BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI
KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
SIFA ZA WATIIFU NO.3
WAFUASI WAKWELI WA MITUME
* Ni alama gani zinazoonesha ukweli wa wafuasi wa Mitume?.
* Kuna athari gani katika kuwakubali na kuwafuata Mitume?.
Katika makala iliyopita tulielezea kuhusu wafuasi wa kweli wa Mitume ya Mwenyeezi Mungu (s.w) na sifa walizonazo watiifu hao. katika makala hii tutaendelea kuelezea sifa nyengine walizonazo watu hao.
2-4. Kupata salama na Kunufaika na malipo ya Allah (s.w).
Wanaadamu wataokoka na kupata salama ikiwa tu, watamtii Mwenyeezi Mungu na Mitume yake. Kama tunavyosoma ndani ya Qur-ani:-
يُصْلِحْ لَكُمْ اَعْمَالَكُمْ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ وَمَن يُطِعْ اللهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ فَازَ فَوْزاً عَظِيماً[1]
Apate kukutengenezeeni vitendo vyenu na akusameheni madhambi yenu. Na anaye mt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, bila ya shaka amefanikiwa mafanikio makubwa.
Vile vile mwanaadamu, atapata malipo makubwa kwa kumtii Mwenyeezi Mungu na Mitume yake. Kama anavyosema Allah (s.w):-
لَيْسَ عَلـٰي الاَعْمَي حَرَجٌ وَلاَ عَلـٰي الاَعْرَجِ حَرَجٌ وَلاَ عَلـٰي الْمَرِيضِ حَرَجٌ وَمَن يُطِعِ اللهَ وَرَسُولَهُ يُدْخِلْهُ جَنَّاتٍ تَجْرِى مِن تَحْتِهَا الاَنْهَارُ وَمَن يَتَوَلَّ يُعَذِّبْهُ عَذَاباً اَلِيماً[2]
Kipofu hana lawama, wala kiguru hana lawama, wala mgonjwa hana lawama. Na mwenye kumt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, atamuingiza katika Mabustani yapitayo mito kati yake. Na atakaye geuka upande atamuadhibu kwa adhabu chungu.
* Haya ndiyo hayo yanayosemwa kila siku kuwa wanaokubali kuongoka ndio anaowaongoa Mwenyeezi Mungu. Ni jambo lililowazi kabisa kuwa, kuingia Peponi na kuwa mbali na moto, ni alama bora inayoonesha kuwa mwanaadamu ameokolewa, ameongoka, na yuko katika salama. Kama anavyosema Allah (s.w):-
كُلُّ نَفْسٍ ذَآئِقَةُ الْمَوْتِ وَإِنَّمَا تُوَفَّوْنَ اُجُورَكُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ فَمَن زُحْزِحَ عَنِ النَّارِ وَاُدْخِلَ الْجَنَّةَ فَقَدْ فَازَ وَما الْحَيَاةُ الدُّنْيَا إِلاَّ مَتَاعُ الْغُرُورِ[3]
Kila nafsi itaonja mauti. Na bila ya shaka mtapewa ujira wenu kaamili Siku ya Kiyama. Na atakaye epushwa na Moto na akatiwa Peponi basi huyo amefuzu. Na maisha ya dunia si kitu ila ni starehe ya udanganyifu.
*Wanahimizwa watu wayachume ya kuwatia Peponi, na wayaepuke ya kuwatia Motoni, kwani moto ni natija ya amali zao, na Pepo vile vile.
Maelezo kwa ufupi kuhusiana na makala zilizopita
*Wafuasi wa kweli wa Mitume, ni wenye mapenzi na hupendana baina yao, na hukabiliana na kupigana na maadui wa Mitume na washirikina.
*Kuna sifa mbali mbali zinazoonesha utiifu kwa Mitume, miongoni mwa sifa hizo ni: Kuisadiqi Mitume yote, kuwa na mapenzi na wale wanaowapenda Mitume, na kuwa na uadui na wale maadui wa Mitume, kukubali nadharia wanazotoa Mitume, - kwani kila wanalolisema ni kwa idhini yake Allah (s.w) - Kumtasbihi Mwenyeezi Mungu, na kuwa thabiti kwa kufanya jihadi katika njia za Mitume, na kuihifadhi dini ya Allah (s.w).
*Miongoni mwa athari zinazopatikana kwa wale wanaomtii Mwenyeezi Mungu na Mtume wake ni:- Kuondoa ikhtilafu za kielimu na kimatendo, kunufaika na rehema na usaidizi wake Allah (s.w), na kuwa katika amani.
Masuala.
1. Wafuasi wa Mitume wanaweza kufahamika vipi?.
2. Kwa nini Waumini ni lazima wawe na imani na vitabu na Mitume yote?.
3. Qur-ani kariym inausifu vipi uhusiano uliopo baina ya Waumini na makafiri?.
4. sala na kumsabihi Mwenyeezi Mungu kunaleta athari gani kwa Waumini?.
5.Waumini wa kweli hukabiliana vipi na desturi za Mitume?.
6. qur-ani kariym inasema nini kuhusiana na umadhubuti wa Waumini?.
7. Elezea athari na faida zinazopatikana kwa kumtii Mwenyeezi Mungu na Mtume wake.
MWISHO
[1] Surat Al-Ahzaab Aya ya 71
[2] Surat Al-fat-h Aya ya 17
[3] Surat Al-Imrani Aya ya 185