KUMJUA MUNGU KUPITIA QURAN
  • Kichwa: KUMJUA MUNGU KUPITIA QURAN
  • mwandishi: NDUGU ZETU WA KIISLAMU
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 17:26:2 2-11-1403

BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

KUMJUA MUNGU KUPITIA QURANI
Njia ya kumjua Mwenyezi Mungu katika mtazamo wa Qur'ani
Mtoto mdogo anayeyashika maziwa au matiti ya mama yake kwa mikono yake, hunyonya matiti hayo kwa lengo la kupata maziwa. Bila shaka huwa anataka maziwa, na anapokichukua kitu chochote kwa mikono yake kwa lengo la kukila basi bila shaka atakielekeza katika mdomo wake.

Lengo lake halisi ni kula. Iwapo atapata kuwa kitu alichokichukua hakiliki basi hukitupilia mbali. Kwa njia hiyo hiyo mwanadamu hutafuta ukweli na hakika katika kila kitendo anachokifanya. Anapopata kuwa amekosea huumia na kujuta kwa nini alijisumbua bure na kukosea katika kitendo hicho. Daima mwanadamu hujiepusha na makosa na hujaribu kuufikia ukweli na hakika, kadiri ya uwezo wake.

Jambo hili linaweka wazi nukta hii kwamba, kimaumbile na kihisia mwanadamu ni mkweli. Yaani atake au asitake, daima hutafuta ukweli na kufuata haki. Mwanadamu hakufunzwa jambo hili na mtu yoyote wala kutoka sehemu yoyote ile. Iwapo mara nyingine mwanadamu hukana na kukataa haki, huwa ni kwa sababu amechanganyikiwa kutokana na makosa na kutotofautisha kati ya haki na batili na iwapo haki itambainikia, basi bila shaka hawezi kufuata batili.

Mara nyingine pia mwanaadamu hupatwa na maradhi ya nafsi kutokana na tamaa, majivuno na kuipenda nafsi yake kupindukia. Hali hii huibadilisha ladha nzuri ya ukweli kuwa chungu. Kwa hivyo huipinga haki na kutoifuata hata kama anaifahamu vyema. Japokuwa mtu wa aina hii hukubali uzuri wa haki na kukiri umuhimu wa kuifuata lakini yeye mwenyewe huwa hawezi kusalimu amri. Jambo hili ni mfano wa mambo yanayotukia kutokana na mazoea ya kutumia vitu vyenye madhara. Mwanaadamu huikandamiza hisia yake ya kimaumbile (ambayo ni ya kudondoa hatari na kuepuka madhara) na kufanya kitendo cha kumsababishia madhara (kama wale waliozoea sigara, pombe na madawa ya kulevya).

Qur'ani Tukufu humsihi mwanaadamu kuzingatia ukweli na kuifuata haki. Qur'ani inasisitiza juu ya jambo hili kwa njia mbalimbali na kuwataka watu walinde na kuihifadhi hisia yao ya ukweli na inayotatua haki. Mwenyezi Mungu anasema:
"Na nini kiko baada ya (kuacha) haki, isipokuwa upotofu?" (10:32) Katika sehemu nyingine anasema:
"Hakika binadamu yuko khasarani. Isipokuwa wale walioamini na wakafanya vitendo vizuri, na wakausiana (kufuata) haki na wakausiana (kushikamana) na subira, (kustahamiliana)." (103:2-3) Bila shaka maagizo haya ya Mwenyezi Mungu yanaonyesha kuwa iwapo mwanadamu hataihifadhi hisia yake ya kweli na iwapo hatafanya juhudi za kuifuata haki na hakika, basi bila shaka hawezi kuridhika na mafanikio wala saada aliyonayo maishani na kuwa atayafuata mambo mengineyo ya kumvutia kadiri ya tamaa aliyonayo. Matokeo ya hali hii ni kuwa atakumbwa na fikra mbaya zisizokuwa na msingi. Hatimaye kama vile mnyama wa miguu minne aliyepotea njia (ambayo ni rasilimali ya mwanadamu) huwa mhanga wa matamanio na kutojizuia kwake kutokana na ujahili na upumbavu wake.

