NAFASI YA FATIMA (A.S)
  • Kichwa: NAFASI YA FATIMA (A.S)
  • mwandishi: BARAZA
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 7:32:47 24-8-1403

BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

NAFASI YA BIBI FATIMA AZ-ZAHRAA (A.S)

Waandishi wengi wa masuala ya historia ya Kiislamu, wa Kishia na Kisuni, wanaamini kwamba uzawa wa Bibi Fatimatu az-Zahra (AS) ulitimia mjini Makka tarehe 20 Jumadi Thani mwaka wa Tano wa kubaathiwa Mtume Mtukufu (SAW). Wengine wanasema kuwa ulikuwa ni mwaka wa tatu ilhali wengine wanaamini kuwa ulikuwa ni mwaka wa pili wa kupewa utume Mtume Mtukufu (SAW). Mwanahistoria na mwanahadithi mwingine wa Kisuni anasema kuwa bibi Zahra (AS) alizaliwa katika mwaka wa kwanza wa kubaathiwa Mtume (SAW).

Bibi Fatimatu az-Zahra (AS) ni binti wa Mtume Mtukufu (SAW) na Bibi Khadija Kubra. Alikuwa binti wa nne wa Mtume. Lakabu zake Bibi Zahra (AS) ni: Zahra, Swiddiqa, Twahira, Mubaraka, Zakiyya, Radhiya, Mardhiyya, Muhaddatha na Batul. Ni wazi kuwa hata kama siku au mwaka wa kuzaliwa mtu na shakhsia yoyote mkubwa una thamani katika masuala ya uhakiki na utafiti wa kihistoria, lakini bila shaka jambo hilo halina umuhimu mkubwa katika uchambuzi wa tabia na maisha yake. Bibi Fatimatu az-Zahra (AS) alizaliwa na kulelewa kando ya baba yake, Mtume Mtukufu wa Mwenyezi Mungu (SAW) na katika nyumba ya utume, nyumba ambayo ilikuwa ni sehemu ya kuteremkia wahyi na aya za Qur'ani Tukufu. Hapo ni mahala ambapo kundi la mwanzo la Waislamu lilikuwa limekiri na kumwamini Mwenyezi Mungu mmoja na wakati huohuo kusimama imara katika imani hiyo.

Hiyo ilikuwa nyumba ya pekee katika Bara Arabu na katika ulimwengu mzima ambapo sauti ya 'Allahu Akbar' alikuwa ikisikika huku Bibi Zahra, binti mdogo wa pekee mjini Makka, akishuhudia tukio hilo mihimu likijiri pembeni yake. Alikuwa peke yake katika nyumba hiyo na kupitisha kipindi chake chote cha utotoni katika hali hiyo ya kuvutia. Dada zake wengine wawili yaani Ruqiyya na Kulthum walikuwa wakubwa kumliko kiumri. Huenda siri ya kuwa peke yake katika kipindi hicho cha utotoni ilikuwa ni kumtayarisha na kumpa mazoezi maalumu ya kimwili na kiroho katika kipindi hicho. Baada ya kuolewa na Imam Ali Amir al-Mu'mineen (AS), Bibi Fatima aling'ara katika giza la karne na zama, kama mwanamke bora zaidi wa kuigwa na wanadamu wenzake. Bibi huyo ambaye alikuwa mfano bora wa kuigwa katika maisha yake ya ndoa, pia alikuwa mfano wa kuigwa katika utiifu wa Mwenyezi Mungu.

Alipomaliza kazi zake za nyumbani alikuwa akimwabudu Mwenyezi Mungu faraghani. Huku akiwa katika hali ya unyenyekevu mkubwa, alikuwa akiswali na kuwaombea dua wenzake kwa Mwenyezi Mungu. Imam Swadiq (AS) ananukuliwa akimnukuu mmoja wa babu zake Imam Hassan bin Ali (AS) akisema: "Mama yangu usiku wa kuamkia Ijumaa alikuwa akikesha kwenye mihrabu ya ibada huku akiwaombea dua waumini wa kiume na wa kike, bila kujiombea dua yeye mwenyewe. Siku moja nilimwambia: Mama yangu! Ni kwa nini haujiombei dua kama unavyowafanyia watu wengine? Alijibu: Mwanangu! Jirani hutangulizwa." Tasbihi zinazojulikana kwa jina la Tasbihi za Fatima (AS) ni jambo mashuhuri sana ambalo limetajwa kwenye vitabu mashuhuri vya Shia na Suni na marejeo mengine ya kuaminika na pande hizo.

