JAMII KUHITAJIA IMAMU
Baada kufahamu mitizamo tofauti katika suala la uimamu, sasa kuna haja ya kulijibu suala hili:-
Kuna umuhimu gani ya kuwepo Imamu kama Mashia wanavyoitakidi, hali ya kua sisi tuna Qur’ani na tuna Sunna vile vile?
JAMII KUHITAJIA IMAMU
Baada kufahamu mitizamo tofauti katika suala la uimamu, sasa kuna haja ya kulijibu suala hili:-
Kuna umuhimu gani ya kuwepo Imamu kama Mashia wanavyoitakidi, hali ya kua sisi tuna Qur’ani na tuna Sunna vile vile?
Kuna dalili nyingi zimetajwa katika umuhimu wa kuwepo Imamu (a.s), lakini tutataja dalili moja:-
Kama ilivyokua jamii inahitajia Mtume basi jamii hiyo inahitajia Imamu baada ya kuondoka Mtume, kwa sababu Uislamu ni dini ya mwisho, na Mtume (s.a..w.w) ni Mtume wa mwisho, kwa hiyo dini hii inatakiwa kuyatatua matatizo yote ya waislamu hadi kufikia siku ya Kiama, na kama inavyoeleweka kua Qur’ani imeelezea misingi mikuu ya dini kiujumla bila ya kufafanua, na mfafanuaji wa misingi hiyo alikua ni Mtume (s.a.w.w), na bila ya shaka Mtume (s.a.w.w) aliifafanua misingi hiyo kwa jinsi hali na mahitajio ya jamii ya zama zake, kwa hiyo basi kila zama zinahitajia Imamu atakayeyatatua matatizo ya watu wa zama hizo na kuifasiri Qur’ani kwa jinsi ya zama zake zilivyo.
Na Maimamu (a.s) ni walinzi wa urithi wa Mtume (s.a.w.w) na ni wafasiri wa Qur’ani, ili Qur’ani hiyo isije kusongomanishwa na maadui, ili dini pamoja na Qur’ani vibaki kua safi mpaka siku ya Kiama.
Na kwa kutokana na kua Imamu (a.s) ni mwanaadamu aliye mkamilifu, basi yeye ni kigezo kwa ajili ya wanaadamu wengine katika nyanja zote za ukamilifu, na wanaadamu wanamhitajia mtu kama huyu ili aweze kuwaongoza na waweze kujilinganisha nae kimatendo na waweze kujiepusha na kutokana na njia za upotofu pamoja na waepukane na Shetani.
Kwa kutokana na ufafanuzi uliopita hapo juu imefahamika vya kutosha kua mahitajio ya jamii kwa Imamu ni mahitajio ya kimaisha.
Nyadhifa za imamu ni hizi:-
1: Kuiongoza jamii (kuunda serikali).
2: Kuihifadhi dini na kuibainisha Qur’ani.
3: Kuzitakasa nafsi za watu na kuwaongoza.
SIFA ZA IMAMU
Mtu mwenye kuikalia nafasi ya Mtume (s.a.w.w) na mwenye kuyadumisha maisha ya kidini, na mwenye kuhusika na utatuzi wa matatizo ya watu, ni mtu mwenye nafasi maalum na cheo maalum, na mtu huyu anatakiwa kua na sifa maalum ambazo ni muhimu, na miongoni mwa sifa hizo ni kama ifuatavyo:-
1: Awe ni mcha Mungu na awe ni maasum kiasi ya kwamba hatakiwi kutenda kosa hata lile kosa la chini kabisa.
2: Awe na elimu ya kutosha inayotokana na Mtume Muhammad (s.a.w) na Allah (s.w) ndiye anayewapa elimu hiyo. Kwa sababu hiyo basi Imam ndiye mwenye kutatuwa matatizo ya watu wote, ya kidunia na akhera.
3. Awe na tabia njema na nzuri katika daraja ya juu kabisa.
4: Awe na nguvu za kuiongoza jamii katika muelekezo wa kidini.
Kutokana na sifa hizo tulizozitaja hakuna shaka kwamba hakuna mtu yeyote ulimwenguni atakayeweza kumchagua mtu huyo isipokuwa Allah (s.w), kwani Allah ndiye anayejua kila kitu anachofanya mwanaadamu kiundani au kidhahiri, basi Allah ndiye mwenye elimu ya kumchaguwa nani atakayeweza kuiongoza jamii baada ya Mitume yake. Basi moja katika sifa za Imam ni kwamba awe amechaguliwa na Allah (s.w).
Kutokana na umuhimu wa sifa hizo hakuna budi kuelezea kwa muhtasari sifa hizo.
ELIMU YA IMAM
Imam ni mtu ambaye anaiongoza jamii, basi ni lazima awe ana elimu na kuelewa kanuni za kidini na dunia, vile vile awe ni mwenye kufahamu tafsiri ya Qur-ani na sunna katika kubainisha masuala na mambo ya kidini, na aweze kuwajibu watu masuala yao yanayohusiana na maudhui tofauti, pia awaongoze katika muongozo ulio bora. Hakuna shaka itakapokuwa kuna kiongozi mwenye sifa kama hizo kutawapelekea watu kumuamini na kuwa na uhakika ya yale ambayo mtu huyo anawaongoza, basi hakuna shaka anaweza kupatikana kiongozi huyo kutokana na elimu inayotoka kwa Allah (s.w)
Kutokana na dalili hii madhehebu ya Shia yanaamini kuwa elimu ya Imam ambaye ni kiongozi baada ya Mtume Muhammad (s.a.w) inatoka kwa Allah (s.w).
Imam Ali (a.s) anasema:-
"Alama zitakazomuonyesha Imam kuwa ni Imamu wa haki ni kama hizi zifuatazo:-
"Imam ni mtu ambae mweye elimu ya hali ya juu kabisa kuliko watu wote duniani, mwenye kufahamu cha halali na haramu, na vile vile ni mwenye kutambua hukumu na kanuni tofauti katika masuala mbali mbali, na anayafahamu yale yote ambayo watu wanayahitajia”.
MWISHO