BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM
ALI BIN ABII TAALIB (A.S)
IMAMU ALI KATIKA KATIKA KALAMU ZA MADHEHEBU YA AHLU SUNNA WAL-JAMAA
ALI BIN ABU TALIB (RA) KHALIFA WA NNE ALIYEONGOKA
Babu Yake
Abdul Muttalib bin Hashim alikuwa mkuu wa kabila la Kikureshi, mbora wao na kiongozi wao wanayemtii. Sifa zake zilienea katika eneo lote la jangwa la (Bara ya) Arabuni kuanzia Kaskazini mpaka Kusini yake. Wote walikuwa wakimheshimu na wakijua kuwa yeye ndiye aliyekichimba kisima cha maji ya Zamzam kwa mikono yake. Kisima kinachoendelea kutowa maji yenye baraka mpaka wakati wetu huu.
Majeshi ya Abraha Mhabeshi yalipotaka kuibomoa Al Kaaba, Abdul Muttalib alitambua kuwa hana uwezo wa kupambana nayo. Aliwataka watu wake wauhame mji na kupanda juu ya majabali. Akawakusanya kondoo zake na kuondoka nao huku akimuomba Mola wake Mtukufu ailinde nyumba Yake hiyo ya Al Kaaba. Alipoulizwa kwa nini anakimbia pamoja na wanyama wake na kuiacha Al Kaaba bila ulinzi, Abdul Muttalib alijibu: "Lilbayti rabbun yah-miyhi", maana yake; "Nyumba ina Mola wake mlezi mwenye kuilinda". Alifurahi kupita kiasi alipoletewa bishara njema ya kuzaliwa kwa mjukuu wake Muhammad bin Abdillahi bin Abdul Muttalib (SAW). Akambeba kwa mikono yake miwili na kukimbia naye mpaka ndani ya msikiti wa Al Kaaba huku akimuomba Mwenyezi Mungu na kumshukuru akisema;
"Alhamdulillahi aliyenipa mtoto huyu mwema na mzuri". Akampa jina la Muhammad, na kabla ya kufariki kwake alimuusia sana mwanawe Abu Talib juu ya mtoto huyo na kumtaka amlee vizuri, akamwambia; "Mwanangu huyu atakuwa na shani kubwa, kwa hivyo umtunze vizuri, asije akafikiwa na dhara yoyote". Abdullahi, baba yake Muhammad (SAW) alifariki dunia kabla ya kuzaliwa kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW). Kwa hivyo Abu Talib akachukuwa jukumu la kumlea mtoto huyo kama alivyousiwa na baba yake Abdul Muttalib, na hata pale Mtume (SAW) alipoanza kufunuliwa Wahyi na kuilingania dini ya Mola wake, Abu Talib alimsaidia sana, akamlinda yeye pamoja na ujumbe aliokuja nao juu ya kuwa yeye mwenyewe (Abu Talib) hakuingia katika dini hii tukufu.
Abu Talib alikuwa na heba na heshima kubwa mbele ya waarabu kama aliyokuwa nayo baba yake. Pia alirithi sifa na tabia njema za baba yake, akaweza kujulikana na kuheshimiwa na Waarabu wote kama alivyokuwa akiheshimiwa baba yake Abul Muttalib.. Alikuwa shujaa na mwenye uwezo wa kuongoza, na kwa vile alikuwa mkubwa wa kabila la Makureshi aliweza kumlinda Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) asidhuriwe na Makureshi.
Katika ukoo huu uliokuwa ukiwaongoza Makureshi na waarabu wote kwa hekima na heshima na utukufu mkubwa kupitia karne nyingi sana, alitokea Ali (RA) mwana wa Abu Talib bin Abdul Muttalib bin Hashim bin Abdu Manaf, aliyerithi kutoka kwa baba yake Abu Talib kila sifa njema za ukarimu, ushujaa na ukweli.
Katika kitabu chake kiitwacho 'Abqariyat Imam Ali', na maana yake (Kipaji cha hekima cha Imam Ali), anasema Abbas al Aqqad; "Ali (RA) anajulikana kuwa ni mtu wa mwanzo katika kabila la Bani Hashim aliyezaliwa kutokana na baba na mama wote wakiwa wanatoka katika ukoo wa Al Hashimiy. Baba yake Ali (RA), jina lake ni Abu Talib bin Abdul Muttalib bin Hashim bin Abdi Manaf na mama yake pia jina lake ni Fatima bint Asad bin Hashim bin Abdi Manaf.
Inasemekana kuwa Ali (RA) alipewa na mamake jina la 'Haidarah', (na maana yake ni 'Simba'), sawa na jina la babu yake (babake mamake) ambaye jina lake lilikuwa 'Asad', na maana yake pia ni Simba, lakini baba yake akalibadilisha na kumpa jina la Ali." Ali (RA) alikuwa mdogo wa ndugu zake, na mkubwa wake alikuwa Jaafar kisha Aqiyl kisha Talib (RA). Inasemekana kuwa Aqiyl alikuwa kipenzi cha baba yake, na hii ndiyo sababu pale Abu Talib alipokuwa katika shida na Mtume (SAW) akifuatana na Hamza na Al Abbas walipomwendea Abu Talib kwa ajili ya kumsaidia ulezi wa watoto wake, akawaambia; "Niachieni mimi Aqil na wachukuweni muwatakao".
Al Abbas akamchukua Talib, Hamza akamchukua Jaafar, na Mtume (SAW) akamchukuwa Ali (Radhiya Llahu anhum).
Wake zake
Vitabu vya historia vinasema kuwa Ali (RA) hajawahi kuoa mke mwengine wakati alipokuwa akiishi na bibi Fatima (RA) binti wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW), lakini baada kufariki, Ali (RA) alioa wake wafuatao:
1. Umama bint Abul Aas (RA) binti yake bibi Zainab (RA) mwana wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW), na Abul Aas mume wa bibi Zainab alikuwa mtoto wa dada yake bibi Khadija binti Khuwaylid (RA).
2. Asmaa binti Umais (RA) aliyekuwa mke wa Jaafar bin Abu Talib na alipofariki Jaafar bibi Asmaa aliolewa na Abubakar (RA), na alipofariki Abubakar (RA) akaolewa na Ali (RA).
3. Fatima Ummul Baniyn.
4. Ummu Said binti Urwa bin Masaud Al Thaqafiy
5. Khaula binti Jaafar bin Qays
6. Al Suhabaa binti Rabia
7. Laila binti Masaud
8. Muhyaat binti Mruul Qays
Inasemekana pia kuwa alioa wake wengine zaidi ya hawa.
Ewe Dunia Mtafute Mwengine!
Muawiya bin Abu Sufyan (RA) alipomtaka Dhirar bin Dhamira Al Kanaaniy azungumze juu ya sifa za Ali bin Abu Talib (RAnhum), Dhirar akasema; "Ali bin Abu Talib alikuwa Wallahi mtu mwenye kuona mbali, mwenye nguvu nyingi, anasema kwa utulivu na anahukumu kwa uadilifu, elimu inabubujika kutoka katika kila sehemu yake, na hekima inazungumza kutoka katika kila kitendo chake, hakuipa thamani yoyote dunia wala mapambo yake.
Alikuwa akistarehe nyakati za usiku (pale anaposali) ndani ya kiza chake. Aikuwa Wallahi mwingi wa mafunzo, mwingi wa kufikiri, akipenda kupindua pindua viganja vya mikono yake pale anapofikiri, akipenda kuvaa nguo zisizokuwa ndefu sana (hakuwa akipenda kuvaa maguo mengi na makubwa yanayoburura), na alikuwa akipenda chakula kisichokuwa laini (hakuwa akipenda vyakula vya fakhari), Alikuwa Wallahi akijiweka kama mmoja wetu, tukimwendea anatusogelea na tunapomwita anatujia, na juu ya kujikurubisha nasi kwake, hatukuwa tukimsemesha sana kwa sababu ya haiba aliyokuwa nayo.
