HOJA ZA MAULIDI YA MTUME (S.A.W.W)
Maulidi ni Kiswahili cha neno la Kiarabu, mawlid. Neno hili lina maana ya "mazazi" au "kuzaliwa kwa…" (birthday). Kwa kawaida, linapotumiwa na Waislamu, huwa na maana ya siku aliyozaliwa Mtume Muhammad (s.a.w.w.), au hafla ya kuisherehekea siku hiyo.
Waislamu wa ulimwengu mzima, ifikapo tarehe 12 ya Mfungo Sita (Rabiul Awwal), husoma maulidi na kuisherehekea siku hiyo kwa furaha kubwa. Sherehe hizo, kwa dasturi, haziishii tarehe hiyo tu, bali huendelea hata kwa miezi miwili mitatu baada ya hapo. Hili huwa ni kwa sababu ya Waislamu wa kila nyumba, kila mtaa, kila mji na kila nchi kutaka kushiriki katika sherehe hizo na kupata baraka zake. Vile vile huwapa Waislamu nafasi ya kutembeleana na kushirikiana katika sherehe hizo - jambo ambalo lisingewezekana lau watu wote wangeliamua kuzifanya sherehe hizo siku hiyo hiyo moja tu.
Kwa nini kusoma maulidi?
Waislamu husoma maulidi kwa sababu mbalimbali. Kati ya hizo ni: (i) kuikumbuka na kuitukuza siku aliyozaliwa mbora wa viumbe vyote, aliyetutoa vizani na kututia kwenye nuru; (ii) ni njia moja ya kutoa shukrani zetu kwa neema hiyo; (iii) katika sherehe hizo, hupatikana fursa ya kukumbushana maisha ya bwana mkubwa huyo na mafunzo yake; (iv) hupatikana fursa ya Waislamu wa madhihabi na mataifa mbalimbali kushirikiana na kuziweka kando hitilafu zao; na (v) mikusanyiko hiyo huleta athari kwa wasio Waislamu ya kuupenda Uislamu, na hata kusilimu.
Wanaopinga na sababu zao
Lakini, hata hivyo, kuna baadhi ya Waislamu -- japokuwa wao si wengi kama wanaoyasoma -- ambao hupinga kusomwa maulidi; na hutoa sababu zao. Kati ya sababu hizo ni: (i) maulidi hayakuwako zama za Mtume Muhammad (s.a.w.w.). Basi kwa nini yazuliwe sasa? (ii) hayakusomwa na maswahaba wala waandamizi wao. Kama kweli yangelikuwa ni sawa kuyasoma, bila shaka mabwana wakubwa hao wangelikuwa ni wa mbele kufanya hivyo; (iii) kuweka ada ya kusoma maulidi ni kuigiza Wakristo walioweka siku ya Krismasi; na Mwislamu haruhusiwi kufanya hivyo; (iv) kwenye sherehe za maulidi hufanywa baadhi ya mambo ambayo ni ya munkar (yanayochukiza, bali ni haramu kamwe, katika sharia ya Kiislamu); na (v) hakuna ushahidi wowote, wa Qur'ani wala Hadithi za Mtume Muhammad (s.a.w.w.), unaothubutisha usawa wa kuyasoma maulidi, sikwambii kuyatilia nguvu.
Kwa nguvu ya hujja hizo, mara nyingi viongozi wa wanaopinga maulidi huwaonyesha wafuasi wao kuwa wale wanaosoma maulidi ni watu waliopotea kwa "kuzua" mambo yasiyo na msingi katika dini yetu hii. Jambo hili limeleta mchafuko -- unaofufuka aghalabu kila ifikiapo miezi ya kusoma maulidi -- ambao unahatarisha umoja na masikizano, sio baina ya Waislamu wa madhihabi mbalimbali peke yao, bali hata wale wa madhihabi mamoja!
