IMAM MAHDI NDANI YA RIWAYA ZA KISUNNI
UTANGULIZI
Imani ya ulazima wa kudhihiri suluhisho la ulimwengu huu na kusimamisha dola yake ni imani isiyohusu watu wa dini tu, bali inayajumuisha hata makundi ya kitheolojia na kifilosofia yasiyokuwa ya kidini. Kwa mfano kundi la wapagani wajulikanao kwa jina la Al-Jadliyyah ambalo limefasiri historia kwa kigezo cha kutokuwepo uwiano kinaamini kuwa ipo siku iliyoahidiwa mpishano huo utatoweka na nafasi yake kuchukuliwa na uwiano na amani.1
Kama pia tunavyowakuta baadhi ya wanafikra wasiokuwa wanadini waki- amini ulazima huu, kwa mfano mwanafikra mashuhuri wa kiingereza Bertrand Russell anasema: “Hakika ulimwengu unalingojea suluhisho litakaloukusanya chini ya bendera moja na tamko moja.”2
Na kauli yenye maana hii hii ameisema mfizikia maarufu Albert Einstein kwa kusema: “Hakika haiko mbali siku ambayo ulimwengu wote utatawaliwa na amani na usafi na watu kuwa katika hali ya kupendana na undugu.”3
Ama mwanafikra wa kiayalandi Bernard Shaw yeye katamka wazi mno na kwa undani kuliko uwazi na undani wa hawa wiwili, katika kutoa wasifu wa suluhisho na kuelezea ulazima wa umri wake kuwa mrefu kabla ya kudhihiri kwake amesema: “Hakika yeye ni mwanadamu hai mwenye mwili wenye afya bora na nguvu ya kiakili isiyokuwa ya kawaida. Ni mwanadamu wa hali ya juu kiasi kwamba mwanadamu huyu wa chini anamfikia baada ya juhudi za muda mrefu. Na hakika umri wake utarefuka mpaka avuke miaka mia tatu, na anaweza kunufaika na yale aliyoyaku- sanya ndani ya muda wote wa uhai wake mrefu.”4
Ama upande wa dini za kimungu zenyewe zimeashiria ulazima wa kudhi- hiri suluhisho la ulimwengu, na atakayefuatilia utabiri wa kimungu ndani ya vitabu vya biblia atavikuta vinaelekeza kwa huyu Mahdi ambaye ndiye anaaminiwa na madhehebu ya Ahlul-Bayt (a.s.), kama ulivyothibitisha hilo uchambuzi mbalimbali unaohusu maelezo ya nukuu hizo za utabiri.5
Al-Qadhi As-Sabatwiy amezungumzia moja ya utabiri unaopatikana ndani ya kitabu cha Yoshua kutoka ndani ya Agano la kale ndani ya biblia unaolihusu suluhisho la ulimwengu, akasema: “Maelezo haya yanamzungumzia Mahdi (a.s.).” Akaendelea mpaka akasema: “Shia Imamiyya wamesema: Yeye ndiye Muhammad bin Hasan Al-Askari ambaye alizaliwa mwaka mia mbili na hamsini na tano na mjakazi wa Hasani Al-Askari aitwaye Nargis huko Samrau zama za mtawala Al-Muutamid, kisha akaenda ghaibu muda wa mwaka mmoja6, kisha akadhihiri na kisha akaenda tena ghaibu na hiyo ndio ghaibu kubwa, na baada ya hapo harejei ila pindi Mwenyezi Mungu atakapotaka.