Alikuwa akiwatukuza wachaMungu na akiwapenda maskini. Mbele yake, mwenye nguvu muovu hawi na tamaa ya kuitimiza batili yake, na aliye dhaifu hakati tamaa ya kupata haki yake - Nashuhudia mbele ya Mwenyezi Mungu kuwa nilikuwa nikimuona wakati unapoingia usiku akiuendea msala wake huku akizishika ndevu zake na kulia kwa huzuni kubwa sana huku akisema; "Ya Rabbana ya Rabbana" - huku akimnyenyekea Mola wake, kisha anasema kuiambia dunia;
"Hay-haata hay-haata (hayawi hayawi). Ewe dunia mhadae mwingine, nimekwisha kukuacha talaka tatu wala sitokurejea tena. Umri wako mdogo, kukaa nawe ni hatari, na hatari zako zinakuja kwa wepesi, Aah! Aah! (nasikitika) kwa machache niliyojitayarishia, na safari ni ndefu na njia ni ya hatari." Muawiya (RA) akawa analia huku akijifuta machozi kwa kitambaa, na wote waliohudhuria hapo siku hiyo wakawa wanalia.
Sali Ubavuni Mwa Bin Ami Yako
Siku moja Abu Talib alimuona mwanawe Ali (RA) akisali nyuma ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW), na hii ilikuwa katika siku za mwanzo za Uislamu, na Ali (RA) hakuogopa wala kubabaika, na baada ya kumaliza kusali akamwendea baba yake na kumwambia kwa ufasaha; "Ewe baba yangu, nimemuamini Mwenyezi Mungu na kumfuata Mtume wake (SAW)".
Baba yake akamwambia; "Yeye hakuiti isipokuwa ndani ya jambo la kheri. Kuwa pamoja naye". Na siku ile Abu Talib alipomuona Ali (RA) akisali nyuma ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) kuliani kwake huku mwanawe Jaafar (RA) akiwa amesimama kwa mbali kidogo akiwatazama, Abu Talib akamwita Jaafar (RA) na kumwambia; "Kamilisha ubawa wa Bin ammi yako, nenda kasali upande wake wa kushoto".
Wa Mwanzo Kusilimu Katika Watoto
Ali (RA) alikuwa miaka minne wakati alipochukuliwa kulelewa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW), na alikuwa kesha timia miaka kumi pale wahyi ulipoanza kuteremka. Na siku ile alipomuona Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) akisali, alimuuliza;
"Unafanya nini?"
Mtume (SAW) akamwambia;
"Ninasali".
"Unamsalia nani?"
Mtume (SAW) akamwambia:
"Mola wa ulimwengu wote".
Ali (RA) akauliza;
"Nani huyu Mola wa ulimwengu wote?"
Mtume (SAW) akamwambia:
"Ni Mungu mmoja asiye na mshirika, aliyeumba, na mikononi mwake imo amri ya kila kitu, Naye ni Mweza wa kila kitu". Ali (RA) akazitamka shahada mbili na kuwa mtoto wa mwanzo kusilimu. Lakini juu ya udogo wa umri wake, alikuwa miongoni mwa wale waliokuwa wakihudhuria darsi za Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) katika nyumba ya Al Arqam bin Abul Arqam pamoja na masahaba wenye umri mkubwa kupita yeye kama vile Abubakar na Othman na Al Zubair na Twalha na Abdul Rahman bin Ouf na Saad bin Abi Waqqaas na wengine (RAnhum) tokea siku za mwanzo za Uislamu.
Niulizeni Kisha Niulizeni
Hakuwa akisema uwongo siku ile alipowaambia watu; "Niulizeni, kisha niulizeni kisha niulizeni mtakacho juu ya kitabu cha Mwenyezi Mungu, kwani Wallahi hapana hata aya moja katika aya zake ila ninaijua iwapo imeteremshwa usiku au mchana". Ali (RA) alilelewa katika nyumba ya Qurani, au tunaweza kusema kuwa alilelewa na yule aliyekabidhiwa Qurani, Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW). Akawa anaipokea kutoka katika kinywa chake kitukufu ikiwa bado mbichi na mpya, Qurani ambayo daima ni mbichi na mpya, maneno yake yasiyokonga wala kuchosha. Alikuwa akiwatangulia wenzake katika kuisikia Qurani pamoja na siri zake, ikimtakasa huku ikibubujika kutoka katika kinywa cha Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) wakati akikumbana na taathira zake. Hii ndiyo sababu iliyomfanya Ali (RA) awe mtiifu wa Qurani maisha yake yote.
Hakusema uwongo siku ile alipomuandikia Muawiya bin Abu Sufyan (RA) na kumwambia; "Mtume Muhammad ni ndugu yangu na mkwe wangu Na Hamza bwana wa mashahidi pia ni ami yangu Jaafar ambaye usiku na mchana anaruka na Malaika ni mtoto wa mama yangu Na binti wa Muhammad ni mke wangu na utulivu wangu Tumechanganya pamoja naye damu yangu na nyama yangu Wajukuu wawili wa Mtume kutoka kwake, nao pia ni wanangu Yupi kati yenu mwenye sehemu kubwa kuliko yangu? Nimetangulia katika Uislamu kabla kubalighi kwangu.
Uadilifu Wake (RA)
Siku moja aliipoteza ngao yake, naye wakati huo alikuwa Khalifa wa Waislamu. Alipokuwa akipita sokoni akaiona ikiwa mikononi mwa Myahudi aliyekuwa akitaka kuiuza. Ali (RA) alimwendea Myahudi huyo na kumwambia; "Ngao hii ni yangu imenianguka usiku wa siku fulani mahali fulani." Myahudi akasema; "Bali hii ni ngao yangu na imo mikononi mwangu ewe Amiri wa Waumini". Ali (RA) akasema; "Hii ni ngano yangu na mimi sikuwahi kumuuzia mtu yeyote wala kumpa zawadi mtu yeyote hata ikaweza kukufikia wewe". Myahudi akasema; "Atakayehukumu baina yetu ni kadhi wa Kiislamu". Ali (RA) akasema; "Sawa! twende kwa kadhi".
Wakaondoka pamoja na kuelekea kwa kadhi Shuraih, anayejulikana kwa uadilifu wake na kwamba ni mtu asiyemuogopa yeyote mbele ya haki. Shureih akasema; "Unasemaje ewe Amiri wa Waislamu?" Ali (RA) akasema; "Nimeiona ngao yangu hii kwa mtu huyu, na mimi ilinianguka usiku kadha na mahali kadha (akapataja mahala ilipomuanguka). Nashangaa vipi imekuwa yake wakati mimi sikupata kumuuzia mtu wala kuigawa". Shureih akasema kumuuliza Myahudi; "Unasemaje na wewe?"
Akajibu; "Ngao ni yangu na imo mikononi mwangu na mimi simtuhumu Amiri wa Waumini kuwa anasema uongo". Shureih akamgeukia Ali (RA) na kumwambia; "Mimi sina shaka yoyote kuwa maneno yako ni kweli tupu ewe Amiri wa Waumini, na kwamba ngao hii ni yako kama ulivyosema, lakini huna budi kuleta mashahidi wawili watakaoshuhudia juu ya madai yako". Ali (RA) akasema; "Ndiyo nitawaleta, nitamleta aliyekuwa mtumwa wangu niliyemuacha huru Qambar na mwanangu Al Hassan, nao watashuhudia juu ya ukweli wa madai yangu". Kadhi Shureih akasema:
"Lakini ushahidi wa mwana kwa ajili ya babake haukubaliwi ewe Amiri wa Waisalmu". Ali (RA) akasema; "Subhanallah! Mtu katika watu wa Peponi ushahidi wake haukubaliwi! Kwani hukumsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) akisema;
"Al Hassan na Al Hussein ni mabwana wa vijana wa Peponi?". Shureih akasema; "Naam! nimemsikia ewe Amiri wa Waislamu, isipokuwa mimi siukubali ushahidi wa mwana kwa ajili ya babake". Ali (RA) akamgeukia Myahudi yule na kumwambia; "Ichukue! kwani sina mashahidi wengine isipokuwa hao'. Myahudi akasema;
"Lakini mimi nashuhudia kuwa ngao hii ni yako ewe Amiri wa Waislamu". Kisha akaongeza kusema; "Ya Allah! Amiri wa Waislamu anahukumiwa na kadhi wake, na kadhi huyo anahukumu dhidi yake? Nashuhudia kwamba hapana Mola anayestahiki kuabudiwa isipokuwa Allah, na kwamba Muhammad ni Mtume wake. Nakujulisha ewe kadhi kuwa ngao hii ni ya Amiri wa Waumini na kwamba mimi nilikuwa nikimfuata alipokuwa akenda na jeshi lake mpaka alipofika mji wa Siffiyn na hapo ndipo ngao hiyo ilipomuanguka kutoka juu ya ngamia wake na mimi nikaiokota". Ali (RA) akamwambia;
"Kwa vile umesilimu, basi nakupa wewe ngao hii kama ni zawadi yako na pia nakupa zawadi farasi wangu huyu".