Mchafuko huu huzidi kukua kwa sababu ya lugha kali inayotumiwa na pande zote mbili -- za wanaounga na wanaopinga maulidi -- katika kutetea misimamo yao; na hilo haliwezi kusaidia katika kutatua usawa uko wapi. Liwezalo kutatua hitilafu hii ni kuijadili ki-ilimu na kwa lugha nzuri ya kuhishimiana. Na hilo ndilo nililokusudia kulifanya, kuanzia makala yanayofuatia haya, Inshallah.
HUJJA ZA WAPINZANI NA MAJIBU YETU
Hujja yao ya kwanza ni kwamba:
maulidi hayakuwako zama za Mtume Muhammad (s.a.w.w.) Kwa hivyo, kuyaleta baada ya yeye kufariki dunia, ni bid'a (uzushi). Na kila bid'a, kwa maneno yake mwenyewe Bwana Mtume (s.a.w.w.), ni upotevu. Kwa hivyo, kila anayesoma maulidi amepotea!
MAJIBU YETU:
Ni kweli kwamba maulidi, hivi tunavyoyasoma, hayakuwako zama za Mtume Muhammad (s.a.w.w.). Lakini si kweli kwamba, kulifanya kila ambalo halikuwako zama hizo, ni upotevu. Kama ni hivyo, basi bila shaka Waislamu wote leo -- wakiwamo wanaopinga maulidi -- wangelikuwa wamepotea kwa kuwa (katika zama zao mbalimbali) wamefanya, na wanaendelea kufanya, mambo ambayo hayakuwako zama za Bwana Mtume (s.a.w.w.)!
Kwa mfano, katika zama za Bwana Mtume (s.a.w.w.), misikiti haikuwa ikitandikwa chochote (watu wakisujudu juu ya mchanga); lakini leo inatandikwa majamvi, busati na mazulia! Kiwanja kitakatifu cha Al-Kaaba kilikuwa ni mchanga mtupu na mawe; lakini leo kimetandikwa marumaru! Watu walikuwa wakenda kuhiji kwa kupanda ngamia au majahazi; lakini leo wanakwenda kwa ndege, meli za kisasa na mabasi ya anasa (luxury)! Watu, walipokuwa wengi msikitini, walikikhutubu kwa kupaza sauti zao; lakini leo wanatumia vipaza sauti (loud speakers)! Misahafu ilikiandikwa kwa mkono, juu ya ngozi na mifupa, na kutolewa nakala chache; lakini leo inachapwa kwa mashini, juu ya karatasi za fakhari, na kutolewa nakala mamilioni kwa mamilioni!
Lakini hakuna anayesema -- hata hao wanaopinga maulidi hawasemi -- kwamba Waislamu waliobuni mambo hayo wametuletea bid'a au wamepotea. Kwa nini? Kwa sababu kwao wao, na kwa wanaosoma maulidi, uzushi wa aina hiyo si bid'a; sio alioukusudia Bwana Mtume (s.a.w.w.). Alioukusudia yeye ni ule wa kuzua jambo katika dini hii ambalo halitokani nayo (maa laysa minhu). Hilo ndilo lililo wazi kutokana na Hadithi mashuhuri ya Bwana Mtume (s.a.w.w.) inayosema: "Yoyote atakayezua, katika dini yetu hii, jambo ambalo halitokani nayo, litarudishwa (litakataliwa)."
Ukiitaamali vizuri Hadithi hiyo, itakudhihirikia kwamba Bwana Mtume (s.a.w.w.) hakutuzuia kuzua (kubuni), katika dini hii, kila ambalo halikuwako zama zake. Kama angelitaka kutuzuia hivyo, Hadithi hiyo isingelisema hivyo, bali ingelisema hivi: "Yoyoye atakayezua jambo katika dini yetu hii, litakataliwa." Na lau ingelisema hivyo, basi yote yale tuliyoyataja hapo juu yasingeliruhusiwa; yangelikuwa bid'a.