Mwenyezi Mungu anasema: "Je! Umemwona aliyeyafanya matamanio yake kuwa ndio mungu wake? Basi je, wewe utakuwa ni wakili wake? Au wewe unadhani kwamba wengi wao wanasikia au wanaelewa? Hawakuwa wao ila ni kama nyama, bali wao wamepotea njia zaidi. (25: 43-44)

Kwa ufupi Mwenyezi Mungu anasema: Unafikiriaje kuhusu wale watu wanaoyaabudu matamanio yao? Je, unadhani kuwa unaweza kuwaelimisha na kuwafahamisha watu hao? Je, unadhani kuwa wanaweza kusikiliza na kuelewa? Ni watu waliopotea zaidi kuliko wanyama. Hata hivyo hisia zao za kibinadamu zinapofufuka tena na moyo wa kutaka kufuata haki kuanza kufanya kazi tena, mambo huanza kuwabainikia moja baada ya jingine na hukubali mara moja kila ukweli na haki inapowabainikia. Huchukua hatua mpya na inayofaa kuelekea mafanikio na saada kila siku inayopita.

Mafundisho ya Qurani kuhusiana na Muumba wa ulimwengu: Kuwepo Muumba "…Je! Mnamfanyia shaka Mwenyezi Mungu, Muumba wa Mbingu na ardhi?" (14:10) Maelezo:
Mchana, kila kitu huonekana, tunaweza kujiona sisi wenyewe, watu wengine, nyumba, mji, jangwa, milima, msitu na pia bahari. Lakini giza la usiku liingiapo, vitu hivi vyote tulivyokuwa tukiviona hupoteza mwanga wake na kutoweka. Hapo ndipo sisi hugundua kuwa mwanga uliokuwa katika vitu hivyo haukuwa mwanga wavyo bali ni jua ndilo lililokuwa likiviangaza kwa njia fulani ya uhisiano. Jua ni angavu, na linapoangaza hufanya dunia na kila kitu kilichoko juu yake kung'ara na kuonekana. Iwapo vitu hivi vingekuwa na mwangaza wavyo vyenyewe, basi bila shaka havingeupoteza.

Wanadamu na viumbe vingine vyenye uhai huvitambua vitu mbalimbali kupitia macho, masikio na hisia. Hufanya vitendo kwa mikono, miguu na viungo vingine vya ndani na nje ya mwili. Baada ya kuizingatia hali hii, tunapata natija hii kwamba fikra, azma na mienendo au harakati ya viumbe hivi vyenye uhai haitokani na umbo la viumbe hivyo bali inatokana na roho vilivyo nazo. Wakati ambapo roho hizo zinapoondoka viumbe hivyo hupoteza maisha na harakati zao.

Kwa mfano, iwapo kuona na kusikia kungewezekana tu kupitia macho na masikio basi mambo hayo yangelikuwepo madamu viungo hivyo viwili vitaendelea kuwepo, lakini hali ya mambo is hivi hata kidogo. Kwa njia hiyo hiyo dunia hii pana ambayo bila shaka sisi ni sehemu ya viumbe vyake, iwapo kweli ilijiumba yenyewe basi bila shaka haingeliisha na kufikia mwisho. Pamoja na hayo tunaona kwamba baadhi ya sehemu ya dunia hii hutoweka moja baada ya nyingine. Daima sehemu hizo ziko katika hali ya mapinduzi na mabadiliko. Sehemu hizo huchukua nafasi ya sehemu nyingine na kuchukua umbo tofauti kabisa.

Kwa hivyo ni lazima tuhukumu moja kwa moja kuwa viumbe na vitu hivi vyote vilivyomo duniani vinatokana na kitu kingine ambacho kimevimba. Mara tu Muumba anapokata uhusiano wa uumbaji na kiumbe fulani, kiumbe hicho huangamia na kutoweka. Muumba huyo ambaye hana mwisho, ambaye ni tegemeo la viumbe vyote na ambaye anawahifadhi walimwengu wote ni Mwenyezi Mungu. Yeye ni Mwenyezi Mungu ambaye hana mwisho na kama angekuwa na mwisho kama vile viumbe vinginevyo basi uhai wake haungekuwa unatokana na Yeye Mwenyewe bali ungekuwa unategemea na kuwahitajia wengine.

Quran na Tauhid
Iwapo mwanadamu atakuwa na maumbile safi na moyo mtulivu na kisha autizame ulimwengu ataona athari za Muumba katika kila sehemu ya ulimwengu huu. Atapata dalili kutoka kila sehemu kuthibitisha ukweli huu. Kila kiumbe mwanadamu akionacho humu duniania ama ni kiumbe kilichoumbwa na Mwenyezi Mungu au kina sifa maalumu kiliyopewa na Mwenyezi Mungu au mfumo unaoongoza kila kitu kwa amri ya Mwenyezi Mungu. Mwanadamu ni mfano mmoja wa viumbe hivyo na mwili wake wote unalithibitisha jambo hili. Uhali alio nao mwanadamu si wake mwenyewe, wala sifa anazojipa mwenyewe kwa hiari yake.

