TAALUMA NA MAFUNZO YA AMALI
  • Kichwa: TAALUMA NA MAFUNZO YA AMALI
  • mwandishi: BARAZA
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 7:29:7 24-8-1403

BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

TAALUMA NA MAFUNZO YA AMALI

Tuko katika siku za mwisho za mwezi wa Dhul Qaada, ambazo ni siku za kuuawa shahidi mmoja wa Watu wa Nyumba ya Mtume Muhammad (saw). Katika siku kama hizi mwaka 220 Hijiria, Imam Jawad (as), kiongozi mkubwa na mtukufu wa Kiislamu, aliaga dunia na hivyo kuuachia ulimwengu wa Kiislamu huzuni kubwa.

Watu wa Nyumba ya Mtume katika utekelezaji wa majukumu yao makubwa waliyopewa na Mwenyezi Mungu, walikuwa waanzilishi wa matukio makubwa ya kifikra, kiutamaduni na kijamii katika ulimwengu wa Kiislamu. Iwapo tutatalii vyema historia na maisha ya Ahlul Beit (as), tunaona kuwa walikuwa na nafasi muhimu katika kulinda misingi na nguzo za dini.

Walisimama na kupambana vikali na madhihirisho ya dhulma, upotovu na ufisadi na kufanya jitihada kubwa za kulinda misingi ya Uislamu halisi ili dini hii tukufu idumu milele. Imam Jawad (as) ni miongoni mwa Watu wa Nyumba ya Mtume (saw) ambaye katika kipindi cha miaka 17 ya uimamu wake, daima alikuwa akifanya jitihada za kueneza Uislamu na kuimarisha mafundisho yake tajiri ulimwenguni. Huku tukitoa mkono wa pole kwa Waislamu wote wapenda haki kwa mnasaba wa kuwadia siku ya kukumbuka kuuawa shahidi Imam Jawad (as), tunazungumzia hapa angaa kwa ufupi, maisha ya mtukufu huyo.

Imam Jawad (as) amesema: "Iwapo mtu atakuwa na sifa tatu anaweza kupata ridhaa ya Mwenyezi Mungu. Kwanza awe ni mwingi wa kuomba maghfira kutoka kwa Mwenyezi Mungu, pili aamiliane vyema na watu na tatu atoe sadaka kwa wingi." Imam alikuwa akisema kuwa kuwasaidia watu humteremshia mwanadamu rehema za Mwenyezi Mungu, kwa kadiri kwamba iwapo atazembea katika suala hilo, kuna uwezekano wa kuondokewa na neema za Mungu Muumba. Anasema: "Mtu anapozidishiwa neema za Mwenyezi Mungu, mahitaji ya watu kwake huongezeka. Kila mtu asiyefanya juhudi za kukidhi mahitaji hayo, huhatarisha neema hizo."

Imam Jawad alikuwa mwanawe Imam Ridha (as) ambaye alizaliwa mwaka 195 Hijiria katika mji mtakatifu wa Madina. Mtukufu huyo aliishi kwa karibu miaka 25 na katika muda huo alikuwa na nafasi kubwa katika kunyanyua kiwango cha fikra za watu. Imam Jawad (as) alichukua hatamu za uimamu akiwa na umri wa miaka minane tu. Uimamu wake katika umri huo mdogo uliwashangaza baadhi ya watu na kuwafanya wawe na shaka. Shaka yao ilitokana na ukweli kwamba walikuwa wakipima mambo ya dunia kwa vipimo vva kidhahiri na kimaada tu.

Hii ni katika hali ambayo, kutokana na maslahi fulani, Mwenyezi Mungu anaweza kumpa mwanadamu akili na ukamilifu mkubwa wa kufikia kilele cha mambo licha ya kuwa na umri mdogo. Kwa mujibu wa aya za Qur'ani, hilo ni jambo ambalo tayari limeshatokea katika historia ya umma na kaumu zilizopita. Utume wa Nabii Yahya akiwa utotoni na kuzungumza kwa Nabii Isah (as) akiwa kwenye susu ni baadhi tu ya miujiza ya Mwenyezi Mungu kuhusiana na jambo hilo.