Lakini Hadithi haikusema hivyo. Ilivyosema ni: "Yoyote atakayezua … ambalo halitokani nayo, litakataliwa." Kwa kuongeza kifungu cha maneno tulichokichapa kwa italiki (yaani "ambalo halitokani nayo"), ni wazi kwamba Mtume Muhammad (s.a.w.w.) hakukusudia kuwazuia Waislamu kufanya kila ambalo halikuwako zama zake. Alilolikusudia ni kutuachia wazi mlango wa kubuni mambo katika dini hii bora tu yawe yanatokana nayo.
Sasa suali hapa ni: jee, maulidi si katika mambo yanayotokana na "dini hii", hata kama hayakuwako zama za Bwana Mtume (s.a.w.w.)? Majibu yetu ni: Maulidi, na yaliyomo maulidini, si mageni na "dini hii", bali yanatokana nayo, kama tutakavyobainisha kwa urefu zaidi katika majibu yetu ya hujja Na. (v) ya wapinzani wake inshallah. Kwa hivyo, kuwa tu jambo halikuwako zama za Mtume Muhammad (s.a.w.w.) si hujja ya kuwazuia Waislamu kulifanya. Wanalozuiliwa Waislamu kulifanya ni kuzua jambo na kulifanya ni dini hali ya kuwa halina asili na dini. Na maulidi si hivyo!
Katika hoja yao ya pili wanasema:
Maulidi hayakusomwa na maswahaba wala waandamizi wao (taabi'in). Kama kweli yangelikuwa ni sawa kuyasoma, bila shaka mabwana wakubwa hao wangelikuwa ni wa mbele kufanya hivyo.
MAJIBU YETU:
Hakuna Mwislamu yoyote anayekataa kuwa maswahaba ni watu watukufu. Wala hakuna anayekataa kuwa wao ndio kiungo chetu sisi na Bwana Mtume (s.a.w.w.). Lakini, pamoja na utukufu wote huo, wao walikuwa ni binadamu; hawakuwa ni ma'asumin. Walikiweza kufanya jambo, wakaswibu (wakapata); kama ambavyo walikiweza kufanya jambo, wakakosea. Na mifano ya yote mawili hayo ni mingi katika historia yao.
Kwa hivyo, kuwa tu jambo fulani halikufanywa na maswahaba, haliwi ni hujja sahihi ya kuwazuilia Waislamu kulifanya jambo hilo. Hujja ya pekee iliyo sahihi ni iwapo lile ambalo hawakulifanya wao, waliacha kulifanya kwa sababu ndivyo alivyoamrisha Mwenyezi Mungu na Mtume Wake (s.a.w.w.), au waliacha kulifanya kwa sababu linapingana na maamrisho ya Mwenyezi Mungu na Mtume Wake (s.a.w.w.). Ikiwa walifanya hivyo ndipo jambo hilo litakapokuwa ni hujja; lakini si kwa sababu ya kuwa halikufanywa na maswahaba, bali ni kwa sababu tu ya kuwa ndivyo alivyoamrisha Mwenyezi Mungu na Mtume Wake (s.a.w.w.), au ni kwa sababu tu ya kuwa linapingana na mafunzo ya Mwenyezi Mungu na Mtume Wake (s.a.w.w.) -- na hivyo ndivyo Kiislamu.
Kwa hivyo si sawa kuyapinga maulidi kwa sababu tu hayakusomwa na maswahaba na waandamizi wao. La sawa ni kuyapinga kwa sababu tu yamekatazwa na Mwenyezi Mungu au Mtume Wake (s.a.w.w.), au yanapingana na maamrisho yao. Na hilo, mpaka hivi sasa, wapinzani wa maulidi hawajaweza kulithubutisha.
Tunasema hivyo kwa sababu, mmoja kati ya misingi muhimu ya sharia ya Kiislamu, inayokubaliwa na wanazuoni wa wanaosoma maulidi na wale wa wanaopinga maulidi, ni kwamba -- tunapokuja kwenye mambo kama ya maulidi, ujenzi wa msikiti, mavazi, na kadhaalika -- kila kitu ni halali mpaka kithubutishwe kuwa ni haramu. Kwa hivyo, kwa msingi huu, uharamu wa maulidi haitaki uthubutishwe na wanaoyasoma, bali inataka uthubutishwe na wanaoyapinga. Wala wasilithubutishe hilo kwa vichwa vyao (Sura 16:116), bali kwa kutoa ushahidi wa maneno ya Mwenyezi Mungu au Mtume Wake s.a.w.w. (Sura 4:59). Na hilo pia, mpaka dakika hii, wapinzani wa maulidi hawajaweza kulifanya.
