DHULMA KWA UISLAMU NA WAISLAMU
  • Kichwa: DHULMA KWA UISLAMU NA WAISLAMU
  • mwandishi: SALIM SAID AL-RAAJIHIY
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 4:35:3 3-11-1403

DHULMA KWA UISLAMU NA WAISLAMU

UTANGULIZI

Nina mshukuru Muumba Mkamilifu kwa kunipa nguvu za kuweza kuleta picha maalumu iwezayo kutoa ufafanuzi juu ya dhulma mbali mbali zinazofanyika katika ulimwengu huu, na nina mshukuru tena kwa mara ya pili kwa kutuletea Mjumbe wake (s.a.w.w) aliyeweza kuingarisha dunia hii kwa nuru ya elimu itokayo kwa Muumba wake. Katika makala hii nitajaribu kuizungumzia hali halisi ya matokeo yanayotokea katika dunia hii, huku wengi wakidhania kuwa ni matokeo ya kawaida tu. Na wengi wetu huwa tunayaangalia matokeo mbali mbali ya ulimwengu huu kuwa ni yenye kutiririka kwa kupitia sindikizo lake wenyewe, na si wengi wanao zitafuta sababu matokeo haya.

Nia hasa ya kuandika makala hii, ilikuwa ni kumzungumzia mwanamke mashuhuri wa Kiislamu aliye uliwa huko Ujerumani kwa sababu ya kuvaa hijabu. Lakini niliona kuwa kuna umuhimu kwanza kutoa ufafanuzi maalumu, juu ya mambo mbali mbali yanayotokea katika ulimwengu wetu huu.

Ulimwengu leo umeyafikia mapevuko ya ufisadi wa aina mbali mbali, huku kila mmoja akidhania kuwa yeye ni mwenye kuujenga ulimwengu kwa matendo yake. Hakuna mtu katika ulumwengu huu anaye kubali kuwa yeye ni muovo, na kila mmoja hujitetea kwa kutumia njia tofauti ili aonekana kuwa yeye ni mjenga nchi.

Kwa muda mrefu mno ulimwengu umekuwa ukishuhudia madai ya uhuru kutoka nchi za Kimagharibi, na kila mmoja wetu anaposikia sifa za nchi za Kimagharibi, hufikiria kuwa Umagharibi ndio Uwanaadamu.

Uhuru ni madai ya kila mmoja anayetaka kuleta mabadiliko katika jamii fulani, lakini ukweli hubakia na nembo yake asili isiyo weza kubadilika. Umagharibi umejaribu kuzitangatia uhuru wa jamii zake kwa matakwa ya kuzitawala jamii hizo kwa urahisi zaidi, lakini kila mmoja wetu anafahamu vyema kuwa hakuna uhuru usio kuwa na mipaka maalumu. Nembo ya haki na uhuru ni nembo isiyo kubali kugeuzika, haidhiuru wamo wanajamii wanaoweza kudanganyika, lakini kudangantika kwao hakuto dumu maishani mwao, na bila shaka iko siku ukweli utawadhihirikia.

Nchi za Kimagharibi zimejaribu kuutangazia ulimwengu kuwa: wao ni wenye uhuru wa kila aina ndani ya nchi zao, moja kati ya uhuru unaodaiwa kuwepo katika nchi hizo, ni uhuru wa mavazi. Kila mmoja akiwa ndani ya nchi za Kimagharibi huzingatiwa kuwa yeye ni mwenye uhuru wa kuvaa vazi alitakalo, na hii ndiyo siasa ya Kimagharibi ilivyokuwa mwanzo. Msingi huu wa mtu kuwa na uhuru wa kila aina usio na mipaka maalumu, ndiyo madai ya Wamagharibi duniani. Sera hizi zimekuwa zikitangazwa na nchi hizo kwa ajili ya ulimwengu mzima, jambo ambalo wengi miongoni mwetu walilifikiria kuwa ni ukweli na ni haki ya kila mwananchi anayeishi ndani ya jamii fulani.

