NJIA YA UZIMANI
  • Kichwa: NJIA YA UZIMANI
  • mwandishi: Yasin Valerian Massawe
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 7:27:11 24-8-1403

BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

NJIA YA UZIMANI

Njia ya uzimani ni nyembamba, waionao ni wachache.

UKWELI ni kwamba, Wakristo wana shahada (ubatizo) ambao hauhusiki na Nabii yeyote wa Mwenyezi Mungu. Sasa itakuwaje? Haya ni mambo ambayo Yesu aliyaona katika Roho kwamba watu watadanganywa kwa nguvu za shetani wamuitikadi kinyume na jinsi yeye mwenyewe alivyofundisha, hata akasema asiyeshika maneno yake atafananishwa na mtu mpumbavu aliyejenga nyumba juu ya mchanga. Kujenga nyumba juu ya mchanga hata kama utaipamba namna gani na kuigharamia namna gani lakini ulilofanya ni sifuri (ziro).

Mfano huu katika dini ni kushindwa kuelewa ile amri kuu (upweke wa Mungu) na kuwatambua Manabii wake wote kama alivyowaleta kwa haki ili wafundishe tumjue. Lile alilolilaani Yesu ndilo Wakristo wamelishika na lile alilolitukuza ndilo Wakristo wamelitupa. Hii inatokana na utabiri uliotoka mbali, kwani hata Nabii Isaya aliona katika Roho jinsi hali itakavyokuwa kuhusu chuo cha Qur'an kwani anasema: "... Vipofu wataona katika upofu na wenye akili, akili zao zitafichwa..." (Isaya 29:18) Qur'an imeletwa ili kuondoa giza. Basi wasiotaka kuelewa walete mfano wake kama wataweza (Qur'an 17:88). Na kama kweli ingelikuwa Qur'an ni mashairi aliyoyatunga Muhammad (s.a.w.) nadhani hicho kitabu kingesambaratikia mbali hata kizazi hicho kisijue jina la kitabu hicho isipokuwa labda katika historia tu.