Anayependwa na Mwenyezi Mungu na Mtume Wake
Kutoka kwa Abul Abbas Sahal bin Saad Al Saidiy (RA), amesema kwamba siku ya vita vya Khaibar, Mtume (SAW) alisema; "Kesho nitampa bendera mtu ambaye kwa mikono yake Mwenyezi Mungu atatupa ushindi. Mtu huyo anampenda Mwenyezi Mungu na Mtume wake na anapendwa na Mwenyezi Mungu na Mtume wake". Anaendelea kusema Sahal (RA); "Usiku kucha watu walikuwa wakiwaza kwa kutaka kujua ni nani huyo mwenye kupendwa na Mwenyezi Mungu na Mtume wake atakayepewa bendera hiyo. Asubuhi yake watu wote wakaamkia kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW). Kila mmoja akitamani apewe yeye bendera siku hiyo".
Imepokelewa kuwa; Omar (RA) alisema; "Hakuna siku niliyotamani kupewa bendera kuliko siku hiyo". Baada ya watu kujikusanya mbele yake, Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) akauliza; "Yuwapi Ali bin Abu Talib?" Akajibiwa;
"Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, Ali anaumwa macho". Mtume (SAW) akasema; "Niitieni" Akaitwa, Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) akamtemea mate machoni pake huku akimpangusa na kuomba dua. Hapo hapo Ali (RA) akapona na kukabidhiwa yeye bendera hiyo. Ali (RA) akauliza; "Nipigane nao mpaka wawe kama sisi?" Mtume (SAW) akamwambia; "Nenda mpaka utakapofika katika mji wao. Kisha waite katika Uislamu na uwajulishe juu ya yale Mwenyezi Mungu anayotaka kutoka kwao…." Imeelezwa kuwa Ali (RA) alipoufikia mlango wa Khaibar (mji wa Mayahudi), alipiga ukelele na kusema; "Mimi Ali Bin Abu Talib".
Anasema Khalid Muhammed Khaled katika kitabu cha 'Khulafaa Rrasuul'; "Ali (RA) alikuwa akielewa namna gani jina hilo linavyoingiza khofu ndani ya nyoyo za makafiri, kwani mara baada ya kulitaja jina lake, kwa ghafla alishambuliwa na kupigwa pigo la nguvu mpaka ngao yake ikamuanguka, na mbele yake akawaona walinzi wa mlango huo waliokuwa wakimshambulia wakijitayarisha kummaliza, na yeye akiwa amelala chini bila ya kuwa na hata ngao ya kujikinga. Akasema moyoni mwake; "Leo ama nitaonja yale yaliyomkuta Hamza au Mwenyezi Mungu atanipa ushindi". Akainuka na kuwaendea walinzi hao na kuanza kuwasukuma huku na kule kwa nguvu zake zote. Ikisha akauendea mlango wa ngome hiyo ya Khaibar na kuung'oa kwa mikono yake". Anaendelea kusema Dr. Khaled;
"Watu kabla hawakujua nini kinachotendeka walistukia Ali (RA) akitoa takbir kwa sauti kali; "Allahu Akbar", na kumuona keshaubeba mlango huo kwa mikono yake miwili. Anasema Abu Raafi-a (RA) ambaye alikuwa katika kikosi cha Ali (RA); "Tulijaribu mimi na wenzangu saba kuubeba mlango huo tukashindwa". Ali (RA) pamoja na majeshi yake wakawa wanashambulia huku wakiingia ndani ya mji wa Khaibar. Haukupita muda mrefu wakafanikiwa kuuteka mji huo. Alipoletewa habari za kutekwa kwa mji huo Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) akasema; "Allahu Akbar! ishaangamia Khaibar - Hakika sisi tunaposhuka uwanja wa watu itakuwa asubuhi mbaya kwa wale walioonywa (wasionyeke)".
Bukhari na Muslim
Askari Mwenye Adabu
Ali (RA) alikuwa askari mwenye wingi wa adabu na heshima. Na kwanini asiwe hivyo wakati amelelewa katika nyumba ya mwalimu wa adabu Muhammad (SAW) aliyefundishwa adabu na Mola wake Subhanahu wa Taala. Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) amesema; "Amenifundisha Mola wangu na amenifundisha vizuri". Katika vita vya Uhud, Abu Saad bin Abi Twalha aliyekuwa msitari wa mbele katika majeshi ya makafiri alipaza sauti yake juu akimwita Ali bin Abu Talib (RA) kumtaka apambane naye. Ali akauitikia mwito huo kwa kujisogeza mbele mpaka wakawa uso kwa uso na mapambano makali yakaanza baina yao. Ali (RA) alifanikiwa kumpiga Abu Saad pigo la nguvu na kumuangusha chini huku akilia kutokana na maumivu makali, lakini alipounyanyua upanga wake juu tayari kumuuwa, nguo ya Abu Saad ikafunuka na utupu wake ukawa unaonekana. Ali (RA) akafumba macho huku akigeuka na kurudi nyuma kuelekea msitari wa mbele wa jeshi la Waislamu akimwacha adui yake huyo amelala chini.
Alipoulizwa; "Kwa nini hujamuua?" Akajibu; "Alinikabili kwa utupu wake nikamuonea huruma". Si hivyo tu, bali hata baada ya majeshi ya Ali (RA) kushinda katika vita vya Al Jamal, na kabla ya vita vya Siffiyn kuanza, Ali (RA) alipata habari kuwa watu wawili katika jeshi lake na majina yao ni Hajar bin Uday na Omar bin Al Hamaq walikuwa wakimtukana Muawiya bin Abu Sufyan (RA) kwa dhahiri, jambo lililomkasirisha sana Ali (RA) aliyewaita na kuwataka waache matusi yao. Wakamuuliza; "Ewe Amiri wa waumini, kwani sisi si tupo katika haki?" Ali (RA) akajibu;
"Ndiyo, naapa kwa Mungu wa Al Kaaba (kuwa sisi tupo katika haki)". Wakamuuliza; "Sasa kwa nini basi unatukataza tusiwatukane?" Ali (RA) akawaambia; "Sipendi muwe watukanaji wanaopenda kulaani watu. Bora mseme; "Mola wetu zuwia damu yetu na damu yao isimwagike na utupatanishe, na uwatowe kutoka katika makosa yao mpaka waijuwe haki na batil ili wasijiingize ndani yake (batili hiyo)". Anasema Dr. Khalid Muhammad Khalid; "Huyu ni mpiganaji mwenye heshima ya hali ya juu, na huu ni ushujaa wa hali ya juu usiopatikana isipokuwa kwa mwanamume wa kweli, na unaofaa kuigwa na wanaume wa kweli".
Abu Sufyan
Abu Sufyan alitumwa na makafiri wa Makka kwenda Madina kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) kumuomba msamaha baada ya wao Makureshi kuvunja baadhi ya masharti ya mkataba wa Hudaibia. Alipowasili Madina hapana hata Muislamu mmoja aliyekubali kukaa au kuzungumza naye. Alipoamua kwenda nyumbani kwa binti yake Umm Habiba Ramlah bint Abu Sufyan (RA) ambaye ni mke wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW), binti yake huyo alikataa kumuacha baba yake akae hata juu ya tandiko la mumewe, akalikunja na kumuacha baba yake akae chini. Alipomuuliza binti yake: "Kwa nini hutaki nilikalie tandiko hili?" Akamwambia;
"Kwa sababu wewe ni mshirikina na kwa ajili hiyo hustahiki kulikalia tandiko la Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW)". Aliporudi Makka Abu Sufyan akawahadithia Makureshi yaliyomkuta Madina, akasema; "Nikamwendea mwana wa Abi Quhafa (Abubakar Al Siddiq (RA)) lakini sikupata msaada wowote kutoka kwake. Kisha nikamwendea Ibni l Khattab (Omar (RA)) nikamuona amegeuka kuwa adui mkubwa., akanambia; "Unataka mimi nikakuombeeni msamaha kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu? Wallahi lau kama sitapata kitu cha kukupigeni isipokuwa punje ndogo ndogo basi nitapigana nanyi jihadi kwa punje hizo", kisha nikamwendea Ali, nikamuona ni mwenye huruma kupita wote".