Mwandamu hajabuni mfumo wa maisha anaoufuata tangu mwanzoni mwa maisha yake wala hawezi kusema kuwa mfumo huo umejengeka katika msingi wa bahati na sadfa na hivyo kujitenga. Mwanadamu hawezi kuuhuisha uhai wake pamoja na mfumo wa uhai wake na mazingira aliyoumbwa nayo. Hii ni kwa sababu kuwepo kwa mazingira yaliyotajwa na mfumo unaoyaongoza, havijaumbwa na mazingira wala havipo kibahati wala kisadfa.

Kwa hivyo mwanadamu hana njia nyingine yoyote ila kuthibitisha chanzo cha kuumbwa ulimwengu. Chanzo hicho huumba na kulea vitu. Hukipa uhai kila kitu chenye uhai na kukiongoza katika njia ya wokovu ili kifiikie ukamilifu wake kwa msingi wa mfumo mahsusi.

Mwanadamu anapoona kuwa kuumbwa kwa viumbe kunahusiana na kuwa kuna mfumo wa aina moja ulimwenguni, hulazimika kukubali kuwa chanzo cha uumbaji na mwongozaji wa mfumo wake si mwingine bali ni Mwenyezi Mungu. Qur'ani Tukufu inasema: "Lau wangelikuwamo humo miungu wengine isipokuwa Mwenyezi Mungu basi bila ya shaka hizo mbingu na ardhi zingeharibika... "(21:22)

Maelezo: Iwapo wangelikuwako miungu wanaouongoza ulimwengu kama wanavyosema washirikina kuwa kuna miungu wanaoongoza sehemu mbalimbali za ulimwengu, basi ardhi, mbingu, bahari na misitu kila kimoja cha vitu hivi kingelikuwa na mungu wake. Kutokana na tofauti kati ya miungu hiyo, kungedhihiri mifumo tofauti ulimwenguni jambo ambalo lingepelekea kutokea ghasia na ulimwengu kuangamia.

Hata hivyo tunashuhudia kuwa viungo vyote vya ulimwengu vina uhusiano mkubwa na vinaunda mfumo mmoja. Kwa hivyo ni lazima tusema kuwa hapana mshirika wa Mwenyezi Mungu ambaye ni Muumba wa Ulimwengu. Watu wengine huenda wakasema kuwa, kwa vile miungu hiyo inatambua kuwa tofauti zao hupelekea kuangamia kwa ulimwengu, basi huwa haitofautiani. Lakini hiyo ni dhana isiyokuwa na msingi wowote kwa vile Mwenyezi Mungu ambaye huuongoza ulimwengu wa viumbe au sehemu fulani ya ulimwengu ambaye vitendo vyake vinahusiana na mfumo wa uumbaji, hatumii akili tunavyoitumia sisi.

Tangu siku ya kwanza tunapoanza kuuona ulimwengu wa viumbe na kutazama mfumo unaouongoza hupata mtazamo fulani kuhusiana na mfumo huo. Hii ndio elimu yetu. Tunapofanya juhudi za kukidhi mahitaji yetu huviambatanisha vitendo vyetu na ile picha iliyoko katika fikra zeti ili vitendo hivyo viambatane na mfumo wa uumbaji. Kwa mfano sisi hula chakula kwa lengo la kuondoa njaa na ili kuondoa kiu tuliyo nayo sisi hunywa maji. Kwa lengo la kujikinga na baridi na vile vile joto, huvaa nguzo zinazofaa kwa sababu hutambua kuwa mahitaji kama hayo hukidhiwa na vitu vinavyonasibiana navyo katika mfumo wa ulimwegu.

Kwa hivyo kitendo chetu (katika mtazamo huu) hutegemea fikra yetu na huja baada ya fikra, ambayo hutegemea mfumo wa ulimwengu. Kwa hivyo vitendo vyetu viko hatua mbili kabla ya mfumo wa ulimwengu. Lakini kuhusiana na Mwenyezi Mungu ambaye huuongoza ulimwengu au sehemu moja ya ulimwengu huu, mfumo wa nje wa ulimwengu ni kitendo. Si sawa kuamini kuwa vitendo vyake hutokea kutokana na kutafaraki mfumo.

Marejeo
Muhtasari wa Mafunzo ya Kiislamu cha Allamah Muhammad Hussein Tabatabai

MWISHO