Leo dunia imeandamwa na teknolojia ya utandawazi wa hali ya juu kabisa usioweza kuzuilika, jambo ambalo limekuwa likihujumu hali mbali mbali za kijamii, kimaendeleo na kiuchumi. Wamagharibi walikuwa wana malengu makubwa katika kuleta utandawazi huu, lakini hawakufikiria kuwa utandawazi huu unaweza kutumiwa na Waislamu katika kuleta maendeleo mbali mbali ya dini yao, kwani bado wao waliwafikiria Waislamu kuwa ni wenye fikra za Kiwahabi zinazo haramisha kila kitu kilicho kuwa hakikuwepo katika zama za Mtume (s.a.w.w). Leo hali imewabadilikia kwani Waislamu wamekuwa wakizitumia teknolojia za kileo katika kuusambaza Uislamu duniani kote, na hata Mawahabi leo wamebadilika na sio tena wale Mawahabi wa jana na juzi. Jambo hili limeweza kuwatia khofu sana watu wa Magharibi na hasa viongozi wa nchi za Kimagharibi. Leo viongozi hawa wameamua kutumia kila hila, kuweza kulizuwia kurudumu la Uislamu linaloendelea kwa nguvu ndani ya nchi za Kimagharibi.

SILAHA YA KUUZUIA UISLAMU

Wamagharibi baada ya kuliona wimbi la Uislamu liliozivamia nchi zao, uliamua kuchukuwa juhudi za kila namna ili kuwafahamisha wana jamii wao kuwa, Uislamu ni ugaidi na ni sumu katika nchi zao. Haidhuru wengi miongoni mwa wananchi wa nchi hizo wameweza kujengeka na imani hiyo isemayo kuwa Uislamu ni ugaidi, huku fikra hizo zikisadiwa katika kujengeka kwake na yale matendo ya baadhi ya watu wanaojiita kuwa ni Waislamu.

Fikra za kuufikiria Uislamu kuwa ni ugaidi zimepata nguvu kwa kupitia Waislamu bandia wanao jaribu kufanya mauwaji ya watu wasio kuwa na hatia, jambo ambalo lilizisaidia nchi za Kimagharibi kupata mdomo wa kuutukana Uislamu pamoja na Waslamu wenyewe. Kuutangaza Uislamu kuwa ni dini ya mauwaji, kulitumika kuwa ni kama kengele ya hatari iliyosikika ulimwengu mzima. Jambo ambalo liliwafanya Waislamu waonekane kuwa ni viumbe waovu wasiostahiki kuisha ndani ya dunia hii.

Baada ya juhudi kubwa za Waislamu wa makundi mbali mbali kuweza kutowa picha halisi ya Uislamu duniani, hivi sasa joto la roho za watu ndani ya nchi mbali mbali limepunguka kwa kiwango kikubwa kabisa, na hilo ndilo lililo wafahaisha Wamagharibi kuwa Uislamu ni dini ya amani, na siyo kila Muislamu anaweza kuyatetea matendo yake ya haramu kwa kuusingizia Uislamu. Jambo hili limeusadia sana Uislamu kwa mara nyengine tena kuenea huko barani Ulaya. Huku jambo hilo likiwakasirisha sana viongozi wa nchi hizo, na kuwafanya wachukuwe juhudi nyengine mpya za kuuzuia Uislamu.

HIJABU

Kila mmoja wetu Muislamu na asiye kuwa Muislamu, anafahamu vya kutosha umuhimu wa hijabu kwa mwanamke wa Kiislamu, kiasi ya kwamba hakuna mtu katika ulimwengu huu anayeweza kumtuhumu Muislamu wa kike kwa ajili ya hijabu yake, kwani hijabu inatambulika kuwa ni vazi maalumu la kumstiri mwanamke, na sio vazi la kuuficha ouvu wa ndani ya vazi hilo, kama ifanavyo fanywa na baadhi ya Waislamu waovu wasiokuwa na wivu wa dini yao.