Vita Vya Al Ahzab (Khandaq)
Makabila mbali mbali ya washirikina yaliungana na kuunda jeshi kubwa la watu wapatao elfu kumi kwa ajili ya kuwapiga vita Waislamu hapo Madina, na hii ilikuwa baada ya washirikina hao kuchochewa na Mayahudi wa mji huo. Riwaya nyingine zinasema kuwa jeshi hilo lilikuwa la watu wapatao elfu ishirini na nne, na idadi hii ilikuwa kubwa kuliko idadi ya watu wote wanaoishi Madina wakijumuishwa na wanawake na watoto wa mji huo. Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) aliitisha baraza la ushauri kuzungumzia mpango wa kuuhami mji wao kutokana na uadui huo, na baada ya mashauriano na rai mbali mbali, wakakubaliana juu ya rai ya Salman Al Farsiy (RA) aliyesema: "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, katika ardhi ya Wafursi tulikuwa pale tunapozungukwa tukichimba handaki lenye kuuzunguka mji wetu".
Anasema Al Mubarak Furriy katika kitabu cha 'Al Rahiyq al Makhtum; "Haya yalikuwa maarifa mazuri ambayo Waarabu kabla ya hapo hawakuwa wakiyajua". Wachache sana miongoni mwa makafiri akiwemo Amr bin Abd Wud Al Amry aliyekuwa mpiganaji mwenye nguvu nyingi anayejulikana kwa ujabari na ukhabithi wake waliweza kuvuka na kuwafikia Waislamu waliokuwa upande wa pili wa handanki hilo kwa kupitia njia ndogo iliyojibana. Ali (RA) alipambana na Amr na akaweza kumuuwa, na Al Zubair (RA) alipambana na Nofel bin Abdullahi al Mughiyra al Makhzumiy naye pia akafanikiwa kumuua.
Fathul Bari (Sharhi ya Sahih al Bukhari). Imepokelwa katika Mustadrak ya Al Hakim hadithi iliyo sahihi kwa shuruti zilizowekwa na Maimam Bukhari na Muslim inayosema kuwa; "Miongoni mwa walioweza kulivuka handaki hilo kupitia njia iliyojibana alikuwa Amr bin Abdu Wud Al Amry aliyewahi kupigana katika vita vya Badr akaumizwa mguu, na hakuwahi kupigana vita vya Uhud. Ali (RA) akamtokea na kumwambia; "Ewe Amr, niliwahi kukusikia pale penye Al Kaaba ukisema kuwa mtu akikuita katika mambo mawili utakubali moja wapo". Akasema; "Ndiyo"
Akamwambia; "Basi mimi nakwita utoe shahada ya 'Laa ilaaha illa Llah wa anna Muhammadan rasuulu Llah' na nakwita katika Uislamu". Amr akasema; "Sina haja na yoyote katika mawili hayo". Ali (RA) akamwambia; "Basi nakwita tupambane mimi na wewe". Akasema; "Mimi sitaki kukuua". Ali (RA) akasema; "Lakini mimi nataka kukuua". Wakapambana na Ali (RA) akamuua Amr."
Msitari wa Mbele
Ali (RA) alikuwa msitari wa mbele katika kila anachowaamrisha au kuwanasihi Waislamu. Alikuwa msitari wa mbele katika ucha Mungu, katika kupigana jihadi, katika mwenendo na tabia njema, katika kutoa, katika ustahamilivu, katika kuikinai dunia na katika kila nyanja ya maamrisho ya Kiislamu. Siku moja alipokuwa katika mji wa Al Kufa na baada ya kuwasalisha Waislamu Sala ya Alfajiri, alikaa kimya muda kidogo huku uso wake ukionesha dalili ya huzuni nyingi. Aliendela kukaa akiwa katika hali hiyo huku watu wakimuangalia na kuuheshimu ukimya wake huo mpaka jua lilipochomoza vizuri na miale yake kuenea katika kuta za msikiti, kisha akainuka na kusali raka-a mbili kisha akatikisa kichwa chake kwa masikitiko na kuvipindua pindua viganja vya mikono yake huku akisema;
"Wallahi nimewaona Masahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW), na wala simuoni kati yenu yeyote anayefanana nao. Walikuwa wakati wa asubuhi zinaonekana juu ya nyuso zao dalili ya kukesha kwao huku wakifanya ibada na kusoma Qurani na kurukuu na kusujudu. Na wanapokuwa wakimdhukuru Mwenyezi Mungu, utaviona vichwa vyao vimeinama kwa unyenyekevu mfano wa miti inavyoinama siku za upepo mkali huku macho yao yakibubujika machozi mpaka nguo zao kuroa". Anasema Khalid Muhammed Khalid katika kitabu chake 'Khulafaa Rrasuul'; "Ali (RA) anatujulisha hapa juu ya hali ilivyokuwa katika zama tukufu kupita zote, siku za Wahyi na utume, siku ambazo nafsi ya Ali (RA) ingali inaishi ndani yake na akawa anaendelea kuishi ndani yake katika maisha yake yote. Hata wakati ukisonga mbele namna gani, hawezi kuusahau utukufu ule na mapenzi yake juu ya Masahaba wa Mtume (SAW) ambao pia ni Sahibu zake. Hawezi kuiondoa heshima yake juu yao, wala kuwasahau, na hawezi pia kuuondoa utukufu na mapenzi yake juu ya siku hizo ndani ya moyo wake, ndani ya dhati yake, kwa sababu huo ndio mwenendo wake na hayo ndiyo makimbizi yake".
Maneno ya Hekima
Ali (RA) alikuwa mwingi wa hekima, na zifuatazo ni baadhi ya kauli zilizonukuliwa kutoka kwake; "Jifunzeni ilimu ili muwe watu wake. Jueni kuwa dunia tunaiacha nyuma na akhera tunaikabili, na kila moja kati ya nyumba mbili hizo ina watu wake. Basi kuweni watu wa akhera na wala msiwe watu wa dunia. Wale waloikinai dunia, wameijaalia ardhi yake kuwa busati lao, udongo kuwa tandiko lao, na maji kuwa pambo lao. Mwenye kuipenda akhera lazima ajiweke mbali na matamanio, na mwenye kuuogopa moto ajiweke mbali na yaliyoharamishwa. Mwenye kuitaka Pepo akimbilie kumtii Mwenyezi Mungu, na aliyeikinai dunia hayapi umuhimu wowote masaibu yake. Jueni kuwa Mwenyezi Mungu ana waja wake, amewahifadhi wasifanye shari, nyoyo zao za huzuni, nafsi zao zimekinai, matakwa yao machache, wamesubiri siku chache ili wapata raha za milele".
Anapomsikia mtu akiitukana dunia alikuwa akimwambia; "Dunia ni nyumba ya ukweli, mahali panapoteremka Wahyi, msikiti wa Mitume, mahala pa kufanya biashara (na Mwenyezi Mungu) kwa wanaomjua (Mwenyezi Mungu). Kwa hivyo ndani ya dunia chumeni rehema za Mwenyezi Mungu ili muipate Pepo Yake". Hakubadilika hata kidogo (RA) tokea utoto wake mpaka ukubwani. Na hata katika zama za hatari, zama za vita, Ali (RA) alikuwa akiuweka mbele ucha Mungu wake. Hakuwa akiongoza watu kwa akili zake, na hekima yake ya hali ya juu peke yake, bali kwa ucha Mungu wake pia. Hakuwa akitaka chochote kutoka kwao isipokuwa wawe wacha Mungu, kwa sababu anayemuogopa Mola wake, ndiye askari wa kuaminika.
