NAFASI YA IMAMU HUSEIN
  • Kichwa: NAFASI YA IMAMU HUSEIN
  • mwandishi: BARAZA
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 7:31:28 24-8-1403

BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

NAFASI YA IMAMU HUSEIN

Kila mwaka unapowadia mwezi wa Muharram nyoyo za wapenzi wa Watu wa Nyumba ya Mtume wetu Muhammad saw na Ahlubaiti zake zinashikwa na hali ya huzuni na majonzi makubwa. Siku hizi zinakwenda sambamba na harakati na vikao vya kuhuisha mapambano makubwa ya mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) Imam Hussein bin Ali (as) katika ardhi ya Karbala. Kwa mnasaba huo pia tunatuma sala na salamu zetu kwa mkombozi mkubwa wa mwanadamu Nabii Muhammad amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake, Ali zake na Ahlubaiti wake waliotakaswa na dhambi na mambo machafu. Sala za salamu za Mwenyezi Mungu zikufikie wewe Abu Abdillah Hussein bin Ali na roho zilizouawa shahidi katika kupigania haki na dini ya Allah. Salamu zaAllah ziwafikie usiku na mchana hadi siku ya kufufuliwa viumbe kwa ajili ya hesabu.

Risala na ujumbe mkubwa wa Manabii na mawalii wote wa Mwenyezi Mungu ilikuwa ni kupambana na dhulma na uonevu na kusimamisha haki na uadilifu. Mitume na mawalii wote walikuwa na jukumu la kusimamisha dini ya haki, uhuru na kumuonesha mwanadamu njia ya saada na uongofu.

Hapana shaka kuwa jambo lilaloipa harakati yoyote ile heshima na utukufu wa milele ni malengo yake aali na yanayomfikisha mwanadamu kwenye saada ya milele. Mapambano ya Imam Hussein ni miongoni mwa harakati hizo zilizofanyika katika njia ya Mwenyezi Mungu na kwa ajili ya kuhuisha dini yake.

Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana hata baada ya kupita karne 13 sasa tangu baada ya tukio hilo, kamwe harakati na mapambano hayo ya Imam Hussein hayajasahaulika na yanaendelea kuwa tochi na mwanga unaomulikia wapigania uhuru, haki na uadilifu miaka na dahari.

Harakati ya Imam Hussein (as) ilikuwa tukio la aina yake na lenye sura kadhaa. Wachambuzi wengi wa masuala ya kihistoria na kijamii wanaamini kwamba, kuna masuala mengi yaliyochangia katika harakati hiyo. Hata hivyo wanakubaliana kwamba sababu na malengo hayo yote yanaweza kujumuishwa katika lengo moja aali ambalo ni kuhuisha dini ya Mwenyezi Mungu.

Uislamu ambayo ndiyo dini ya mwisho ya Allah, iliwafikia wanadamu kupitia Mtume wake Muhammad (saw) na baadaye Ahlubaiti wake watoharifu. Baada ya kuondoka na kufariki dunia mtukufu Mtume, kulijitokeza baadhi ya makundi yaliyopotosha mafundisho ya dini hiyo na kuzusha baadhi ya mambo yasiyooana na mafundisho ya Mtume Muhammad (saw). Katika kipindi hicho, Ahlul Bait wa mtukufu Mtume ndio waliobeba jukumu la kulinda dini na kufichua uzushi na opotofu uliokuwa ikizushwa katika mafundisho ya dini ya Mwenyezi Mungu na kubeba bendera ya kuhuisha dini hiyo katika vipindi mbalimbali vya historia.

Ushahidi wa kihistoria umeonyesha kwamba baada ya kufariki dunia mtukufu Mtume, ada za kijahilia, bid'a na uzushi vilitawala anga ya jamii ya Waislamu kwa kutumia mghafala uliokuwa ukitawala fikra za watu wa wakati huo.

