UTUME WA NABII MUHAMMAD (S.A.W.W)
  • Kichwa: UTUME WA NABII MUHAMMAD (S.A.W.W)
  • mwandishi: NDUGU ZETU WA KIISLAMU
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 20:0:58 24-8-1403

BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

UTUME WA NABII MUHAMMAD (S.A.W.W)

Kupewa Utume Nabii Muhammad (saw) Lilikuwa Tukio Muhimu katika Historia ya Mwanadamu
Kiongozi Mauadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran amesema kuwa kubaathiwa na kupewa utume Nabii Muhammad (saw) lilikuwa tukio muhimu katika historia ya mwanadamu na akaongeza kuwa haja kubwa zaidi ya jamii ya Kiislamu hii leo ni kutekeleza ujumbe wa kubaathiwa Mtume, kuipa umuhimu akili na mantiki, kueneza maadili mema na kuheshimu sheria na nidhamu katika jamii. Ayatullah Ali Khamenei ameyasema hayo katika hadhara kubwa ya viongozi wa mfumo wa Kiislamu na matabaka mbalimbali ya wananchi waliokwenda kuonana naye kwa mnasaba wa kuadhimisha siku ya kupewa utume na kubaathiwa Nabii Muhammad rehma na amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake na Aali zake. Amesisitiza kuwa wadhifa wa wasomi na shakhsia wakuu wa jamii ni mkubwa na wenye umuhimu zaidi katika uwanja huo.

Ayatullah Khamenei ametoa mkono wa baraka na fanaka kwa umma wa Kiislamu na taifa la Iran kwa mnasaba wa maadhimisho ya sikukuu ya kupewa utume Nabi Muhammad (saw) na akasema, sehemu muhimu zaidi ya ujumbe wa kubaathiwa mtukufu huyo ilikuwa ni kutoa malezi yanayooana na akili na kusisitiza juu ya utumiaji wa akili na kutafakari. Amesema kuwa kazi ya kwanza ya Mtume Mtukufu wa Uislamu ilikuwa ni kuimarisha utumiaji wa akili katika jamii ya Kiislamu kwani kulea na kukuza uwezo wa kutafakari na nguvu ya akili katika jamii ndiyo suluhisho la matatizo yote, wenzo wa kudhibiti nafsi na chombo kinachomtayarishia mwanadamu uwanja mzuri wa kuwa mja halisi wa Mwenyezi Mungu.

Ayatullah Khamenei ameyataja malezi ya kimaadili kuwa ni sehemu ya pili muhimu zaidi ya ujumbe wa kubaathiwa Mtume Muhammad (saw) na akasema: kueneza maadili bola katika jamii ni mithili ya upepo mwanana ambao hutayarisha uwanja wa maisha bora na kumuweka mwanadamu mbali na tamaa, ujahili, kupenda jaha, uhasama wa kibinafsi na kudhaniana vibaya. Amesisitiza kuwa, ni kwa sababu hiyo ndiyo maana katika dini ya Kiislamu, suala la kuitakasa nafsi na kuimarisha maadili bora likawekwa mbele ya kutafuta elimu.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyataja malezi na nidhamu katika utekelezaji wa sheria kuwa ni sehemu muhimu zaidi ya tatu ya ujumbe wa tukio la kubaathiwa Mtume Muhammad (saw). Amesema kuwa mtukufu huyo daima alikuwa mstari wa mbele katika kutekeleza sheria na kanuni za Kiislamu na kuongeza kuwa mambo hayo yote ni kigezo cha kuigwa na kipimo kwa ajili ya jamii ya Kiislamu na kwamba uwanja wa maisha ni medani ya kuwatahini na kuwajaribu wanadamu.

Ayatullah Khamenei amesema kuwa hadhi na utukufu wa sasa wa taifa la Iran ni matokeo ya mafanikio katika mtihani na majaribio ya kipindi cha miaka thalathini iliyopita na akasisitiza kwamba: Mwenyezi Mungu amelilipa taifa la Iran kwa kulipa mafanikio makubwa na hii leo wananchi wa Iran wanapiga hatua na kufanya harakati za kufikia malengo aali ya Uislamu.

