DU’A YA MWEZI WA RAMADHANI (SEHEMU YA 4)
اللّهُمَّ اكْسُ كُلَّ عُرْيَانٍ
Ewe Mola Mvishe Kila Aliye Uchi
LENGO LA KUUMBWA MWANADAMU
Msiba mkubwa wa maisha ya mwanadamu unatokana na kutofahamu madhumuni ya kuumbwa mwanadamu. Maadamu mwanadamu atakuwa hajui ‘lengo la maisha’ atakuwa daima kwenye matatizo. Kanuni hii inatumika kwa matajiri pia. Muulize kila tajiri iwapo pesa zake zinamfanya awe na furaha daima, bila shaka jawabu litakuwa ni la. Qur’an Tukufu na pia Ahlulbayt (a.s.) wametufahamisha kwamba makusudio ya lengo la kuumbwa kwa mwanadamu ni ili apate ujirani na ukaribu wa Mwenyezi Mungu. Na njia ya kumuongoza mtu kutambua hamu hii si nyingine bali ni ibada, kama ilivyoelezwa kwenya aya zifuatazo:-
Katika sura ya 51 aya ya 56. Mwenyezi Mungu anasema ya kwamba:
وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنْسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ
“Na sikuwaumba majini na wanaadamu ila waniabudu”
Hapa lengo linaonyesha ya kuwa ni kumuabudu Mwenyezi Mungu. Lakini jee hili ndilo lengo la kipekee la kuumbwa kwa mwanadamu? Ili tuweze kulijibu swali hili, tunawajibika kuiangalia aya ya 99 katika sura ya 15, ya Qur’an, isemayo:
وَاعْبُدْ رَبَّكَ حَتَّىٰ يَأْتِيَكَ الْيَقِينُ
“Na muabudu Mola wako mpaka ikufikie hiyo yakini”
Kwa hivyo kitu cha mwisho ni kumjua Mwenyezi Mungu (s.w.t.) na kila anapojikurubisha mtu kwa Mola wake ndivyo elimu kumhusu Muumba wake inavyoongezeka.
Madokezo mazuri yamefanywa vile vile katika beti za du’a zifuatazo kuhusu hatima ya mwanadamu:
1. Imam Ali (a.s.) katika dua yake maarufu ya Kumeil analia:
يَا غَايَةَ آمَاِل العَارِفِين
“Ewe mwisho wa matarajio ya wacha Mungu”
2. Na katika dua ya Arafa ya Seyyid Shuhada (Imam Husain (a.s.) anaomba:
إِلهِيْ أُطْلُبْنِيْ بِرَحْمَتِكَ حَتّى أَصِلَ إِلَيْكَ
“Mungu wangu nitafute kwa Rehema yako (nishushie rehema yako) mpaka nifikie kwako (kwenye ukuruba wako)”
Ibada ya Mwenyezi Mungu ndio ambayo humuinua mwanadamu juu kiasi cha kumwezesha kumuona Mwenyezi Mungu (s.w.t.) lakini kwa kiwango chake kama ilivyo elezewa kwenye baadhi ya hadithi za Ahlul bayt (a.s.).
Baada ya kujua hayo, lazima tujue ya kwamba kwa kuwa mwanadamu anaishi kwenye ulimwengu wa maada, na analo umbile ambalo hujisalimisha kwenye kanuni za maada, ana haja na mahitaji mbali mbali vilivyo ambayo yangemwezesha kujikimu kimaisha na kufikia lengo lake katika maisha. Mifano ya mahitaji haya ya msingi ambayo vile vile tunaweza kuyaita kama “njia za maisha,” ni chakula, maji nguo, nyumba n.k..
NJIA NA LENGO
Wengi wa wale wasiojua lengo la maisha ya mwanadamu hujishughulisha na njia na kusahau lengo. Na wanapo angalia fahari ya aina mbali mbali ya vitu vya kidunia vinavyozalishwa na nchi ziitwazo, zilizo endelea, huchukulia kuwa ndio ‘maendaleo ya kibinadamu’, na hata hupatwa na shaka kuhusu usahihi wa Uislamu.
Maendeleo ya kisayansi na teknolojia sio kitu kinacho chukiza kwenye Uislamu hata kidogo, bali kinatiliwa nguvu. Hata hivyo bado inakuja chini ya mwamvuli wa ‘njia za lengo’ hivyo mtu asije akakosea kwa kuyachukulia kuwa ndio ‘kipimo cha maendeleo ya mwanadamu’. Na inafaa mtu ajiulize kama kweli ‘vitu vyakimaada’ vinakidhi kama ‘njia’ katika njia ya kumfikisha mtu kwa Allah au la. kwa mfano VCR na Internet zote ni njia zinazo saidia katika mawasiliano. Lakini kama vitamzuia mwanadamu kufikia njia ya furaha ya milele zitakuwa na faida gani ya kutumiwa kama ‘njia’ ya kufikia lengo?
