UHAKIKI WA DINI KATIKA DINI YA KIISLAMU
  • Kichwa: UHAKIKI WA DINI KATIKA DINI YA KIISLAMU
  • mwandishi: NDUGU ZETU WA KIISLAMU
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 2:15:57 23-8-1403

 

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

UHAKIKI WA DINI KATIKA DINI YA KIISLAMU

Kipengele cha kwanza: Misingi na malengo muhimu ya uhakiki wa dini:

Ikiwa kila jambo lililo na uhakika na linalokubalika kiakili haliwezi kuwepo bila  madhumuni maalumu, basi uhakiki wa dini (makusudio ni diniya Kiislamu) ukiwa kama ni uhakika unaokubalika kiakili hauwezi kuwepo bila ya malengo maalumu, ijapokuwa maadui na wapingaji wa dini wanafanya jitihada zao zote ili kuitambua dini, wakiwa na malengo ya kutafuta njia zitakazoweza kuiharifu dini hiyo, na kuwapotosha watu ambao wanafuata maamrisho na maelekezo ya dini hiyo, kutokana na sababu hizo  wale wote walio na itikadi na wanaoikubali dini hiyo inawapasa kuweka wazi malengo yao ili kuweza kufahamu haki na hali halisi  ya uhakika wa dini yao. Vile vile inawapasa kuwa na elimu ya kutosha juu ya dini yao ili kuweza kufahamu fikra za maadui hao na kuweza kujibu kasumba na madai yao yanayohusiana na dini hiyo takatifu.

Wahakiki wa dini wanaweza kuwa na malengo tofauti katika uhakiki wao, baadhi ya wakati malengo yao yanaweza yakawa yanahusiana na dini kijumla, baadhi ya wakati malengo yao  yanaweza yakawa yanahusiana na vipengele maalumu tu, na baadhi ya wakati inawezekana ikawa malengo yao ni kuhusiana na desturi, maamrisho na makatazo ya dini, kwa upande mwengine malengo ya uhakiki wa dini yanaweza kuwa ni kuzalisha fikra mpya, kumkuza mwanaadamu kifikra, kwa sababu kukuwa kifikra kwa mwanaadamu hutokana na udadisi wake wa kutaka kutambua mambo tofauti, hivyo baadhi ya wahakiki hufanya uhakiki wa dini wakiwa na malengo ya kumtekelezea mwanaadamu mahitajio yake anayoyahitaji katika maisha yake, na baadhi ya wakati inawezekana malengo ya uhakiki wa dini yakawa ni kumtatulia mwanaadamu matatizo yanayoweza kumkuta katika maisha yake.

KIPENGELE CHA PILI:

Msingi wa mipango na program za kitengo cha uhakiki wa dini:

Mwanaadamu ni kiumbe asiyetambulika, na utambulikanaji wa kiumbe huyo unaweza kupatikana baada ya kupita muda mrefu.

Iliposemwa mwanaadamu ni kiumbe asiyetambulika imekusudiwa asiyetambulika uumbwaji wake, kwa sababu uumbwaji wake unatokana na utukufu wa rehema zake Mwenyeezi Mungu. Yeye ameviumba viumbe vingi, lakini alipomuumba mwanaadamu ulithibitika utukufu wa rehema na elimu yake aliyonayo Mola Muwezi, elimu ambayo aliithibitisha pale aliposema:-

ثُمَّ خَلَقْنَا النُّطْفَةَ عَلَقَةً فَخَلَقْنَا الْعَلَقَةَ مُضْغَةً فَخَلَقْنَا الْمُضْغَةَ عِظَاماً فَكَسَوْنَا الْعِظَامَ لَحْماً ثُمَّ اَنشَاْنَاهُ خَلْقاً آخَرَ فَتَبَارَكَ اللهُ اَحْسَنُ الْخَالِقِينَ[1]

 Kisha tukaiumba tone kuwa damu iliyo ganda, na tukaiumba damu kuwa pande la nyama, kisha tukaliumba pande la nyama kuwa mifupa, na mifupa tukaivika nyama. Kisha tukamfanya kiumbe mwengine. Basi ametukuka Mwenyezi Mungu Mbora wa waumbaji.

Tukizingatia kwa uangalifu Aya hiyo tutafahamu kuwa Mwenyeezi Mungu amemuumba mwanaadamu katika hatua mbali mbali, hatua ambazo ndizo alizozitumia katika kuwaumba viumbe wengine, kwa mfano wanyama, lakini mbali ya hatua hizo aliongeza ujuzi wake pale alipoiumba roho na kumpulizia mwanaadamu huyo, mwanaadamu ambaye amempa akili, akili ambayo ndiyo itakayomsaidia kufikia katika saada njema ya duniani na Akhera. Basi wakati huo ndipo ulipothibitika utukufu wa rehema zake. Baadae akamfanya mwanaadamu huyo kuwa ni kiumbe bora kuliko viumbe wengine, kiumbe ambaye ikiwa ataitumia akili yake kwa mtindo unaokubalika na yeye Allah (s.w), anaweza kufikia daraja ya juu zaidi kuliko ya Malaika Na kwa sababu hiyo basi akamchagua mwanaadamu huyo kuwa ni khalifa juu ya ardhi yake. Pale alipowaambia Malaika:-

Na pale Mola wako Mlezi alipo waambia Malaika: Mimi nitamweka katika ardhi Khalifa (mfwatizi), wakasema: Utaweka humo atakaye fanya uharibifu humo na kumwaga damu, hali sisi tunakutakasa kwa sifa zako na tunakutaja kwa utakatifu wako? Akasema: Hakika Mimi nayajua msiyo yajua[2]

 Kwa hiyo, ikiwa mwanaadamu sio mwenye kutambulika isipokuwa kwa muda mrefu basi na dini vile vile iko katika nyanja mbali mbali na upeo usiotambulika, upeo ambao mwanaadamu hawezi kuufikia uhakika wake hata kama atapewa makarne ya miaka. Kwa hiyo, ni dini pekee inayoweza kumletea mwanaadamu saada ya duniani na Akhera.

Kwa ufafanuzi huo itakuwa imeshaeleweka kuwa dini ni taaluma ambayo imesambaa katika kila upande, na mwanaadamu siku zote ni mwenye udadisi wa kutaka kujua mambo mbali mbali yanayohusiana na maisha yake na ulimwengu kwa ujumla, kwa sababu hiyo basi mwanaadamu huyo anahitajia kundi au kipengele cha dini ambacho kitapanga mipango mbali mbali ya kumsaidia mwanaadamu huyo ili kuweza kupata mahitajio yake na kumuongoza katika uongofu, kwa hiyo ili kutekelezeka mipango hiyo ya dini ni lazima kitengo cha uhakiki wa dini kupanga mipango kwa uangalifu wa hali ya juu kabisa, mipango ambayo itakuwa inaendana na kukubalika kiakili na kibinaadamu, kwa upande mwengine, mipango hiyo ni lazima iwe inaendana na mahitajio ya wanaadamu, kundi au kitengo hicho cha uhakiki wa dini kinatakiwa kutambua njia wanazotumia maadui au wapingaji dini katika kuhujumu fikra za jamii.

Kipengele cha tatu tutakielezea katika makala zinazofuata.

[1] Surat Al-Muuminuun Aya ya 14

[2] Surat Albaqarah Aya ya 30