Na kwa kuwa kauli yao iko karibu mno na kile kinachozungumziwa na maelezo haya, na kwa kuwa lengo langu ni kuutetea umma wa Muhammad (s.a.w.w.) bila kujali upendeleo wa kimadhehebu ndio maana nimek- wambia kuwa lile wanalodai Shia Imamiyya ndilo lenye kuoana na maele- zo haya (ya agano la kale).”7
Pia Allamah Muhammad Ridha Fakhrul-Islam ambaye mwanzo alikuwa mkiristo kisha akawa mwislamu na kujiunga na madhehebu ya Ahlul-Bayti naye amefikia kwenye natija hii ambayo aliifikia As-Sabatwiy. Na ame- andika kitabu cha maarifa “Anisul-Aalam” akiwajibu mayahudi na wakris- to, na katika uchambuzi wake amezungumzia utabiri mbalimbali, na mwisho akahitimisha kuwa unaoana na Mahdi bin Hasan Al-Askari (a.s.).8
Hivyo anayechunguza kwa makini ndani ya maelezo hayo ya utabiri anakuta yanatoa wasifu wa suluhisho la ulimwengu usiyooana na mwingine asiyekuwa Mahdi mwenye kungojewa kwa mujibu wa imani ya kambi ya Ahlul-Bayt (a.s.). Hivyo asiyekubali imani hii hawezi kupata mfano halisi unaozungumziwa na utabiri huo, kama tunavyolishuhudia hilo kwenye kauli za wafafanuzi wa Injili wanapozungumzia msitari wa kwanza mpaka wa kumi na saba wa kitabu cha ufunuo wa Yohana sura ya kumi na mbili, wao wametamka wazi kuwa mtu anayezungumziwa na utabiri huu uliyomo ndani ya mistari hii bado hajazaliwa, na hivyo tafsiri yake ya uwazi na maana yake dhahiri imeachwa mpaka mbele na muda usiojulikana ambao ndani yake atadhihiri.”9
Na kuna baadhi ya wanavyuoni wa kisunni wanaamini uchunguzi huo na natija hiyo, kwa mfano ustadhi Said Ayyub ameongoka kwa kusema kuwa mfano halisi unaozungumziwa na misitari iliyotangulia ya kitabu cha ufun- uo wa Yohana ni ule mfano halisi unaoaminiwa na kambi ya Ahlul-Bayt, akasema: “Imeandikwa ndani ya vitabu vya manabii kuwa Mahdi katika matendo yake hamna dosari.” Kisha maelezo haya akayaongezea kwa kusema: “Nakiri hakika mimi nimeyakuta hivyo hivyo ndani ya vitabu vya watu wa kitabu, hakika watu wa kitabu wamefuatilia habari za Mahdi kama walivyofatilia habari za babu yake (s.a.w.w.), na hivyo habari za kitabu cha ufunuo wa Yohana zikaelekeza kwa mwanamke ambaye ndani ya mgongo wake kutatoka wanaume kumi na wawili.” Kisha akaashiria mwanamke mwingine, yaani ambaye atazaa mwanaume wa mwisho ambaye yeye ni kutoka kwenye mgongo wa babu yake. Kitabu kimesema: “Hakika mwanamke huyu atazingirwa na hatari, na alama ya hatari ni kwa jina la “At-Tanin” (joka kubwa). Na ikasema: “At-Tanin alisimama mbele ya mwanamke mwenye kujiandaa kujifungua ili ammeze mtoto pindi tu atakapojifungua.”10
Maana yake ni kuwa utawala ulikuwa unataka kumuua kijana huyu, lakini baada ya mtoto kuzaliwa; Barkel anasema ndani ya ufafanuzi wake kuwa: “Pindi hatari ilipomshambulia, Mwenyezi Mungu alimnyakua mwanawe na kumuhifadhi.” Na maelezo “Mwenyezi Mungu alimnyakua mwanawe.”11 Maana yake ni: “Hakika Mwenyezi Mungu alimpeleka ghaibu mtoto huyu.” Kama ilivyo ndani ya kauli ya Barkel: “Kitabu kime- sema kuwa: “Hakika ghaibu ya kijana itakuwa siku elfu moja na mia mbili na sitini.12” Nao ndio muda wake na alama yake kwa watu wa kitabu.”
