BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM
RAMADHANI TANZANIA
Tanzania haitafautiani na nchi nyingine za Afrika Mashariki katika kuupokea Mwezi Mtukufu wa Ramadhani .
Unapokaribia mwezi wa Ramadhani Waislamu wa Tanzania hujitayarisha kwa hali na mali , wengi huwa na furaha isiyokifani kwani Wanaamini kwamba mwezi huu wa baraka na Imani za waja huongezeka maradufu.
Unapoingia mwezi 29 Shaabani Waisilamu huanza kufuatilia kuandama mwezi na baada ya sala ya Magharibi tu Waumini hushughulika katika kuangalia mwezi.Mandhari za watu na mienendo yao iliyozoeleka nayo hubadilika , Mahoteli mengi hufungwa na hili huonekana wazi kwa upande wa visiwa vya Zanzibar, vyenye wakaazi wengi waislamu, wakinamama nao huvaa huijabu na kujitanda vizuri wakielewa kuwa mwezi wa Ibada umewadia.
Misikiti inamiminika Waumini kwa kutekeleza ibada za swala za faradhi na za Sunna kama vile Tarawehe ,Tahajudi, na Witri katika sura ambayo Waumini wanaiishi katika kipindi chote cha kuingia hadi kumalizika mwezi Mtukufu, na hasa katika kumi la mwisho la Ramadhani ambapo Waislamu humiminika misikitini kwa ibada ya Itikafu kwa lengo la kutafuta Fadhila za Lailatul Kadri .Mgeni yeyote anayetembelea Tanzania hasa Zanzibar anaelewa kuwa , ni kweli mwezi Mtukufu umeingia.Darsa nyingi hufanyikamisikitini baada ya Sala ya Alasiri.
Huu ni upande wa Ibada , ama upande wa vyakula, watu wengi wa Tanzania hupendelea sana kula mihogo, ndizi mbichi, mbatata ( viazi mviringo), viazi vitamu, ndizi mbivu ambazo kwa kweli mara nyingi bei yake huwa ya juu sana, na ni watu wachache katika jamii wanaoweza kumudu kununua. Chai ni moja ya kinywaji kinachopendelewa katika futari ya jioni, lakini uji ndio unaoongoza kupendwa bila ya kusahau tende japo nne tano kwenye kisahani cha chai.
Pamoja nakuwa ni mwezi wa Saumu ( Funga) lakini matumizi huongezeka, na hii ni kutikana na kupanda bei bidhaa za vyakula lakini pia, mfungaji hatosheki na futari moja au mbili, wengi hupendelea zaidi ya hapo, wengi hufurahi kuona jamvi lina vyakula kama muhogo hivi, ndizi mbivu, ndizi mbichi, viazi vikuu, kaimati nakadhalika hapo mtu roho humtulia kidogo.
Ama kuhusu Daku siwengi wanaoweza kufuata Sunnah ya Usiku wa Manane, mtu hujipatia wali wake saa tano usiku na kuchapa mchago, lakini wengine wanaokwendana na Sunnah huamka saa tisa za usiku kwa Daku na kujipatia Fadhila za kuchelewesha Daku.
Kwa upande wa vyombo vya habari na hasa Sauti ya Tanzania Zanzibar, Matangazo yote hubadilika , vipindi vya Dini ya Kiislamu kama Qur'ani na Mawaidha ndio vinatawala, Kassida mbalimbali na waislamu wa maeneo ya Tanzania na mwambao wote wa Afrika ya Mashariki hujivunia sana Redio hii katika kuwapatia kile ambacho kinatakikana ndani ya Mwezi Mtukufu.
Hivi ndivyo Waislamu wa Tanzania wanavyoukaribisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ambapo mapenzi kati yao huongezeka na wale kipato huwasaidia wale wasionacho ili nao wajisikie furaha katika nyoyo zao.
Aidha katika hali hii ya kusaidiana, waislamu wengi wenye uwezo huwandaa Chakula cha kuwafutarisha watu katika misikiti ili kujipatia fadhila za wema huo, si hivyo tu bali kuna mwenendo mwengine mzuri ambao mshikamano kati ya watu katika mwezi huu mtukufu huongezeka , nao ni kule kukusanyika watu wa Familia moja au nyumba kadhaa za majirani katika sehemu moja na kujipatia futari yao kwa kila mtu kuleta kile alichomjaalia Mungu katika vyakula, hali hii huonekana zaidi katika maeneo ya viunga au vijijini.
Mwenyezi Mungu atupe afya njema na uwezo wa kuufunga mwezi huu Mtukufu na awajaalie kheri na fanaka Waislamu wote duniani.
AMIN
MWISHO