Wateteaji wa maendeleo siku zote hutoa bidhaa za aina mbili:
1. Zenye hali na uwezekano wa kubadilika
2. Zisizo kuwa na hali ya kubadilika
Bidhaa za aina ya kwanza zinamruhusu mwanadamu kutafakari na kujitahidi kwenye njia inayoelekea kwenye ukamilifu kabla na baada ya kuinunua. Kwa mfano, mtu anapo nunua televisheni (T.V) ana uwezo wa kuamua kuitumia au kutoitumia katika kuviangalia vipindi ambavyo vitamjenga kiakili na kiroho peke yake lakini bidhaa ya aina ya pili baada ya kuinunua chaguo hili halipo. Kwa mfano lau mtu atanunua filamu yenye mambo machafu kwa kufuata matamanio ya nafsi na baadaye akataka kuibadilisha kwa matumizi mazuri hatoweza kufanya hivyo kwa kuwa hatoweza kuibadilisha filamu hiyo ili imjenge kiakili, anachoweza kufanya ni kuifuta filamu yenyewe yote na kunakili kile kinachoweza kumjenga kiroho. Hali kadhalika hali ni hivyo hivyo ilivyo kuhusiana na vitu vya kidunia ambavyo vinahusika moja kwa moja na maendeleo ya mwanadamu na kujikimu kama vile chakula, maji na mavazi. Aina nyingi za vyakula na nguo za aina mbalimbali zinakatazwa kwenye Uislamu kwa hivyo haviwezi kuitwa kama ‘njia’ kwa ajili ya lengo la mwanadamu.
Kwa hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kujua tofauti baina ya ‘lengo’ na ‘njia’. Kwa bahati mbaya wengi wetu tumejenga maisha yetu kujitahidi tu kwa ajili ya wingi wa ‘njia’ na tunasau ‘lengo’. Tutaujua ukweli huu tutakapoingia makaburini mwetu. Qur’an [Sura ya 102:1-2] inasema:
أَلْهَاكُمُ التَّكَاثُرُ. حَتَّىٰ زُرْتُمُ الْمَقَابِرَ .
“Kumekughafilisheni kutafuta wingi wa mambo ya kidunia mpaka mumekwenda makaburini”
LENGO LA MAVAZI
‘Nguo’ ni moja katika mahitaji ya kimsingi katika maisha ya mwanadamu, na kwa kweli ni neema ya Mwenyezi Mungu kwa mwanadamu. Na kujua sababu iliyoko kwenye mavazi kutafungulia milango mbali mbali ya kufahamu na kutuwezesha kuyafanya yanayo hitajika tunapo muomba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) awavishe wasio na nguo.
Zifuatazo ni aya za Qur’an na dua zinazo stahiki kuangaliwa kwa makini:
1. [Sura al-A’raf - 7:26]:
يَا بَنِي آدَمَ قَدْ أَنْزَلْنَا عَلَيْكُمْ لِبَاسًا يُوَارِي سَوْآتِكُمْ وَرِيشًا ۖ وَلِبَاسُ التَّقْوَىٰ ذَٰلِكَ خَيْرٌ ۚ ذَٰلِكَ مِنْ آيَاتِ اللَّهِ لَعَلَّهُمْ يَذَّكَّرُونَ
“Enyi wanadamu hakika tumewateremshieni nguo (mavazi) zifichazo tupu zenu na nguo za pambo na nguo ya uchamungu ndiyo bora...”
2. Imepokewa kutoka kwa Imam Musa (bin Ja’far) al-Kadhim (a.s.) kwamba mtu anapotaka kuivaa nguo mpya anatakiwa apitishe mkono wake kwenye nguo hiyo kwa kuipapasa na aseme:
الْحَمْدُ لِلّهِ الَّذِيْ كَسَانِيْ مَا أُوَارِيْ بِهِ عَوْرَتِيْ و أَتَجَمَّلُ بِهِ فِي النَّاسِ...
