BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI
KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
UMUHIMU WA DINI KATIKA TAMADUNI NA MAADILI YA JAMII
Dini ni utamaduni na maadili ya kijamii, na imechukua nafasi kubwa katika suna zake Allah (s.w) (hii haimaanishi kuwa dini imejifunga katika suna za Mwenyeezi Mungu na mambo ya kijamii tu), bali suna za Mwenyeezi Mungu ni sehemu ndogo tu ya dini, na sio dini yote kamili, kwa hiyo ufafanuzi wa Marhumu Alame Tabatabai kuwa:-
“Dini ni taratibu na suna za kijamii ambazo mwanaadamu anazitekeleza katika maisha yake ya kijamii…na dini ni suna za kimatendo zinazoendeshwa kupitia mtazamo wa kidunia na mtazamo wa kibiologia[1]
Ufafanuzi huo wa alame Tabatabai sio wenye kukubalika; kwa sababu:-
Mila, desturi na tamaduni za kijamii, au hata suna zake Mola Mtakatifu ni sehemu ya dini, na sio dini kamili, ni sahihi kuwa katika sunna za Mwenyeezi Mungu na Mitume yake kumekusanya elimu na taaluma nyingi zilizo na thamani, lakini inafaa tuzingatie kuwa ufafanuzi huo hautoshelezi kuiarifisha au kuifafanua dini, kwa hakika kuifafanua dini katika mtindo huo ni kuiwekea dini mipaka maalumu, na kuisambaza dini au kuipa upeo katika mambo ya kijamii tu. Hali ya kwamba dini ina nafasi katika mambo na sehemu tofauti za maisha ya mwanaadamu.
Zingatio:
Kuwa na itikadi katika vipengele mbali mbali vya dini, (kwa mfano, Misingi, nyanja, maamrisho, mabainisho, na desturi za dini) haimaanishi kuwa ni mtu mwenye imani na dini (ya Kiislamu), kwa hiyo wale walioifafanua dini kwa mtazamo huu kuwa; “Dini ni mwanaadamu kuwa na itikadi na Mola muumba” basi ufafanuzi huo haukubalili kwa sababu:-
Moja: Haki na uhakika wa dini hauko katika itikadi na nyanja zake tu, bali mbali ya kuwa na itikadi hizo kunahitajika kukubali mambo mengine ambayo vile vile ni maamrisho yake Allah (s.w).
Mbili: Tukizingatia kuwa, katika taaluma na elimu nyingi za dini kuwa na itikadi na Mwenyeezi Mungu, haimaanishi kuwa katika vitu hivyo viwili (elimu na kuwa na itikadi na Mola Muumba) hakuna malazimiano yasiyoweza kutengana, kwa sababu baadhi ya wakati mtu anaweza kujenga fungamano na maamrisho hayo kutokana na nadharia mbali mbali zilizotolewa na watu tofauti, kwa hiyo ufafanuzi huo wa dini hauwezi kukusanya maarifa na taaluma zote za dini inayokusudiwa.
Tatu: Mwenyeezi Mungu Mtukufu amekusanya sifa mbali mbali, sifa ambazo watu huzitumia kwa kumnasibisha Yeye na sifa hizo,miongoni mwa sifa hizo ni sifa za dhati (sifa asili) za Mwenyeezi Mungu, sifa jalal, na sifa jamal,n.k.
Sifa ya uumbaji ni miongoni mwa sifa za matendo yake Mwenyeezi Mungu, kwa hiyo haiwezekani kuifafanua na kuifunga dini katika nyanja moja tu, yaani, kuwa na itikadi na Mola muumba, hivyo ingawaje kuwa na itikadi na Mola muumba ni sehemu ya dini, lakini haiwezekani kuifafanua dini kwa kuiangalia dini katika mtazamo huo tu, kwani kuna mitizamo mbali mbali na sifa mbali mbali za Mwenyeezi Mungu ambazo kila mmoja anatakiwa kuwa na imani nazo na kuzitekelezea maamrisho yake. Kwa hiyo huo si mtazamo wa kiakili na ni fikra finyu.