Mwanzo mwanzo wa kuzuka madhihabi haya ya kupinga maulidi, wafuasi wake waliyapinga mambo mengi yaliyozuka katika zama zao. Kati ya mambo hayo ni kuvuta sigara, kupiga simu ya mdomo (telephone), kujiwekea kashida mbele ya mtu anaposwali, kumwamkia mtu kwa: "Umeamkaje?", kupana mikono baada ya swala, kutandika busati misikitini, na hata kuvaa nguo yenye thamani inayozidi dirhamu 100 (mia)! Yote hayo waliyapinga kwa hujja ya kuwa hayakuwako zama za Mtume (s.a.w.w.), na kwamba hayakufanywa na maswahaba na waandamizi wao! Lakini, baada ya kutambua walikosea wapi, walirudi nyuma, wakayakubali yote hayo. Kwa maneno mengine, yakawa sio bid'a tena! Leo, kwa hujja hizo hizo, waandamizi wao wameanza kusema vibula vivunjwe! Kesho watasema na minara nayo ivunjwe! Kesho kutwa watasema mimbari za mbao au za mawe, nazo pia ziondolewe, zirudishwe zile za vigogo vya mtende; hata vya mnazi havitafaa! Baada ya hapo ni nini kitakachowazuia wasitwambie tuondoe banka (panka) misikitini, turudi kujipepea kwa nguo zetu kama ilivyokuwa zama za Bwana Mtume (s.a.w.w.)? Au twende hijja kwa ngamia au farasi badali ya ndege? Au ni lipi litakalowazuia kutuamrisha kuisoma Qur'ani katika ngozi na mbao, kama ilivyokuwa zama za Bwana Mtume (s.a.w.w.) na maswahaba, badali ya hii miswahafu mizuri mizuri tuliyonayo?
Ni matumaini yetu kwamba, kama ambavyo watangulizi wao walirudi nyuma na kuyakubali yale waliyoyafanya ni bid'a mwanzo, wao nao watafuata nyayo zao, wayaone maulidi, na mengine kama maulidi, kuwa sio bid'a iliyokatazwa na Mtume Muhammad (s.a.w.w.). Alhamdulillaah, baadhi yao wameanza kuona hivyo na kufanya sherehe za mazazi ya Bwana Mtume (s.a.w.w.). Lakini badali ya kuyaita maulidi, huyaita seera!
Hoja yao ya tatu ni kuwa:
kuweka ada ya kusoma maulidi ni kuigiza Wakristo walioweka siku ya Krismasi; na Mwislamu haruhusiwi kufanya hivyo. MAJIBU YETU: Mwislamu hazuiliwi kufanya jambo kwa sababu tu linafanywa na Mkristo au kafiri yoyote mwengine. Analozuiwa ni kufanya jambo kama linalofanywa na Mkristo, au kafiri yoyote mwengine, linapokuwa linakwenda kinyume na mafunzo ya Kiislamu; na hilo sio linapofanywa na Mkristo au kafiri yoyote tu, bali hata linapofanywa na Mwislamu mwenziwe; haruhusiwi kulifanya.
Tunaposoma historia, kwa mfano, tunaona jinsi Bwana Mtume (s.a.w.w.) -- katika Vita vya Handaki -- alivyokubali shauri la Salman Farisi la kuchimba handaki kama walivyokifanya Wafursi kwao. Na Wafursi, wakati huo, hawakuwa ni Waislamu, bali walikuwa ni makafiri waliokiabudu moto! Jee, kwa kuwaigiza makafiri hao katika uchimbaji wa handaki, Bwana Mtume (s.a.w.w.) alikosea?