“Shukrani zote zinamstahiki Mwenyezi Mungu ambaye amenivisha kinacho ficha uchi wangu na najipamba nayo mbele za watu.”1
Tukichunguza yaliyotajwa hapo juu tunafahamu ya kwamba sababu mbili muhimu za kuvaa nguo ni:
1. Kuficha uchi
2. Kujipamba mtu mwenyewe
VAZI LA NDANI
Baada ya kuzungumzia neema hii kubwa, Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anampeleka msomaji kwenye ukweli ulio muhimu sana, ambao lau utapuuzwa utasababisha majuto yenye kuendelea. Anamkumbusha mwanadamu ya kwamba hakuumbwa katika mwili wa kiumbo pekee ili ahitajie ‘vazi la kimwili’ tu, bali ‘vazi la ndani’ (ucha mungu), ndio la msingi muhimu zaidi. Katika maneno ya Qur’an: (‘dhalika khayr’ - hilo ni bora). ‘Allama Tabataba’i katika kitabu chake kikubwa ‘al-Mizan’ ana maelezo mazuri kuhusiana na nukta hii. Ili kuonyesha hali mbaya ya ‘uchungu’ anaousikia mwanadamu wakati aibu zake zinapodhihirishwa, anasema:
...إلاَّ اَنَّ ظُهُوْرَ سَوْءاتِ البَاطِنِيَّةِ أّشدُّ...
“…Isipokuwa kudhihiri kwa mabaya ya ndani kuna uchungu zaidi…”
Aya zingine za Qur’an zinaelezea kikamilifu msiba ulioko wa hali kama hii kwa mfano:
1. [Sura ya al-Tariq - 86:9]:
يَوْمَ تُبْلَى السَّرَائِرُ
“…Siku zitakapo dhihirishwa siri…”
2. [Sura ya Ali ‘Imran - 3:30]:
يَوْمَ تَجِدُ كُلُّ نَفْسٍ مَا عَمِلَتْ مِنْ خَيْرٍ مُحْضَرًا وَمَا عَمِلَتْ مِنْ سُوءٍ تَوَدُّ لَوْ أَنَّ بَيْنَهَا وَبَيْنَهُ أَمَدًا بَعِيدًا ۗ وَيُحَذِّرُكُمُ اللَّهُ نَفْسَهُ ۗ وَاللَّهُ رَءُوفٌ بِالْعِبَادِ
“siku ambayo kila nafsi itakuta iliyoyafanya katika mema yamehudhurishwa, na katika maovu iliyoyafanya. Itatamani lau kungelikuwa na masafa marefu baina yake na maovu hayo…”
3. [Sura ya Ali ‘Imran - 3:192]:
رَبَّنَا إِنَّكَ مَنْ تُدْخِلِ النَّارَ فَقَدْ أَخْزَيْتَهُ ۖ وَمَا لِلظَّالِمِينَ مِنْ أَنْصَارٍ
“Mola wetu, hakika unayemtia motoni umemhizi (na walio dhulumu hawana wasaidizi)”
Kwa hiyo tunapoisoma sehemu hii ya dua tunawajibika kutafakari ili tujue kama tuko miongoni mwa wale wasio na mavazi ya kiroho au la. Na ikiwa tu miongoni mwao tunatakiwa tumuombe Mwenyezi Mungu (s.w.t.) aturuzuku taqwā ili tusije kupata aibu hiyo ambayo ni kali sana kuivumilia.
Msingi mwingine wa kutumia nguo ulikuwa ni kumfanya mtu apendeze mbele za watu. Mwelekeo wa kupendeza umerithiwa katika kila mwanadamu, na kuna dalili nyingi katika hadithi zetu tukufu ambazo zinamhimiza mtu kuwa nadhifu na kupendeza mbele za watu katika kiwango kinachokubaliwa na sheria. Ili kuchunga uchache wa maneno wa maelezo haya, tutaepuka kuzitaja (hadithi hizo).
Hata hivyo lazima tufahamu ya kwamba taqwā na uchaji ndiyo chanzo cha kinga ya maovu na mambo ya aibu, na pia ni chanzo cha mapambo. Hii ni kwa sababu kuwa hupamba umbo la ndani la mwanadamu pamoja na tabia nzuri, na kumfanya kipenzi wa Allah (s.w.t.). Ni umbali ulioje wa ‘mpendwa wa uzuri wa dhahiri’ kutoka kwa ‘Mpendwa wa uzuri wa kiroho’: razaqanallahu jami’an [Allah atuwezeshe sisi sote kulipata hilo].
Du’a
Ewe Mola tunapokuomba kwa unyenyekevu uwavishe walio uchi kimwili na kiroho, na tunaomba msaada wako uwasaaidie wale ambao hawana nguo za kustahili katika hali zao za kimaisha, utuwezeshe tujitahidi katika kujivisha mavazi ya taqwā, ili tupate stahiki ya kuwavisha wengine pia.
• 1. ‘Allāma Majlisi, Hilyatu‘l Muttaqin, sura ya 9.
MWISHO