Nne:Dini haijateremshwa kwa ajili ya wanaadamu tu, (bali dini imeteremshwa kwa ajili ya viumbe wote, na binaadamu ni miongoni mwao). kwa hiyo kuifafanua dini kwa mtazamo huo, yaani (mwanaadamu kuwa ni itikadi na Mola Mtakatifu) sio jambo linalokubalika.
Tano: Ikiwa dini ni kuwa na itikadi na Mola Muumba basi washirikina pia wana itikadi hiyo, kama inavyosema qur-ani:-
وَلَئِن سَاَلْتَهُم مَّنْ خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالاَرْضَ لَيَقُولُنَّ اللهُ قُلْ اَفَرَاَيْتُم مَّا تَدْعُونَ مِن دُونِ اللهِ إِنْ اَرَادَنِيَ اللهُ بِضُرٍّ هَلْ هُنَّ كَاشِفَاتُ ضُرِّهِ اَوْ اَرَادَنِى بِرَحْمَةٍ هَلْ هُنَّ مُمْسِكَاتُ رَحْمَتِهِ قُلْ حَسْبِيَ اللهُ عَلَيْهِ يَتَوَكَّلُ الْمُتَوَكِّلُونَ[2]
Na ukiwauliza “Ni nani aliyeziumba mbingu na ardhi?” bila ya shaka watasema: “Ni Mwenyeezi Mungu.” Sema: “Je, mnawaonaje wale mnaowaomba kinyume cha Mwenyeezi Mungu?, kama Mwenyeezi Mungu akitaka kunidhuru, wao wanaweza kuniondolea dhara yake? Au akitaka kunirehemu, je, wao wanaweza kuzuia rehema yake?” Sema: “ Mwenyeezi Mungu ananitosha, kwake wategemee wanaotegemea.”
Hivyo, vipi tunaweza kuwatambua watu kama hao kuwa ni wenye dini hali ya kwamba hawakuwa na dini kamwe?.
Zingatio :
Kuarifishwa dini katika maana tofauti haimaanishi kukubalika kwa dini tofauti au kutokuwa sahihi dini inayokusudiwa (dini ya Kiislamu). Bali kuwepo kwa dini tofauti ni kwa sababu mwanaadamu ni mwenye kutafuta hali halisi ya undani wa dini, na kwa sababu hana elimu ya kutosha kuhusiana na dini huiarifisha dini kutokana na mtazamo wake binafsi au kutegemea nadharia zilizotolewa na watu wengine kuhusiana na dini, watu wengi walioifafanua dini wameifafanua kwa mujibu wa mitazamo yao, kimsingi watu hao hawajaitambua dini, na baadhi yao wameifafanua dini kwa mujibu wa itikadi walizonazo kuhusiana na dini fulani, dini ambayo pengine ndiyo waliyo na imani nayo, na baadhi yao wameifafanua dini kulingana na nadharia walizonazo au kwa upendeleo wa dini fulani, kwa hiyo ikiwa ufafanuzi huo sio wenye kukubaliwa na watu wote haimaanishi kuwa dini inayokusudiwa ina upungufu fulani au sio sahihi, kwa sababu walioifafanua dini wameifafanua kulingana na kile walichokifahamu kuhusiana na dini, dalili nyengine iliyosababisha kuja kwa dini tofauti ni kwa sababu ya uwiano uliopo katika neno hilo (dini), yaani neno hilo lina maana tofauti, lakini watu hulitumia kwa mujibu wa ile dini wanayoifafanua bila ya kuzingatia maana asili ya neno hilo, Kwa hiyo dini tofauti hazimaanishi upungufu fulani wa dini au kutokuwepo haki au uhakika wa dini hiyo .
[1] Shia katika Uislamu, Marhum Alame Tabatabai. Uk 20-25.
[2] Surat azumar Aya ya 38