Itikadi na sheria za Kiislamu zilifasiriwa kwa mujibu wa maslahi ya watawala, suala ambalo lilifikia kileleni katika zama za utawala wa Bani Umayyah katika ulimwengu wa Kiislamu. Sambamba na hali hiyo, Ahlul Bait wa Mtume Muhammad (saw) ambao ndio watu waliokuwa karibu naye mno na ambao alituamuru kushikamana nao wao pamoja na kitabu cha Mwenyezi Mungu Qur'ani Tukufu, walibanwa na kutengwa zaidi na zaidi.

Mambo mengi yaliingizwa katika dini na mafundisho halisi ya Nabii Muhammad (saw) yakapotoshwa au kuwekwa kando na watawala kadiri siku zilivyosonga mbele. Watu wa kawaida nao walianza kuzoea bid'a na uzusha huo wa watawala bila ya kuwa na uwezo wa kupinga au kukabiliana nao. Ni katika hali hii ndipo warithi halisi wa njia ya Mtume waliposimama kuhuisha dini na ujumbe wake na kufuta vumbi la upotofu na uzushi katika uso wa dini tukufu ya Kiislamu. Hata hivyo ili kuweza kutimiza lengo hilo, wakati mwingine ilibidi kujitoa mhanga kwa shabaha ya kuamsha na kuzindua jamii na kuhuisha thamani za kidini.

Upotoshaji na uzushi katika dini ulishamiri na kushika kasi zaidi katika kipindi cha utawala wa Yazid bin Muawiya kwa kadiri kwamba ilihofiwa kuwa hakika ya dini tukufu ya Kiislamu ingechafuliwa na kuvurugwa kikamilifu. Thamani za dini zilidunisha na fikra za jamii zikabadilishwa na kutiwa tashwishi. Jamii ya Kiislamu ilipatwa na maradhi ya hisia za kikaumu na kikabila, ulimbikizaji wa mali, kukanyagwa thamani za kidini na kimaadili, dhulma na ufisadi wa tabaka la watawala.

Matatizo hayo yaliuzonga mno umma wa Kiislamu. Hali hiyo ya kusikitisha ilimfanya mjukuu wa Mtume Imam Hussein bin Ali (as) aanzishe haralati kubwa ya mageuzi na marekebisho ndani ya umma wa Kiisalmu kwa ajili ya kuhuisha dini hiyo, mafundisho asili ya babu yake na thamani za Kiislamu.

Kuhusu hali iliyokuwa ikitawala jamii ya Waislamu ya wakati huo: Imam Hussein (as) alisema akiwahutubu Waislamu kwamba: "Hivi hamuoni kuwa haki haitendeki na dhulma inaedelea kufanyika? Katika hali kama hii muumini anafadhili mauati na kwenda kukutana na Mola wake Mlezi kuliko kuishi maisha kama kama haya. Hakika mimi sioni mauti ila saada na ufanisi na kuishi na madhalimu kwangu ni fedheha kubwa". (Tarikh Tabari)

Katika kipindi hicho Imam Hussein pia aliwaandikia barua wazee na wakuu wa mji wa Basra huko Iraq akiwataka kutafakari kuhusu Kitabu cha Mwenyezi Mungu SW na Suna za Mtume Muhammad (saw) na kutoghafilika na masuala yanayotendeka katika jamii. Kwani katika kipindi hicho suna na mwenendo mzuri wa Kiislamu ulikuwa umetoweka na ada za kijahilia kushika mahala pake. Sehemu moja ya barua ya Imam Hussein kwa wazee na Basra ilisema: "Ninawalingania kufuata Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Suna za Mtume wake, kwa sababu uzushi na sheria sizofaa zimehuishwa tena. Iwapo mtasikia ujumbe huu na kuukubali nitawaongoza katika njia ya saada na ufanisi.."

