VUNJA JUNGU NI MAASI
  • Kichwa: VUNJA JUNGU NI MAASI
  • mwandishi: NDUGU ZETU WA KIISLAMU
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 4:40:32 3-11-1403

BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

VUNJA JUNGU NI MAASI

Assalaamu Alaykum Warahmatullah!
Ni baada ya siku chache tu kwa msaada wake Allah Karim utakuwa unapumua na kuishi ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhani. Mwezi ambao huwapa waislamu fursa ya kuitekeleza mojawapo ya nguzo tano za Uislamu, swaumu ya Ramadhani. Katika kuuheshimu, kuutukuza na kuuenzi mwezi huu mtukufu.

Naam, Ramadhani hiyo mlangoni mwako inabisha hodi. Wewe kama muislamu umejiandaje kuupokea mwezi wako huu mtukufu? Je, wewe ni mmoja wa wale wanaoupokea mwezi wa Ramadhani kwa kile kinachojulikana kama VUNJA JUNGU?

Hebu na tujiulize kwa pamoja, tulivunjao hilo jungu mwaka hata mwaka na wale tusiolivunja, vunja jungu ni nini khasa? Bila ya shaka mtakubaliana nasi kwamba vunja jungu kama litafsirikanavyo kutokana na matendo yatendwayo na wavunja jungu katika kulivunja kwao hilo jungu. Ni mkono wa kwaheri unaopungwa kwa maasi mbalimbali kwa ajili ya kuingia kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani. Wavunja jungu huitumia fursa ya zile siku mbili tatu kabla ya kuandama kwa mwezi mwandamo unaoashiria kuanza kwa funga tukufu ya Ramadhani.

Kuogelea na kupiga mbizi maradufu katika maasi waliyokuwa wakiishi nayo katika kipindi cha ile miezi kumi na moja nje ya Ramadhani. Kwa hivyo basi, vunja jungu kwa mlevi ni kulewa sana kwani hataipata fursa hiyo tena ila baada ya kumalizika kwa mwezi wa Ramadhani.

Vunja jungu kwa mzinifu ni kuzini sana na kutengana na kimada wake kuipisha Ramadhani, kisha mchezo uendelee baada ya Ramadhani. Vunja jungu kwa mpenzi wa muziki ni kukesha katika kumbi za starehe akicheza na kunywa kufidia ile fursa atakayoikosa kwa sababu ya kuingia kwa mwezi mtukufu. Mbele za watu hawa Ramadhani ni mithili ya gereza/kifungo kinachowaondolea na kuwanyang`anya uhuru wa kuishi kama wapendavyo kwa kufuata matashi na matamanio ya nafsi zao.

Hawa wanasahau kwamba wanawajibika kuishi kwa mujibu wa muongozo wa Mola Muumba wao na sio kwa kuongozwa na matashi yao! Kwa ujumla vunja jungu ni kushindana katika aina mbalimbali za maasi kwa sababu ya kuingia kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani ambao hautoi uwanja wa maasi hayo kwa mijibu wa fikra zao potofu. Kwa nini tunasema kwa mujibu wa fikra zao potofu, hilo linatokana na ukweli kwamba hakuna kibali wala uhalali wa kufanya maasi na mtu kuishi kama apendavyo nje ya Ramadhani.

Ikiwa vunja jungu linaashiria jambo, basi jambo hilo halitakuwa jingine zaidi ya kuonyesha kufilisika kiimani kwa huyo mvunja jungu. Kwani muumini wa kweli hawezi kuvunja jungu, kwa kuwa anatambua kwamba kufanya hivyo ni kumuasi Allah Mola Muumba wake. Kwa muumini wa kweli kujiepusha na maasi na kumtii Mola wake ni zoezi linaloyatawala maisha yake yote. Bila ya kuangalia kuwa huu ni mwezi wa Ramadhani au ni nje ya Ramadhani. Kuagana na maasi eti kwa sababu tu ya kuingia kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani, kisha kuyarejea tena baada ya kumalizika kwake.

