BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI
KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
DARAJA ILIYO BORA YA MTUME MUHAMMAD (S.A.W.W).
* Kwa nini Mtume Muhammad (s.a.w.w) ana daraja kubwa zaidi Ukilinganisha na Mitume wengine?.
*Ni alama gani zinazoonesha ubora wa Mtume Muhammad (s.a.w.w.) kulinganisha na Mitume wengine?.
Mitume yote ya Mwenyeezi Mungu imeshirikiana katika sifa ya daraja ya kiutume, - yaani Mitume yote imepewa sifa hii tukufu na Mola wao – na vile vile Mitume hao wana nuru ya elimu waliyopewa na Mola wao, elimu hiyo ni kwa ajili ya kuwaongowa wanaadamu na kuwaongoza katika njia njema, vile vile kwa elimu hiyo huweza kuwajibu watu masuala yao.
Sifa nyengine waliyonayo Mitume ni wao kuwa maasumu, na wameepukana na kila machafu, na sifa hii huwafanya wanaadamu wawe na imani na Mitume hiyo, na kuwa na uhakika na yale ambayo Mitume hiyo inawalingania. Sifa nyengine waliyonayo Mitume ni kuwa wote walikuwa wakifanya jitihada katika kuufikisha ujumbe waliopewa na Mola wao, na vile vile walikuwa na huruma na watu wao.
Lakini vile vile ni lazima tuzingatie kuwa sifa ya elimu na isma zinakhitilafiana katika ubora au udhaifu wake, kama tunavyoshuhudia katika kauli ya Mtume wetu Muhammad (s.a.w.w) alipomuomba Mola wake pale aliposema:-
رب زدنی علما
Yaani, Ewe Mola wangu nakuomba unizidishie elimu yangu.
Vile vile Mitume wanakhitilafiana katika jitihada zao, kama anavyosema Allah (s.w):-
وَلَقَدْ عَهِدْنَا إِلَي آدَمَ مِن قَبْلُ فَنَسِيَ وَلَمْ نَجِدْ لَهُ عَزْماً[1]
Na hapo zamani tuliagana na Adam, lakini alisahau, wala hatukuona kwake azma kubwa.
Na ni kwa sababu hiyo basi baadhi ya Mitume wanakhitilafiana na baadhi yao kifadhila na daraja katika ubora wao, kama anavyosema Allah (s.w):-
تِلْكَ الرُّسُلُ فَضَّلْنَا بَعْضَهُمْ عَلـٰي بَعْضٍ مِّنْهُم مَّن كَلَّمَ اللّهُ وَرَفَعَ بَعْضَهُمْ دَرَجَاتٍ وَآتَيْنَا عِيسَي ابْنَ مَرْيَمَ الْبَيِّنَاتِ وَاَيَّدْنَاهُ بِرُوحِ الْقُدُسِ وَلَوْ شَاء اللّهُ مَا اقْتَتَلَ الَّذِينَ مِن بَعْدِهِم مِّن بَعْدِ مَا جَاءتْهُمُ الْبَيِّنَاتُ وَلَـكِنِ اخْتَلَفُواْ فَمِنْهُم مَّنْ آمَنَ وَمِنْهُم مَّن كَفَرَ وَلَوْ شَاء اللّهُ مَا اقْتَتَلُواْ وَلَـكِنَّ اللّهَ يَفْعَلُ مَا يُرِيدُ[2]
MITUME hao tumewatukuza baadhi yao juu ya wengineo. Katika wao wapo ambao Mwenyezi Mungu alisema nao, na wengine akawapandisha vyeo. Na tukampa Isa mwana wa Mariyam hoja zilizo wazi, na tukamtia nguvu kwa Roho Takatifu. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu alipenda wasingeli pigana walio kuwa baada yao baada ya kuwajia hoja zilizo wazi. Lakini walikhitalifiana. Basi wapo kati yao walio amini, na wengine kati yao walio kufuru. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu alipenda wasingeli pigana. Lakini Mwenyezi Mungu hutenda atakavyo.
*Aya hii inaonsha kuwa Mitume daraja zao ni mbali mbali kwa Mwenyeezi Mungu kama binaadamu wengine na Malaika na majini na vinginevyo, wanazidiana kwa fadhila za Mwenyeezi Mungu na kwa amali zao, walizofanya ambazo si sawa sawa, za wengine ni kubwa zaidi au ni nyingi zaidi kuliko za wenziwao.
