BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI
KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
KUDHUHURU KWA IMAM MAHDI (A.j). NO.2
SABABU ZA KUDHUHURU IMAM MAHDI (A.S).
Kudhuhuru kwa Imam kuna sababu na alama maalum na sababu hizo pamoja na alama zinaeleweka kuwa ndio matayarisho ya kuja kwake, tofauti ya vitu hivi viwili (alama na matayarisho) ni kwamba matayarisho yana athari muhimu katika kudhuhuru kwa Imam kiasi ya kwamba yakikamilika matayarisho hayo basi kudhihiri kwa Imam ni lazima kutokee, na kukosekana kwake kudhihiri kwa Imam hakutotokea, lakini alama za kudhihiri haziathiri kitu chochote katika kudhihiri kwake, bali alama hizo zinasaidia kuelewa umbali na ukaribu wa kudhihiri kwake. Kwa kutokana na tofauti tulizozielezea itakuwa ni rahisi kuelewa ya kwamba matayarisho pamoja na masharti yana umuhimu zaidi kuliko alama za kudhihiri, kwa hiyo basi kabla ya kuzifukuzia alama na kuzifuatilia ni bora zaidi tufuatilie
matayarisho na kila mmoja ajitahidi kwa kadri ya uwezo wake katika kuyatekeleza matayarisho hayo, ndio maana mwanzo kabisa tulizielezea shuruti pamoja na matayarisho, na sasa tutazitaja baadhi ya shuruti na matayarisho hayo.
MATAYARISHO YA KUMFANYA ADHIHIRI
B) UONGOZI
Katika harakati za aina zote kunahitajika kupatikana kiongozi, na jambo hili linahesabiwa kuwa ni moja kati ya mambo muhimu katika harakati, na kila harakati zikiwa kubwa zaidi na zenye malengo makubwa zaidi ni lazima apatikane kiongozi anayenasibiana na harakati hizo pamoja na malengo yake, na kiu ya kupatikana kiongozi kama huyo huwa inahisiwa zaidi. Katika muelekeo wa mapigano ya kidunia katika kupambana na dhulma na kuweka uongozi wa uadilifu na usawa katika ulimwengu, nguzo yake ya asili ni kupatikana kiongozi mwenye mitizamo ya hali ya juu mwenye uwezo na huruma, ambaye anatakiwa kuwa na uongozi ulio sahihi, na kupatikana kwa kiongozi huyo ndio msingi mkuu wa mapinduzi. Imam mahdi ambaye ni tunda la Manabii na Mawalii ndiye kiongozi wa mapinduzi makuu, naye yuko hai naye ni kiongozi pekee wa mapinduai hayo, kwa kutokana na kuwa na mawasiliano na Mwenyeezi Mungu naye anatambua kila kitu kilichomo katika ulimwengu huu, na ni mwenye elimu kuliko wote waliobakia katika zama hizi. Mtume (s.a.w) amesema:-
"Tambueni ya kuwa Imam Mahdi ni mrithi wa elimu zote na amezizunguka elimu zote (amezimiliki)[1].
Imam ni kiongozi pekee asiye fungamana na upande wowote ule wa kidunia bali yupo pamoja na radhi za Mwenyeezi Mungu. Kwa hiyo basi Serikali na mapinduzi ya kidunia ambayo ni serikali ya Imamu itakua na nidhamu bora zaidi kuliko serikali nyengine zilizopita.
