BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM
MTUME (S.A.W.W)
UMUHIMU WA MITUME KWA JAMII
UTUME
si jambo lisilojulikana katika dini za Kiyahudi na Kikristo. Katika Uislamu, utume umepewa hadhi na umuhimu mkubwa na wa kipekee kabisa. Kutokana na maelekezo ya Uislamu, Mwenyezi Mungu alimuumba mwanadamu kwa lengo takatifu ambalo ni kumuabudu Mwenyezi Mungu na kuishi kwa kufuata mafundisho na muongozo itokayo Kwake. Mwanadamu angewezaje kujua wajibu wake kwa Mwenyezi Mungu na lengo la kuumbwa na kuishi kwake hapa ulimwenguni bila ya kupata mwongozo sahihi na ulio wazi kutoka kwa Mwenyezi Mungu?
HIVYO Mwenyezi Mungu alimchagua kutoka katika kila jamii, Mtume (mteule au nabii) ili apitishie ujumbe wake kwa watu au jamii kama alivyokusudia iwe.
Mitume walichaguliwaje?
Mtu anaweza kujiuliza ni vipi mitume walichaguliwa, na ni mitume wangapi walipewa kazi hiyo tukufu ya kufikisha ujumbe wa Mwenyezi Mungu kwa wanadamu?
Utume au Unabii ni baraka au neema zitokazo kwa Mwenyezi Mungu na ni mapenzi yake anayomjaalia mja wake ampendaye. Lakini labda baada ya kupitia historia ya maisha ya Manabii kwa wanadamu, tunaweza kuelewa ni vigezo (mambo) gani muhimu vinavyomtofautisha Mtume na mtu au watu wengine.
Kwanza, ni kuwa na tabia tukufu na maarifa zaidi kuliko mtu yeyote yule katika jamii ile anamoishi yeye. Hili ni jambo muhimu kabisa kwa ajili ya yeye kuwa kigezo cha tabia kwa wafuasi wake. Sura, umbo, tabia na maarifa ya mtume yeyote ni lazima viwe ni kivutio kwa watu kumkubali badala ya kumkimbia au kufuatilia ujumbe wake pindi anapoanza kazi hiyo. Na mara baada ya kupewa ufunuo toka kwa Mwenyezi Mungu, maisha yote ya mtume huyo yanakuwa matakatifu (hafanyi dhambi tena) yakiongozwa tu na ufunuo kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ingawaje anaweza kufanya makosa madogo madogo ambayo pia huwa yanasahihishwa mara moja na Mwenyezi Mungu kupitia ufunuo.
Pili, ili kuonyesha kuwa si mtu muongo, ujumbe wa mtume yeyote huambatana na kupewa uwezo wa kufanya miujiza. Miujiza hii hufanyika kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, na hakika yeye huwa yuko pamoja na mtume huyo pale anapokuwa anatenda hiyo miujiza, ambayo pia huwa inaendana na utamaduni wa jamii ile. Hapa tunaweza kuinukuu miujiza iliyotendwa na mitume wa Mwenyezi Mungu kama ifuatavyo:
Jamii alimoishi Nabii Musa, ilikuwa imebobea katika elimu ya uchawi. Hivyo ilimbidi Musa kuwa na uwezo wa kufanya miujiza kushinda elimu ya uchawi wa Wa-Misri.
Jamii ya Nabii Isa (Yesu), ilijulikana katika elimu ya utabibu au uganga (i.e. elimu ya madawa) na mafumbo. Hivyo, ilimbidi Yesu aweze kufanya miujiza zaidi na kuwapiku watu wote wenye elimu hiyo katika jamii ile. Na ndiyo maana tunaambiwa kuwa aliweza kuwatibu watu magonjwa mbalimbali bila ya kutumia dawa yoyote bali kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu tu. Kwa mfano, aliweza kuwafufua baadhi ya watu na kuyatibu maradhi mbalimbali na yaliyokwisha shindikana. Lakini yeye hakuwa ametumwa kwa ajili ya kuendelea kufanya hayo bali ilikuwa ni katika kupewa ishara ya Utume wake ili aweze kukubaliwa ama kuaminiwa na watu pindi anapokuwa anatoa ujumbe aliotumwa na Mwenyezi Mungu kuwafikishia watu waliokusudiwa.