Ukusanyaji elimu wa Fatima Tokea mwanzoni Bibi Fatima (AS) alipata na kunufaika na maarifa makubwa moja kwa moja kutoka kwenye chemchemi ya wahyi. Aliandikiwa na Imam Ali (AS) kila elimu na siri aliyoambiwa na baba yake na kisha Fatima kuikusanya na kuihifadhi katika kitabu maalumu kilichojulikana baadaye kwa jina la Mus'hafu Fatima. Kuwafundisha wenzake. Bibi Fatima alikuwa akiwajulisha wanawake wenzake majukumu yao kwa kuwafundisha mafundisho na sheria za dini tukufu ya Kiislamu. Bi Fedha, mtumishi wake Bibi Fatima ambaye alimlea na kumpa maarifa mengi ya Kiislamu kwa kipindi cha miaka 20 alikuwa hasemi wala kubainisha jambo ila kwa kutaja na kutumia aya za Qur'ani Tukufu. Kila mara alipotaka kusema jambo au kubainisha maudhui yoyote ile alifanya hivyo kupitia aya iliyonasibiana vyema na maudhui hiyo. Si tu kwamba Bibi Fatima (AS) hakuchoka katika ukusanyaji wa elimu bali alikuwa pia na subira kubwa katika kuwafundisha wenzake elimu hiyo. Siku moja mwanamke mmoja alimkujia na kumwambia: "Nina mama mzee ambaye amekosea katika swala yake na amenituma kwako ili nikuulize jambo." Baada ya kupata jibu la swali lake, mwanamke huyo aliondoka na kisha kurejea tena kwa mara ya pili na tatu huku akiwa anauliza mwaswali tofauti. Baada ya kujibiwa aliondoka na kurejea tena kwa Bibi Fatima (AS). Alifanya hivyo mara 10 na kila alipokuwa akiuliza likuwa akipewa jibu la kuridhisha na Bibi huyo muhimu wa Kiislamu.

Mwanamke huyo aliona haya kutokana na kurejearejea kwake kwa Bibi Fatima na kusema: "Sikusumbui tena." Bibi Fatima alimwambia: "Rejea tena na uulize maswali yako. Sitakasirika kadiri utakavyoniuliza kwa sababu nilimsikia baba yangu Mtume (SAW) akisema: "Siku ya Kiama maulama wanaotufuata watafufuliwa na kuvishwa mavazi ya heshima yenye thamani kubwa kwa mujibu wa viwango vya elimu yao na kupewa malipo kwa mujibu wa juhudi walizofanya katika kuwaongoza waja wa Mwenyezi Mungu."

Ibada ya Fatima (AS) Bibi Fatima alikuwa akitumia sehemu ya usiku kufanya ibada na kumtukuza Mwenyezi Mungu. Swala zake za usiku zilikuwa zikichukua muda mrefu na kusimama kwa muda mrefu kwenye ibada kiasi kwamba miguu yake ilikuwa ikivimba. Hassan Basri aliyeaga dunia mwaka 110 Hijiria anasema hivi kuhusiana na jambo hilo: "Hakuna mtu yoyote katika umma aliyekuwa na kiwango cha juu cha zuhudi na uchaji Mungu kama Fatima (AS)."

Mkufu wa baraka Siku moja Mtume Mtukufu (SAW) alikuwa ameketi msikitini huku akiwa amezungukwa na masahaba wake. Ghafla mtu mmoja aliyekuwa na nguo chafu na aliyekuwa katika hali ya kusikitisha na kutia huruma alifika mahala hapo. Udhaifu na uzee ulikuwa umempokonya nguvu zake. Mtume alimwendea na kumjulia hali. Alijibu kwa kusema: "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Mimi ni masikini aliyechanganyikiwa, ni mwenye njaa nipe chakula, niko uchi nivishe nguo, sijiwezi nisaidie." Mtume alimwambia: "Sina chochote kwa hivi sasa lakini 'muelekezaji kwenye kheri ni kama mtendaji wa kheri hiyo.'" Kisha alimuelekeza kwenye nyumba ya Fatima (AS).