Badala ya watu kutafuta yakini ya mambo, wanapoteza muda kulumbana kwa hoja za upuuzi kama kuangalia kiji - aya fulani cha Biblia au Qur'an. Yesu alipomtaja Muhammad alisema mafundisho yake yatakaa na watu milele kwnai BWANA atayahifadhi. Na ndivyo ilivyonenwa kwamba maneno ya Qur'an hayatafikiwa na batili mbele yake wala nyuma yake (Qur'an 41:42). Mimi nashangaa watu wanalumbana magazetini kwa hoja dhaifu kabisa eti "Paulo na Muhammad (s.a.w.) ni yupi aliyefundisha watu kuacha Torati?" Jawabu la wale wanaolumbana kwa jambo hili ni kama ifuatavyo: "Mtu kama hajui, ni hajui tu! Paulo aliporomosha msingi wa mafundisho ya Manabii na wanaomfuata wamejenga nyumba juu ya mchanga. Muhammad (s.a.w.) ni Nabii wa Mwenyezi Mungu na Rais wa Manabii.
Qur'an ni Agano Jipya ambalo halijaharibu hata chembe ya uadilifu kama ilivyofundishwa katika Agano la kwanza isipokuwa watu wengine wanachukulia udhaifu wa Akili za baadhi ya watu na kuhusisha na dini. Au mila na tabia ya jamii ya Waislamu, au baadhi ya Hadith dhaifu (zisizoaminika) ndani ya baadhi ya vitabu fulani fulani vinajulikana kama vya Kiislamu. Akili ya kawaida tu inamhakikishia mtu kwamba Nabii wa Mwenyezi Mungu hawezi kufundisha jambo la uovu au jambo lenye kombo hata kidogo. Uislamu kama Uislamu ni "pambo" kwa "mcha Mungu" Muislamu (mkweli) ni yule aonaye mbali ambaye yuko radhi kufa bila kuzini na kusema uongo. Mwenyezi Mungu haangalii sura, umbo, wala chochote alichonacho mtu ila moyo wake. Hivyo kumwelewa Mungu hakuzungumziwi kwa wasiokuwa Waislamu tu bali kwa Waislamu ndiyo walioshika anwani au shahada sahihi kulingana na tuliyoyaona.
Hivyo Muislamu yuko katika njia iliyonyooka, analotakiwa ni kupalilia njia hiyo iwe safi (asijitie madoa). Udhaifu wa kufasiri au kuelewa maneno ya Mwenyezi Mungu hauchagui asiye na dini, Mkristo wala Muislamu. Kwa mfano mtu asiyeamini Qur'an hata kama ana heshima gani mbele za watu, ana tofauti gani na mtu mwingine yeyote asiye na habari na Mungu? Au mfuasi wa Uislamu asiyetaka kuwa muumini sawasawa ana tofauti gani na bendera ambayo hufuata upepo? Ili kuthibitisha ukweli wa hoja zangu kuhusu kumjua Mungu yaani umuhimu wa kuangalia kwa makini sana dini iliyo sawa, Yesu anasema:
Luka 11:27-28 - "Ikawa alipokisema maneno maneno hayo, mwanamke mmoja katika mkutano alipaza sauti yake, akamwambia, heri tumbo lililokuzaa, na matiti uliyoyanyonya. Lakini yeye alisema, Afadhali, heri walisikiao neno la Mungu na kulishika". Yesu alizaliwa, akanyonya maziwa, akakua, akala chakula, akaishi kama wengine na alikuwa mwanamume, akavaa nguo kama wengine, akafundisha dini, akawa anasali kwa kusujudu kama wengine na akasema ametumwa na BWANA ... n.k. Basi je, wale wanaomuitakidi kama Mungu Mwana au Mungu mwenyewe, ni kipi kiwadanganyacho? Wanadhani Yesu alisema aitwe Mungu Mwana? Bila shaka haiwezekani. Basi je, ni kipi kiwadanganyacho? Hawatazami mbingu na ardhi na bahari na aina ya mimea na wanyama? Hawatazami wakafikiri ni nani aliumba?
Hawaoni kuwa aliyeumba ni mwenye uweza juu ya kila kitu? Hawaoni kuwa Mwenyezi Mungu husema atakacho kiwe na kinakuwa? Basi, je ndiyo atashindwa kumwambia Maryam "zaa na akazaa?" Basi je, mwana wa Maryam amekuwa mshirika wa Mwenyezi Mungu? Bila shaka haiwezekani Mwenyezi Mungu kuwa na mshirika. Basi je, imani itampeleka mtu peponi kwakuwa ni imani tu hata kama inamkufuru Mwenyezi Mungu?
Nani mwerevu mbele ya BWANA? Yeremia 9:23-24 - "BWANA asema hivi, mwenye hekima asijisifu kwa sababu ya hekima yake, wala mwenye nguvu asijisifu kwa nguvu zake, wala tajiri asijisifu kwa sababu ya utajiri wake. Bali ajisifuye na ajisifu kwa sababu hii, ya kwamba ananifahamu Mimi, na kunijua ya kuwa Mimi ni BWANA, nitendaye wema, na hukumu na haki, katika nchi, maana mimi napendezwa na ambo hayo, asema BWANA.
Mwerevu mbele ya BWANA ni yule atafutaye undani wa mafundisho ya manabii na kuyashika. Yesu kasema Amri Kuu kuliko zote ni "usimsimshirikishe BWANA", mpende kwa moyo wote, akili zote na ufahamu wote na kisha umpende jirani kama nafsi yako. Ina maana kabla hajafanya lolote kwa ajili ya BWANA ili upate katiak dunia na Akhera (mwisho) unatakiwa uhakikishe kwanza kwamba umemjua.
Kama ni sala, zaka, sadaka na mazuri nyingine yote na amri nyingine zote, lakini linalotakiwa kutangulia ni kukiri moyoni na kutamka kwamba BWANA ndiye Mungu Mmoja tu wa Pekee asiyezaa wala kuzaliwa wala kufanana na mwenye kukusudiwa kwa hoja zote. Ndiyo maana BWANA amesema, mwenye hekima asijisifu kwa sababu ya hekima yake bali ajisifuye ajisifu kwa sababu moja tu ya kwamba "Amenijua BWANA".
Sasa, kumjua BWANA maana yake ni nini? Maana jambo hili ni zito kwani BWANA mwenyewe kasema ijapokuwa mtu ana hekima lakini asimjue BWANA basi hana faida na hekima yake. Je, wapo wangapi wenye hekima na matendo mema kabisa lakini hawamjui BWANA? Mambo haya ndiyo yale aliyoyasisitiza Yesu katika Mathayo 7:24-27. Kumjua BWANA ni mfano wa mtu aliyepata dhabiti ili asimamishe nyumba juu yake. Hivyo anayetaka kumjua Mungu aelewe kwanza ni nini hasa anachokitaka Mungu kutoka kwake.
Kwanza anataka kumjua yeye na sifa zake zilizo sahihi na uwajue Manabii wake wote ndipo utekeleze yaliyosalia. Anayetaka kufanya jema lolote na kutumainia malipo yake hapa duniani na Akhera (mwisho) ajue lifuatalo:
"Mwabudiwa wa haki ni Mwenyezi Mungu asiye na mshirika, na Muhammad (s.a.w.) ni Nabii wake wa mwisho". Hiyo ndiyo kauli ya haki na njia iliyonyooka kwa mtu awaye yeyote anayetaka kufahamu. Utukufu wa Mwenyezi Mungu ni mbali na kujifananisha na kitu au kujifanya mwanadamu. Mahubiri ya Paulo juu ya Yesu ni ya kiwazimu na wote wanaoyatumainia wanatafuta njia ya kuzimu pasipo kujua. (Isaya 42:8, 44:24-26, 45:21-24 n.k.). Haya ndio kinyume na Uislamu, hiyo ni ibada batili. Hakuna cha asiyekuwa na dini, wala mwenye dini bali ukweli uko katika Uislamu tu. Namalizia kwa kusema kwamba tatizo ni watu hawaelewi tu, lakini hakuna shaka kwamba Qur'an ni uteremsho kutoka kwa Mola wa walimwengu, Mwenyezi Mungu, hakuna abudiwaye kwa haki ila Yeye tu.

MWISHO