Tukizingatia uhuru wa mavazi ulio kuwapo ndani ya nchi mbali mbali, tutakutia kuwa kila mmoja wetu ni mwenye uhuru wa kuvaa kwa mujibu wa utamaduni aliyo nao au kwa mijibu wa sheria za dini anayo ifuata. Na hiyo huwa ni haki ya kila mwanachi, na kwa upande mwengine tunafahamu tosha kuwa: uhuru Umagharibi una maana ya kumpa kila mtu uhuru wa kula, kuabudu, pamoja na kuvaa kile anachotaka kuvaa bila ya kubughudhiwa na mtu yeyote yule, na hiyo ndiyo imani ya kila mmoja wetu.

Hali ya jana siyo hali ya leo ndani ya nchi mbali mbali, kwani leo baada ya viongozi wa Kimagharibi kuyaona maendeleo ya Kiislamu yakisonga mbele ndani ya nchi zao, waeamua kuyapindua mabakuli ya sheria za uhuru. Jana kila mmoja alipewa uhuru wa kuvaa akitakacho lakini leo uhuru huu umesha futwa, kwani Muislamu yeyote wa kike anaye ishi Umagharibini, huyo huwa hana haki ya kuvaa hijabu. Jana wao walikuwa wakitutuhumu kumyanyasa mwanamke, jee leo wao wanafanya nini?

Usemi wa Wamagharibi kuhusiana na suala la hijabu ni kwamba: wanadai kuwa wao hawataki kumuona mwanamke aliye dhulumiwa ndani ya jamii ya Kimagharibi. Usemi huu tunaweza kuufasiri katika sehemu mbili:
1- Ima dhulma juu ya mwanamke inatokana na imani ya dini yake.
2- Ima dhula hiyo inatokana na wana jamii wa jamii fulani anayo ishi ndani yake.
Iwapo tutaamini kuwa dini ndiyo inayomdhulumu mwanamke wa Kiislamu, hapo basi itatubidi tutowe dalili zitakazo onyesha kuwa: Uislamu unamtukuza Mwanamke kuliko dini nyengine zote zilizomo ndani ya ulimwengu huu. Na kwa upande mwengine Usilamu haukumlazimisha mtu kukubaliana na dini hiyo, na iwapo mtu ataukataa Uislamu, basi hatolazimika kuvaa hijabu.

Hakuna jamii inayomlazimisha mwanamke kuvaa hijabu, na kama suala hilo litatokea katika jamii fulani, hapo basi mwanamke atakuwa na uhuru wa kumshtaki aliye mlazimisha kufanya jambo hilo asilo kubaliana nalo. Lakini wanawake wanaonekana kuvaa hijabu ndani ya jamii mbali mbali za Kiislamu, huwa hawana madai ya kulazimishwa kufanya hivyo, bali hilo linatokana na utiifu wao wenyewe juu ya dini yao waliyo ikubali kwa mioyo yao na kwa hiyari zao, na si kwa kulazimishwa na mtu yeyote. Hata hivyo kinacho onekana katika usemi wa Kimagharibi kuhusiana na hijabu, huwa kinawahusu wanawake wa Kiislamu tu na wala hawajawahi kuwadadisi Masister (Watawa) wa dini ya Kikristo, hali ya kwamba Watawa huwa wanadhulumiwa zaidi kama kutakuwa na madai ya kudhulumiwa kwa mwanamke, kwani wao si tu ni wenye kuvaa hijabu, bali ni wenye kuzuiliwa kufanya tendo la ndoa, hali ya kuwa tendo hilo ni uhuru na ni haki ya kila mwanamke, hasa hasa ukizingatia kuwa tendo la ndoa lina fuatana na hali halisi ya kimaumbile yalivyo.

Wakiristo basi wasilishangirie suala la kuwataka wanawake Wakiislamu kuzivua hijabu zao, kwani haya ni madai yasiyo kuwa na msingi wowote unaokubaliana na akili za wenye akili timamu, na suala hili haliwagusi tu Waislamu bali linamgusa kila mwanamke asiye penda kuufanya mwili wake kuwa ni T.V ya kutangazia matangazo ya biashara ya sexi kwa wanajamii wa ulimwengu huu. Dhulma na ubaguzi wa kidini ambao unadaiwa kuwepo ndani ya dini ya Kiislamu, ni tuhuma tu. Mtu yeyote yule anaye taka kuufahamu udini au ubaguzi wa rangi, basi na aelekee katika nchi za Kimagharibi, kwani huko ataweza kuufahamu vizuri ukweli wa maneno hayo.