Nayo jamii alimoishi Nabii Muhammad (s.a.w.), ilijulikana sana katika elimu ya Fasihi na Tenzi. Hivyo ilibidi muujiza wake uwe ni kuwa mwana fasihi aliyebobea zaidi kuliko wengine wote katika jamii ile. Na muujiza wa Mtume Muhammad ni hii Qur'an ambayo utunzi wake umeonyesha ufundi mkubwa ambao haulinganishwi na wa mwanadamu yeyote. Tofauti na miujiza ya mitume waliopita, ni kwamba wakati miujiza iliyotendwa na mitume hao wa zamani ilikuwa ni ya muda tu (yaani yenye kikomo) na kwa ajili ya watu maalum, na haikuwa ni yenye kudumu, muujiza na Muhammad umekuwa ni wa kudumu kwa sababu umebeba ujumbe kwa wanadamu wote. Ujumbe huu ulishuhudiwa na kuviongoza vizazi vilivyopita na unaendelea kuviongoza vizazi vya sasa utaendelea kushuhudiwa na kuviongoza vizazi vijavyo kutokana na muundo wake, na mafunzo ya kiroho yaliyomo ndani yake. Yote yaliyomo ndani ya Qur'an yamekuwa ni vigumu kuyahujumu au kufikia aina na muundo wa utunzi kama huu na hii inaonyesha kuwa asili ya Qur'an ni Mwenyezi Mungu tu.
Tatu, kila mtume husema wazi kabisa kuwa mafundisho ayatoayo si yake bali ni funuo kutoka kwa Mwenyezi Mungu ili yaweze kuwanufaisha wanadamu. Pia, humbidi ayathibitishe yale yote yaliyofunuliwa kwa mitume wengine waliomtangulia zamani, na hutabiri yale yatakayotokea mbeleni (siku zijazo). Mtume au Nabii yeyote hufanya haya ili kuonyesha kuwa yeye ni njia (mjumbe) tu ya kuakisi ujumbe wa Mwenyezi Mungu huyo huyo mmoja ili uwafikie watu na kwamba Mwenyezi Mungu ni wa watu wote na wa zama zote.
Hivyo, ujumbe wa mitume huwa ni wa aina moja, wenye lengo moja na utokao kwa Mungu huyo huyo mmoja. Hivyo haitakiwi ujumbe huo kuyaacha yaliyo funuliwa kwa mitume wengine wa kabla yake yale yatakayofunuliwa zama zitakazofuata baada yake. Na kwa kuwa Mwenyezi Mungu hawezi kuongea na watu ana kwa ana, Mitume au wateule wake wana umuhimu mkubwa kabisa kwa jamii, kama njia za Mwenyezi Mungu kupitishia ujumbe wake ili uweze kuwafikia wanadamu. Hatungeweza kufahamu ni kwa nini tuliumbwa, au yatatutokea yapi baada ya kufa kwetu, au kama kuna kuishi tena (baada ya kufufuliwa) baada ya kufa kwetu na kama tunawajibika kwa kila tulitendalo. Kwa maana nyingine tungejuaje kama kuna malipo au mateso (adhabu) kutokana na matendo yetu ya kila siku za maisha yetu haya?
Maswali kama haya na mengine mengi ya kiroho kuhusu kuwepo kwa Mwenyezi Mungu moja tu, malaika wake, pepo, moto (jehanamu), n.k. yasingeweza kujibika bila ya mitume kupewa ufunuo utokao kwa Mwenyezi Mungu aliyeumba kila kitu na ambaye ni mjuzi wa vitu vyote vikiwemo vile visivyoonekana kwa macho na fahamu zetu za kimaumbile. Majibu ya maswali kama haya, inabidi yawe sahihi (yasiwe na shaka) na lazima yatolewe na watu wanaoaminika na kuheshimiwa zaidi katika jamii zao kutokana na tabia na busara walizo nazo kuwa ni za hali ya juu kuliko za watu wengine katika jamii ile. Na ndiyo maana kila mtume ana sifa ya kuitwa "Bwana" katika jamii yake.