Huo tukubali au tukatae ni UDHAIFU WA IMANI na si vinginevyo. Kwani huyo Mola wa Ramadhani unayeacha maasi ndani yake kwa ajili yake, ndiye Mola wa hiyo miezi mingine unayojihalalishia maasi ndani yake. Amri ya kumtii Mola wako kwa kuyatekeleza yote aliyokuamrisha na kuyaacha yote aliyokukataza inauhusu mwezi wa Ramadhani na baki ya miezi mingine isiyo Ramadhani.

Kumuabudu Mola wako ndani ya Ramadhani tu ni kujiuundia utaratibu wa ibada kinyume na ule aliokupangia Allah Mola Muumba wako. Elewa kufanya kwako hivi ni sawa na kusema kuwa utaratibu wa ibada aliokuwekea Mola wako aliye mjuzi wa manufaa na maslahi yako ama haufai au umepitwa na wakati. Na kwamba wewe kama kiumbe unaweza kujiundia utaratibu utakaokudhaminia manufaa na mafanikio katika ulimwengu wako huu na ule ujao. Elewa kwa mtindo na mtaji wako huo siku ya kiyama Allah atakuambia ujilipe wewe mwenyewe kwa kuwa yeye hakukuamrisha kufanya ibada kwa utaratibu huu unaokwenda nao sasa.

Ewe ndugu mpenzi wee! Elewa na ufahamu fika kwamba Ramadhani ipokelewayo na kukaribishwa na vunja jungu haitakuwa na athari yo yote kwako wewe ambaye ndiwe mlengwa wa Ramadhani na wala sio Mola wako. Kwako Ramadhani haitakuwa ila mithili ya kujenga nyumba angani bila ya kuwa na msingi imara uliokita ardhini.

Ewe ndugu mpenzi mvunja jungu, utaendelea kulivunja hilo jungu na kumuasi Mola wako mpaka lini?! Hebu jiulize, nini utakuwa mwisho wa huku kuvunja jungu kwako?! Tangu umeanza kuvunja jungu na bila shaka ni jungu la maasi umepata na kuvuna nini?! Ndugu mpenzi hebu ihurumie nafsi yako kwa kuitegea sikio la usikivu kauli hii tukufu ya Mola wako: "ANAYEFANYA MEMA ANAJIFANYIA (mwenyewe) NAFSI YAKE, NA MWENYE KUTENDA UBAYA NI JUU (ya nafsi) YAKE (vile vile)…" [41:46]

Aya inakuongoza kutambua kwamba unapovunja jungu, hufanyi hivyo ila ni kwa hilaki na maangamivu ya nafsi yako wewe mwenyewe leo hapa duniani na kesho kule akhera. Ambapo utapewa daftari la amali zako uikute na vunja jungu yako, hapo ndipo utasema: "…OLE WETU! NAMNA GANI MADAFTARI HAYA! HAYALIACHI DOGO WALA KUBWA ILA YAMELIDHIBITI (yameliandika)! NA WATAKUTA YOTE YALE WALIYOYAFANYA YAMEHUDHURIA HAPO; NA MOLA WAKO HAMDHULUMU YO YOTE". [18:49]

Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-anasema: "Jibril alinijia na akaniambia: Ewe Muhammad! Ishi utakavyoishi, hakika wewe ni mwenye kufa. Na penda ukipendacho hakika utatengana nacho, na tenda ulitakalo hakika utalipwa kwalo…" Al-Baihaqiy Elewa ewe ndugu mpenzi ukiwa mwana kuelewa, elewa kwamba kwa mujibu wa hadithi hii:-
Vunja jungu yako ina mwisho wake ambao ni kufa kunakoashiria mwanzo wa safari ngumu ya kuhudhurishwa mbele ya Mola wako. Hii ndiyo siku anayoitaja Mola wako kwa kauli yake tukufu: "NA IOGOPENI SIKU AMBAYO MTARUDISHWA KWA ALLAH, KISHA VIUMBE WOTE WATALIPWA KWA UKAMILIFU YOTE WALIYOYACHUMA; NAO HAWATADHULUMIWA". [2:281]

