SUALI KUHUSU  MAHDI (A.S)
  • Kichwa: SUALI KUHUSU MAHDI (A.S)
  • mwandishi: NDUGU ZETU WA KIISLAMU
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 7:35:32 24-8-1403

BSMILAHI AR-RAHMANI AR-RAHIIMI

SUALI KUHUSU  MAHDI (A.S)

Hivi karibuni nilisoma kitabu kimoja kinachosema kuwa Imam Hassan Askari (AS) alibaidishwa na Mutawakil al-Abbasi na kupelekwa katika mji wa Samarra. Hatimaye alifungwa katika mojawapo ya jela za mji huo na kufia humohumo. Mwandishi wa kitabu hicho alisema, baada ya kufariki dunia Imam Hassan Askari, mwanawe aliyekuwa na umri wa miaka mitano ndiye aliyechukua nafasi ya uongozi wa umma wa Kiislamu. Baada ya kupewa jukumu hilo alienda katika mojawapo ya mapango ya karibu na kwamba hakuonekana tena baada ya hapo.

Kitabu hicho kinasema kwamba, jambo hilo lilipelekea kutokea imani hii miongoni mwa Washia kwamba, mtoto huyo wa Imam Hassan Askari (AS), ndiye Imam Mahdi muahidiwa ambaye atadhihiri tena kwa lengo la kuleta uadilifu na usawa duniani baada ya kujaa dhulma na uonevu. Kitabu hicho kinasema kuwa, suala hilo ni bida'a katika Uslamu, kuendelea kudai kwamba suala hilo pia limeashiriwa katika dini za Kizartoshti na Kikristo, na kwamba, ni aina moja ya kumshirikisha Mwenyezi Mungu katika dini tukufu ya Kiislamu. Kwa hivyo, nielezeni ukweli wa jambo hili.- Abdulrahiim Musa Dungu wa Mtwara Tanzania.

Bwana Dungu Kuna nadharia na mitazamo tofauti kuhusiana na maisha ya Imam Hassan Askari na mwanawe mtukufu Imam Mahdi (AS), mitazamo ambayo huenda baadhi yao si sawa. Kuna vitabu vingi sana vya Kishia na Kisunni ambavyo vina hadithi nyingi zilizo sahihi kutoka kwa Mtume Mtukufu (SAW), ambazo zinaelezea maisha na jinsi ya kudhihiri Imam Mahdi ( Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake).

Kila Mtume alikuwa akitoa habari za kuja Mtume mwingine baada yake. Hata kama Mtume Muhammad alikuwa Mtume wa Mwisho kutumwa na Mwenyezi Mungu duniani, lakini alibashiri mambo na matukio mengi sana amabyo yangetokea baada yake kukiwemo kudhihiri kwa Imam Mahdi (AF). Alisema Imam huyo ndiye angekuwa wa mwisho kati ya Maimamu na kwamba, ndiye angekuwa wa mwisho kuuongoza Umma wa Kiislamu kama Imam.

Kwa hivyo, huo ni uhakika wa kidini na wala hauwezi kuchukuliwa kuwa ni bida'a wala ushirikiana katika dini. Imani ya kuwepo Mahdi Muahidiwa, imekuwepo tokea kudhihiri kwa Uislamu na kwa hivyo sio jambo geni lilanoweza kudaiwa kuwa ni Bida'a. Tokea abaathiwe kuwa Mtume hadi siku aliyoaga dunia, Mtume alielezea mara kwa mara jina, alama za kudhihiri Imam huyo pamoja na serikali yake ya kiadilifu duaniani.

Kwa kadiri kwamba hata watu walioishi katika zama za Mtume huyo Mtukufu walikuwa wakimtarajia. Baada ya kuaga Mtume na hadi leo bado watu wanamtarajia Imam huyo, na hata katika vipindi mbalimbali vya historia, baadhi ya watu wamekuwa wakiwadhani wengine kuwa ndio Imam huyo mtukufu.

Baadhi ya vitabu vifuatavyo vya Kisunni vimezungumzia kwa undani maisha na jinsi ya kudhihiri Imam Mahdi (AF): Mishkatul Maswabiih, Yanabiul Mawadda, Nurul Abswaar, Swahih Ibn Dawoud, al-Bayaan na kadhalika. Na katika madhehebu ya Kishia kuna vitabu kama vile Ithbaatul Hudaat, Nahjul Balagha, Khiswaalu Swaduq, Man La Yahdhuruhul Faqih, Kafi, Irshadul Qulub ambavyo vina hadithi nyingi kuhusu Maisha na jinsi ya kudhihiri Imam Mahdi (AF).

