NABII MUSA (A.S) NA SIASA YA KUWAKABILI WATAWALA
  • Kichwa: NABII MUSA (A.S) NA SIASA YA KUWAKABILI WATAWALA
  • mwandishi: NDUGU ZETU WA KIISLAMU
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 4:35:38 3-11-1403

BSMILAHI AR-RAHMANI AR-RAHIIMI.

NABII MUSA (A.S) NA SIASA YA KUWAKABILI WATAWALA

PUNDE tu Nabii Mussa alipoteuliwa kuwa Mtume,  hakuanza kwa kufanya yale mambo ambayo sisi hivi leo huyaona kuwa ndio dini yaani kama vile kuswali, kufunga, kutoa zaka na kadhalika. Bali jukumu la awali alilopewa ni lile la kwenda Ikulu kumkabili Firauni aliyekuwa akitawala kidhalimu.

"...Wakumbushe watu Mola wako alipomwita Musa, akamwambia nenda kwa wale watu madhalimu. (26:10) Na kwa yakini tulimtuma Musa kwa Firauni na Hamana na Karuni (40:24) Nenda kwa Firauni. Bila shaka yeye amepindukia mipaka (20:24) Nendeni kwa Firauni kwa hakika amepindukia mipaka (20:43)

Kwa mujibu wa aya zote hizo, ni sahihi kusema kuwa Nabii Musa alianza kazi ya Utume kisiasa, kwa sababu hicho alichokifanya ndicho kinachofanywa na wanasiasa wa upinzani hivi leo, tofauti tu ni kwamba yeye alifanya hivyo kwa muongozo wa Mwenyezi Mungu. Kwa maana hiyo basi, wanadini ambao ndio warithi wa Mitume ndio wanaopaswa kubeba jukumu alilobeba Musa. Kwa mantiki hiyo, wao ndio hasa wanaotakiwa kuwa mstari wa mbele katika harakati za kuondoa serikali za kidhalimu kwa misingi ya kisiasa.

Lakini jambo la kustaajabisha kuwa baadhi ya viongozi wa dini wamekuwa wakiunga mkono madai ni kuwa dini isichanganywe na siasa! Matokeo yake wakandamizaji wanathubutu hata kusema maneno ya uongo dhidi ya Mitume. Mathalan yule aliyedai kuwa Mtume Muhammad (s.a.w.) hakufundisha siasa Misikitini!

Weledi wa dini lazima wahoji kuwa inakuwaje mtu asiyejua sira ya Mtume (s.a.w.) adiriki kujipa mamlaka ya kumzungumzia Mtume? Huyo lazima asutwe kuwa laiti angeliijua historia ya Mitume, basi angeelewa kuwa misikiti ndiyo ilioanza kuendesha siasa kabla ya CCM. Na kama Mtume angekuwepo, basi wale wote wanaoitwa watawala hivi sasa wangekuwa raia tu wa kawaida chini ya serikali ya Mtume.

Historia ya Mitume inathibitisha kuwa dhima ya dini ni kusimamisha utawala adilifu na wa haki. Ndio maana, katika harakati zao, Mitume walikabiliana na watawala. Ni vema tukirejea kwa kurefu kisa cha ugomvi wa Musa na Firauni ili tuone nafasi na maana ya dini kwa mawanda yake sahihi na kwa mawanda hayo, tuone jinsi dhima ya dini inavyopingana na dhana ya dini iliyojikita vichwani mwa wanadini na wanasiasa walioafikiana kuchora mpaka wa kutenganisha dini na siasa.

Kabla ya kwenda kwa Firauni, kwanza Mussa aliomba apewe msaidizi wa kumsaidia katika uzungumzaji. Akamteua Haruni ambaye kwa mujibu wa historia alikuwa mzungumzaji hodari na mzoefu wa masuala ya kisiasa. Wote wawili wakamwendea Firauni. Baada ya kujitambulisha kwake kuwa wao ni Mitume wa Mola wake na kumfikishia ujumbe waliopewa kuwa awaachie huru wana wa Israili na asiwatese, Firauni akauliza "huyo Mola wenu ni nani? (20:49)
Firauni aliuliza swali hilo kwa sababu yeye mwenyewe pia alijiita mungu, Na 'uungu' huo ndio uliokuwa msingi wa utawala wake wa kisiasa, Kwa kuuliza swali hilo, lengo lake hasa lilikuwa ni kutaka kujua mtazamo wa Musa juu ya madaraka yake. Kwa hiyo jibu la Musa lingemwezesha kung'amua mwelekeo wa Utume wake katika siasa za Misri. Musa alipozieleza sifa za Mungu Muumba ambaye ndiye anayestahili kuabudiwa na kuogopwa, Firauni akauliza swali lingine kuwa kama yeye Musa alipewa ujumbe ule katika kipindi kile, vipi basi kuhusu watu wa karne zilizopita ambao hawakuishi kwa mujibu wa ujumbe huo. (20:5)

