BSMILAHI AR-RAHMANI AR-RAHIIMI
KWANI NI LAZIMA KUSUJUDU JUU YA UDONGO WA KARBALA?
Hapana si lazima! Bali Mashia wanapendelea kusujudu juu ya mchanga uliotoka mji wa Karbala kwa sababu ya umuhimu wake uliopewa na Mtume (s.a.w.w.) na Maimam kutoka kwenye kizazi chake (Ahl al-Bayt). Na baada ya kuuwawa shahid kwa Imam Husein (a.s.), mwanawe Imam Zayn al-'Abidin (a.s.) aliuteka mchanga wa hapo kidogo na akautangaza kwamba huo ni mchanga mtukufu na akauhifadhi kwenye mkoba. Na Maimam (a.s.) walikuwa waki sujudu juu ya udongo huo wa Karbala na wakiutengenezea tasbih, kwa kumtakasa Mwenyezi Mungu kwayo.
[Ibn Shahrashub, al-Manaqib, Juz. 2, Uk. 251]
Vilevile waliwahimiza Mashia kusujudu juu ya udongo huo, kwa kuelewa kwamba si wajib, bali kwa mtazamo wa kupata thawabu zaidi. Maimam (a.s.) wamesisitiza kwamba kumsujudia Mwenyezi Mungu ni lazima kufanywe juu ya ardhi tohara tu, na hivyo wakapendelea kufanywe juu ya udongo wa Karbala.
[al-Tusi, Misbah al-Mutahajjad, Uk. 511]
[al-Saduq, Man la yahduruhu'l faqih, Juz. 1, Uk. 174]
Mashia, kwa muda mrefu wameuhifadhi udongo huu. Na kwa kuchelea usije ukavunjiwa heshima, ndipo wakautengeneza vipande vidogo vidogo vinavyoitwa Muhr au Turbah. Wakati wa Swala, tunasujudu juu ya udongo huo, lakini si kwa kuwa ni wajib, bali ni kwa mtazamo wa kuwa huo ni umbile maalum. Vinginevyo, tunapokuwa hatuna udongo tohara, tunasujudu kwenye ardhi liyo tohara, au juu ya kitu kinachotokana nayo.
Kwa kweli ni jambo la kusikitisha kwamba baadhi ya watu - kwa nia mbaya - husisitiza kwamba Shia wanaabudu mawe, au wanamuabudu Husein (a.s.). lakini ukweli ni kwamba sisi tunamuabudu Mwenyezi Mungu peke yake kwa kusujudu juu ya Turbah, na sio kuisujudia. Na kamwe hatumuabudu Imam Husein, Imam Ali, au Mtume Muhammad (s.a.w.w.). Tunamuabudu Mwenyezi Mungu pekee, na ni kulingana na amri yake huwa tunasujudu juu ya ardhi tohara tu.
Hitimisho:
Hii ndio sababu ya Waislamu wa madhehebu ya Shia huchukua vijiwe vidogo, ambavyo kwa kawaida hutengenezwa kutokana na udongo wa Karbala, uaowawezesha kusujudu juu ya vijiwe hivi vinavyopendelewa, vilevile hufuata sunnah za Mtume (s.a.w.w.). Basi mtukuze Mola wako pamoja na kumsifu, na uwe ni miongoni mwa wanaosujudu.
(Qur'an 15:98)
Kwa nini Mashia wanasujudu juu ya Turbah?
Waislamu wa madhehebu ya Shia wanapendelea kusujudu juu ya vijiwe vidogo vya udongo, viitwavyo Turbah, ambavyo kwa kawaida hutengenezwa kutokana na udongo wa ardhi ya Karbala iliyoko Iraq. Kulingana na fiqh ya madhehebu ya Shi'ah Ja'fari - ambayo ni moja miongoni mwa madhehebu tano za kiislamu - Sijda ni lazima ifanywe juu ya ardhi iliyo tohara au kinachoota juu yake, kwa sharti kwamba kisiwe ni kitu kinacholiwa au kuvaliwa. Hii - kufaa kusujudu juu yake - ikiwa ni pamoja na vumbi, jiwe, mchanga na nyasi, kwa sharti kwamba visiwe ni madini. Inaruhusiwa kusujudu juu ya karatasi, kwa sababu imetengenezwa kutokana na kinachomea ardhini, lakini haifai juu ya nguo au zulia. Wanavyuoni wa madhehebu yote ya Sunni wanakubaliana na kujuzu kwa kusujudu juu ya ardhi na kinachoota juu yake.
Je Mtume na Maswahaba wake walifanya hivi?
Kuswali juu ya ardhi kulikuwa kukifanywa na Mtume (s.a.w.w.) na waliokuwa karibu naye. " Amehadithia Abu Sa'id al-Khudri: "Nilimuona Mtume wa Mwenyezi Mungu akisujudu juu ya matope na maji, nikaona alama ya matope kwenye paji lake la uso.