Mitume humtegemea Mwenyezi Mungu peke yake, ambaye naye huwahami kwa kuwapa uwezo wa kutenda miujiza ili waweze kusimama kidete katika kuendeleza kazi ya kueneza ujumbe wa Mwenyezi Mungu kwa watu. Na mara zote, ujumbe wao kwa kifupi huwa na mambo muhimu yafuatayo:
(1) Dhana sahihi kuhusu kuwepo kwa Mungu mmoja tu, sifa zake, uumbaji wake, yapi yanamstahili na yapi hayamstahili kama Mwenyezi Mungu.
(2) Lengo la kuumbwa watu, kuhusu mambo wanayotakiwa kuyafanya, na wasiyotakiwa kuyafanya, malipo au adhabu kwa kumtii au kutokumtii Mwenyezi Mungu.
(3) Wazo sahihi na la wazi kuhusu mambo yasiyoonekana kama kuwepo kwa malaika, majini, pepo na moto.
(4) Jinsi ya kuziongoza familia na jamii zetu kwa kufuata mwongozo sahihi utokao kwa Mwenyezi Mungu (ambao huwa na sheria, kanuni na taratibu) na ambao ukifuatwa kikamilifu huinufaisha jamii.
Ni wazi kutokana na maelezo hayo kuwa, hakuna mtu yeyote anayeweza kuwa na uwezo zaidi ya mitume katika jamii husika. Hata katika zama zetu hizi ambazo zimetawaliwa na maendeleo ya sayansi na teknolojia, chanzo sahihi na chenye kuaminika kuhusu mambo ya kiroho na uwezo wa Mwenyezi Mungu ni kwa njia ya ufunuo kupitia kwa mitume tu basi.
Mambo muhimu kuhusu Utume
Kwa uchache, kuna mambo muhimu mawili kuhusiana na kuwepo UTUME. Mambo haya yanahusu majukumu waliyopewa mitume Isa (Yesu) na Muhammad. Mitume hawa ndio ambao wamekuwa wakieleweka vibaya. Maelezo kumhbusu Mtume Isa (Yesu) ndani ya Qur'an, ni wazi hukataa dhana ya kumwita Mwana wa Mungu, hivyo humuelezea kama mmojawapo wa mitume wakuu wa Mwenyezi Mungu. Qur'an 'huweka wazi kuwa kuzaliwa kwa Nabii Isa bila ya kuwa na baba hakumfanyi yeye kuwa mwana wa Mungu (kibiolojia). Inaendelea Qur'an kumtaja pia Nabii Adam aliyeumbwa na Mungu na ambaye hakuwa na baba wala mama.
"Mfano wa Isa bin Mariam kwa Mwenyezi Mungu ni sawa na ule wa Adam, yeye aliu7mbwa kutokana na udongo na kisha (Mungu) akasema na awe mtu naye akawa" (3:59)
Kama mitume wengine, Nabii Isa pia aitenda miujiza. Kwa mfano, alifufua wafu, aliwatibu wenye ukoma na kuwaponya vipofu, lakini wakati akiyafanya haya alieleza waziwazi kuwa miujiza hiyo ilikuwa ni ishara tu zitokazo kwa Mwenyezi Mungu kuuthibitisha Utume (Unabii) wake.
Hakika kutokuifahamu vizuri nafsi na lengo la kuletwa kwake Nabii Isa, ni mambo yaliyo jiingiza katika mafundisho ya waumini wake kwa sababu aidha mafundisho yake hayakuwekwa rekodi wakati huohuo alipokuwa akifundisha, au mafundisho yake yaliandikwa na baadae kupotea hadi baadhi yake yalipoanza kukusanywa na kutokana na masimulizi ya watu walioweza kuyakumbuka baada ya miaka kati ya 60 hadi 100 baada ya kutoweka kwa Nabii Isa (Luke 1:1-4).
Kwa mujibu wa maelezo ya Qur'an, Nabii Isa alitumwa kwa wana-Israel tu, na alithibitisha umuhimu wa kuitekeleza Torati iliyofunuliwa kwa Nabii Musa (a.s.) na pia alibashiri habari njema ya kuletwa kwa Mtume wa mwisho baada ya yeye kuondoka. "Na Isa mwana wa Mariam aliwaambia wana-Israel kuwa 'mimi ni mtume wa Mwenyezi Mungu kwenu', naisadikisha torati iliyonitangulia na kuwabashiria habari njema ya kuja kwa Nabii mwingine atakayenifuatia, ambaye jina lake ataitwa Ahmad-yaani msifika sana" (61:6).