Firauni aliuliza swali hili la pili kimtego. Yeye tayari alikuwa na jawabu kuwa, kwa karne nyingi wazee wao walikuwa wakiabudu miungu bandia isipokuwa alitaka tu Musa ajibu kuwa wazee wao walipotea kutokana na jibu hilo, Firauni angeyateka mazingatio ya watu wake kwamba, badala ya akili zao kutafakari hoja nzito za Musa zifikirie matamshi ya Musa dhidi ya wazee wao. Kwa mbinu hiyo, alitaraji angemmaliza Musa mapema ili ule ujumbe wake usipate kusambaa nchini, kwani ingepatikana hoja ya kusambazia propaganda kuwa Musa amewakebehi wazee wao. Mbinu kama hizi mara nyingi zimetumika kuwahadaa watu wenye upeo mdogo wa kufikiri, Hata wapinzani wa Mtume Muhammad, Makka walitumia mbinu za aina hiyo.

Lakini kinyume na matarajio ya Firauni, kwa hekima, Musa alijibu kuwa habari za watu hao wa zamani anazijua Mwenyezi Mungu ambaye ana rekodi ya kila jambo katika kitabu chake na hana udhaifu wa kupoteza kumbukumbu. (20:52) Kama Musa angejibu kuwa watu hao wa zamani walikuwa wapotevu na hivyo watakuwa kuni za Jahanamu lingemsaidia Firauni kufikia lile lengo lake alilokuwa nalo kichwani wakati alipoulizwa swali. Baada ya jibu la Musa kumvurugia shabaha yake, Firauni sasa akamtaka Musa atoe hoja za kuthibitisha ukweli wa madai yake (7:106). Ndipo Musa alipoonesha miujiza, Kwanza alitupa fimbo yake ambayo iligeuka nyoka (7:107) na kisha akatoa mkono wake ambao ulikuwa unang'ara (7:108).

Kuona miujiza hiyo, Firauni akachanganyikiwa na kuuliza kwa hamaki, "kumbe wewe Musa umekuja kututoa nchini mwetu kwa nguvu za uchawi wako (20:57). Hapa Firauni alitumia mbinu nyingine ya kujinusuru na hatari ya Musa. Badala ya kusema, umetujia na miujiza, yeye akasema umetujia na uchawi. Lengo lake lilelile la kuvuruga mazingatio ya watu waliokuwa wakitazama kwamba waione ile miujiza kama uchawi tu ambao hata watu wengine wa kawaida wengeweza kuufanya. Kwa mbinu hiyo, angevunjilia mbali hoja ya ile ya miujiza ambayo ingethibitisha utume wa Musa na hivyo kuwafanya watu wamkubali Mungu aliyemtuma mtume huyo jambo ambalo lingeshusha hadhi ya 'uungu' ya Firauni na kumpotezea nguvu zake za kisiasa na hatimaye madaraka yake.

Ifahamike kuwa, Firauni alikwishabaini kuwa Musa alikuwa na dalili za Utume, kwa maana hiyo, alikwishadhihirikiwa na ukweli wa yale yote aliyokuwa akiyasema Musa. Lakini alikuwa anakwepa kukiri kwa hofu ya kupoteza ufalme wake. Ni sawa kabisa na watawala wa hivi leo, kuwa wanakubali nyoyoni kwamba mwanasiasa fulani anasema ukweli lakini wanakwepa kukiri anachosema kwa sababu ya madaraka yao, Watajitahidi kutumia kila mbinu kuwazubaisha wananchi wenye uoni hafifu wasimkubali mtu huyo hatari kwa maslahi yao.