Amesema kuwa nara na kaulimbiu ya madola makubwa ya kibeberu ya kukabiliana na Jamhuri ya Kiislamu na kuutambua utawala wa Kiislamu hapa nchini kuwa ndio kizuizi cha kufikia malengo yao maovu husussan katika eneo la Mashariki ya Kati, ni dalili ya adhama na utukufu wa taifa, utawala na serikali ya Kiislamu ya Iran.

Ayatullah Khamenei amesema kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya harakati ya taifa la Iran katika kutekeleza sheria za dini. Amekumbusha nafasi ya utendaji wa shakhsia wakuu wa jamii na viongozi wa nyanja mbalimbali ambao ni vigezo vya wananchi na akasema kuwa katika kipindi cha miaka thalathini iliyopita taifa la Iran limeonyesha kwamba ni taifa aminifu na lenye kujitolea na sifa hiyo imeonekana wazi zaidi katika matukio ya baada ya uchaguzi wa Rais ulioanyika hivi karibuni hapa nchini.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa kuna dhuku na mielekeo mbalimbali ya maisha ya kijamii kati ya wananchi wa Iran na kila mwelekeo unabainisha mtazamo wake; lakini pale taifa linapohisi kuwepo uadui dhidi ya mfumo wa Kiislamu na kwamba kuna mtu unayetaka kutoa pigo dhidi ya mfumo huo na utawala wake hujitenga mbali naye, hata kama atatoa nara na kaulimbiu zinazoaminiwa na taila la Iran.

Amesema kuwa matukio ya hivi karibuni ni tajiriba na somo jingine muhimu kwa taifa la Iran na akaongeza kuwa matukio hayo yameambatana na tajiriba na somo kwamba, hatupasi kughafilika na njama za maadui hata wakati harakati kubwa inapokuwa ikifanyika kwa utulivu kamili.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, wakati watu wote walikuwa wamekiri kwamba uchaguzi wa hivi karibuni wa Rais uliowashirikisha watu milioni arubaini ni hadhi na fahari isiyokuwa na kifani tangu mwanzoni mwa Mapinduzi ya Kiislamu na ishara ya uwezo wa utawala wa Kiislamu wa kuwaleta wananchi katika medani mbalimbali licha ya kupita miaka thalathini baada ya mapinduzi , wakati huo ilitambulika kwamba katika mazingira hayo pia hatupasi kughafilika na mitego na njama za adui za kutaka kuangamiza taifa.

Ayatullah Ali Khamenei ameashiria pia madai ya maadui wa taifa la Iran kwamba hawaingilii masuala ya ndani ya nchi hii na akasema: Madai hayo yamefichua ukosefu wa haya wa maadui hao baada ya kuonekana wazi uingiliaji wao katika masuala ya ndani ya Iran, hususan vyombo vyao vya habari.

Amekumbusha tahadhari aliyotoa miaka kadhaa iliyopita kuhusu mipango kabambe ya vyombo vya propaganda na ujasusi vya madola ya kibeberu kwa ajili ya kukabiliana na kujitawala kwa mataifa mbalimbali na kuzuia harakati ya ustawi na kujitawala kwao na akasema: Maadui wa taifa la Iran wanatumia vyombo vyao vya habari kutoa mafunzo kwa makundi yaliyoghafilika na ya majahili watenda ghasia kuhusu jinsi ya kuvuruga usalama, kufanya uharibifu na kuzusha mapigano, na wakati huo huo wanadai kuwa hawaingilii masuala ya ndani ya Iran.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza juu ya udharura wa kutofautisha kati ya watu wanaofanya ghasia na wananchi wa kawaida na akasema kuwa vyombo vya madola ya kibeberu vinawataja watu hao wanaofanya ghasia na machafuko kuwa ni wananchi kwa lengo la kuwaunga mkono wafanyaghasia hao ilhali wananchi ni mamilioni ya wale ambao wanapowaona wafanya ghasia hao hujitenga nao na kuwatazama kwa jicho la hasira na kuchukizwa na matendo yao.

Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa mtu yeyeto yule wa ngazi na cheo chochote anayetaka kuielekeleza jamii katika ghasia na ukosefu wa amani hutambuliwa na taifa la Iran kuwa ni mtu muovu. Amesisitiza kuwa malengo makuu ya Taifa la Iran yatafikiwa chini ya kivuli cha amani na usamala na akasema kuwa kuvuruga amani ni kosa kubwa mno. Vilevile amewahutubu watu wenye nafasi za juu na hadhi katika jamii akiwataka kuwa macho kwani matamshi, uchambuzi au hatua yoyote inayovuruga amani ya jamii ya watu hao ni harakati inayokwenda tofauti na njia ya taifa la Iran.

Ayatullah Ali Khamenei amewataka wananchi wote kuchunga maneno, misimamo na hata kimya chao kwani kunyamazia kimya masuala yanayopaswa kusemwa kuna maana ya kutotekeleza wajibu, na kusema yasiyopaswa kusemwa ni kutenda kinyume cha wajibu.

Amewataka watu wa tabaka hilo kuwa macho kwani wako kwenye mtihani mkubwa na kwamba kufeli katika mtihani huo hakuna maana ya kushindwa pekee, bali pia hupelekea kuporoka kwao.

Ayatullah Khamenei amesema kuwa njia pekee ya kujiokoa na hatima hiyo ni kutilia maanani akili na mantiki na akaongeza kwamba kutia maanani akili na mantiki hakuna maana ya michezo ya kisiasa kwa sababu michezo hiyo inapingana na akili na mantiki, na wale wanaodhani kwamba michezo ya hiyo ya kisiasa ni hatua ya busara, wanakosea.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa njia sahihi ya kimantiki ni njia inayotayarisha uwanja wa kumwabudu Mwenyezi Mungu na kigezo chake ni kutazama kwamba je, matamshi na misimamo yetu ni kwa ajili ya ikhlasi na kumridhisha Mwenyezi Mungu au ni kwa ajili ya kuwaridhisha baadhi ya watu, na kwa msingi huo hatupaswi kujidanganya.

Ayatullah Ali Khamenei amesisitiza juu ya udharura wa kutaamali tukio la kubaathiwa na kupewa utume Nabii Muhammad (saw)na akasema: Tukio la kupewa utume Nabii Muhammad amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake na Aali zake ni tukio lenye umuhimu mkubwa mno kwa mwanadamu kwa sababu harakati iliyofanywa na mtukufu huyo katika kipindi cha miaka kumi ya serikali yake na mabadiliko makubwa aliyofanya katika historia ya mwanadamu haiwezi kulinganishwa na harakati au hatua yoyote ile.

Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu, Rais Mahmoud Ahmadinejad wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alitoa hotuba fupi akitoa mkono wa baraka kwa mnasaba wa maadhimisho ya siku ya kupewa utume Nabii Muhammad (saw). Ameashiria nafasi ya tukio hilo kubwa la kihistoria katika kuwaondoa wanadamu katika giza la ujinga na dhulma na kuwaelekeza katika nuru ya uongofu na akasema kuwa: Mtume wa Uislamu daima alikuwa mstari wa mbele katika kutekeleza sheria za dini na kwamba matatizo ya sasa ya mwanadamu yanatokana na kujitenga na njia ya Mtume Muhammad (saw).

Rais Ahmadinejad ameashiria subira, ukakamavu na juhudi kubwa za taifa la Iran katika kipindi cha miaka thalathini iliyopita na akasema kuwa jamii ya Kiislamu ya Iran inajifaharisha kwa kufuata njia yenye nuru na mwanga ya Mtume Muhammad (saw) na taifa hili, kwa kufuata sira ya mtukufu huyo, halitawaruhusu maadui kukanyaga haki za binadamu.

Dakta Ahmadinejad ameshiria uchaguzi wa Rais uliofanyika mapema mwezi uliopita hapa nchini na akasema kuwa uchaguzi huo uliokuwa huru na usio na kifani ni bishara ya mustakbali wenye mwanga kwa taifa la Iran na wanadamu wote kwa ujumla.

MWISHO