Lengo la harakati ya Imam Hussein (sa) lilikuwa kuhuisha adhama ya dini ya Kiislamu na thamani zake na kutekeleza mipaka na sheria za Mwenyezi Mungu. Katika harakati hiyo Imam alisisitiza mno juu ya udharura wa kueneza maarifa na kuwazindua watu wa matabaka yote ya jamii. Alipokuwa njia akielekea Basra huko Iraq, Imam Hussein alikuwa na mshairi maarufu wa Kiarabu kwa jina la Farazdaq na kumwambia: "Ewe Farazdaq! Hakika watu hawa wameamua kumfuata shetani na wametupilia mbali taa na kumcha Mungu kueneza ufisadi katika nchi. Limesimamisha utekelezaji wa sheria za adhabu za Mwenyezi Mungu, na kupora mali, kuhalalisha aliyoyaharamisha Mwenyezi Mungu na kuharamisha aliyoyahalalisha na mimi ndiye ninayestahili kufanya mabadiliko". (Tarikh Tabari, Juz-3)

Wahuishaji wa dini katika kipindi chote cha historia walikuwa wakihisi mtengano baina ya thamani za Kiislamu na mambo yanayotendeka katika jamii, suala ambalo ilikuwa vigumu kutambuliwa na watu wengine. Mtengano huo mara nyingine ulitokea katika utumiaji wa dini katika jamii au katika masuala ya kisaisa na maisha ya Waislamu. Katika hali kama hiyo akili na mantiki inahukumu kwamba kuna udharura wa kufanyika marekebisho makubwa katika jamii.

Imam Hussein (as) alianza harakati ya kuhuisha thamani za Kiislamu kwa mawaidha mema na kuwazindua Waislamu hususan viongozi wa jamii. Alisema: "Enyi watu! Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema: Anayemuona mtawala dhalimu akihalalisha mambo yaliyoharamishwa na Mwenyezi Mungu na kukiuka ahadi zake, akienda kinyume na suna za Mtume wa Mwenyezi Mungu akiamiliana na waja wa Allah kwa uovu na uadui kisha asifanye mabadiliko yoyote kwa matendo au kauli, basi itakuwa haki ya Mwenyezi Mungu kumuingiza mahala pake (motoni)".

(Tazama Tarikh Tabari, Juzuu ya 3) Hata hivyo baada ya kuona kwamba njia na mbinu hiyo haikuwa na matunda, Imam aliamua kuchukua hatua kubwa zaidi baada ya kutimiza huja, kiasi kwamba hatimaye alichukua uamuzi wa kukabiliana moja kwa moja na kambi ya ufuska, dhulma na uonevu. Imam alitambua kwamba, kuna ulazima wa kuanzisha harakati ya mapambano dhidi ya uzushi na opotofu huo.

Alikusudia kuziamsha nyoyo zilizolala za Waislamu na kuwakumbusha wajibu wao wa kupambana na dhulma, uonevu na upotoshaji wa dini. Mwenendo, harakati na maamuzi ya Imam yalionesha uwezo wake mkubwa wa kutabiri mambo na kutaza mbali.

Imam Hussein bin Ali (as) alisisitiza mno katika hotuba zake juu ya utukufu wa mwanadamu, hadhi ya kiumbe huyo na udharura wa kulindwa thamani za kidini. Alibainisha kwamba dhulma, uonevu na maovu yanapotawala jamii ya mwananadamu huzima taa na mwanga wa mambo mema, hadhi na thamani za kibinadamu.

Kwa msingi huo kuna udharura wa kusimama kidete kukabiliana na hali hiyo hata kama itabidi kujitoa mhanga na kuuawa shahidi. Ni kwa msingi huo ndipo mtukufu huyo akakhitari njia ya mapambano matakatifu kama njia pekee ya uokovu na kuhuisha Uislamu na matukufu yake.

Aliandamana na familia yake yote, watoto wadogo wake kwa waume na masahaba zake katika medani ya vita ili kudhihirisha sura ya Uislamu halisi kwa watu wa zama hizo na vizazi vya baada yake. Salam za Allah ziwe juu ya Imam Hussein bin Ali (as) ahlubaiti wake na masahaba zake waliojitoa mhanga kwa ajili ya dini ya Mwenyezi Mungu, uadilifu na matukufu ya kibinadamu.

MWISHO