuru wa Kimaanawi, utulivu wa kirho na Kiongozi anayefaa na ninayempenda. Kwa kuukubali Uislamu, nimeipata barua ya Allah SWT kwa wanaadamu, yaani Qur'ani Tukufu na kitabu hiki ndio mtaji wangu mkubwa zaidi. Katika usiku mmoja mrefu nikiwa na umri wa miaka 20 niliweza kupata pambazuko katika maisha yangu. Ni pambazuko ambalo liliniletea mwamko na machipuo mapya maishani.