Na siku ile ya mapamabano baina yake na Muawiya (Radhiyallahu Anhuma), alipoambiwa na bin ammi yake Abdullahi bin Abbas (RA), ambaye naye pia ni mcha Mungu; "Tumia hadaa, kwa sababu vita ni hadaa". Ali (RA) akamjibu; "Abadan, sitoiuza dini yangu kwa dunia". Anasema Khalid Muhammed Khalid; "Mtu adhimu aliyekuwa akiufundisha ulimwengu uaminifu, utakatifu, na utiifu kwa Mola wake".
Hotuba yake ya mwanzo alipowasili mji wa Al Kufa
Katika hutoba yake ya Ijumaa ya mwanzo aliyowahutubia Waislamu mara baada ya kuwasili mji wa Al Kufa, Ali (RA) alianza hotuba yake kwa kuwausia Waislamu katika kumcha Mwenyezi Mungu, akasema; "Nakuusieni waja wa Allah kumuogopa Allah, kwani Taqwa ni jambo bora la kunasihiana baina ya waja wa Allah, na ndiyo amali anayoridhika nayo Mwenyezi Mungu kutoka kwa waja wake. Mumeamrishwa kumcha Mungu na kwa ajili ya wema mumeumbwa, kwa hivyo ogopeni yale Allah aliyokutahadharisheni nayo, kwa sababu amekutahadharisheni na adhabu kali kabisa.
Muogopeni Mwenyezi Mungu kuogopa kwa kweli na tendeni matendo yenu bila ya kujionesha kwa watu wala kutaka sifa au umaarufu, kwani mwenye kufanya amali yoyote ile kwa ajili ya kujipendekeza kwa mwengine asiyekuwa Allah, basi Mwenyezi Mungu humsukumiza nazo amali zake kwa huyo aliyemfanyia amali hiyo. Ogopeni adhabu ya Mwenyezi Mungu, kwa sababu hajakuumbeni kwa upuuzi, na wala hakuacha chochote kiende ovyo. Keshataja athari zenu na keshajua siri zenu na kuzihesabu amali zenu na kuziandika ajali zenu. Kwa hivyo dunia isikubabaisheni kwani inawaghururisha watu wake, na ameghurika yule atakayebabaishwa nayo.
Na jueni ya kuwa Akhera ndiyo makazi ya milele".
Siku moja kabla majeshi yake na majeshi ya Muawiya (RA) kupambana katika vita vya Siffiyn, Ali (RA) hakuwahutubia majeshi yake kwa maneno ya hamasa, bali aliwahutubia kwa kuwaambia maneno yanayohitalifiana kabisa na maneno yanayosemwa na majemadari katika hali kama hiyo. Ali (RA) alisema; "Kesho mtapambana na kaumu, kwa hivyo usiku wenu ufanyeni uwe mrefu kwa kusali na zidisheni katika kusoma Qurani na muombeni Mwenyezi Mungu akupeni subira, maghufira na afya." Katika wakati wa amani au katika wakati wa vita, anapokuwa ameshinda au anapokuwa katika shida yoyote ile, hapana kinachomshughulisha isipokuwa kumcha Mola wake Subhanahu wa Taala.
Isipokuwa vita vya Tabuk
Huo ndio msimamo wake, na namna hii ndivyo alivyokuwa akivikabili vita vyote alivyoshiriki. Ali (RA) alishiriki katika vita vyote vilivyopiganwa wakati wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) isipokuwa vita vya Tabuk, wakati Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) alipomuamrisha abaki Madina kwa ajili ya kuwalinda watu wa nyumba yake. Jambo hilo lilimhuzunisha sana Ali (RA), kwa sababu katika vita hivi hapana aliyebaki Madina isipokuwa wanawake, wazee, watoto wadogo, na wanafiki waliokuwa wakijulikana kwa unafiki wao, na walibaki pia Wale Watatu Waliongojeshwa ambao kisa chao kimetajwa katika Suratu al Tawba.aya ya 18 na kuendelea mbele. Ali (RA) akamwambia Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW); "Unaniweka mlinzi juu ya wanawake na watoto?"
Mtume (SAW) akamjibu mbele ya Masahaba wake wote (RAnhum) kwa kumwambia; "Haikuridhishi kuwa wewe kwangu mfano wa Harun alivyokuwa kwa Musa, isipokuwa hapana tena Mtume baada yangu?"
Khalifa na mfano mwema
Mwenyezi Mungu amejaalia Ali (RA) awe Khalifa katika wakati mgumu sana, wakati ambao hapana mwengine katika wakati wake angeliweza kuumudu, na Waislamu walikuwa na haja kubwa sana ya uongozi wa mcha Mungu mfano wake, muadilifu pamoja na hekima yake, kwa sababu wakati wa utawala wake yalizuka masaibu na matatizo mengi magumu sana pamoja na fitna nyingi baina ya Waislamu, lakini mwanafunzi huyu ambaye ni miongoni mwa wanafunzi wa mwanzo wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) alisimama imara mbele ya kimbunga hicho kilichomkabili yeye, pamoja na umma wa Kiislamu. Katika maamuzi yake alikuwa daima akikumbuka jinsi Ustadhi wake Mtume wa Mwenyezi Mungu Muhammad (SAW) alivyokuwa akiyakabili kwa hekima kubwa mitihani mingi iliyokuwa ikimkuta, alikuwa akikumbuka maneno aliyowahi kumsikia akimuambia Ammi yake Abu Talib pale alipomshauri kuacha kuulingania Uislamu kutokana na mateso na maudhi aliyokuwa akiyapata kutoka kwa Makureshi, na Mtume (SAW) akamjibu;
"Wallahi lau kama wataliweka jua katika mkono wangu wa kulia na mwezi mkono wangu wa kushoto, basi sitoicha amri hii mpaka Mwenyezi Mungu atakapoidhihirisha au nife kwa ajili yake". Hakuisahau pia siku ile ya 'Fat'hi Makka', siku Waislamu walipouteka mji wa Makka, na hakuzisahau zile nyuso za makafiri wa Makka waliokuwa kabla ya hapo wakiwatesa na kuwauwa Waislamu, wakiwadhulumu na kuwadhulumu kila walichokimiliki. Na pia katika vita vya Uhud namna walivyomuuwa ami yake, Hamza (RA) bwana wa Mashahidi. Siku hiyo Makureshi waligeuka wao kuwa mateka wa majeshi ya Kiislamu, wakakusanywa upande mmoja wakingojea hukumu kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) itakayoamua mustakbali wao; hukumu kwa walivyokuwa wakitaraji kuwa hawatosalimika.
Akakumbuka pia namna gani siku ile Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) alivyosimama mbele ya mateka hao na kuwahutubia akiwauliza; "Mnadhani nitakufanyeni nini?" Wakajibu; "Kheri, ewe ndugu mkarimu na mwana wa ndugu mkarimu". Mtume (SAW) akawaambia; "Nendeni, nyote mko huru".
Ali (RA) hakuisahau pia siku ile ami yake Al Abbas (RA) alipomwendea Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) na kumuomba ampe ugavana katika mojawapo ya wilaya za Kiislamu. Juu ya kuwa Al Abbas (RA) ni ami yake Mtume (SAW) tena ni mtu muadilifu, mcha Mungu na shujaa, lakini Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) alimjibu kwa kumuambia; "Sisi Wallahi ewe ammi yangu, hatumpi kazi hii mwenye kuiomba wala hatumpi mwenye kuichunga ". Alikuwa akipenda kujikumbusha maneno na maamuzi ya hekima pamoja na uvumilivu na ushujaa wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW), na kuyafanya kuwa dira yake na mfano wake bora wa kuufuata.
