BIBLIA IMETAJA HIJABU
Mavazi Ya Wanaume Na Wudhuu?
Kuna Mkristo Mmoja alimuuliza Sheikh Swali hili,
SWALI:
Mimi ni mkristo, niliwahi kuambiwa kuwa kwenye biblia kuna aya zinazoonyesha kuwa ukristo unafundisha kuwa wanawake wavae hijabu. Na kuwa wanaume wavae kanzu na vilemba (hayo ndiyo mavazi matakatifu). Na kuwa Yesu alitawadha km waislam wanavyofanya. NAOMBA MNIPE MNISAIDIE MAANDIKO HAYO.
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Tunashukuru ndugu yetu katika utu na ubinadamu kwa swali lako hilo. Tunatumai kuwa katika majibu yetu utapata ukweli wa mambo na Dini ili kwa akili uliyopewa na Mungu uweze kujua ya haki na tunamuomba Mwenyezi Mungu Akupe moyo wa kuweza kuufuata ukweli. Hakika ni kuwa Mwenyezi Mungu Alituma Mitume na Manabii ili wawaelimishe na kuwafahamisha wanadamu kuwa njia ya kumjua na kumtambua Mwenyezi Mungu ni kufuata muongozo waliokuja nao. Mwenyezi Mungu Aliteremsha kitabu cha mwisho, Qur-aan ili kiwe ni uongofu kwa wanadamu wote. Mwenyezi Mungu Anasema: "Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa humo Qur-aan kuwa ni uongofu kwa watu, na hoja zilizo wazi za uongofu na upambanuzi" (2: 185). "Hiki ni kitabu ambacho hakina shaka ndani yake ni uongofu kwa wamchao Mwenyezi Mungu" (2: 2).
Wanadamu kwa kupita zama waliweza kubadilisha andiko ili wafuate matamanio ya nafsi zao. Jambo hili limebaki kuwa wazi hata katika mkusanyiko wa vitabu vilivyoteremshiwa Manabii wengine. Kubadilishwa huku kwa andiko kumewekwa wazi na Yeremia pale aliposema: "Mnawezaje kusema: 'Sisi tuna hekima, sisi tunayo sheria ya Mwenyezi Mungu,' hali waandishi wa sheria, wameipotosha sheria yangu" (Yeremia 8: . Katika nakala nyengine za Biblia zinasema: "Mwawezaje kusema kuwa sisi tuna akili kwa kuwa tuna Taurati ya Bwana ilhali kalamu za waandishi zimeifanya kuwa uongo". Hakika ni kuwa katika ile mistari iliyobakia utapata mambo mengi ambayo yanafanywa na Waislamu ilhali Wakristo wenyewe wameyawacha kabisa. Kati ya hayo ni kuwaita watu kwa ajili ya kuja kwa Ibada. Tazama Hesabu 10: 1-3, ambapo Mose anaagiziwa kufanya tarumbeta za fedha ili kuwaita watu wakati wa kuvunja kambi. Njia hii ya kuita watu haitumiki tena kwa tarumbeta bali sauti ya mtu ambaye anawaita watu kwa ajili ya Swalah (ibada), ambaye anaitwa muadhini.
Kutawadha ambako ni kuosha baadhi ya sehemu za mwili ili kujiandaa kwa ajili ya ibada pia kumetajwa katika Kutoka 40: 30-32, Mose aliweka birika la kutawadhia katikati ya hema na kutia maji ya kutawadha. Mose, Aroni na wanawe wote walinawa mikono na miguu ya humo walipoingia ndani ya hema. Waliosha kama walivyoamuriwa na Mwenyezi Mungu. Pia kuelekea sehemu fulani anapokuwa mtu yu katika ibada. Sisi Waislamu huwa tunaelekea nyumba Tukufu iliyoko Makkah. Katika kitabu cha Danieli 6: 10 kina maneno yafuatayo: "Danieli alirudi nyumbani kwake ghorofani katika chumba chake kilichokuwa na madirisha yaliyofunguka kuelekea Yerusalemu. Humo.. kama kawaida yake, alipiga magoti mara tatu kila siku akamwomba na kumshukuru Mungu wake".
