BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI
KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
HALI HALISI YA UHAKIKA WA DINI NO.2
Katika makala iliyopita tulielezea kuhusu hali halisi ya uhakika wa dini, na kupitia yale yaliyoelezewa na kutolewa nadharia tukapata natija ya kuwa ufafanuzi wao haukuwa wenye kutosheleza, katika makala hii tutaendelea na mada yetu hiyo hiyo inayohusiana na uhakika wa dini hadi kupata natija itakayoridhisha.
5. Kuifafanua dini kwa namna hiyo kunaonyesha hofu aliyonayo mwanaadamu kuhusiana na dini, mwanaadamu ambaye hana imani wala hana itikadi na Mwenyeezi Mungu, bali ni hofu ndiyo inayomfanya awe na shauku ya kumtafuta Mola wake, hali ya kwamba kumuamini Mwenyeezi Mungu pia ni sehemu ya uhakika wa dini.
6. Shauku gani ya mwanaadamu ni kigezo cha dini, kigezo ambacho kinamfanya mwanaadamu huyo awe ni mwenye dini. Hivi matamanio ya kijinsia yaliyokithiri mpaka ya mwanaadamu (mwanaadamu kutafuta ridhaa ya nafsi yake kwa kujenga uhusiano wa kijinsia kwa mwanamme na mwanamme au mwanamke kwa mwanamke) ndiyo yanayomfanya mwanaadamu awe na shauku ya kumtafuta Mola wake? Hivyo mtu kama huyo ambaye dini yake inawiana na matamanio yake yaliyotokana na uasi wake tunaweza kuiarifisha kuwa hiyo ni dini? Au mtu kama huyo inawezekana kukubaliwa kuwa ni mtu mwenye dini?!
7. Kuna dalili gani zinazothibitisha kuwa mwanaadamu kumtafuta Mola wake kwa njia yoyote ile kunampelekea mwanaadamu huyo kumfikia Mola wake? Na kuna dalili gani zinazothibitisha kuwa kila anayemfikia Mola wake atakuwa ameshikamana na dini au atakuwa ni mtu mwenye dini? Hali ya kwamba ikiwa kafiri mkuu miongoni mwa wanaadamu ataulizwa itikadi yake kuhusiana na Mwenyeezi Mungu kwa hakika atasema ni Mwenye imani ya kuwepo kwake Mola Mtakatifu, kama inavyothibitisha Aya hii tukufu:-
وَلَئِن سَاَلْتَهُم مَّنْ خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالاَرْضَ لَيَقُولُنَّ اللهُ قُلِ الْحَمْدُ للهِ بَلْ اَكْثَرُهُمْ لاَ يَعْلَمُونَ[1]
Na ukiwauliza: Nani aliye ziumba mbingu na ardhi? Bila ya shaka watasema: Mwenyezi Mungu. Wewe sema: Alhamdulillahi! Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu. Lakini wengi wao hawajui.
8. Ufafanuzi huo wa dini wa watu hao sio sahihi na haukubaliki kwa sababu hizi zifuatazo:-
a) Katika kuifafanua na kuiarifisha dini wametumia nadharia zao za kibinafsi.
b)Wameifafanua dini kwa kuzingatia nyanja ya ufahamu wa dini tu, na sio katika nyanja ya hisia za dhati zilizomo katika nafsi ya binaadamu, na hawakutilia maanani utendaji wa amali na matendo yaliyoamrishwa katika dini.
c) Watu hao wameifafanua na kuiarifisha dini bila ya kuzingatia hukumu na maamrisho yake Mola Mtakatifu.
d) Wameifafanua dini kwa kuzingatia baadhi tu ya nafasi za dini, na hawakubainisha uhakika wa dini.
e) Ufafanuzi huo ni kwa mujibu wa nadharia za watu wa nchi za kimagharibi[2] .
MFUMO WA UHAKIKI WA ELIMU YA DINI
Njia na mfumo wa uhakiki wa dini:
1. Madhumuni ya uhakiki wa dini ni kutalii mafunzo ya dini yaliyomo ndani na nje mwa matini za dini. Kwa hiyo elimu ya dini imekusanya mafunzo na elimu zote za dini, ikiwemo elimu ya falsafa ya dini, elimu inayohusiana na mambo ya itikadi za dini, elimu ya fiqhi, elimu inayohusiana na tabia, mwenendo, na itikadi za dini.