Mwanzo wa kuhukumu kwake
Ali (RA) alikuwa mwingi wa hekima na hodari wa kutoa hukumu. Mara nyingi Abu Bakar (RA) alipokuwa khalifa wa Waislamu alikuwa akimwendea kutaka msaada wake huku akimwambia; "Tupe fatwa juu ya jambo hili ewe Abal Hassan (baba wa Hassan)". Omar bin Khattab (RA) naye pia mara nyingi alikuwa akimwendea Ali (RA) kutaka ushauri wake, na aliwahi kumwambia; "Lau kama si Ali, basi Omar angeangamia". Othman (RA) alipokuwa khalifa naye pia mara nyingi alikuwa akimwita Ali (RA) na kumtaka ushauri wake katika matatizo mbali mbali,na hili si jambo la kushangaza kwani Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) aliwahi kusema; "Mbora wenu katika kutoa hukumu ni Ali." Ibni Majah - Sehemu ya (1) mlango wa fadhila za Masahaba Abu Yaala Sayuty katika Jameal Saghiyr -mlango wa herufi ya hamza, na wengine
Jukumu lake la kuhukumu lilianza pale waasi waliokuwa wameizunguka nyumba ya Othman bin Affan (RA) waliporudi mara ya pili baada ya kukubali ushauri wa Ali (RA) hapo mwanzo wa kuondoka kuelekea makwao. Waasi hao walirudi baada ya kuikamata barua inayowataka magavana wa Misri na AlKufa kuwauwa waasi hao wote mara watakapowasili huko. Ali (RA) alijaribu tena kuwataka waasi hao waondoke na kurudi makwao, lakini mara hii walikataa. Juu ya kuwa Othman (RA) alikanusha, na sisi tunaamini kuwa Othman (RA) amesema kweli alipokanusha, kwani huyu ni mtu ambaye Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) amesema juu yake kuwa hata Malaika wanamsitahi. Kwa hivyo ikajulikana kuwa waasi hao hawakurudi mara hii isipokuwa kwa sababu ile ile iliyowaleta hapo mwanzo nayo ni kumuuwa Khalifa wa Waislamu Othman bin Affan (RA).
Katika riwaya iliyopokelewa na Shaddad bin Aus (RA) anasema; "Baada ya kutambua hayo, Ali (RA) akatoka nyumbani kwake akiwa amevaa kilemba cha Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) na kuubeba upanga wake akielekea moja kwa moja nyumbani kwa Khalifa Othman (RA), akiwa amefuatana na mwanawe Al Hassan na Abdullahi bin Omar bin Khattab pamoja na baadhi ya Masahaba watu wa Makka na wa Madina (RAnhum). Akaingia nyumbani kwa Khalifa na kumsalimia kisha akamwambia; "Naona watu hawa hawataridhika isipokuwa kukuuwa, kwa hivyo tuamrishe tupigane nao". Othman (RA) akasema;
"Nakuombeni kwa jina la Mwenyezi Mungu ikiwa yupo kati yenu anayemshuhudia Mwenyezi Mungu kikweli na akaelewa kuwa mimi nina haki yoyote ile juu yake, basi arudishe upanga ndani ya ala yake na aondoke na isimwagike damu kwa ajili yangu". Ali (RA) akarudia tena na tena kumwambia maneno hayo, lakini Othman (RA) akaendelea kukataa., kwa hivyo Ali (RA) akatoka na kuelekea msikitini, na Sala iliposimamishwa watu wakamtaka Ali (RA) awasalishe, wakamwambia; "Ewe Abul Hasan, tangulia usalishe watu". Akawajibu;
"Sitakusalisheni wakati nyumba ya Khalifa wa Waislamu imezungukwa, nitasali peke yangu". Akasali peke yake. Kisha akatoka na kuelekea nyumbani kwake akiwaacha wanawe wawili pamoja na baadhi ya Masahaba (RA) waulinde mlango wa nyumba ya Othman (RA). Waasi walielewa kuwa kila wakikawia kuutimiza uadui wao, mambo hayatakuwa mazuri upande wao. Yakatokea yaliyotokea, na Khalifa wa Waislamu Othman bin Affan (RA) akauliwa kwa njia ya kikhabithi, na mkewe Bibi Naila (RA) alipokuwa akijaribu kumkinga akakatwa vidole vya mkono wake pamoja na sehemu ya kiganja, na hapo ndipo uti wa mgongo wa mwanzo wa Waislamu ulipovunjika.
Ali (RA) anaukataa Ukhalifa mara tatu
Ali (RA) alikuwa ameketi msikitini pamoja na watu wapatao kumi zilipomfikia habari za kuuliwa kwa Khalifa Othman (RA), akaondoka haraka kuelekea nyumba ya Khalifa na alipowasili akaanza kwa kuwapiga wanawe Al Hassan na Al Hussein huku akiwaambia; "'Tabban lakum' (Mtaangamia), vipi anauliwa Khalifa wa Waumini na nyinyi mpo mlangoni pake?". Mji wa Madina ulibaki bila ya khalifa muda wa siku tano, na katika siku zote hizo aliyekuwa akitamba mjini hapo na kutoa amri alikuwa Al Ghafiqiy bin Harb mtu aliyemuuwa Khalifa wa Waislamu Othman bin Affan (RA). Wamisri waliokuwa wengi wa waasi hao walimuendea Ali (RA) mara mbili wakimtaka awe Khalifa wa Waislamu lakini Ali (RA) alikataa. Wakamwendea Twalha (RA) naye pia akakataa, kisha wakatoka na kumwendea Al Zubair (RA) naye pia akakataa, kisha wakamwendea Abdillahi bin Omar (RA), naye akakataa na mwisho wakamwendea Saad bin Abi Waqaas (RA) ambaye pia alikataa, na walipomrudia tena Ali bin Abu Talib (RA) akakataa tena .
Hapana aliyethubutu kubeba jukumu la ukhalifa wakati umma umekabiliwa na tatizo kubwa kama hilo, na nani atakayethubutu ikiwa Ali mwenyewe (RA) ameukataa? Wote walioukataa walikuwa wakihofia yale yatakayotokea baadaye, kwani atakayeshika uongozi itambidi awahukumu wauaji wa khalifa wa tatu wa Waislamu Othman (RA) kwa kifo kwa ajili ya kitendo kiovu hicho. Lakini wakati huo huo lazima ajitokeze mtu wa kuiongoza dola ya Kiislamu. Lazima achaguliwe Khalifa kwa sababu kila wakati unaposogea na nchi kuwa bila ya Khalifa, hatari inayotokana na wenye tamaa inaongezeka. Hatari inayoweza kuiparaganya dola ya Kiislamu, kuutawanya umma na kuupotezea mustakbali wake. Anasema Dr.Khalid Mohammad Khalid;
"Watu waliitambua hatari hiyo, pamoja na hatari ya waasi ambao baada ya kumuuwa Othman (RA) wakawa wanaeneza chuki, bughudha pamoja na uongo mwingi juu ya Khalifa huyo mtukufu (RA). Wote waliitambua hatari ambayo mfano wake ilikuwa kama kimbunga kitakachouangamiza umma wote. Wakatambua kuwa lazima awepo kiongozi madhubuti atakayezishika hatamu na kuuongoza umma na kuwavusha nje ya bahari hii iliyochafuka. Wakakusanyika watu wema katika watu wa Makka na wa Madina na kumwendea Ali (RA), na baada ya mazungumzo ya hekima kupita baina yao, Ali (RA) akakubali kufungamana ili awe Khalifa wao. Hapakuwa katika Masahaba wa Mtume (RA) wakati ule aliyestahiki kuwa Khalifa kupita Ali (RA), na hapakuwa na mtu aliye na kipaji, uwezo, hekima na ushujaa kupita yeye. Wakati huo ukhalifa wenyewe haukuwa kitu chenye manufaa yoyote ya kidunia, bali ulikuwa ni mzigo mkubwa kwa yule atakayeubeba na ulikuwa ni hatari kubwa kwa mwenye kumuogopa Mola wake". (Mwisho wa maneno ya Dr. Khalid).