ELIMU NI HAKI YA WOTE

Ni usemi wa kila mpenda haki kuwa: alimu ni haki ya kila Mwanaadamu. Iwapo wana jamii wa jamii fulani watakuwa na elimu, hapo basi jamii hiyo itaweza kupata maendeleo kwa haraka zaidi kuliko jamii nyengine. Kuwafanya wana jamii wa jamii zetu kuwa na elimu kunaweza vile vile kumsaidia kiongozi wa jamii hiyo kufahamika malengo yake kwa haraka zaidi. Waislamu wa kike wamekuwa wakibughudhiwa katika nchi mbali mbali kwa kuwa tu wao ni wenye kuvaa hijabu, leo hii kuna watoto chungu nzima walioshindwa kuendelea na masomo yao katika nchi ya Ufaransa na Ubelgiji, kwa kuwa tu wao ni wenye kuvaa hijabu. Ufaransa imeweka sheria ya kuwafukuza watoto wote wa kike wanaovaa hijabu mashuleni mwao, jambo ambalo limewasababishia watoto hao kukosa neema ya elimu, neema ambayo imetangazwa kuwa ni haki ya kila Mwanaadamu bila ya kujali tofauti zetu za rangi, dini, na tamaduni tulizo nazo.

HARAKATI ZA UMALAYA DUNIANI

Vuguvugu la kuwanyanyasa watoto wakike kwa kutokana na mavazi yao, limeweza kusonga mbele kwa kasi katika nchi mbali mbali duniani, huku Waislamu wakiendelea kunyamaza kimya bila ya kuwa na khofu yeyote ile juu ya suala hilo. Kumtaka mtoto wa Kiislamu augeuze umalaya kuwa ndiyo biashara yake, ndiyo lengo hasa la kutunyanyasia dada zetu. Mashetani mbali mbali wa nchi zote duniani wamekua na jukumu la kuugeuza ulimwengu mzima kuwa ni danguro. Huku wakijaribu kuzalisha biashara hiyo ndani ya wizara za serikali mbali mbali duniani, hatua ambayo ingelisaidia kuwafedhehesha viongozi mbali mbali pale inapojiri kufanya hivyo.

Umalaya duniani imeanza kutumiwa na maadui mbali mbali, ukiwa ni kama silaha au ni kama tisha toto ya kuwatishia viongozi wa serikali dhaifu au serikali zinyonywazo na nchi za kibeberu. Kwa upande mwengine umalaya ulisambazwa au unasambazwa katika nchi mbali mbali kwa ajili ya kueneza maridhi, maradhi ambayo hutumika kuwa ni kama chanzo cha kiuchumi kinachoweza kutumiwa na nchi zinazozalisha madawa duniani. Harakati mbali mbali huanzishwa kwa ajili ya kusambaza maradhi duniani, jambo ambalo huwa ni kama msingi wa kibiashara katika uuzaji wa madawa, kwani iwapo watu hawatokuwa na magonjwa basi biashara ya madawa itazorota duniani humu.

Yote hayo si mambo yaliyo jificha, lakini kwa kutokana na kuwa mlo unaopatikana huwa unawahusu viongozi wakubwa duniani, hilo basi ndilo linaloufinika ukweli, na kuufanya kuwa ni usiku wa giza. Yote hayo yanayofanywa na viongozi wa Kimagharibi huwa sio kosa kwao, kwani msingi mkuu wa kisiasa unaofuatwa na viongozi hao, ni msingi wa kupigania maisha kwa ajili kubaki hai katika dunia nia hii, msingi ambao huwa hauwajali wengeni, bali huwa unawatumia wengine kuwa ni watumwa wa Kimagharibi kwa kuwanufaisha wao.