Maelezo ya historia ya Musa katika Qur'an inaonesha kuwa Musa alipelekwa kwa wakuu wa Misri yaani Firauni, Amana na Karuni akiwa na muelekeo wa wazi wa kupiku mamlaka yao yaliyosimamia juu ya msingi wa dhana ya uungu bandia. Kwanza, kule kujitokeza kwa Musa mbele yao bila hofu licha ya kukabiliwa na jinai ya kuua mtu wa Taifa la Firauni. Musa alilazimika kukimbilia nchi nyingine kujificha baada ya Firauni kutoa amri akamatwe. Sasa iweje mtu huyo aibuke na kwenda moja kwa moja Ikulu si kwa minajili ya kuomba msamaha bali kwa lengo la kumtaka Rais na Mawaziri wake wamtambue kuwa yeye ni Mtume wa Mungu Muumba wa ulimwengu na kwamba wao watawala waache sheria na kanuni au sera zao na badala yake wafanye vile atakavyo Mungu.

Ujasiri huo tu ulitosha kuwa ishara ya utume wa Musa. Isingelikuwa rahisi kwa mtu wa kawaida tena basi mwenye hatia ya mauaji kuwakabili watawala namna hiyo. Isitoshe taifa la Musa lilikuwa dhaifu au tuseme nyonge chini ya utumwa hivyo hatakama Musa angekamatwa na kuhukumiwa kifo, lisingeweza kumtetea kwa namna yoyote ile. Na huenda baadhi yao wangemlaumu kwa jaribio hilo hatari!

Kwa hali hiyo, hata kabla ya kuonesha miujiza, Firauni na watu wake walikwishagundua kuwa Musa alikuwa na nguvu fulani kubwa nyuma yake iliyomfanya ajiamini kiasi hicho. Pili, kila muujiza alioonesha Musa ulitofuatiana kabisa na uchawi, Miujiza yote ilidhihirisha nguvu isiyo ya kawaida kwa sababu uchawi hauwezi kugeuza fimbo kuwa nyoka halisi. Ndio maana Firauni na washirika wake wakasema kuwa Musa ni "mchawi" mkubwa (40:24), (7:109). Jina "mchawi mkubwa" kama ilivyokwishaeleza lilificha ukweli kwa sababu za kisiasa. Na tatu, ule uzungumzaji wa Musa uliojaa hekima na hoja zinazoingia akilini nao pia ulidhirihisha ukweli wa maneno ya Musa kuwa yeye ni Mtume. Firauni alikuwa anamjua Musa vizuri sana kwa sababu aliishi nyumbani kwake. Kwa hiyo aliweza kugundua kuwa Musa hakuwa na uwezo wa kuzungumza hivyo kabla ya hapo.

Baada ya Musa kuitia msukosuko serikali ya Firauni, mtawala huyo akataka ushauri kwa washirika wake (26:35). Wakamshauri kuwa akabiliane na Mussa kwa nguvu za uchawi. Hivyo, wakamtaka atume watu wapigao mbiu ya mgambo wakusanye wachawi wote wakubwa yaani 'magwiji' ili kumkabili Musa (26:36-37). Ikumbukwe kuwa kulikuwa na mamia ya wachawi katika nchi hiyo ambao mara nyingi walikuwa wakifanya mazingaombwe kwa lengo la kujipatia zawadi na tuzo. Kwa maneno mengine uchawi, kwa watu hao ulikuwa kama ajira. Ndio maana walipoitwa kwa Firauni wakauliza kuwa wangepata ujira gani kama wangemshinda Musa. (7:113).

Kama ilivyodokezwa awali kuwa, Firauni alikwishaiona hatari ya Musa kisiasa kwamba miujiza ya Musa ingewateka sio tu watu wake wa karibu bali hata wananchi wa kawaida pia. Ndio sababu akakwepa kuita miujiza na badala yake akaiita uchawi na akamwita Musa mchawi stadi (26:34). Kauli hizo zililenga kuwapotosha watu ili waone kuwa mbona hata watu wengine wanaweza kufanya uchawi. Kwa hiyo Musa aonekane mchawi tu kama wachawi wengine.