Wa mwanzo kufungamana naye
Wa mwanzo kufungamana naye, aliyeuingiza mkono wake ndani ya mkono wa Ali (RA) siku hiyo alikuwa ni Twalha bin Ubaidullah (RA) aliyefungamana naye kwa mkono wake wa kulia uliokatika katika vita vya Uhud pale alipokuwa akipigana kwa ajili ya kumkinga Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) aliyekuwa amezungukwa na maadui . Anasema Ibn Kathir katika 'Al Bidaya wal Nihaya; "Ali (RA) akatoka moja kwa moja na kuelekea msikitini. Akapanda juu ya membari akiwa amevaa nguo zake pamoja na kilemba huku akiwa amekamata bakora yake. Akasimama akiwa ameiegemea bakora hiyo, na watu wote wakafungamana naye hapo. Hiyo ilikuwa ni siku ya Jumamosi tarehe kumi na tisa mwezi wa Dhul Hijjah.
Wa mwanzo kufungamana naye alikuwa Twalha (RA) kwa mkono wake uliokatwa siku ya vita vya Uhud, na yule aliyemuuwa Othman (RA) alipoona vile akasema (kwa kejeli); "Inna lillahai wa inna ilayhi raajiun". Na wa pili kufungamana naye alikuwa Al Zubair (RA) kisha wakafuatilia Waislamu wote kufungamana naye mmoja baada ya mmoja". Anaendelea kusema Ibni Kathir;
"Na katika hotuba yake ya mwanzo siku hiyo, Ali (RA) alimshukuru Mwenyezi Mungu akampwekesha, kisha akasema; "Hakika Mwenyezi Mungu ameteremsha kitabu kinachotujulisha nini kheri na nini shari. Kwa hivyo ifuateni kheri na epukaneni na shari. Mwenyezi Mungu ameharamisha mengi, akaitukuza heshima ya Muislamu na kuifadhilisha kupita kila kitu". Ali (RA) akawataka Waislamu waheshimiane na wawe na ikhlasi katika amali zao na katika Tauhid pamoja na kuhurumiana na kupendana, na akawajulisha kuwa Mwislamu mwema ni yule ambaye Waislamu wenzake watasalimika na ulimi wake pamoja na mkono wake na kwamba si halali kwa Muislamu kumuudhi Muislamu mwenzake. Akasema; "Kumbukeni kuwa watu wapo mbele yenu na akhera ipo nyuma yenu (inakuja). Mnapoiona kheri, ifuateni, na mnapiona shari, iepukeni, na kumbukeni pale mlipokuwa wachache madhaifu mlipokuwa mkionewa juu ya ardhi". (Mwisho wa maneno ya Ibni Kathir).
Kuwalani wauaji wa Othman (RA)
Atakayechunguza maisha ya Ali (RA) ataona kuwa yale matatizo na mapambano mbali mbali aliyokuwa akikabiliana nayo tokea utotoni mwake, pamoja na hekima na busara kubwa iliyojificha ndani ya dhati yake, ilikuwa muda wote huo ikimlea Khalifa huyu mtukufu kwa ajili ya kumtayarisha na mitihani mbali mbali atakayopambana nayo katika wakati huu mgumu kupita nyakati zote katika historia ya Waislamu. Kuanzia siku ya mwanzo ya utawala wake baadhi ya Masahaba (RA) walimwendea nyumbani kwake wakimtaka awakamate wauaji wa Othman (RA) na kuwahukumu, lakini Ali (RA) aliwaambia; "Wakati bado haujafika, kwani waasi hawa ni wengi sana na idadi yao inapindukia watu elfu kumi. Kwa hivyo itakuwa bora kama tutasubiri mpaka pale nitakapojimakinisha barabara."
Maneno hayo yaliwakasirisha masahaba hao (RA), wakatoka kwa ghadhabu huku wakimtuhumu Ali (RA) kuwa hataki kuwakamata waasi. Miongoni mwa waliochukuwa msimamo mkali sana katika jambo hili walikuwa Twalha, Al Zubair na Muawiya bin Abu Sufyan (Mwenyezi Mungu awe radhi nao wote). Anasema Ibni Jariyr; "Mara baada ya watu kufungamana na Ali (RA), Naila, mke wa Othman bin Affan (RA) alimwita Al Noaman bin Bashir (RA) na kumpa nguo ya Othman iliyojaa damu aliyokuwa ameivaa siku aliyouliwa, pamoja na vidole vyake (Bibi Naila) kikiwemo kiganja chake kilichokatwa na waasi pale alipokuwa akimkinga mumewe, na kumtaka Al Noaman avipeleke nchi ya Sham kwa Muawiya bin Abu Sufyan (RA).
Muawiya alilia sana alipoviona vitu hivyo, akavichukuwa na kuvipeleka moja kwa moja mpaka ndani ya msikiti wa Damascus na kuvitundika juu ya membari ya msikiti ili kila mtu aweze kuviona na kuhamasika katika kudai kisasi cha kuuliwa Khalifa huyo wa tatu wa Waislamu . Akapanda juu ya membari na kuwahutubia watu waliokuwa wakilizana kwa uchungu mkubwa sana na kwikwi kila anapovinyanyua vitu hivyo ili wavione, na akaendela na kazi hii ya kuhamasisha watu muda wa karibu mwaka mzima. Al Zubair (RA) naye aliwahi kumuomba Ali (RA) ampe ugavana wa mji wa Al Kufa, na Twalha (RA) akataka apewe ugavana wa Basra ili waweze kukusanya watu wengi na kutayarisha jeshi kubwa la kupambana na wauaji wa Khalifa Othman (RA), lakini Ali (RA) akawataka msamaha na kuwaambia;
"Mtanisamehe sana, lakini kwa wakati huu jambo hili haliwezekani kutendeka". Masahaba hao hawakuridhika na msimamo huo. Wakaondoka kwa ghadhabu, jambo lililosababisha kuvunjika kwa mfupa wa pili wa mgongo wa Kiislamu.
Chanzo cha tukio la ngamia (Waqa'at al Jamal)
Kilichozidi kuharibu mambo na kuyafanya yawe magumu zaidi kwa Ali (RA), ni kule kujiunga kwa Bibi Aisha (RA) pamoja na wale wanaodai kisasi cha kuuliwa kwa Khalifa Othman (RA). Wakati Othman (RA) alipouliwa, Bibi Aisha pamoja na wake wenzake wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) walikuwa Makka kwa ajili ya kufanya Umra, na pia kwa ajili ya kuwa mbali na uasi ulioanza kudhihiri wakati ule dhidi ya Othman (RA), na Bibi Aisha (RA) alipata msituko mkubwa aliposikia habari za mauaji hayo. Al Zubair bin Al Awaam na Twalha (RAnhum) waliondoka Madina baada ya kuruhusiwa na Ali (RA), ingawaje baadhi ya Masahaba (RA) walimshauri Ali (RA) asiwaruhusu kuondoka wakihofia wasije kuungana na Muawiya (RA) na kusababisha upinzani mkubwa dhidi yake.
Masahaba wawili hao (RA) pamoja na maelfu ya watu waliokuwa nao waliungana na Bibi Aisha (Radhiyallahu anha), na wote kwa pamoja wakaondoka kuelekea mji wa Basra kwa ajili ya kujaribu kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huo. Ali (RA) naye aliondoka Madina kuelekea Al Kufa akiwa na kundi kubwa la watu, na katika kila mji aloupitia watu wengi wa miji hiyo waliungana naye, isipokuwa alistushwa sana alipopata habari za kujiunga kwa Bibi Aisha (Radhiyallahu anha) na kundi la wanaotaka kisasi cha damu ya Othman (RA) kilipwe kwa haraka. Ali (RA) alikuwa na uhakika kuwa Bibi Aisha, Al Zubair na Twalha (RA), wote hao wanaelewa vizuri kuwa yeye hawaungi mkono wauwaji wa Othman (RA), na kwamba wakati utakapofika atawakamata na kuwahukumu, lakini kilichomhuzunisha ni ule uamuzi wao wa kutoka na makundi makubwa ya watu kwa ajili ya kuharakisha kukamatwa kwa wauaji hao. Habari zilizomfikia zilisema kuwa kundi hilo linaelekea Basra kwa nia ya kuwajumuisha watu wema wa mji huo, pamoja na wa nchi yote ya Iraq na kukusanya jeshi kubwa kwa ajili ya mapamabano.