Kwa hivyo, je, kuwepo hadithi nyingi kama hizo ambazo bila shaka zinapindukia 1000, kunaweza kumpelekea mtu kutilia shaka usahihi wa hadithi hizo na kusema kuwa ni bida'a na tena kuinasibisha kwa Mashia tu? Kwa kutegemea hadithi hizo zinazopatikana katika vitabu vya madhehebu zote mbili muhimu katika Uislamu yaani Shia na Sunni, tunaashiria kwa ufupi maisha ya Maimamu Hassan Askari na Mahdi (AS).

Katika kipindi cha miaka 27 ya Maisha ya Imam Hassan Askari (AS), Imam huyo aliishi katika zama za watawala watatu wa ufalme wa ukoo Abbasi, ambao ni Mu'taz, Mahtada na Mu'tamid. Watawala wa Kiabbasi ambao waliingia madarakani kwa kupiga nara za kuwaunga mkono na kuwahami watu wa Nyumba ya Mtume (SAW) na pia kutaka kulipiza kisasi kwa ukoo wa Banu Ummaiyya, baada ya kupata madaraka hayo, walisahau kabisa nara walizokuwa wakitoa mwanzoni kabla ya kuingia madarakani, na kuanzisha siasa mbovu za kuwakandamiza pamoja na kuwadhulumu wananchi akiwemo Imam Hassan Askari (AS).

Watawala hao walikuwa wamepata habari kwamba kupitia riwaya mbalimbali za Kiislamu kwamba, Imam Hassan Askari, angepata mtoto ambaye ndiyo huyo Imam Mahdi, ambaye angedhihiri katika kipindi cha kutawaliwa ulimwengu na dhulma pamoja na utovu wa maadili, na kuujaza kwa uadilifu na usawa bila ya kutendeka dhulma yoyote. Ilisemekana kwamba Imam huyo angeridhiwa na viumbe wote wa humu duniani na mbinguni na kwamba angegawa mali zote kwa watu humu duniani kwa usawa kamili bila ya kufanya upendeleo wowote.

Kwa mujibu wa riwaya za kuaminika, Imam Mahdi alizaliwa mwaka 255 Hijiria katika nyumba ya Imam Hassan Askari huko katika mji wa Samarra nchini Iraq ya hivi sasa. Kama ulivyokuwa uzawa wa Nabii Musa, Mwenyezi Mungu pia aliufanya uzawa wa Imam Mahdi kuwa jambo la siri ambalo halikutakiwa kujulikana na kila mtu. Katika kipindi hicho Imam Hassan Askari aliwapa habari za kuzaliwa Imam Mahdi, baadhi tu ya wafuasi wake wa karibu na waaminifu, na akiwaambia baadhi ya misukosuko, matatizo na hatari kubwa ambayo ingemkabili Imam huyo katika maisha yake. Imam Askari alikuwa hai katika kipindi cha miaka mitano ya kwanza ya maisha ya Imam Mahdi (AF).

Katika kipindi hicho alikuwa akiwaanda wafuasi wake kukubali kipindi cha kwenda kwenye gheiba Imam Mahdi. Baada ya kifo cha baba yake, kwa kipindi fulani Imam Mahdi alichukua nafasi ya kuwaongoza Waislamu, lakini alilazimika kuchukua hatua za tahadhari na za kiusalama ili kujilinda kutokana na kuwa watalwa wa Kiabbasi katika kipindi hicho walikuwa wakipanga mikakati ya kutaka kumuua, kwa vile walimchukulia kuwa tishio kubwa kwa utawala wao.

Kwa hivyo kwa uwezo wake Mwenyezi Mungu, Imam huyo alitoweka machoni pa walimwengu na hivyo kuingia katika kipindi cha gheiba. Gheiba ya Imam huyo ni ya sehemu mbili, ndogo na kubwa. Gheiba ndogo ilitimia kati ya miaka ya 260 hadi 329 Hijiria. Katika kipindi hicho Imam huyo wa Zama alikuwa akionana na kukutana na baadhi tu ya wafuasi wake wachache na hivyo kuuongoza umma wa Kiislamu kwa njia hiyo.

Kipindi hicho cha gheiba ndogo kilichukua muda wa karibu miaka 70. Gheiba kubwa ambayo ilianza baada ya kupita muda huo bado inaendelea hadi sasa. Kwa hivyo gheiba ya Imam huyo ilitimia kwa amri ya Mwenyezi Mungu. Hakuna riwaya yoyote ya Kiislamu inayodai kwamba Imam huyo alitowekea pangoni huko Samarra, kama kitabu kilichotajwa na msikilizaji wetu huyu kinavyodai.

MWISHO