RUHUSA YA KUOMBOLEZA
  • Kichwa: RUHUSA YA KUOMBOLEZA
  • mwandishi: Sayyid Abdul Hussein Sharafuddin
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 7:33:56 24-8-1403

MAJLIS YA PILl YAH: RUHUSA YA KUOMBOLEZA

Hapana shaka kwamba ipo ruhusa ya kuomboleza vifo vya Waumini, na kwamba jambo hilo ni halali, na hapana dalili iliyo kinyume cha hivi.

Kwa hakika baba yetu Nabii Adam (a.s.) aliomboleza kifo cha mwanawe Habil, na maombolezo yakawa yanaendelea mpaka leo kila inapotokea jambo la kifo katika kizazi cha wanaadamu bila upinzani.

Ama Mtume Muhammad (s.a.w.w) aliwaruhusu Masahaba wake kufanya maombolezo kwa wingi kutokana na huzuni, na pia aliruhusu kutaja mema ya waliofariki na kutoa sifa zao katika tabia nzuri na matendo mazuri.

Na wakati Mtume (s.a.w.w) alipofariki, Masahaba walishindana katika kutaja sifa zake walipokuwa wakiomboleza kifo chake.

Katika kifo hicho cha Mtume (s.a.w.w) Bibi Fatma binti wa Mtume (s.a.w.w) pia aliomboleza wazi wazi na kuonesha huzuni yake kwa kusoma beti za Kishairi.

Taz. Ir-Shad As-Saari cha Al-Qas-Talan Uk.318 Juz. 3.

Kadhalika kifo cha Bwana Mtume kiliombolezwa na shangazi yake Mtume (s.a.w.) Bibi Safia kama inavyoonesha katika Istiiab cha Ibnu Abdil-Bari. Pia lbnu ami yake Mtume Bwana Abu Sufian bin Harith Bin Abdil-Mutalib na Bwana Abu-Dhuarib AlHadh-li, Bwana Abul-Haithami At-Taihani, Ummu Ra-Ala AlQushairiyya na Bwana Amir bin At-Tufail na wengineo wote waliomboleza.

Taz. AI-Istiiab na AI-Isaba

Pamoja na maelezo haya, ili kumkinaisha mtu kuhusu suala la maombolezo, yafaa sana kukiangalia na kukisoma kitabu kiitwacho Al Istiiab na pia At-Tabaqat cha Ibn Saad na Usudul Ghaaba na al-Isaba, kwani humo atakuta mambo mengi yanayohusu maomboIezo yaliyofanywa na Masahaba.

Katika Masahaba walioomboleza sana-sana kutokana na vifo ni; Sahaba wa Kike Bibi Al-Khinsaa, ambaye aliomboleza vifo vya nduguze wawili, Mabwana Sakhr na Muawiya ambao walikuwa makafiri.

Bibi huyu alikuwa miongoni mwa watu wachamungu kiasi kwamba alitoa wanawe kwa ajili ya kutumikia Uislamu, na wote waliuawa katika njia ya kutumikia Uislamu, kitu ambacho Bibi huyu alikifurahia.

Lakini pamoja na yote hayo hakuacha kuomboleza mauti ya nduguze mpaka alipofariki na wala hakutokea mtu wa kumkemea kwa tendo hilo.

Kwa kifupi suala la kuomboleza ni mashuhuri katika kila zama na kila mahali baina ya Waislamu na wala hawapingani katika hilo.

Sisi tunatosheka na dalili ya kuhalalisha maombolezo yetu tuyafanyayo kama walivyopokea wapokezi wetu kutoka kwa Bwana Zaidi bin As-Shuhaam amesema: "Tulikuwa mbele ya Abu Abdullahi Al-Sadiq (a.s.) huku tukiwa na kundi la watu kutoka Al-Kufah, mara akaingia Jaafar bin Af-Fan basi Imam Al- Sadiq akamkaribisha na akamsogeza karibu yake kisha akasema: "Ewe Jaafar nimepata habari kwamba wewe unasoma mashairi juu ya Imam Husein na unayasema vizuri, Jaafar bin Af-Fan akasema: "Ndiyo", Imam Jaafar akasema: "Hebu soma mashairi hayo, nikasoma".

Baada ya Mashairi hayo kusomwa katika hali ya kuomboleza mauaji ya Imam Husein (a.s), Imam Jaafar Al-Sadiq (a.s.) alilia na wakalia watu waliokuwa wamemzunguka kiasi ambacho machozi yalimtiririka usoni mwake hadi kwenye ndevu, kisha Imam akasema: "Ewe Jaafar WalIah wamekushuhudia Malaika Watukufu na wao wanasikiliza maneno yako unapoomboleza kwa ajili ya Imam Husein (a.s.), na kwa hakika wamelia kama tulivyolia sisi na zaidi ya hapo, na Mwenyezi Mungu Mtukufu amefaradhisha kwako Pepo katika muda huu na amekusamehe".

Kisha Imam Jaafar Al-Sadiq akasema kumwambia Jaafar bin Af-Fan, "Je. nikuongezee ubora kwa wenye kuomboleza mauaji ya Imam Husein (a.s.)", akasema Jaafar bin Afan: "Ndiyo Ewe Bwana wangu".

Akasema Imam Jaafar (a.s.): "Hapana yeyote yule atakayesoma Shairi la maombolezo ya Imam Husein (a.s.), na kwa maombolezo hayo akalia na akawaliza wengine isipokuwa Mwenyezi Mungu atamsamehe na kumuwajibishia kupata Pepo".

Imam Muhammad bin Idris As-Shafii (Imam Shafii) ni miongoni mwa watu waliombeleza mauaji ya Imam Husein (a.s.) aliposoma mashairi ambayo tafsiri yake ni kama ifuatavyo:

Ulimwengu ulitingishika kwa ajili ya kuuawa kizazi cha Mtume Muhammad (s.a.w.), Milima migumu ilikuwa karibu kuyeyuka kwa ajili ya kuuawa kizazi cha Mtume Muhammad (s.a.w.w), Milima migumu ilikuwa karibu kuyeyuka kwa ajili ya kuwahuzunikia wao (kizazi cha Mtume), Basi nani atanifikishia barua ya huzuni kwa Husein? Nitaomboleza kifo cha Husein japo nafsi za watu na nyoyo zitachukia.

Taz. Maarij al-Usul.