Mbali na propaganda hiyo, Firauni alieneza propaganda kwa wananchi kuwa Musa amewakejeli wazee wao wa zamani kuwa walikuwa wapotevu na walistahili kuangamizwa. Hivyo wajihadhari naye, sio Mtume bali ni mchawi anayetaka kutumia uchawi wake kukutoeni nchini mwenu. Anataka wana wa Israeili wanyakue tena madaraka kama ilivyokuwa wakati wa Yusuf. Sasa lengo la Firauni na washirika wake lilikuwa ni kuwakusanya wananchi wote nchini ili waone ule uwezo wa wachawi wakubwa ambao alitaraji ungevuruga shabaha ya Musa. Firauni aliamini kuwa mara wale wachawi watakapoyazuga macho ya watazamaji yaone fimbo zao kuwa ni nyoka, athari za muujiza wa Musa zingefutika vichwani mwa watu.

Ni kwa sababu hiyo, walikubaliana na Musa kuwa mpambano huo ufanyike siku ya sikukuu ili watu kutoka sehemu mbalimbali washuhudie. Na ufanyike mahala pa wazi, asubuhi kweupe ili watazamaji waone vizuri. Kutokana na uzito na umuhimu wa pambano hilo, Firauni alitoa ahadi nono kwa wachawi wake kwamba wangepata cheo cha kuwa karibu naye (7:114). Firauni na washirika wake wakaliona pambano hilo kama karata yao muhimu ya kumshinda Musa ili kunusuru madaraka yao, hivyo watu wakahamasishwa mno kuhudhuria pambano hilo. Walitangaziwa propaganda kuwa Musa "anataka kuwatoa katika nchi yao" (20:57). Pili "anataka kuvuruga mfumo wao wa maisha na kuleta matata katika nchi". (40:26). Tatu mchawi anayetaka kundoa sera zao zilizokuwa bora kabisa (20:63).
Kwa hiyo basi, nusura ya dini yao na nchi yao ilitegemea nguvu za wachawi wao. Yaani nchi yao pamoja na utaratibu wao wa maisha vitasalimika iwapo tu upande wao utashinda. Hiyo ni kusema kuwa kama Musa akishinda na watawala kupoteza madaraka yao ndio basi tena mfumo wa maisha utabadilishwa na kwa ajili hiyo, utamaduni wao, sanaa zao, ustaarabu wao na vizazi vyao vyote vitaangamia. Kwa ujumla propaganda zote hizo zililenga kuwashawishi watu waiunge mkono serikali katika mapambano yake dhidi ya Musa. Hata watawala wa leo hutumia propaganda kama hizo kuwahadaa wananchi. Propaganda za amani na utulivu, umoja na mshikamano wa kitaifa, kusamehewa madeni, kudumisha muungano ndizo zinazotumiwa na watawala wa nchi yetu ili kuwashawishi wananchi waiunge mkono serikali katika kampeni zake dhidi ya wapinzani.

Watu wa Firauni walipouona ukweli kamwe hawakuyumbishwa hata na vitisho vya Firauni (26:50-51). Fundisho kutoka historia ya Musa lazima lizingatiwe na wale wanaojiita wanadini pamoja na wale waitwao wanasiasa. Hakuna mtu yeyote miongoni mwetu anayeweza kuthubutu kudai kuwa yeye anaijua dini zaidi ya Musa. Kinyume chake sisi ndio tunaojifunza dini kutoka kwa Musa na Mitume wengine. Sasa basi, ile dhana ya kutenganisha dini na siasa haionekani katika historia ya Mtume Musa. Kama tulivyokwishaona, wakati Musa anapewa Utume, jukumu la kwanza alilopewa sio kujenga Msikiti bali kwenda kumkabili mtawala aliyekuwa akiwakandamiza wananchi.

Kwa maana hiyo basi, wajibu wa wacha Mungu ambao wamechukua nafasi ya Musa ni kuwakabili hawa watawala wa leo wasiozingatia haki. Katika harakati za kisiasa, ni wajibu kwa Masheikh, Maimamu, Maulamaa na Maustadhi kuwa mstari wa mbele kupigania utawala wa kiadilifu. Ni dhambi kukaa kimya au kuwaunga mkono wale wanaotawala kidhalimu. Mtu yeyote anayesema dini itenganishwe na siasa, basi huyo hajui dini wala siasa.

MWISHO