ALIYOYASEMA MTUME (S.A.W.W) KUHUSU IMAM HUSEIN (A.S)
  • Kichwa: ALIYOYASEMA MTUME (S.A.W.W) KUHUSU IMAM HUSEIN (A.S)
  • mwandishi: Salim said mwaega
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 7:24:24 24-8-1403

ALIYOSEMA MTUME (S.A.W.W) KUHUSU IMAM HUSEIN (A.S)

Imam Hussein(as) ni mtoto wa Imam Ali bin Abi talib(as) bin Abdul Muthwalib bin Hashim. Mama yake ni Fatimatuz-zahra(sa), ambaye ni binti ya mtume Muhammad(saww). kwa hivyo ni mjukuu wa mtume Muhammad(saw). Jambo hilo lipo wazi kwa kila aliyesoma tarehe ya kiislamu,kwani amesikika mtume(saww) mara kwa mara akisema kuwa Hassana na Hussein ni watoto wake mwenyewe. Pia ziko hadithi zengine zinazothibitisha baadhi ya nyakati kuwa mtume (saww) alisikika akisema kuwa mitume wote waliyokuwa kabla yake vizazi vyao vilitokana na wao wenyewe, ila yeye kizazi  chake kinatokana na binti yake Fatimahz-zahra(sa).  Swali ambalo labda watu wengi wanajiuliza juu ya hii hadithi maarufu iliyoandikwa na wanazuoni wa hadihti kuwa mtume(saw) alisema:
“Hussein anatokana nami na mimi natokana na Hussein,mwenyezi Mungu ampende ampendaye Hussein”
Swali lenyewe ni kwamba,ni vipi mtume(saww)atokane na Imam Hussein(as)?
Tangu lini babu akatokana na mjukuu? Inawezekana kuwa mjukuu atokane na babu na wala sio kinyume chake.
Jawabu la swali hili ni kuwa,kila asemacho mtume (saww) kinatokana na hekima yake na maana muhimu ambayo ni juu ya waumini wa dini ya kiislamu kuzingatia ili kupata mafunzo na muongozo ndani yake. Mtume (saww) hakuwa ni mwenye kusema tu pasina hekima yoyote, bali alikuwa ni mwenye kusema yaliyo na manufaa katika dini ya mwenyezi Mungu(sw). Kwa hivyo kama kila alichokisema mtume(saww) kilitokana na wahay(ufunuo) na hekima kama ithibitishavyo Qur’an tukufu kuwa hasemi ila ni ufunuo kutoka kwa mwenyezi Mungu mkarimu,basi hekima ya kusema kuwa Hussein(as) anatokana naye ni nini? Jawabu la swali hili linathibitishwa na historia ya usilamu na matukio yaliyo tokea baada ya mtume(saww) kuaga duania. Laiti mtu atachukuwa fursa na kuisoma tarehe ya uislamu, atapata kuwa kuna baadhi ya matukio yaliyotokea ambayo yanamuunga mkono mtume (saw) katika kauli yake. Nalo ni tukio la Karbala. Tukio la Karbala halikutokea bila sababu tu,bali ziko sababu nyingi ambazo zilichangia katika kutokea tukio hili. Baadhi  ya sababu hizo ni tamaa ya uongozi na kuyapenda maisha ya dunia tunayoishi. Historia imenukuu kuwa hata baada ya mtume(saw) kubainisha kuwa kuna viongozi ambao wanafaa kufuatwa baada yake,wako watu waliomhalifu kwa tama zao za kuipenda dunia na kupenda uongozi na kuenda dhidi ya wasia wake yeye mtume(saw). Kati ya vitu walivyo vifanya ni kuwapokonya au kuwanyang’anya uongozi waliochaguliwa na mtume(saw) kuwa viongozi baada yake. Na kama tulivyosema hapo awali kuwa asemapo mtume(saw) huwa anasema na hekima na kwa ufunuo alioupata kutoka kwa Mola wake. Huwa anajuwa kuwa watu aliowachaguwa hawawezi kuenda kinyume na Qur’an na mafunzo yake katika kuwaongoza watu,kwa sababu hawaongozi kwa shahawa na matamanio yao bali ni kwa amri ya Allah(swt),mwenye elimu na mjuzi. Sasa baada ya mtume(saw) kuaga dunia,kulingana na hadithi za mtume zilizo sahihi ni kuwa Viongozi waliochaguliwa ni kumi na wawili naye imam Hussein akiwa watatu wao na baba yake Ali bin Abi Talib(as) akiwa ndiye wa kwanza aliyechaguliwa na mtume(sa) katika hijja yake ya mwisho. Sasa tunaona kuwa kuna watu walioenda kinyume na maagizo ya mtume(saw) kwa kuchukuwa uongozi pasi na kustahiki. Nao na kati ya watu hao ni Yazid motto wa Muawiyya bin Abi sufiyan.Yazidi kama wanavyoandika wasomi wa kisunni ni kuwa alikuwa na sifa zifuatazo:
1.Mnywa pombe.
2.Mcheza kamari.
3.Mzinifu hata kwa mama zake na madada zake.
4.Mwenye kuuwa watu bila ya sababu.
5.Mwenye kuacha swala baali hata kutoswali kabisa.
Baada ya kuchukuwa uongozi,aliharibu kila kitu katika dini.katika vitu alivyo vifanya ni kuihalalisha Madina(mji wa mtume(saw) kwa muda wa siku tatu. Kuivunja Kaaba ya mwenyezi Mungu, na mengine mengi. Sasa imam kwa kuwa yeye ndiye aliyekuwa na haki ya kuongoza,ilikuwa ni wajibu wake kuihami dini kwa njia yoyoye ile. Na kuamrisha mema ni wajibu hususan ikiwa itapelekea katika kuharibika dini na watu kuihama na kuiacha dini.
Imam katika kuihami na kuihifadhi dini,ilimbidi asimame na kuipinga dhulma iliyo kithiri katika wakati ule. Na laiti imam Hussein(as) hangesimama basi dini ingepotea. Na kupotea kwa dini inamaanisha kupotea na kusahaulika kwa jina la mtume(saw) katika ndimi za watu na katika historia. Mtume(saw) ametajwa na anatajwa hadi sasa kwenye sehemu mbali mbali zikiwemo:
1.Katika Adhana.
2.Wakati wa kumtakia rehma pamoja na watu wa nyumba yake(salawat).
3.Katika swala.
Lakini laiti imam Hussein hangesimama haya  yote yangesahaulika. Kwa kusimama kwa imam Hussein(as) na kupinga dhulma katika uwanja wa karbala na kuuawa kishahidi pamoja na watu wake 72 ilikuwa ni sawa na kuzaliwa tena mtume (saw). Kwa sababu baada ya hapo dini ilirudi kuwa na msimamo tena,kwani watu baada ya kuuawa imam Hussein(as) waliamka na kuzinduka kujuwa kuwa walikuwa wanaangamia. Sasa ni kwa sababu hii ndiyo mtume alitamka matamshi yale ya kuwa anatokana na Hussein. Na maanaye anatoka na Husein  siku ya Ashura hapo karbala ambapo dini yake na jina lake litapata mwelekeo tena baada ya hapo.