C) WAFUASI
Moja kati ya masharti ya kuja kwa Imam ni kuwepo kwa wafuasi wenye sifa za ufuasi watakaoyatetea mapinduzi na kusimamia kazi za serikali, ni jambo la wazi kabisa kua itapokua kiongozi wa mapinduzi atakua ni mfuasi wa Mwenyeezi Mungu, kutakua kunahitajika kupatukana wafuasi wenye kunasibiana na kiongozi huyo, na sio kwamba kila mtu anayedai kua naye ni mfuasi anaweza kuhesabiwa kua ni mfuasi, katika suala hili hebu angalia kisa kifuatacho:-
Mmoja kati ya wafuasi wa Imam Sadiq (a.s) anayejulikana kwa jina la Sahli bin Hasan Khurasaniy alimwambia Imam Sadiq (a.s): "ni kipi kilichokuzuiya usiichukue serekali ambayo ni haki yako hali ya kua una wafuasi laki moja walio wapambanaji? Imam (a.s) alaamrisha uwashwe moto, na ulipokolea barabara Imam akamwambia Sahli, ewe Khurasaniy inuka uingie kwenye tanuri ya moto, Sahli akadhania kua Imam amemkasirikia, akaanza kutaka samahani na kusema, bwana wangu nisamehe na usiniadhibu kwa moto, Imam akamwambia nimekusamehe, hapo hapo akatokea Harun Makkiy ambaye ni mfuasi madhubuti wa Imam Sadiq (a.s), alipofika akamsalimia Imam na Imam akamjibu salamu yake, kisha bila ya kucherewa Imam akamwambia nenda kakae ndani ya tanuri moto, naye bila ya kuuliza kitu akenda haraka kukaa kwenye tanuri ya moto na baada ya muda Imam akamwambia Khurasaniy, inuka ukaangalie ndani ya tanuri, Khurasaniy akaenda kuangalia na akamuona Hasan Makkiy amepiaga magoti kwenye moto!
Hapo Imam akamuuliza Khurasaniy "katika mji wa Khurasani kuna watu wangapi unaowajua wanaofanana na Hasan Makkiy?" Khurasaniy akamjibu kwa kusema: "nakuapia kwa Mungu kua sina hata mtu mmoja anayefanana naye" Imam akamwambia "elewa ya kua iwapo hatutopata wafuasi watano walio madhubuti, basi hatufanyi mapinduzi, sisi tunatambua zaidi ni zama gani za kufanya mapimduzi[2].
" Kwa hiyo basi kuna haja ya sisi kurejea Hadithi ili kuweza kuzitambua sifa za wafuasi wa Imam Mahdi (a.s) ili tuweze kujirejea na kujirekebisha katika sifa zetu.
SIFA YA KWANZA NI ELIMU NA UTIIFU
Wafuasi wa Imam Mahdi (a.s) ni watu wenye kumtambua vyema Mola pamoja na Imam wao na wataingia uwanjani huku wakiwa ni wenye utambuzi wa hali ya juu kabisa.
Imam Ali (a.s) anasema hivi kuhusiana na wafuasi hao: "wafuasi wa Imam Mahdi ni watu waliomuelewa Mola wao kama vile ipaswavo kumuelewa[3]"
Wafuasi wa Imam wana imani na Imamu wao kwa kupitia nyoyo zao zilizojaa utambuzi wa Imam huyo, na kuelewa kwa aina kama hii kuna upana zaidi kuliko kule kumuelewa kwa kupitia jina alama au nasabu, kumuelewa Imamu na kuelewa nafasi yake iliyo juu ni moja kati ya mambo makuu ya kilimwengu, na kuelewa kwa wafuasi wake nafasi yake hii ndio kulikosababisha kuwa na mapendo naye, na kumtii pamoja na kusikiliza amri zake kwa sababu wao wanaelewa ya kwamba maneno ya Imamu ni maneno ya Mwenyeezi Mungu na kumtii yeye ni kumtii Mwenyeezi Mungu.
Mtume Muhammad (s.a.w) akizungumzia sifa za watu hawa amesema hivi:-
"Wao katika kumtii Imamu wao ni wenye jitihada kubwa[4]"
[1] Rejea kitabu Najmu- Thaqib.
[2] Rejea kitabu Safinatul bihaar.
[3] Rejea Muntakhabul athar mlango wa nane juzuu ya pili ukurasa 611).
[4] Rejea kitabu yawmul-khalas, ukurasa wa 223).
MWISHO