Mmoja miongoni mwa Mitume waliostahamili tabu na mashaka katika njia ya Mwenyeezi Mungu ni (Halilu llah), kama anavyosema Allah (s.w) kuhusiana na Nabii Ibrahimu (a.s):-
وَمَنْ اَحْسَنُ دِيناً مِّمَّنْ اَسْلَمَ وَجْهَهُ لله وَهُوَ مُحْسِنٌ واتَّبَعَ مِلَّةَ إِبْرَاهِيمَ حَنِيفاً وَاتَّخَذَ اللّهُ إِبْرَاهِيمَ خَلِيلاً[3]
Na nani aliye bora kwa dini kuliko yule aliye usilimisha uso wake kwa Mwenyezi Mungu, naye akawa mwema, na anafuata mila ya Ibrahim mwongofu? Na Mwenyezi Mungu alimfanya Ibrahim kuwa ni rafiki mwendani. Na miongoni mwa Mitume walimtakasa Mwenyeezi Mungu, kama anavyosema Allah (s.w) kuhusiana na Nabii Mussa (a.s)
وکلم الله موسی تکلیما
Na Mwenyeezi Mungu alizungumza na Mussa.
Na miongoni mwao waliwahuisha viumbe wafu na kuwapa uhai, kama anavyosema Allah (s.w) kuhusiana na Nabii Issa (a.s):-
وَلَقَدْ آتَيْنَا مُوسَي الْكِتَابَ وَقَفَّيْنَا مِن بَعْدِهِ بِالرُّسُلِ وَآتَيْنَا عِيسَي ابْنَ مَرْيَمَ الْبَيِّنَاتِ وَاَيَّدْنَاهُ بِرُوحِ الْقُدُسِ اَفَكُلَّمَا جَاءكُمْ رَسُولٌ بِمَا لاَ تَهْوَي اَنفُسُكُمُ اسْتَكْبَرْتُمْ فَفَرِيقاً كَذَّبْتُمْ وَفَرِيقاً تَقْتُلُونَ[4]
Na hakika tulimpa Musa Kitabu na tukafuatisha baada yake Mitume wengine. Na tukampa Isa, mwana wa Mariamu, hoja zilizo waziwazi, na tukamtia nguvu kwa Roho Takatifu. Basi kila walipo kufikieni Mitume kwa yale ambayo hayapendwi na nafsi zenu, mlijivuna; wengine mkawakanusha, na wengine mkawauwa.
Na miongoni mwa Mitume kwa sababu ya kuwa na vyeo vyote na m-bora kuliko wote ameitwa (mjumbe wa Mwenyeezi Mungu) na yuko karibu zaidi na Mwenyeezi Mungu, kama tunavyosoma kuhusiana na Nabii Muhammad (s.a.w.w).
سُبْحَانَ الَّذِى اَسْرَي بِعَبْدِهِ لَيْلاً مِّنَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ إِلَي الْمَسْجِدِ الاَقْصَي الَّذِى بَارَكْنَا حَوْلَهُ لِنُرِيَهُ مِنْ آيَاتِنَا إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ البَصِيرُ[5]
SUBHANA, Ametakasika aliye mchukua mja wake usiku mmoja kutoka Msikiti Mtukufu mpaka Msikiti wa Mbali, ambao tumevibariki vilivyo uzunguka, ili tumuonyeshe baadhi ya Ishara zetu. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia na Mwenye kuona.
Mtume wetu Muhammad (s.a.w.w) mbali ya kuwa na sifa nyingi tukufu ambazo ameshirikiana na Mitume wengine waliopita, vile vile ana sifa nyengine ambazo Mitume wengine hawana, kwa mfano Yeye ni M-bora wa Mitume, ili kuelezea zaidi, katika katika sehemu hii tutaelezea ubora wa Mtume Muhammad (s.a.w.w.) kulinganisha na Mitume iliyopita, na hii inaweza kuwa ni dalili bora inayoweza kuwafanya watu kuwa na imani na ulazima uliopo wa kumuamini Mtume huyu Mtukufu na huu ni wadhifa unaowawajibikia watu wote kuufuata.
[1] Surat Taha Aya ya 115
[2] Surat Albaqarah Aya ya 253
[3] Suratun Nisaa Aya ya 125
[4] Suratul-baqarah Aya ya 87
[5] Surat Al-Israa Aya ya 1