Ali (RA) kwa vile yeye ndiye kiongozi na mtu wa mwanzo kulibeba jukumu la kulipa kisasi hicho, bila shaka hatokubali dhulma kubwa kama hiyo ipite bila ya yule aliyedhulumu kutiwa adabu. Lakini kilichomhuzunisha ni kule kutoachwa yeye kama ni mkuu wa dola hiyo ya Kiislamu kutumia hekima zake na uwezo wake katika kutafuta ufumbuzi wa tatizo hili. Baadhi ya Masahaba wakubwa kama vile Abdullahi bin Omar, Osama bin Zaid, Saad bin Abi Waqqaas, Muhammad bin Muslamah na wengineo (RAnhum) walikataa kujiunga na kundi lolote katika hayo mawili wakihofia visitokee vita vya wenyewe kwa wenyewe, na Ali (RA) alipokuwa akiondoka kuelekea Basra walikataa kuungana naye, wakamwambia; "Mwenyezi Mungu ametuamrisha kupigana vita na washirikina, ama vita hivi vikitokea baina ya Waislamu wenyewe kwa wenyewe, sisi hatupendezewi kuitia mikono yetu ndani yake."
Hata hivyo walimjulisha Ali (RA) kuwa wao wanatambua kuwa yeye yupo upande wa haki, lakini hawakutaka kunyanyua panga zao na kuzielekeza katika vifua vya Waislamu wenzao. Hakika kuuliwa kwa Othman (RA) kulisababisha fitna kubwa sana baina ya Waislamu. Katika kambi ya pili, Bibi Aisha (RA) aliwahutubia watu na kuwajulisha ubaya wa waasi hao waliomuuwa Khalifa Othman (RA) tena ndani ya mwezi ulioharamishwa umwagaji wa damu ndani yake na katika mji ambao Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) aliharamisha kupigana vita ndani yake, kisha wakakikata kiganja cha mkono wa Bibi Naila (RA) mke wa Othman (RA) na kuvikata vidole vyake pamoja na kuiba mali yao.
Watu wengi wakaungana na Bibi Aisha (RA), huku wakimwambia; "Popote utakapokwenda sisi tuko nyuma yako". Kabla ya Bibi Aisha (RA) kuondoka Makka, hitilafu ilitokea kati ya wake za Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW). Wapo miongoni mwao waliotaka kwenda moja kwa moja mpaka Madina kumtaka Ali (RA) awakamate wauaji hao na kuwahukumu, na wengine wakataka wende Basra kukusanya jeshi kubwa kwa ajili ya kupambana na wauaji hao. Bibi Aisha (RA) aliunga mkono rai ya kwenda Basra, na walipokuwa njiani, wao pia wakaungwa mkono na baadhi ya watu, na idadi yao ikafika kiasi cha watu wapatao elfu tatu. Wakaondoka huku Bibi Aisha (RA) akiwa amebebwa ndani ya hema linalofungwa juu ya ngamia (Hawdaj).
Ali (RA) naye alipowasili mji wa Al Kufa alipata wafuasi wengi waliokuwa na hamasa kubwa ya kutaka kupigana vita kwa ajili ya kumnusuru Khalifa wao mpya ambaye ni mtoto wa ammi yake Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW). Alipoona hamasa zao zinaongezeka, Ali (RA) aliwatuliza kwa kuwaambia kuwa; haki haipatikani kwa mapambano peke yake, bali hupatikana kwa njia nyingi na kwamba kupigana vita kuwe ni jambo la mwisho la kulitegemea. Akamwita Al Qaa qaa (RA) na kumtaka ende Basra kwa Mama wa Waislamu Bibi Aisha (RA) na kuzungumza naye ili mambo haya yamalizike kwa amani.
Mazungumzo baina ya makundi mawili
Alipowasili mji wa Basra, Al Qaa qaa (RA) alikwenda moja kwa moja kuonana na Bibi Aisha (RA) kwa ajili ya mazungumzo ya kutafuta amani akamwambia: "Ewe Mama wa Waislamu, kipi kilichokuleta mji huu? Bibi Aisha (RA) akasema; "Kupatanisha baina ya watu". Al Qaa qaa (RA); "Na wewe Twalha na Zubeir, kipi kilichokuleteni?" Nao pia wakasema; "Kupatanisha baina ya watu". Al Qaa qaa (RA) akasema; "Hebu niambieni, mtu vipi anaweza kusuluhisha baina ya watu?" Twalha na Al Zubeir wakasema; "Kwa kulipa kisasi cha kuuliwa kwa Othman kwa kuwauwa waliomuuwa, kwa sababu tukiwaacha tutakuwa tumekwenda kinyume na mafundisho ya Qurani."
Al Qaa qaa (RA); "Kwanini hamuukubali udhuru wa Ali wa kuchelewesha kuwakamata wauaji hao, wakati mnaelewa kuwa waliomuuwa wanao wafuasi wengi sana, tena kwa maelfu, na kwamba kitendo cha kuwauwa wauaji hao hivi sasa kitasababisha umwagaji mkubwa wa damu. Nyinyi wenyewe huko mlikotoka mliwauwa (baadhi ya) wauwaji wa Ali, na mkajikuta mnapambana na watu wapatao elfu sita wenye silaha, hatimaye mkaamuwa kuwaacha. Isitoshe, Ali hakuwasamehe wauaji hao, isipokuwa anasubiri mpaka pale fursa nzuri itakapopatikana, hapo atawakamata na kuwahukumu. Lakini wakati huu umma upo katika hali mbaya, watu wanakhitalifiana, na maelfu ya watu wamejikusanya ili waanzishe vita vikali baina yao. Msitupoteze!, umma utaangamia!" Bibi Aisha (RA) akasema; "Nini rai yako ewe Qaa qaa?" Al Qaa qaa (RA) akasema;
"Mimi naona kuwa bora tuyatulize mambo hivi sasa, na nyinyi mfungamane na Ali, kwani kufungamana kwenu naye ni dalili ya kheri. Lakini mkikataa na mkaendelea kufanya upinzani, hii itakuwa ni dalili ya shari na kutoweka kwa ufalme, na mimi naogopa ikiwa mtashikilia kuifuata njia hii ya shari mtakuja dhurika nyinyi pamoja na sisi. Naogopa Mwenyezi Mungu asije akatuteremshia ghadhabu yake. Kwa hivyo kuweni funguo za kheri kama ilivyo kawaida yenu, na tusijiingize katika balaa mpaka ikatusibu. Bora tuyatulize mambo". Mazungumzo yakaishia hapo na wakakubaliana kuwa Al Qaa qaa atakuja pamoja na Ali (RAnhum) mpaka Basra ili wote wafungamane naye.
Al Qaa qaa akarudi kwa Ali (RA) na kumpa habari hizi njema zilizoingiza furaha isiyo na kifani ndani ya kifua chake, kwa kuweza kuikinga damu ya Waislamu isimwagike. Ali (RA) akainuka na kuwahutubia watu na kuwakumbusha wakati wa ujahilia (kabla ya Uislamu) na upotovu wake na matendo yake, kisha akazungumza juu ya Uislamu na uongofu wake pamoja na kuongoka kwa watu wake kwa kuweza kuwafanya wawe kitu kimoja. Akasema; "Mwenyezi Mungu ametujumuisha baada ya kufa kwa Mtume wake (SAW) chini ya uongozi wa Khalifa Abubakar, kisha baada yake chini ya uongozi wa Khalifa Omar bin Khattab, kisha chini ya Khalifa Othman, kisha yakatokea haya yaliyotokea ndani ya mwili wa umma.
Watu wanaikimbilia dunia na kuwaonea husda wale Mwenyezi Mungu aliowaneemesha na kuwapa fadhila alizowapa.Wakataka kuturudisha nyuma, lakini Mwenyezi Mungu lazima atalifanikisha lile alitakalo". Kisha akasema;
"Mimi kesho naondoka na sitaki anifuate yeyote kati ya wale waliosaidia kuuwawa kwa Othman". Ilipoingia asubuhi, Ali (RA) akaondoka pamoja na maaskari wake kuelekea Basra kwa ajili ya kukamilisha mazungumzo ya amani. Wakawasili wakati wa usiku, na kila mtu alilala katika kambi yake kwa furaha wakiingoja siku ya pili yake kwa hamu kubwa.
MWISHO