Lewa sana kwani pesa ni zako,zini sana na endelea kuvunja jungu, lakini tambua kuwa iko siku moja utalipwa kwa yote uliyoyatenda hapa duniani: "BASI ANAYEFANYA WEMA (hata) WA KIASI CHA UZITO WA MDUDU CHUNGU ATAONA JAZAA YAKE. NA ANAYEFANYA UOVU (hata) WA KIASI CHA UZITO WA MDUDU CHUNGU ATAONA JAZAA YAKE". [99:7-8]

Ewe mvunja jungu wee! Hebu waidhika na sehemu hii ya kauli ya swahaba wa Mtume;Sayyidna Abdullah Ibn Abbas-Allah amuwiye radhi: "Ewe mtenda dhambi wee! Usijiaminishe na matokeo ya dhambi yako na tambua kwamba kiifuatiacho dhambi hiyo ni kikubwa kuliko dhambi yenyewe.

Kwani kule kutokuwaonea kwako haya malaika walioko kuliani na kushotoni kwako wakati unapofanya dhambi, hakupungui kuwa ni dhambi. Na kicheko chako wakati unatenda dhambi na ilhali hujui Allah atakufanya nini, ni kikubwa zaidi kuliko hiyo dhambi uitendayo.

Na kuichelea kwako dhambi unapofanikiwa kuitenda, ni kukubwa zaidi kuliko hiyo dhambi yenyewe. Na kuihuzunikia kwako dhambi kwa kushindwa kuitenda, ni kukubwa zaidi kuliko dhambi husika. Haya mpenzi mvunja jungu, ikiwa mpaka hapa bado hujawaaidhika na ukaacha kulivunja hilo jungu, hebu zidi kutega sikio:

Mtu mmoja alimwambia Sufyaan Thauriy-Allah amuwiye radhi-nipe nasaha ambazo nikizifanyia kazi sitathubutu kumuasi Allah. Sufyaan akamwambia: Yakumbuke mambo matano:
Je, inastahiki kwako kumuasi Allah na ilhali yeye ndiye anayekuruzuku?
Je, unadhani kuwa wewe unamuasi Allah na ilhali yeye anakuona?
Je, unaweza kumuasi Allah nje ya ufalme/milki yake?
Je, unaweza kuyaakhirisha mauti yakikujia?
Je, siku ya kiyama utakuwa una uwezo wa kujiondoshea adhabu?
Yule mtu akajibu: Siwezi lo lote katika hayo. Sufyaan akamwambia: Basi vipi unathubutu kumuasi yule anayekuruzuku, anakuona, nawe uko katika milki yake, akakuandikia mauti na wala huwezi kuizuia adhabu yake isikufike? Akasema mtu yule: Wallah sitamuasi muda wa uhai wangu.

Hebu nawe mvunja jungu, jiulize maswali matano hayo halafu ndio uamue ama kulivunja jungu au kutokulivunja. Kumbuka ewe ndugu muislamu kwamba:-
Kuvunja jungu ni kumuasi Allah na Mtume wake: "NA ANAYEMUASI ALLAH NA MTUME WAKE, NA KUIRUKA MIPAKA YAKE (Allah) ATAMUINGIZA MOTONI. HUMO ATAKAA MILELE NA ATAPATA ADHABU ZIFEDHEHESHAZO". [4:14]

Kuvunja jungu ni kuudhihaki mwezi mtukufu wa Ramadhani. Na kuudhihaki mwezi huu hakumaanishi kingine zaidi ya kuidhihaki Qur-ani Tukufu. Nako huku kuidhihaki Qur-ani, hakika si vinginevyo ila ni kumdhihaki aliyeshushiwa Qur-ani Mtume. Na hakuna anayethubutu kupinga kwamba kumdhihaki Bwana Mtume ni kumdhihaki Allah akiyemtuma. Na huko kumdhihaki Allah ni ukafiri tu na si vinginevyo: "AMA WALE WALIOKUFURU, NITAWAADHIBU ADHABU KALI KATIKA DUNIA NA AKHERA, WALA HAWATAPATA WASAIDIZI WA KUWASAIDIA". [3:56] Vunja jungu ni khadaa na ghururi za dunia. Uovu basi si huko kukhadaika, bali ni kushikilia kukhadaika baada ya kutanabahishwa. Wasalaamu Alaykum Warahmatullah.
MWISHO