Tokea umri wake wa utotoni na kwenye ujana, Imam Jawad (as) alikuwa wa kupigiwa mfano katika masuala ya kielimu, ufasaha, subira na takwa. Mtukufu huyo alikuwa na werevu wa hali ya juu pamoja na kipawa kikubwa cha kubainisha mambo. Licha ya kuwa na umri mdogo likini alikuwa chimbuko la elimu, fadhila na marejeo ya wakuu wa zama hizo. Historia inatwambia kwamba katika msimu mmoja wa hija, wanazuonina wasomi 80 wa Baghdad na miji mingine waliazimia kwenda Madina na kukutana na Imam Jawad (as).

Walimuuliza Imam Jawad maswali mengi ya kielimu na kupata majibu ya kukinaisha kutoka kwake. Kwa utaratibu huo, shaka yote waliyokuwa nayo kuhusiana na uimamau wa Imam Jawad (as) iliondoka. Imam Jawad alikuwa akishiriki katika mijadala mbalimbali ya kielimu ambapo baadhi ya mijada hiyo ilikuwa ya kusisimua sana. Uwezo na kipawa kikubwa cha elimu aliyokuwa nayo Imam kilidhihirika wazi katika mijadala na midahalo hiyo ya kielimu.

Hoja alizokuwa akizitoa Imam katika midahalo hiyo ziliweza kuvunja vikwazo vya kielimu na kufungua milango mingi ya maarifa ambapo masuala mengi nyeti na magumu ya kielimu yaliweza kubainika kwa urahisi. Kwa msingi huo wasomi na hata wapinzani wa mtukufu huyo walikiri kuhusiana na uwezo wake mkubwa wa kielimu na kimaanawi.

Siku moja, Ma'mun, khalifa wa ukoo wa Abbas aliandaa kikao cha kielimu ambapo aliwaalika wanafikra kadhaa wa zama hizo ili kumpima kielimu Imam Jawad (as). Katika kikao hicho, Yahya bin Aktham, mmoja wa wasomi mashuhuri wa zama hizo alimuuliza Imam Jawad swali linalohusiana na hukumu ya kisheria ya hujaji anayewinda mnyama hali ya kuwa yuko kwenye vazi la ihramu. Imam aliligawa swali hilo katika vipengee 22 tofauti na kisha kulijibu kwa ufasaha mkubwa.

Ni wazi kuwa kila jibu alilotoa kuhusiana na vipengee hivyo lilitofautiana na jingine. Mbinu hiyo ya kujibu swali aliloulizwa ilibainisha wazi kipawa kikubwa, cha kipekee na cha kushangaza cha elimu ya Imam Jawad (as).

Kipindi cha miaka 17 ya uimamu wa Imam Jawad yaani tokea mwaka 203 hadi 220 Hijiria, kilitimia sambamba na utawala wa makhalifa wawili wa ukoo wa Abbas walioitwa Maamun na Mu'taswim. Watawala hao hawakuheshimu wala kutekeleza sheria za Mwenyezi Mungu bali walikuwa wakipotosha na kutumia vibaya sheria hizo kwa maslahi yao binafsi. Imam hakulinyamazia kimya suala hilo.

Upinzani wa Imam kuhusiana na suala hilo ulikuwa na athari kubwa miongoni mwa watu. Kwa msingi huo, makhalifa wa Abbasi, walizidisha maudhi, vikwazo, na mashinikizo yao dhidi ya Imam Jawad (as). Kufuatia mashinikizo hayo Imam Jawad alilazimishwa na Ma'mun kuuhama mji mtakatifu wa Madina na kuelekea Baghdad nchini Iraq, makao makuu ya utawala wa Bani Abbas.

