MALINGANIO YA MITUME NO.4
  • Kichwa: MALINGANIO YA MITUME NO.4
  • mwandishi: NDUGU ZETU WA KIISLAMU
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 19:39:22 29-6-1403

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

MALINGANIO YA MITUME YA ALLAH (S.W) NO.4

Katika makala iliyopita (makala namba tatu) tulielezea njia walizotumia Mitume na malinganio yao katika kufikisha ujumbe wa Mwenyeezi Mungu kwa walimwengu. katika makala hii vile vile tutaendelea kuelezea njia nyengine walizotumia Mitume katika kutimiza wadhifa wao huo wa kufikisha ujumbe waliopewa na Mola wao Mtakatifu.

*Namna ya kuwalingania watu, ni maneno mazuri yenye hekima yanayoweza kumtoa nyoka pangoni, seuze yawe ni ya akili pia.

Mitume ya Mwenyeezi Mungu ilitumia njia mbali mbali katika kufikisha ujumbe wa Mola wao. miongoni mwa hizo ni:-

2. BISHARA NJEMA

Miongoni mwa njia walizotumia Mitume katika kuwalingania watu ni kuja na bishara njema, bishara njema huwatia wanaadamu furaha, ijapokuwa kuingiwa na hofu ni dalili muhimu inayowafanya wanaadamu wazinduke kutokana na kughafilika kwao, lakini Mitume kwa kuwapa wanaadamu bishara njema imewafanya wanaadamu hao kuwa na shauku ya kufanya matendo mema, na imani zao kupanda kwa daraja ya juu kabisa, katika hali ambayo wanaadamu hao kwa kusikia aya zinazobainisha rehema za Mwenyeezi Mungu, na malipo mazuri watakayolipwa na Mola wao pindi wanapofanya amali njema, watu hao huingiwa na hamu na mapenzi ya kufanya amali hizo njema. Katika sehemu hii tutaelezea baadhi ya bishara njema walizobashiriwa watu na Mola wao:-

2-1. KUWABASHIRIA MAFANIKIO NA USHINDI.

Mitume iliwabashiria watu kutokana na mambo ya ghayb ya Mwenyeezi Mungu, na kuwapa matumaini ya moyo kuwa watashinda katika vita, na hii ilwafanya wao kuingiwa na imani zaidi ya kumuamini Mola wao, kiasi ya kwamba baadhi ya wakati mtu mmoja Muislamu alisimama na kuwa madhubuti mbele na kupingana na makafiri ishirini au zaidi, kama tunavyosoma kuhusiana na vita vya Badri:-

وَمَا جَعَلَهُ اللّهُ إِلاَّ بُشْرَي لَكُمْ وَلِتَطْمَئِنَّ قُلُوبُكُم بِهِ وَمَا النَّصْرُ إِلاَّ مِنْ عِندِ اللهِ الْعَزِيزِ الْحَكِيمِ[1]

Na Mwenyezi Mungu hakufanya haya ila kuwa ni bishara kwenu, na ili nyoyo zenu zipate kutua. Na msaada hautoki isipo kuwa kwa Mwenyezi Mungu, Aliye tukuka, Mwenye nguvu na Mwenye hikima.

Vile vile Mitume ya Mwenyeezi Mungu walipokuwa wakifikisha ujumbe wa Mwenyeezi Mungu kwa watu, waliwaashiria watu baraka watakazozipata pindi wakimtii Mwenyeezi Mungu, na athari watakazoziona pindi watakapokuwa wacha Mungu, na wasighafilike na mali au vyeo vya maadui wa kiislamu, Qur-ani takatifu inasema:-

فَإِذَا بَلَغْنَ اَجَلَهُنَّ فَاَمْسِكُوهُنَّ بِمَعْرُوفٍ اَوْ فَارِقُوهُنَّ بِمَعْرُوفٍ وَاَشْهِدُوا ذَوَيْ عَدْلٍ مِّنكُمْ وَاَقِيمُوا الشَّهَادَةَ لِلَّهِ ذٰلِكُمْ يُوعَظُ بِهِ مَن كَانَ يُؤْمِنُ بِاللهِ وَالْيَوْمِ الآخِرِ وَمَن يَتَّقِ اللهَ يَجْعَل لَّهُ مَخْرَجاً

وَيَرْزُقْهُ مِنْ حَيْثُ لاَ يَحْتَسِبُ وَمَن يَتَوَكَّلْ عَلـٰي اللهِ فَهُوَ حَسْبُهُ إِنَّ اللهَ بَالِغُ اَمْرِهِ قَدْ جَعَلَ اللهُ لِكُلِّ شَيْءٍ قَدْراً[2]

Basi wanapo fikia muda wao, ima warejeeni muwaweke kwa wema, au farikianeni nao kwa wema. Na mshuhudishe mashahidi wawili waadilifu miongoni mwenu. Na simamisheni ushahidi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Hivyo ndivyo anavyo agizwa anaye muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Na anaye mcha Mwenyezi Mungu humtengezea njia ya kutokea.

Na humruzuku kwa jiha asiyo tazamia. Na anaye mtegemea Mwenyezi Mungu Yeye humtosha. Hakika Mwenyezi Mungu anatimiza amri yake. Mwenyezi Mungu kajaalia kila kitu na kipimo chake.

[1] Surat Al-Imrani Aya ya 126

[2] Surat Talaq Aya ya 2-3

MWISHO