2. Fikra na akili za wanaadamu siku hadi siku zinakua na ziko katika hali ya kufichua na kuvumbua mambo tofauti, na kwa sababu akili ni yenye kudiriki uhakika wa mambo mbali mbali, vile vile imeweza kufahamu fitra ya kimaumbile aliyonayo mwanaadamu kuhusiana na umuhimu wa dini, kwa upande mwengine akili hiyo imeweza kudiriki haki na uhakika wa dini. Katika zama za leo, siku hadi siku watu wengi wamekuwa wakivutiwa na dini na wamekuwa na hamu ya kutaka kuitambua hali halisi ya uhakika wa dini, kwa hiyo, kutokana na ulazima uliopo baina ya fitra ya dini iliyomo katika nafsi ya mwanaadamu na umuhimu uliopo katika kuifahamu elimu ya dini, hapana shaka watu watayapokea mafunzo hayo ya elimu ya dini kwa shauku kubwa.
3. Siku zote haki ni moja tu, na ikiwa hakuna dini ya haki isipokuwa dini ya Mwenyeezi Mungu basi ni dini ya Kiislamu tu ndio dini ya haki, kama anavyothibitisha Allah (s.w) katika kitabu chake kitukufu:-
إِنَّ الدِّينَ عِندَ اللهِ الإِسْلاَمُ وَمَا اخْتَلَفَ الَّذِينَ اُوْتُواْ الْكِتَابَ إِلاَّ مِن بَعْدِ مَا جَاءهُمُ الْعِلْمُ بَغْياً بَيْنَهُمْ وَمَن يَكْفُرْ بِآيَاتِ اللهِ فَإِنَّ اللهِ سَرِيعُ الْحِسَابِ[3]
Bila ya shaka Dini mbele ya Mwenyezi Mungu ni Uislamu. Na walio pewa Kitabu hawakukhitalifiana ila baada ya kuwajia ujuzi, kwa sababu ya uhasidi ulio kuwa baina yao. Na anaye zikataa Ishara za Mwenyezi Mungu basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhisabu.
na Waislamu wa kweli mbele ya Mwenyeezi Mungu na Mtume wake ni wale ambao watafuata maamrisho ya Mola wao Mitume yake, na Ahlulbayt (a.s), kwa hiyo kwa wale ambao wamefuata njia nyengine wakiwa na matumaini ya kuwa wamefuata njia sahihi, kwa hakika njia hizo sio sahihi, na hakuna maslahi yoyote watakayoyapata kwa kuzifuata njia hizo. Kwa sababu ingawa zinatokana na wahyi wa Mwenyeezi Mungu, lakini njia hizo zimepotoshwa na wanafiki waliodai kuwa ni wafuasi au viongozi wa dini ya Mwenyeezi Mungu, hali ya kwamba walikuwa wakiiharifu na kuiharibu dini ya Kiislamu na hukumu zake Mwenyeezi Mungu (s.w) nje ya pazia, watu hao waliwadhulumu na kuwanyan`ganya watu haki zao, watu hao waliwadhulumu makhalifa wa Mwenyeezi Mungu, makhalifa ambao tayari Allah (s.w) alikwisha wachagua kuwa ni viongozi wa dini yake, lakini kwa sababu kulitokea wanafiki walio na tamaa na utawala au mali za dunia walifanya jitihada zao zote hata wakadiriki kupinga maamrisho yake Allah (s.w) ili kufikia katika yale ambayo yanawaridhisha nafsi zao. Basi ni wadhifa wa kila mwenye akili salama kufikiria njia hizo walizozifuata, na kuzitafutia utafiti njia hizo ili kupata ufumbuzi wake, hapo mtu huyo anaweza kutambua haki iko wapi, basi wakati huo ni wadhifa wake kuhukumu kwa insafu na kuifuata njia hiyo ya haki.
4. Mtawala asili wa dini ni elimu ya dini na yule aliyeviumba viumbe na kuvipa akili, akili ambayo ndio kigezo bora kinachoweza kupambanua zuri na baya, na haki na batili, kwa hiyo, kwa kutumia elimu ya dini
tunaweza kuisaidia jamii kwa kuhuisha utamaduni na maadili mema ya Kiislamu, na ni elimu ya dini pekee ndio inayoweza kuleta utawala katika mambo ya kisiasa na kuipeleka jamii katika ukamilifu. Tukiachana na hayo, kimsingi utawala wa uhakika wa dini ni mafunzo yanayotokana na elimu ya dini.
[1] Surat Luqmani Aya ya 25
[2] Rohnamoi Ilahiyati Prutistan, Pul Tilakh.uk,147-148
[3] Surat Al-Imrani Aya ya 19
MWISHO