Si uongo iwapo nitasema kuwa: kuna wengi wanaogombanai madaraka kwa ajili ya matumbo yao, watu ambao huwa wako tayari kuuza utu wao kwa ajili ya matumbo yao. Hao basi hawato jali nchi wala mwana nchi katika kujikweza kimali na kiutajiri. Nao ndiyo wanaotumika kutuletea aina mbali mbali za magonjwa kwa manufaa yao. Kuna aina mbali mbali za ubadhirifu wa mali za jamii kwa manufaa ya walio kidogo, huku wana jamii wakijihisi kuwa wako huru katika kazi za kucheza ngoma na kulewa ovyo.

Na iwapo mtu atasema kweli, hapo basi ataambiwa kuwa yeye analeta udini, hali ya kuwa serikali haina dini. Serikali kuto kuwa na dini si msingi mkuuu uwezao kutegemewa kwa ajili ya kuyatetea makosa yanayotendeka katika jamii zetu. La msingi sio kuwa na dini au kuto kuwa na dini, bali la msingi kushikamana na misingi iwezayo kutuletea manufaa katika jamii zetu za Kiafrika.

KESI YA JINAI YA SHETANI ALEX

Wamagharibi hawakutosheka tu na kutukandamiza kifikra pamoja na kielimu, bali wamepiga hatua zaidi hadi kutuvua nguo hadharani. Jambo ambalo haliwezi kustahamiliwa na Mwanaadamu mwenye heshima kamili. Si wote miongoni mwa wana jamii Wakimagharibi kuwa ni washenzi, bali mna wengi ambao ni waungwana wanao uheshimu Uwanaadamu kwa usawa bila ya ubaguzi. Hivyo basi tunapokuwa tunauzungumzia uhalifu wa Kimagharibi, huwa hatumaanishi kuwa wana jamii wote wa jamii hizo kuwa ni wa aina moja, bali huwa tunakusudia hasa kuzigusa serikali zinazoziongoza jamii hizo katika utendaji wa makosa mbali mbali ya uhalifu.

Kuwatangaza Waislamu kuwa wao ni wachokozi au ni wajinga na ni magaidi, huwa kunatoa mfululizo wa mvua za matusi kutoka kwa baadhi ya wana jamii wasio ufahamu Uislamu kiukamilifu, jambo ambalo huonekana kusababisha maafa makubwa kwa Waislamu wanaoishi nchi za Ulaya. Bado donda litabakia kuwepo ndani ya nyoyo za wasio kuwa Waislamu, kwani matibabu ya aina hii ya madonda huwa ni kuufahamisha ulimwengu ukweli wa Uilsamu ulivyo.

Kumvamia mtu kwa matusi huwa ni jambo geni kwa mtu mwenye akili timamu, na kila mmoja wetu anapolisikia hilo huwa ni mwenye kushangaa. Matusi yalitoka kwa Mjerumani ajulikanaye kwa jina la Alex, hayakumtukana tu bibi Marwa al Sherbini, bali yalimalizikia kuichua roho ya bibi huyu wa Kimisri aliyekuwa akiishi nchini Ujerumani, huku mumewe akiwa ni kama mwanafunzi anayesomea masuala ya genetic engineering katika nchi hiyo.

Bibi Marwa al Sherbini alikuwa na mumewe akitembea katika bustani moja huko Ujerumani, ndipo ghafla alipovamiwa kwa matusi na mtu huyu ajulikanaye kwa jina la Alex, na mwishowe akafikia kumrukia na kumvua hijbu yake huku akimtukana na kumuita kuwa yeye ni gaidi wa Kimisri. Tendo hilo lilimkasirisha sana bibi Marwa al Sherbini, lakini ujasiri na hekima ya Uislamu ilimzuia bibi huyo kujichukulia sheria mikononi mwake, na hapo ndipo alipo amua kuenda katika vyombo vya sheria na kumshitaki Alex aliye mbughudhi kwa matusi mabli mbali, na mwishowe kumvunjia heshima yake kwa kumvua hijabu.

Kulifumbia macho sula hilo kungelileta picha ya wazi juu ya ubaguzi unaofanywa na serikali ya Kijerumani, hivyo basi Mahakama ya Kijerumani ilimuita Alexi kizimbani kwa tuhuma za kitendo chake hicho cha kigaidi, na mwishowe ikamtaka kulipa faini ya Euro 750. Alex aliamua kukata rufaa kutokana na hukumu iliyo tolewa na Mhakama hiyo, na hapo hapo mahakamani akatoa kisu na kumpiga tumboni bibi Marwa al Sherbini mara 18, bibi ambaye alikuwa ni mja mzito wa mimba ya miezi mitatu.

