NABII ISA (A.S)
  • Kichwa: NABII ISA (A.S)
  • mwandishi: NDUGU ZETU WA KIISLAMU
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 7:24:1 24-8-1403

BSMILAHI AR-RAHMANI AR-RAHIIMI

NABII ISA (A.S)

Tarehe 25 Disemba inasadifiana na siku ya kuzaliwa Nabii Issa Masiih amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake. Kuzaliwa kwa mtukufu huyu kulihuisha moyo wa udugu, imani, upendo na mahaba kati ya wanadamu. Issa Masiih (as) alizaliwa katika kizazi kilichokuwa mashuhuri kwa usafi na utukufu. Alitumwa kuondoa ujinga na dhulma na kueneza nuru ya imani, maarifa na upendo baina ya Banii Israel. Bibi Maryam mtakasifu, mama yake Nabii Issa (as) alipopata habari kuwa ni mja mzito, alishikwa na mshangao mkubwa na huzuni na baadaye kidogo akajiwa na bishara njema kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Malaika wa wahyi na ufunuo alimwendea na kumwambia: Ewe Maryam! Mola wako amesema kazi hii ni nyepesi mno kwangu, ili tumfanye muujiza kwa watu na rehema kutoka kwatu na jambo hilo limekwishahukumiwa". (Maryam-21)

Nabii Issa ambaye alizaliwa kwa muujiza wa Mola Muumba alitumwa akiwa na ujumbe wa nuru na mwangaza kutoka kwa Mola wake. Mwenyezi Mungu alizungumza na Mtume wake mteule Issa akisema Ewe Issa! Mimi ni Mola wako Mlezi. Mungu Mmoja niliyeumba kila kitu. Nitaje na kunikumbuka na unipende mimi rohoni mwako. Ewe Issa! Wewe ndiye Masiih kwa amri yangu mimi. Utaumba vitu kutokana na udongo kwa ruhusa yangu na kuhuisha wafu kwa idhini yangu. Ewe Issa! Umebarikiwa utotoni na ukubwani na utakuwa na baraka popote utakapokuwa. Nitegemee mimi ili nikutosheleze." Katika aya zake nyingi Qur'ani tukufu inazungumzia na kutoa picha ya maisha ya Mitume na Manabii wa Mwenyezi Mungu. Kwa mujibu wa kitabu hicho kitukufu, Mitume wote walitumwa kuja kuwaongoza wanadamu kwenye tauhidi na imani ya Mungu Mmoja, kusimamisha uadilifu na kupambana na dhulma.

Nabii Issa Masih amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake ni miongoni mwa Mitume adhimu wa Mwenyezi Mungu waliotajwa na kuzungumziwa mno katika aya za Qur'ani Tukufu. Mtume huyo alipatwa na mashaka na tabu nyingi katika njia ya kuwaongoza wanadamu na kuwaondoa katika giza la ujinga, dhulma na upotofu. Aya za Qur'ani zinamtukuza Mtume huyo mkubwa kwa kutaja sifa zake mbalimbali kama "Neno la Mungu", Mteule, "Mja Mwema" Mtenda Wema" na Mtoa Bishara Njema". Issa Masiih ni miongoni mwa Mitume waliofundishwa kitabu na hikima na Mwenyezi Mungu na kufanywa aya na dalili yake Mola Muumba. Nabii Issa (as) alizaliwa bila ya kuwa na baba. Qur'ani Tukufu inakutaja kuzaliwa kwake kuwa ulikuwa muujiza na hikma ya Mwenyezi Mungu. Aya nyingine kadhaa za kitabu hicho zinataja na kuzungumzia maisha na mwenendo mwema wa mtukufu bibi Maryam, mama yake Issa Masih. Zinamtaja mwanamke huyo mwema kuwa alikuwa mtakasifu na miongoni mwa wanawake bora duniani.

Nabii Issa Masiih alifanya kazi kubwa kurekebisha mafundisho ya Nabii Mussa ambayo yalikuwa yamepotoshwa na kuchanganywa na uzushi kadiri muda ulivyopita. Aliweka wazi opotofu na uzushi huo kwa maneno na matendo yake na akapambana na dhulma na uonevu wa zama zake. Hata hivyo mtukufu huyo, kama walivyokuwa Mitume wengine wa Mwenyezi Mungu, alipingwa na kupigwa vita na wapinzani wa haki na uadilifu. Mabeberu na wahalifu wa zama hizo walimkadhibisha Nabii Issa na kumfanyia maudhi ya aina mbalimbali. Hata hivyo aliendelea kulingania ujumbe wa Mola wake Muumba licha ya njama na mashaka makubwa aliyokabiliana nayo. Daima alikuwa akisema: "Ole wenu ninyi mnaojiweka mbali na pepo kwa sababu ya dunia isiyokuwa na thamani na matamanio maovu ambao mmesahau siku ya kufufuliwa." Japokuwa masahaba wa Nabii Issa waliokuwa wakijulukana kwa jina la Hawariyyun walikuwa wachache, lakini walikuwa watu bora zaidi wa zama zao.