Kisha Barkel akasema kuhusu kizazi cha mwanamke wa kwanza kwa ujumla: “Hakika At-Tanin atafanya vita kali pamoja na kizazi cha mwanamke, kama alivyosema ndani ya kitabu: “At-Tanin akamkasirikia mwanamke na akaenda kuweka vita pamoja na kizazi chake kingine, ambao wanahifadhi usia wa Mwenyezi Mungu.”13
Baada ya maelezo hayo yaliyotangulia, ustadh Abu Said Ayyub akasema: “Huu ndio wasifu wa Mahdi na ndio ule ule wasifu wake kwa Shia Imamiyya wafuasi wa Maimamu kumi na wawili.14
Na akaipa nguvu kauli yake kwa maelezo aliyoyaweka pambizoni yaki- husu uonaji wa wasifu wa Mahdi na Mahdi wa nyumba ya Mtukufu Mtume.15
Hivyo uchunguzi mwingi umesisitiza kuwa utabiri unamwashiria Mahdi Al-Muntadhir mwenyewe anayeaminiwa na madhehebu ya Ahlul-Bayt (a.s.). Hebu sasa tuelekee kwenye riwaya za kambi ya Sunni ambazo zime- toka zikimzungumzia Imamu na kitambulisho chake, ili tuone je, zenyewe zimevuka kutoka kwenye anuani mpaka zikafika kuzungumzia utu wake baada ya riwaya za kudhihiri kwake kuwa nyingi mno, au ziliishia kwenye anuani tu?
Jibu ni: Inajulikana wazi kuwa anayeamini kudhihiri na ana yakini kabisa kuwa atatokea lakini hajapambanukiwa ni nani Mahdi aliyeahidiwa zama za mwisho, hatohesabiwa kuwa anamwamini Mahdi kama utakavyo Uislamu, kwa sababu anamwamini Mahdi kama anuani tu, lakini hamwamini mlengwa mwenyewe, ilihali kitendo cha kutofautisha kati ya kumwamini Imam mlengwa na kuamini kudhihiri kwake kinaharibu imani ya Mahdi, ni mfano wa imani ya mtu anayeamini wajibu wa Swala lakini yeye hajui nguzo zake.
Hivyo ili tufikie kumjua Imam Mahdi mwenyewe aliyelengwa na aliye hal- isi kwa kupitia riwaya za kisunni tutalazimika kuugawa uchambuzi katika mambo mbalimbali.
REJEA:
• 1. Buhuth Hawlal-Mahd cha As-Sayyid As-Shahid Muhammad Baqir As-Sadri: 87.
• 2. Al-Mahdi Al-Maw’uud wadaf ’ush-Shubhati An’hu cha As-Sayyid Abdur-Ridha As-Shuhrustaniy: 6.
• 3. Al-Mahdi Al-Maw’uud wadaf ’ush-Shubhati An’hu cha As-Sayyid Abdur-Ridha As-Shuhrustaniy: 6.
• 4. Bernadisho: Abbas Mahmuud Al-Uqad: 124 – 125.
• 5. Rejea kitabu Basharati Ahadayni cha Shaikh As-Sadiqiy, kimetafsiriwa kwa kiarabu kwa jina la “Al-Basharatu Wal-Muqaranatu”.
• 6. Kilichothibiti ni kuwa ghaibu ya Imam Mahdi baada ya kifo cha baba yake ilien-
delea mpaka mwaka wa 69 A.H.
• 7. Al-Barahin As-Sabtwiyyah: Imenukuliwa kutoka kwenye kitabu Kashful-Astar
cha Al-Mirza An-Nuriyyu: 84.
• 8. Basharati Ahadayni cha Muhammad As-Sadiqiy: 232.
• 9. Basharati Ahadayni cha Muhammad As-Sadiqiy: 232.
• 10. Ufunuo wa Yohana 12: 3.
• 11. Ufunuo wa Yohana 12: 5.
• 12. Muda wake umepatikana ndani ya kiebrania kwa kusema: “Atakwenda ghaibu
dhidi ya At-Tanin zama moja, zama mbili na nusu zama.” Rejea Basharati Al- Ahadayn: 263.
• 13. Ufunuo wa Yohana 12: 13.
• 14. Al-Masih Ad-Dajjal: Said Ayyub 379 – 380 imenukuliwa kutoka kwenye Al- Mahdi Al-Muntadhar Fil-Fikri Al-Islamiy: Imetolewa na Markazi Ar-Risalah: 13 – 14.
• 15. Rejea Al-Imam Al-Mahdi Dhimnu Silsilatu Aalamul-Hidayah cha Jumuiya ya kimataifa ya Ahlul-Bayt: 9 – 24.
ITAENDELEA KATIKA MAKALA ZIJAZO