Tendo hilo lilichukuwa kipindi kisicho pungua muda wa dakika tatu, huku wana Mahakama na wana sheria waliokuwa wamebeba silaha wakiliangalia tokeo hilo bila ya kuchukuwa hatua yeyote ile ya kumtetea na kumuokoa bibi Marwa al Sherbini. Na hiyo ndiyo ikawa hatima ya maisha ya bibi Marwa al Sherbini pamoja na kiumbe wa miezi mitatu aliye tumboni mwake. Jee huu ndiyo uungwana wa Kimagharibi? Akili kichwani mwako.

UDHAIFU WA NCHI ZETU

Baada tu ya tokeo la mauwaji ya shahidi wa hijabu (Marwa al Sherbini) kutokea huko Ujerumani, Waislamu wanaoishi katika nchi hiyo walijihisi kuto kuwa na amani. Haidhuru unyanyasaji wa wageni ndani ya nchi kama vile Ujerumani na wafuasi wake, huwa si jambo geni. Kwani mara kwa mara masuala kama haya yamekuwa yakionekana kutokea nchini humo. Lakini linalotia huzuni ni kuziona nchi zetu zikiwapiga teke wananchi wake na kuto wajali, na ukiuliza sababu utaambiwa kuwa: "kwani nani aliyewaambia waende huko", na jambo la kiongozi kuto wajali wananchi wa nchi yake, kunatokana na kuto kuwa na hisia ya udugu baina kiongozi huyo na wanao ongozwa na kiongozi huyo.

Misri leo imeshindwa kudai haki ya mwananchi huyu aliye uliwa kikatili, na Ujerumani nayo imezuia usambazaji wa habari za mauwaji hayo nchini mwake. Ujerumani na nchi nyengine za Kimagharibi zinajaribu kuwalani Waislamu kwa tuhuma ya ukatili na ugaidi, je mauwaji ya mwanamke wa Kiislamu ndani ya Mahakama za Kimagharibi ni picha ya ujasiri wa Kimagharibi? Au kufanya hivyo ndio njia ya kuutokomeza ugaidi wa kuvaa hijabu?

Kinacho shangaza ni kwamba muuwaji wa bibi Mrwa alikuwa ni Muumini wa dini ya Kikristo, jambo ambalo linashangaza sana kwani Ukristo si wenye kupinga hijabu! Nchi za Kiislamu nazo hazikuweza kutoa sindikizo lolote lile kuhusiana na mauwaji haya, ila tu zimelinukuu suala hilo katika picha ya mahuzuniko yasiyokuwa na faida yeyote ile katika kutoa sindikizo la kuhukumiwa mtendaji wa tendo hilo. Khofu za viongozi wa Kiislamu katika kutolisimamia kwao suala hilo, ni kukosa sindikizo kutoka nchi za Kimagharibi, lakini yote hayo yaliomo ndani ya vichwa vya viongozi hao ni matamanio yasiyokuwa na uhakika wa kufanikiwa.

Ninasema hivyo kwa sababu ninawajuwa vizuri Wamagharibi wanavyo watumia vibaraka wao duniani, kwani wao huwatumia kwa kuwaona wao si lolote si chochote, na wala hawatokuwa na hadhi mbele yao, mpaka pale wao watakapozikana dini zao na kuwafuata Wamagharibi katika sera zao zote za kidini na kisiasa. Haidhuru Waarabu pamoja na Waislamu wengine ambao utu wao huwa ni kuyaabudu matumbo yao na tupu zao, wanafikiria kuwa Wamagharibi ndiyo ngao zao, lakini hizo ni fikra potofu, kwani Mmagharibi hatomuacha ndugu yake na kufungamana na wewe, hasa hasa pale anapofahamu kuwa wewe hutaweza kumsaidia chochote kile katika maendeleo yake, isipokuwa wewe utatoa msaada tu kwa kuwatumikia wao ukiwa ni kama punda wao, hatimae utafikia wakati watakubadilikia kama walivyo mbadilikia Saddaam Husein, pale walipo hisi kuwa kuna haja ya kumtokomeza kiumbe huyu.