Hali kadhaalika, tukija kwenye hijja mathalan, tunaona jinsi mahujaji wanavyokwenda baina ya Swafaa na Marwa, na jinsi wanavyochinja wanyama mwisho wa hijja yao. Lakini vitendo kama hivyo, kabla ya Uislamu, vilikuwa vikifanywa na makafiri! Basi kama kuigiza Wakristo hakuruhusiwi, kwa nini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake (s.a.w.w.) wakatuamrisha kufanya mambo ambayo dhahiri yake ni sawa na kuwaigiza makafiri?
Ukivizingatia vizuri vitendo hivyo utaona kwamba, japokuwa kwa dhahiri vinafanana na vile vya makafiri, kwa kweli huwezi kusema kuwa ni sawa na kuwaigiza makafiri. Kwa nini? Kwa sababu waliyokuwa wakiyafanya makafiri mwahali humo, walikuwa wakiyafanyia masanamu yao, waliyoyaweka humo. Kwa hivyo yao ilikuwa ni shirk (ushirikina). Lakini tunayoyafanya sisi Waislamu, baada ya kuondolewa mbali masanamu hayo, huwa tunamfanyia Mwenyezi Mungu Mmoja tu, asiye na mwenziwe (mshirika). Kwa hivyo yetu ni tawhid (kumpwekesha Mwenyezi Mungu).
Hali kadhaalika tunapokuja kwenye Krismasi. Japokuwa Krismasi, kama maulidi, hufanywa kwa kusherehekea mazazi ya Mitume ya Mwenyezi Mungu (Nabii Muhammad s.a.w.w. na Nabii Isa a.s.), lakini sherehe mbili hizo -- kama ambavyo kila mtu anajua -- si sawa. Sherehe zinazofanywa Krismasi ni tafauti kabisa na zinazofanywa maulidini, kama ambavyo Wakristo wanavyomchukulia Nabii Isa a.s. (Yesu Kristo) ni tafauti kabisa na vile Waislamu wanavyomchukulia Mtume Muhammad (s.a.w.w.). Kwa mfano, Waislamu hawamchukulii Mtume Muhammad (s.a.w.w.) kuwa ni Mungu, wala ni Mtoto wa Mungu, wala ni Roho Mtakatifu.
Kwa hivyo kuwa tu jambo fulani lilitangulia kufanywa na makafiri -- wawe ni Wakristo ama ni wengineo -- haiwi ni hujja ya kuwazuilia Waislamu kulifanya jambo hilo maadamu watayatoa yote ya ukafiri yaliyokuwamo humo. Na hivyo ndivyo maulidi yalivyo. Zaidi ya kuwa zote mbili -- Krismasi na maulidi -- ni sherehe za mazazi ya Mitume ya Mwenyezi Mungu, hakuna jengine linalofanana katika sherehe hizo.
Kama tutashikilia kuwa ni haramu Waislamu kuwaigiza Wakristo, au makafiri wowote kwa jumla, katika jambo lolote -- hata kama halipingani na dini yetu -- basi sio wanaosoma maulidi tu, bali hata wanaoyapinga pia watakuwa makosani. Kwani ni nani kati yao aliyeacha gari au ndege, akaendelea kupanda punda, farasi au ngamia? Ni nani, anayejimudu, aliyeacha kutumia umeme (spaki), akaendelea na kuni au mafuta ya taa? Ni nani anayeradhiwa kujipepea kwa kipepeo au nguo yake, akaacha -- ikiwa anayo nafasi -- kutumia banka au AC (Air Conditioner)? Ni nani anayepanda kwa miguu mpaka ghorofa ya 15, au ya 10, akaacha lifti? Kwa nini hawayaachi yote hayo ili wasiwe wanawaigiza Wakristo au makafiri wengine, maana yote hayo yameanzishwa na wao.
Kwa hivyo si sawa kuwazuilia Waislamu kusoma maulidi kwa sababu tu ya kuwa, kufanya hivyo, ni kuwaigiza Wakristo katika sherehe zao za Krismasi.