Mzee huyo alikata masafa mafupi yaliyokuwepo kati ya msikiti huo na nyumba ya Bibi Fatuma (AS) na kumfahamisha matatizo yake. Bibi Fatima alimwambia: "Sisi pia hatuna chochote nyumbani kwa hivi sasa." Alifungua mkufu aliokuwa ameuvaa shingoni, aliokuwa amepewa zawadi na binti yake Hamza bin Abdul Muttalib na kumpa mzee yule masikini na kumwambia: "Uuze mkufu huu inshallah utafikia lengo lako." Masikini huyo aliuchukua mkufu huo na kuelekea msikitini. Mtume alikuwa angali ameketi na masahaba zake. Alisema: "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Fatima amenipa mkufu huu niuuze na kisha kutumia fedha zitakazopatikana humo, katika kukidhia mahitaji yangu." Mtume alilia baada ya kuyasikia maneno hayo. Ammar Yassir alimwambia Mtume (SAW): "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Je, unanipa idhini ya kununua mkufu huu?" Mtume alisema: "Mwenyezi Mungu asimuadhibu kila mtu atakayeununua mkufu huu."

Ammar Yassir alimuuliza mzee huyo masikini: "Unauuza pesa ngapi mkufu huu?" Alijibu: "Kwa pesa zitakazoniwezesha kununua chakula cha mkate na nyama itakayonisibisha, nguo itakayofunika mwili wangu na dinari itakayoniwezesha kurejea nyumbani kwangu." Ammar Yassir alimjibu: "Nimenunua mkufu huu kutoka kwako kwa dinari 20 za dhahabu, chakula, nguo na mnyama wa kupanda." Ammar alimpeleka masikini huyo nyumbani kwake na kisha kumpa chakula alichokula akashiba, nguo, mnyama wa kupanda na dinari 20 za dhahabu. Kisha aliupaka mkufu huo maski yenye harufu nzuri na kuufunika kwa kitambaa na kumwambia mtumishi wake mtumwa: "Mpelekee Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) mzigo huu na nimekusalimisha wewe pia kwake."

Mtume naye kwa upande wake alimkabidhi kwa Bibi Fatima (AS) mtumishi huyo pamoja na mkufu aliokuwa amempa mzee yule masikini. Mtumishi huyo mtumwa alimjia Fatima (AS). Bibi Fatima aliuchukua mkufu wake na kumwambia mtumishi huyo: "Nimekuacha huru kwa njia ya Mwenyezi Mungu." Mtumishi huyo akacheka. Bibi Fatima (as) alimuuliza sababu ya kicheko chake naye akamjibu kwa kusema: "Ewe binti ya Mtume! Baraka za mkufu huu zimenifanya nicheke kwa sababu zimemshibisha mwenye njaa, kumvisha nguo mtu aliyekuwa uchi, kumtajirisha masikini, kumpandisha mnyama mtu aliyekuwa akitembea kwa miguu, kumwachilia huru mtumwa na hatimaye kurejea kwa mwenyewe."

Nafasi ya Fatima (AS) katika vita Nafasi ya Fatima (AS) katika vitavya mwanzoni mwa Uislamu. Katika kipindi cha miaka kumi cha serikali ya Mtukufu Mtume (SAW) mjini Madina, vita 27 au 28 vya ghazwa na 35 hadi 90 vya sariyya vimesajiliwa kupiganwa katika historia ya Kiislamu. Ghazwa ambayo wingi wake ni ghazawaat kwa lugha ya Kiarabu, ni vita ambavyo Mtume Mtukufu mwenyewe (SAW) alishiriki moja kwa moja kwenye vita hivyo na kuongoza majeshi ya Kiislamu dhidi ya makafiri na maadui wa Uislamu. Alishiriki katika medani ya vita na kushirikiana bega kwa bega na askari wa Kiislamu katika kupigana dhidi ya maadui. Neno Sariyya ambalo wingi wake ni saraya, ni vita ambavyo licha ya kuwa Mtume hakushiriki moja kwa moja kwenye vita hivyo lakini alimtuma mtu maalumu kuongoza jeshi na askari wa Kiislamu katika medani za vita au katika kulinda mipaka ya nchi ya Kiislamu. Baadhi ya safari na majukumu hayo ya kupigana vita au kulinda mipaka ya nchi ya Kiislamu yalikuwa yakichukua miezi miwili au mitatu kutokana na umbali wa medani za vita kutoka mji mtakatifu wa Madina.

Tunaweza kusema kupitia utafiti wa kihistoria kwamba katika kipindi chote cha maisha yake ya pamoja ya ndoa na Bibi Zahra (AS), Imam Ali (AS) alitumia wakati wake mwingi katika medani za vita vya jihadi au katika safari za tablighi na ulinganiaji dini ya Mwenyezi Mungu. Katika kipindi cha kutokuwa nyumba Imam Ali (AS), mkewe mwaminifu Bibi Fatima (AS) alitekeleza vyema majukumu ya kuendesha masuala ya nyumba na kulea watoto wao. Alitekeleza ipaswavyo majukumu hayo ili kumfanya mumewe, Imam Ali (AS) kutekeleza vyema majukumu yake katika uwanja wa vita bila ya kuwa na wasiwasi wa kuharibika mambo nyumbani. Katika kipindi hicho, Bibi Fatima (AS) pia alikuwa akitekeleza jukumu jingine nalo ni la kutembelea na kuzisaidia kwa hali na mali familia za askari wa Kiislamu walioshiriki kwenye medani za jihadi.