Saddaam alikuwa kiungo kizuri kwa Wamagharibi katika kuleta fujo eneo la mashariki ya kati. Saddam aliweza kutumika vizuri katika kazi za kuipiga vita Iran pale ilipojitangazia serikali ya Kiislamu. Wamarekani walimdhamini yeye kwa hali na mali ili tu serikali ya Iran iweze kuporomoka kwa kupitia sindikizo la kivita kutoka Iraq.

Katika zama hizo za kivita baina ya Iraq na Iran, nchi zote za kiarabu zili iyona Iraq kuwa ni nchi shupavu ipasayo kusaidiwa katika vita hivyo. Ingawaje Waarabu si lolote si chochote katika masuala ya kivita, lakini hawakuacha kuisaidia Iraq katika vita hivyo. Poropaganda zilizotoka katika nchi za kiarabu kumsifu Saddam zilitosha kuwa ni kama silaha ya kuididimiza nchi ya Iran. Waarabu walimtetea Saddam huku wakimuona yeye kuwa ni simba wa Waarabu, lakini wao walisahau kuwa samba si mnyama aaminikaye, vita vilimalizika na ushindi ukawa ni kwa Iran. Miaka ilipita huku Waarabu wakimuona Saddam kuwa ni mtetezi wa Uwarabu ambaye amesimama kidete katika kuupiga Uwajemi (Uirani).

Roho ya ufisadi haiwezi kutulia na wala kiu ya damu kwa mnyonyaji wa damu haiwezi kukatika, haukuchukua muda mrefu kwa mara nyengine tena Saddam akaamua kuivamia Kuweit, nchi ambayo iliyashangiria mavamizi ya Saddam dhidi ya Iran, na hapo ndipo Waarabu walipoanza kuitambua picha halisi ya Saddam Hesein, na huu ndiyo ukawa mwanzo wa uwadui wa Marekani na Saddam, kwani Mmarekani alihisi kuwa Saddam ana nia ya kuihamisha rasilimali ya mafuta na kuiweka kwenye mkono wake, jambo ambalo halikumpa Mmarekani subira ya kumsaili bwana Saddam.

Irani ambayo ilionekana kuwa ni kama adui mkubwa Waarabu ndiyo iliyo chukuwa juhudi kubwa za kuvizima visima vya mafuta vya Kuweit vilivyo tiwa moto na majeshi ya Saddam. Huku kwetu Afrika watu wanamuona Saddam kuwa ni kiongozi shupavu, lakini ukweli sio huo, kwani yeye ni jahili mkubwa aliye wateketeza waumini wa dini ya Kiislamu waliokuwa wakiishi katika kijiji kijulikanacho kwa jina la Halabche kwa kutumia mabomu ya sumu. Na huu ndiyo ushupavu wa viongozi wa nchi zetu, yaani nguvu ni kwa majirani zetu na wala si kwa maadui zetu. Leo sisi tunakubali kugombanishwa wenyewe kwa wenyewe bila ya hata kuwepo sababu maalumu za msingi.

Ukizitazama nchi za Kimagharibi utazikutia kuwa hazikubali kunyanyasiwa Wananchi wao. Na ziko tayari kutumia nguvu dhidi ya mtu yeyote yule anayejaribu kuleta angalau vitisho tu juu ya familia fulani au mtu fulani wa nchi hizo, leo kama kutatokea mtu atakaye muuwa mbwa na wala sio mtu, ubwa ambaye amemilikiwa na nchi za Kimagharibi, basi mchana wa mtu huyo utabadilika kuwa ni usiku kwake, na kutachukuliwa kila juhudi za kumpandisha mahakamani mtu huyo na kumchukulia hatua kali za kisheria kwa matendo ya hayo ya kihalifu. Ndugu wasomaji huu ndio mwisho wa makala hii, Mungu akipenda tutakutana tena katika makala nyengine. Mungu akubarikini nyote kwa ujumla. Aamin.
MWISHO