[Al-Bukhari, Sahih (Tafsiri ya kiingereza), Juz. 1, Kitabu 12, Na. 798; Juz. 3, Kitabu 33, Na. 244]
" Amehadithia Anas bin Malik: "Tulikuwa tukiswali na Mtume kwenye vuguto la joto kali, na ikiwa mmoja wetu hakuweza kuweka uso wake - kwa kusujudu - juu ya ardhi (kwa ajili ya joto), basi yeye alikuwa akiitandika nguo zake chini na kusujudu juu yazo. [Al-Bukhari, Sahih (Tafsiri ya kiingereza), Juz. 2, Kitabu 22, Na. 299]
Kulingana na Hadith hii yaonyesha kwamba ilikuwa ni katika mazingira na hali zisizokuwa za kawaida tu ndipo Mtume (s.a.w.w.) na maswahaba wake waliweza kusujudu juu ya nguo.
Mtume (s.a.w.w.) pia alikuwa akisujudu juu ya Khumra.
" Amehadithia Maymuna: Mtume wa Mwenyezi Mungu alikuwa akisujudu juu ya Khumra. [Al-Bukhari, Sahih (Tafsiri ya kiingereza, Juz. 1, Kitabu 8, Na. 378] " Kulingana na mwanachuoni mashuhuri wa kisunni, Al-Shawkani: Zaidi ya maswahaba kumi wa Mtume (s.a.w.w.) wametaja Hadith kuhusu yeye kusujudu juu ya Khumrah, na ameorodhesha marejeo yote ya kisunni yaliyopokea Hadith hii, ikiwa mni pamoja na Sahih Muslim, Sahih al-Tirmidhi, Sunan Abu Dawud, Sunan al-Nasa'i na nyinginezo.
[Al-Shawkani, Nayl al-Awtar , Sura ya 'Kusujudu juu ya Khumrah', Juz. 2, Uk. 128]
Khumrah ni nini?
" Ni mswala (mkeka) mdogo unaotoshea kuweka uso na mikono pindi mtu anaposujudu wakati wa Swala. [Al-Bukhari, Sahih (Tafsiri ya kiingereza), Juz. 1, Kitabu 8, Na. 376 (kama ilivyofafanuliwa na mfafanuzi)] Ibn al-'Athir, mwanachuoni mwingine wa Sunni, ametaja katika kitabu chake Jami al-'Usul: " "Khumra ni ile ambayo Mashia wa sasa wanasujudia juu yake wanaposwali." [Ibn al-'Athir, Jami' al-Usul, (Cairo, 1969), Juz. 5, Uk. 467] " "Khumra ni mswala dogo uliotengezwa kwa nyuzi za mtende au kwa malighafi nyingine…. Ni kama zile wazitumiazo Mashia wanaposujudu."
[Talkhis al-Sihah, Uk. 81]
Kwa nini udongo wa ardhi ya Karbala?
Sifa maalum za udongo wa mji wa Karbala (nchini Iraq) zinajulikana, na ulikuwa una muhimu maalum wakati wa Mtume (s.a.w.w.) na baadaye: " Umm Salama amesema: Nilimuona Husein (a.s.) ameketi juu ya paja la babu yake, Mtume (s.a.w.w.) aliyekuwa ameshika kipande cha udongo mwekundu mkononi mwake, huku akikibusu na kulia. Hapo nikamuuliza ule udongo ulikuwa ni udongo gani. Mtume (s.a.w.w.) akajibu: "Malaika Jibril amenipa habari kwamba mwanangu huyu Husein atauwawa huko Iraq. Yeye ameniletea mchanga huu utokao huko kwenye ardhi hiyo. Nalia kwa mateso yatakayompata Husein wangu." Kisha Mtume (s.a.w.w.) akampa udongo ule Umm Salama na akamwambia: "Utakapouona udongo huu umebadilika na kuwa rangi ya damu, hapo utajua kuwa Husein wangu amechinjwa." Umm Salama aliuhifadhi udongo huo kwenye chupa, akawa akiuangalia, mpaka siku moja wakati wa siku ya Ashura, tarehe 10 ya Mwezi wa Muharram, mwaka 61 A.H., aliuona umekuwa na rangi ya damu. Kisha akajua kuwa Husein bin Ali (a.s.) ameuwawa.
[al-Hakim, al-Mustadrak, Juz. 4, Uk. 398]
[al-Dhahabi, Siyar a`lam al-nubala', Juz. 3, Uk. 194]
[Ibn Kathir, al-Bidayah wa'l-nihayah, Juz. 6, Uk. 230]
[al-Suyuti, Khasa'is al-kubra, Juz. 2, Uk. 450; Jam` al-Jawami, Juz. 1, Uk. 26]
[Ibn Hajar al-Asqalani, Tahdhib al-tahdhib , Juz. 2, Uk. 346]
" Ali ibn Abi Talib alipita Karbala baada ya vita vya Siffin. Aliuteka mchanga kido kwa mkoono wake akanung'unika akisema: 'Ah, ah, mahali penye alama hii baadhi ya watu watauwawa, na watainggia Peponi bila hisabu!' [Ibn Hajar al-Asqalani, Tahdhib al-tahdhib , Juz. 2, Uk. 348]
MWISHO