Licha ya mazingira hayo magumu, lakini Imam Jawad (as) alifanya juhudi kubwa za kulinda mawasiliano yake na matabaka mbalimbali ya watu wa kawaida. Ili kudumisha mapambano dhidi ya watawala hao dhalimu, Imam alibuni njia na mbinu tofauti. Imam Jawad alikuwa akiwatuma wajumbe wake katika nchi mbalimbali za Kiislamu.

Wajumbe hao walikuwa katika sehemu nyingi kama vile Basra, Sistan, Ahwaz, Hamedan, Kufa, Qum na Rei. Ni wazi kuwa baadhi ya watumishi wa Imam Jawad (as) pia walikuwa wakihudumu katika vyombo vya utawala wa Bani Abbas. Baadhi yao hata walikuwa na nyadhifa muhimu katika utawala huo. Ali bin Mahziyar Ahwazi kutoka mji wa Ahwaz ni mmoja wa watumishi hao waliokuwa na uaminifu mkubwa kwa Imam Jawad (as) licha ya kuwa walikuwa wakifanya kazi katika utawala wa Bani Abbas.

Imam Jawad (as) hakusita hata mara moja katika juhudi zake za kuwaongoza watu na kunyanyua kiwango chao cha fikra na muamko. Mtukufu huyo alikuwa akihisi kuwa na majukumu makubwa na mazito katika kuwaongoza watu na kujaribu kutatua matatizo yaliyokuwa yakiwakabili maishani. Imam Jawad alikuwa na huruma na unyenyekevu mkubwa kwa watu na alipewa lakabu ya Jawad kutokana na wingi wa usamehevu wake.

Katika miaka miwili ya mwisho ya maisha yake, Imam Jawad (as) alikabiliwa na mashaka na matatizo mengi. Alipoingia madarakani, Mu'taswim, mtawala wa Bani Abbas alikuwa na wasiwasi mkubwa kuhusian na ushawishi mkubwa wa kifikra na kimaanawi wa Imam Jawad miongoni mwa wafuasi na matabaka ya watu wa kawaida.

Kwa msingi huo, alitumia kila kisingizio ili kuvuruga shughuli za Imam Jawad (as) na hasa zile zilizohusiana na mawasiliano yake na watu. Alikuwa akimfanyia ujajusi na kumuweka Imam chini ya uangalizi na uchunguzi wa vyombo vya dola. Licha ya kuwa makhalifa wa Bani Abbas walimuweka Imam Jawad chini ya mazingira magumu lakini bado hawakuweza kuwazuia watu waliokuwa na hamu kubwa kumfikia Imam huyo na kumdhihirishia mapenzi yao makubwa.

Kwa hivyo kila mara Imam alipokuwa akipata fursa ndogo tu ya kutembea mjini watu walikuwa wakijitokeza kwa wingi na kumwagika mitaani kwa ajili ya kumwona imam wao. Wengine walikuwa wakipanda kwenye paa za nyumba ili kumwona kwa karibu mjukuu huyo wa Mtume Mtukufu (saw).

Kwa ufupi ni kuwa, harakati za Imam Jawad na ushawishi wa maneno yake ulileta muamko mkubwa miongoni mwa watu na kuwasha moto wa husuda na chuki katika moyo wa Mu'taswim. Kwa msingi huo alipanga njama za kummaliza na kumuua imam huyo mtuufu. Kwa maelezo hayo hatimaye Mu'taswim alimuua mjukuu huyo wa Mtume akiwa na umri wa miaka 25. Kwa mara nyingine tena tunatoa mkono wa pole kwa wasomaji wetu wote kwa mnasaba huu mchungu wa kuuawa shahidi Imam Jawad (as). Tunahitimisha makala hii kwa kuashiria hadithi mbili za Imam huyo Mtukufu (as). Amesema:
*Ujuzi wa dini ni ngazi ya maendeleo na ustawi kwa ajili ya kufikia madaraka yoyote yale ya juu. Pia amesema (as): *Jiepushe kuwa na urafiki na mtu mmbaya. Hakika yeye ni mfano wa upanga ambao unang'ara kidhahiri lakini una matokeo mabaya.

MWISHO