Alikuwa akizitembelea familia hizo na kuziliwaza zile zilizokuwa zimewapoteza wapenzi wao katika medani za vita au kushajiisha na kuzipa moyo zile ambazo waume wao walikuwa wamejeruhiwa vitani. Huku akibainisha majukumu mazito na muhimu ya wanawake wa Kiislamu waliokuwa wakitoa misaada katika medani za vita, Bibi Fatima (AS) mara nyingine alikuwa akiwashajiisha wanawake hao kutibu majeraha ya maharimu zao, yaani watu wasioruhusiwa kuolewa nao (watu wa karibu katika familia).

Katika vita vya Uhud, yapata kilomita sita hivi kutoka mji wa Madina, Bibi Fatima (AS) aliandamana na wanawake wengine kwenda kwenye vita hivyo. Katika vita hivyo, Mtume Mtukufu (SAW) alijeruhiwa vibaya na Imam Ali (AS) pia kupata majeraha kadhaa. Bibi Fatuma alishughulika kufuta na kuosha damu kwenye uso mtukufu wa Mtume (SAW) huku Imam Ali (AS) akijishughulisha kumwagilia maji ngao yake Mtume (SAW). Wakati Bibi Fatima alipoona kwamba damu ya Mtume ilikuwa haikatiki na kuendelea kuvuja, alichukua kipande cha mkeka na kukichoma na kisha kuchukua jivu lake na kulinyunyiza kwenye sehemu ile iliyokuwa imejeruhiwa kwenye uso wa Mtume hadi damu ilipokatika na kutovuja tena. Hamza, Bwana wa Mashahidi, ambaye ni Ami yake Mtume (SAW) aliuawa shahidi katika vita hivyo.

Baada ya kumalizika vita hivyo, Swafiyya, dada yake Hamza aliandamana na Bibi Fatima (AS) kwenda pembeni ya mwili wa shahidi huyo, uliokuwa umekatwa na adui kama alama ya kulipiza kisasi, na kuanza kulia. Fatima (AS) alilia na Mtume naye pia akaungana nao katika kilio hicho. Alimuhutubu Hamza kwa kusema: "Hakuna msiba mkubwa uliowahi kunipata kama msiba wako huu." Kisha aliwahutubu Swafiyya na Fatima kwa kusema:

"Pokeeni habari njema kwamba Jibril amenipasha habari sasa hivi kwamba Hamza ni simba wa Mungu na simba wa Mtume katika mbingu saba." Baada ya kumalizika vita hivyo vya Uhud, Fatima (AS) katika maisha yake yote yaliyosalia, alikuwa akizuru makaburi ya mashihidi wa vita hivyo mara moja, kila baada ya siku mbili au tatu. Katika vita vya Khandak, Bibi Fatima (AS) alimpelekea mkate Mtume Mtukufu (SAW). Mtume alimuuliza: "Nini hii?" Fatima akajibu: "Nimeoka mikate lakini moyo wangu haukutulia hadi nilipokuletea." Mtume akasema: "Hiki ni chakula cha kwanza kwangu kukiweka kinywani baada ya siku tatu."

Katika vita vya Muta, Jaafar bin Abi Talib aliuawa shahidi na Mtume (SAW) kwenda nyumbani kwake kwa ajili ya kutoa mkono wa pole na kuwafariji mkewe na watoto wake. Baadaye alielekea kwenye nyumba ya Bibi Fatima (AS). Alimkuta Fatima akilia. Mtume (SAW) alisema: "Kwa mtu kama Jaafar, watu wanaolia wanapasa kumlilia." Kisha Mtume (SAW) alisema: "itairishieni chakula familia ya Jaffar kwa sababu imejisahau kwa leo." Bibi Fatima (AS) pia alishiriki katika vita vya kukombolewa Makka. Mwishoni, tunatoa mkono wa pongezi na fanaka kwa Waislamu wote duniani kwa mnasaba huu adhimu wa kuzaliwa Bibi huyo mtukufu na mbora wa wanawake wa ulimwengu.

MWISHO