Katika hujja yao ya nne wanasema: Kwenye sherehe za maulidi hufanywa baadhi ya mambo ambayo ni ya munkar (yanayochukiza, bali ni haramu kamwe, katika sharia ya Kiislamu).
MAJIBU YETU:
Hiyo si hujja madhubuti. Kwa nini maulidi yote yatupwe kwa sababu tu ya kufanywa baadhi ya mambo ambayo ni ya munkar katika sherehe zake? Kwa nini hayaondolewi hayo ya munkar, kama yako, yakabakishwa yasiyo ya munkar? Kwani tunda likiwa limeoza kidogo hutupwa lote, au hukatwa pale palipooza likaliwa pale pazuri palipobaki?
Katika hili tuna funzo zuri kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Yeye aliondoa tawafu ya Al-Kaaba, na Swafaa na Marwa, kwa sababu mwahali humo mulikuwa na munkar (masanamu) au aliamrisha yaondolewe hayo masanamu na watu waendelee kutufu? Tutaona kuwa Mwenyezi Mungu hakutuzuia kufanya jambo zuri lililokuwako (kutufu na kusa'yi) kwa sababu tu katika ibada hizo palikuwa na munkar (masanamu). Alilolifanya ni kuondoa munkar uliokuwako, akatuacha tuendelee na mazuri yaliyobaki (tawafu).
Kwa hivyo, kama katika maulidi kuna munkar wowote, la sawa ni uondolewe munkar huo, na maulidi yaachwe yaendelee. Si kumtupa jongoo na ung'ongo (ujiti) wake.
Kidokezo
Baada ya kutoa makaratasi yetu kwa wiki tatu, makundi mawili ya wanaopinga maulidi yamejitokeza. La kwanza limejita "Ahlu-Tawheed"; na la pili linajita "Wakereketwa wa Sunna Malindi". Na yote mawili hayakutoa anwani zao!
Ahlu-Tawheed wametoa makaratasi yenye jina la "Uzushi na Shirk Ndani ya Barzanji na Vitabu Vyengine vya Maulid". Katika makaratasi hayo, wamenukuu baadhi ya madondoo ambayo -- kwa maoni yao -- ni shirki. Lakini hawakutueleza vipi kuwako madondoo hayo katika vitabu hivyo, hata kama yatakuwa ni shirki kweli, yanafanya maulidi yoyote mengine (yasiyo na hayo wanayoyaona wao kuwa ni shirki) hayafai kusomwa.
Wakereketwa wa Sunna Malindi, kwa upande wao, wametoa makaratasi yenye jina la "Chapa ya Kwanza (1): Majibu ya Abdillah Nassir". Katika makaratasi hayo, ambayo wameahidi kuendelea nayo, hawajazungumzia maulidi. Walilolifanya ni kunizungumza mimi binafsi -- kwa ya kweli na ya uwongo! Lakini na wao pia, kama wenzi wao, hawajatueleza vipi vyovyote vile vitakavyokuwa mimi binafsi -- iwe ni kwa wema ama kwa uovu -- ni hujja tosha ya kuyafanya maulidi yawe hayafai kusomwa! Pengine watalieleza hilo katika makala yao yatakayofuatia.
Hata hivyo si nia yangu, kwa sasa, kuyajibu makaratasi hayo kwa sababu kutatutoa nje ya mfululizo wetu huu. Nia yangu inshallah ni kuendelea kuzijibu hujja zao zote nilizozidondoa katika sura ya kwanza humu. Baada ya hapo ndipo nitakapojibu hayo yaliyomo katika makaratasi yao hayo.
Kwa hivi sasa, napenda kuwahakikishia wanaosoma maulidi kwamba yote waliyoyataja katika makaratasi yao mawili hayo tutayajibu kiilimu na kistaarabu, kama ilivyo dasturi yetu, na kama tulivyofanya mpaka sasa, pamoja na kuonyesha kwamba hayana mashiko.
Kwa hivyo, tunawaomba wale walionayo makaratasi hayo wayaweke, wangojee majibu yetu inshallah.
MWISHO