Sala na salamu za Mwenyezi Mungu ziwe juu ya Nabii Issa, Mtume aliyetoa bishara ya rehema, amani na uadilifu. Sala na salamu ziwe juu yake wakati alipozaliwa na atakaporejea kwetu katika zama za akheri zamani. Maulidi ya mwaka huu ya Nabii huyo Mtukufu wa Mwenyezi Mungu imesadifiana na siku za Muharram na kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume wetu mtukufu Imam Hussein (as), shakhsia iliyobadili historia ya Uislamu na inayokumbukwa kila mwaka katika kipindi kama hiki kama mrekebishaji na kiongozi wa mageuzi makubwa katika historia ya mwanadamu. Kama alivyokuwa Nabii Issa Masiih, mjukuu huyu wa Mtume Muhammad (saw) alipamba ukurasa wa historia kwa mapambano ya kupigania uhuru, haki, uadilifu na thamani za kibinadamu. Babu yake ni Mtume wa mwisho wa Mwenyezi Mungu, mama yake ni Bi Fatima, mbora wa wanawake wote duniani na baba yake ni Imam Ali bin Abi Twalib, Simba wa Mungu na Imamu wa mashariki na magharibi. Imam Hussein na Nabii Issa Masiih wanakutana kwanza kwa kuwa mama zao wote wawili Bi Maryam na Bi Fatima Zahra ni wanawake bora kuliko wote ulimwenguni. Hussein (as), kama alivyokuwa Issa Masiih, alikuwa mashuhuri kwa kuwapenda wanadamu na mwingi wa huruma kwa maskini na wasiojiweza. Alikuwa akiketi chini na kula chakula pamoja na watu maskini na akisema: "Mwenyezi Mungu hawapenzi watu wenye kiburi". Imam Hussein alikuwa na masahaba wachache kama Hawariyyun wa Nabii Issa (as). Hata hivyo walipeperusha na kushika bendera ya kupigania haki na uadilifu. Wote wawili walijitolea katika njia hiyo na kulingania watu wa zama zao imani ya tauhidi na kumpekesha Mwenyezi Mungu bila ya kuogopa tawala dhalimu za wakati huo. Imam Hussein aliizindua jamii yake akisema: "Hivi kwani hamuoni kuwa haki haitendeki na batili inaendela kutawala?

Misimamo inayofanana ya Imam Hussein na Nabii Issa (as) imewafanya Wakristo wengi wenye fikra huru kudurusu kwa kina sira na mwenendo wa mjukuu huyo wa Mtume Muhammad (saw). Antoine Bara ni miongoni mwa waandishi mashuhuri wa Kikristo ambaye baada ya uchunguzi wa miaka mingi ameandika kitabu alichokipa jina la "Hussein katika Fikra za Kikristo". Kitabu hicho ni cha aina yake hususan kwa kuzingatia kuwa, kimeandikwa na Mkristo kuhusu Imam Hussein (as). Hadi sasa kitabu hicho kimechapishwa katika lugha hai 17 duniani na kufanyiwa mtihani wa daraja na uzamivu katika vyuo vikuu vitano vya kimataifa. Katika kitabu hicho Antoine Bara anamtaja Imam Hussein kuwa ni Johari ya milele ya dini za mbinguni na kuhitimisha kitabu hicho kwa kuandika: "Hussein atabakia katika roho yangu". Anasema, kuna mambo mengi ya kufanana kati ya Imam Hussein na Nabii Issa Masiih na zaidi ni katika mwenendo, maneno na misimamo yao. Anasema: Nabii Issa amesema: "Wakati moto unapotokea kwenye nyumba moja huzagaa kutoka nyumba hadi nyingine na kuteketeza nyumba nyingi, iwapo moto wa nyumba na kwanza hautazimwa. Hivi ndivyo ilivyo dhulma, iwapo itazuiwa hatatokea dhalimu mwingine na kufuatwa na watu".

Antoine Bara anasema, hivi ndivyo alivyosema pia Imam Hussein na akakabiliana kivitendo na dhulma na madhalimu. Mwandishi huyo Mkristo anasisitiza kuwa rijali hao wawili wa Mwenyezi Mungu walikhitari njia ya haki na kujitolea katika njia hiyo kwa irada yao wenyewe. Anamtaja Imam Hussein kuwa ni shahidi aliyejisabilia yeye, familia na masahaba zake 70 kwa ajili ya kutetea itikadi, haki, uhuru na dini ya babu yake na kwa msingi huo hakuwa kiongozi wa Waislamu pekee, bali kinara wa wapigania haki kote duniani. Antoine Bara anataja baadhi ya vipengee vya Injili vinavyosema kuwa Nabii Issa alitembelea ardhi ya Karbala na akawaambia Bani Israel kwamba, mtu yeyote atakayemuona Hussein anapaswa kumsaidia. Mwandishi huyo anasisitiza kuwa sehemu yenye thamani kubwa zaidi katika shakhsia ya Imam Hussein ni harakati yake ya kihamasa na kimapinduzi. Anamnukuu Imam akisema mwanzoni kabisa mwa harakati yake kwamba: "Sikusimama kupambana na Yazid kwa sababu ya matamanio ya kinafsi, ufisadi au kufanya dhulma, bali kwa ajili ya kufanya marekebisho katika umma wa babu yangu. Ninataka kuamrisha mema na kukataza mabaya na kuhuisha mwenedo wa babu na baba yangu.." Bara anasema, moyo huo wa kimapinduzi unaweza kufanya miujiza katika dunia ya leo na kuanzisha harakati kubwa ya kupigania haki na uadilifu. Sala na salamu za Mwenyezi Mungu ziwashukie wanadamu wote wateule waliopigania uhuru, uadilifu na haki hususan Nabii Muhammad, Issa Masiih na mjukuu wao Hussein bin Ali bi Abi Twalib (as).

MWISHO