Hata hivyo, wengi kati ya Wayahudi, waliyakataa mafundisho yake na hivyo kupanga mikakati ya kumuua. Na kwa imani yao walidhani kuwa walifanikiwa kumsulubu na kumuua, lakini kwa mujibu wa maelezo ya Qur'an, ni kwamba Mwenyezi Mungu alimuepusha na suluba na mauaji hayo ila wao hawajui. Pia kuna aya ndani ya Qur'an yenye kumaanisha kuwa Nabii Isa atarudi tena ulimwenguni na kwamba wakatihuo ataudhihirishia ulimwengu yale yote waliyokuwa wakimsingizia na hapo itabidi Wakristo na Wayahudi wamfuate na kumuamini kama wafanyavyo Waislamu (kwa kumtakasa na yale waliyokuwa wakimhusisha nayo kama kuwa eti ni mwana wa Mungu au kuwa eti yeye ndiye Mungu mwenyewe, kuwa eti alisulubiwa, akifa na akafufuka) kabla ya kufa kwake. Maneno haya puia yanathibitishwa na kauli (hadithi) za Mtume Muhammad (s.a.w.).
Mtume wa Mwenyezi Mungu na wa mwisho, Nabii Muhammad (s.a.w.) alizaliwa bara la Arabuni katika karne ya 6. Hadi kufikia umri wa miaka 40, jamii ya watu wote wa Makkah walimfahamu tu kuwa ni mtu mkamilifu na mwenye tabia njema kabisa (kuliko watu wote) na hivyo walimpa sifa itokanayo na tabia yake na kuwa ni "mkweli na mwaminifu - Al Ameen".
Hata yeye biansi katika ujana wake, pamoja na kuwa na sifa za tabia tukufu, hakujua kuwa hata siku moja ataweza kuwa Mteule wa Mungu na hivyo kuweza kubeba jukumu zito la kuupokea ujumbe wa Mwenyezi Mungu kwa wanadamu. Hata hivyo alikuwa kwa tabia yake akichukizwa na taratibu za watu wa Makkah za kupenda kuyaabudia masanamu. yeyey aliwachukulia watu wale, kuwa wasioweza kuzitumia akili kwani hakuyaona masanamu kuwa na uwezo wowote wa kudhuru au kuponya. yeyey katika fikra zake alikuwa na imani ya kuwepo Mungu mmoja tu na ambaye ndiye aliyeumbwa vitu vyote na ambaye ndiye ambaye angeweza kuponya au kudhuru (dhana ambazo kumbe zilikuwa ni sahihi).
Na alipofikisha umri wa maiak 40, ndipo alipofunuliwa rasmi kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, kwamba ujumbe wake ni kwa watu wote na yeye ni mjumbe wa mwisho, hakutakuja tena mjumbe mwingine baada yake. ujumbe wake uliweza kuhifadhika katika kumbukumbu ya kichwa chake na hata katika kumbu kumbu za vichwa vya wafuasi wake na pia kuweza kuandikwa na kuhifadhiwa katika magome ya miti, mbao, ngozi, juu ya mawe, n.k. kuanzia wakati wa maisha yake kama Mtume wa Mwenyezi Mungu na hadi leo hii umeweza kusomwa na jamii za watu wote ulimwenguni. Hivyo, Qur'an kama tuliyo nayo siku hzi ni ile ile kama ilivyofunuliwa kwake Mtume Muhammad na hakuna hata herufi moja iliyopata kubadilishwa kwani Mwenyezi Mungu mwenyewe ameahidi kuilinda na kila aina ya uzushi au hujuma. hivyo, Qur'an imebakia kuwa ni Kitabu muhimui chenye mwongozo sahihi kwa maisha ya watu wote na kwa nyakati zote. Na pia humtaja Mtume Muhammad kama mtume wa mwisho wa Mwenyezi Mungu.
MWISHO