Kusujudu ni njia muhimu ya Muislamu kujileta karibu na Muumba wake, nako ni kuweka paji lako la uso juu ya ardhi. Amali hii ilifanywa na Manabii waliopita miongoni mwao akiwemo 'Iysa (Yesu). Hebu tutazame maandiko machache kuhusu hilo. "Kisha Yesu akaenda pamoja nao bustanini Gethsemane, akawaambia wanafunzi wake, 'Kaeni hapa nami niende pale mbele kusali'…Basi akaenda mbele kidogo akaanguka kifudifudi, akasali" (Mathayo 26: 36 - 39). Naye Abramu akasujudu (Mwanzo 17: 3). Yoshua akainama chini akasujudu (Yoshua 5: 14). Naye Elia akapanda juu ya mlima Karmeli, na huko akainama hadi chini na kuuweka uso wake katikati ya magoti yake (1 Wafalme 18: 42). Ama kuhusu swali lako na mambo ambayo unayaona huyafahamu yapo wazi kabisa katika Biblia. Hijabu imetajwa katika kifungu kifuatacho: "Hali kadhalika nawataka wanawake wawe wanyofu na wenye busara kuhusu mavazi yao; wavae sawasawa na si kwa urembo wa mitindo ya kusuka nywele, kujipamba kwa dhahabu, lulu au mavazi ya ghar, bali kwa matendo mema kama iwapasavyo wanawake wamchao Mungu. Wanawake wanapaswa kukaa kimya na kuwa wanyenyekevu wakati wa kujifunza" (1 Timetheo 2: 9-11).
Ama kuhusu kanzu, Agano la Kale linasema: "Ataoga mwili wote katika maji, kisha atavaa mavazi matakatifu. Ataingia mahali hapo akiwa amevaa mavazi matakatifu: joho la kitani baada ya nguo ya ndani ya suruali ya kitani na akiwa amevaa kanzu ya kitani na kujifunga mkanda wa kitani" (Walawi 16: 4).
Kuhusu kilemba ni utabiri wa mwisho uliotolewa na Biblia. Utabiri huu unamtabiri Mtume Muhammad (Rehma na amani zimfikie yeye). Kifungu hicho kina maelezo yafuatayo: "Kisha, nikaona mbingu zimefunguliwa; na huko alikuwako farasi mmoja mweupe, na mpandafarasi wake aliitwa "Mwaminifu" na "Kweli". Huyo huhukumu na kupigana kwa ajili ya haki. Macho yake ni kama mwali wa moto, na alikuwa amevaa taji nyingi kichwani" (Ufunuo 19: 11-12). Mwaminifu na mkweli ni sifa za Mtume Muhammad (Rehma na amani zimfikie yeye) alizokuwa akijulikana nazo tangu hajapatiwa unabii.
Haya ni mambo ambayo hayafanywi na Wakristo japokuwa mengine yanafanywa na wakuu na watumishi wa Kanisa. Ukitazama leo watawa wa kike wa Kikatoliki wanajitanda kichwa na kuvaa mara nyengine nguo ndefu, kwa nini jambo hili zuri hawaambiwi wafuasi nao wakafuata? Ukiangalia mapadre wa madhehebu tofauti za Wakristo wanavaa kofia na nguo ndefu inayofanana na kanzu na joho japokuwa wao wanazidisha kwa kuchora misalaba na vitu vyengine. B
Ndugu yetu katika utu na ubinadamu tunakukaribisha kwa moyo mkunjufu kurudi katika asili yako, nako ni kunyenyekea kwa Mola Wako, aliyekuumba na kukupatia kila unachokihitajia katika hii dunia. Usimtoe shukurani kwa kutomuabudu wala kumshukuru.
Mungu Anajua zaidi.
Enyi mlio amini! Msizifuate nyayo za Shet'ani. Na atakaye fuata nyayo za Shet'ani basi yeye huamrisha machafu na maovu. Na lau kuwa si fadhila ya Mwenyezi Mungu na rehema yake juu yenu, asingeli takasika miongoni mwenu kabisa hata mmoja. Lakini Mwenyezi Mungu humtakasa amtakaye, na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua (24:21).
MWISHO