SHEIKH SHALTUT
  • Kichwa: SHEIKH SHALTUT
  • mwandishi: BARAZA
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 7:25:9 24-8-1403

BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

SHEIKH SHALTUT

Sheikh Shaltut: "Madhehebu ya J'afariya maarufu kwa jina la madhehebu ya Shia Ithnaashariya, ni madhehebu ambayo kisheria inajuzu kufuatwa kama zilivyo madhehebu za Kisuni. Kwa msingi huo, ni vyema kwa Waislamu kuelewa ukweli huo na kujiepusha na taasubi (chuki za kimadhehebu) zisizofaa dhidi ya madhehebu makhsusi; kwani dini ya Mwenyezi Mungu na sheria yake haifuati madhehebu wala haiwezi kuhodhiwa na madhehebu makhsusi. Watu wa madhehebu mbalimbali ya Kiislamu wanafanya ijtihadi na kazi yao hiyo itatakabaliwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu."

Sheikh Mahmoud Shaltut alizaliwa tarehe 5 Shawwal mwaka 1310 (Aprili 23, 1893) katika kijiji cha Minyat Bani Mansur katika mkoa wa Buhayrah nchini Misri katika familia ya wanazuoni. Baba yake Sheikh Muhammad alimpa jina la Mahmoud na akafanya jitihada kubwa za kumlea na kumuelemisha mwanae.

Kuanza Masomo Mahmoud Alikuwa na umri wa miaka saba wakati baba yake apofariki dunia na akachukuliwa na ami yake Sheikh Abdulqawy Shaltut. Tangu hapo awali, kijana Mahmoud alionekana kuwa hodari na mwenye kipawa kikubwa katika kazi zake. Kwa sababu hiyo ami yake alimpeleka katika maktaba ya kijiji kwa ajili ya kupata elimu na maarifa ya Kiislamu. Miongoni mwa sheria na kanuni za maktaba za Misri za wakati huo ilikuwa ni mwanafunzi kuhifadhi moyoni Qur'ani nzima kabla ya kuanza kupata masomo ya fasihi ya lugha ya Kiarabu. Mahmoud, kama walivyokuwa wanafunzi wenzake, alilazimika kuhifadhi Qur'ani kabla ya jambo lolote na akafanikiwa kuhifadhi Qur'ani nzima katika kipindi kifupi.

Kipindi cha Kukamilisha Masomo Mwaka 1328 Hijria Kamaria (1906) Mahmoud alihamia katika mji wa Alexandria kwa ajili ya kupata elimu ya juu na akaanza masomo katika Chuo cha Alexandria. Uhodari wake wa kielimu na kipaji chake kikubwa kiliwashangaza walimu na wanafunzi wa chuo hicho. Baada ya kufanya bidii kubwa katika masomo, hatimaye mwaka 1340 (1918) alifanikiwa kupata shahada ya juu kabisa ya Chuo cha Alexandria na kuwa mwanafunzi bora wa chuo hicho akiwa na umri wa miaka 25. Mwaka mmoja baada ya kuhitimu masomo yaani mwaka 1341 Hijria (Februari 1919), Sheikh Shaltut alianza kufundisha katika chuo hicho.

Kazi ya kuanza kufundisha katika Chuo cha Alexandria ya Mahmoud Shaltut ilisadifiana na mapinduzi ya wananchi wa Misri yaliyoongozwa na Saad Zaghlul. Vijiji na miji ya Misri ilishuhudia maandamano makubwa ya kumuunga mkono Saad Zaghlul dhidi ya wakoloni. Sheikh Shaltut pia alijiunga na harakati hiyo na kutekeleza wajibu wake wa kimapinduzi. Alihudumia mapinduzi hayo ya wananchi kwa ulimi na kalamu yake.

Shaltut Ajiunga na Chuo Kikuu cha al Azhar Wakati Sheikh Muhammad Mustafa Maraghi ambaye alikuwa na taathira kubwa mno katika itikadi za Shaltut alipochaguliwa kuwa mkuu wa Chuo cha al Azhar mwaka 1360 Hijria (1938) na kusoma makala iliyokuwa imeandikwa na Sheikh Mahmoud Shaltut, alivutiwa mno na fikra za msomi huyo kijana, umahiri wake mkubwa wa fasihi ya lugha ya Kiarabu na uwezo wake mkubwa wa kutumia lugha hiyo katika maandishi. Kwa msingi huo Sheikh Maraghi alimwalika Sheikh Shaltut kufundisha katika chuo cha al Azha. Shaltut ambaye alikuwa akifundisha na kulea vijana katika Chuo cha Alexandria alikaribisha mwaliko huo na kuelekea Cairo ambako alianza kufunza katika Chuo Kikuu cha al Azhar. Ufanisi wake mkubwa katika uwanja huo ulimfanya achaguliwe kuwa mhadhiri wa wanafunzi wanaochukua masomo makhsusi katika chuo hicho hapo mwaka 1361 (1939).

Walimu wa Shaltut Sheikh Shaltut alisoma kwa walimu wengi japokuwa watatu miongoni mwao ndio waliokuwa na hisa kubwa zaidi kuliko wengine katika kumlea na kumuelimisha mwanazuoni huyo. Walimu hao ni:
1- Ustadh Sheikh al Jizawi, ambaye alimfunza katika Chuo cha Alexandria.
2- Sheikh Abdulmajid Saliim. Mwanazuoni huyu alizaliwa mwaka 1304 Hijria (13 Oktoba 1882) nchini Misri. Baada ya kukamilisha elimu ya msingi alijiunga na Chuo Kikuu cha al Azhar na kuhitimu masomo mwaka 1330 Hijria. Baada ya kukamilisha masomo yake aliteuliwa kuwa kadhi, mhadhiri na mwanachama katika Baraza la Fatuwa. Sheikh Abdulmajid Saliim alikuwa miongoni mwa wanafunzi wa Imam Muhammad Abduh.

Vilevile Sheikh Abdulmajid Saliim ni miongoni mwa waasisi wa Jumuiya ya Kukurubisha Madhehebu ya Kiislamu na alikuwa miongoni mwa wanachama hai na wenye kujituma wa jumuiya hiyo. Moja ya sifa kuu za mwanazuoni huyo ulikuwa uwazi na ushujaa wake. Kutokana na ushujaa na uwazi huo, Sheikh Saliim aliamua kujiuzulu cheo cha Mkuu wa Chuo cha al Azhar mwaka 1368 Hijria baada ya kuona kwamba serikali inaingilia mambo ya chuo hicho. Mkuu wa Mahakama Kuu ambaye alikasirishwa mno na hatua hiyo alimtishia Sheikh Abdulmajid Saliim akisema: "Kutokana na hatua hiyo utakabiliwa na hatari". Hata hivyo Sheikh Saliim alimjibu kwa damu baridi na ushujaa mkubwa akisema: Sitapatwa na hatari yoyote maadamu harakati zangu zinafanyika baina ya masjidi na nyumbani kwangu". (Tazama kitabu cha: Sheikh Mahmoud Shaltut, Kinara wa Kituo cha Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu" kilichoandikwa na Sheikh Biazar Shirazi.)

Sheikh Saliim alifariki dunia tarehe 10 Alkhamisi mwezi wa Safar 1374 Hijria baada ya miaka mingi ya jitihada za kukurubisha pamoja madhehebu za Kiislamu.
3- Sheikh Imam Muhammad Mustafa Maraghi
Sheikh Muhammad Mustafa Maraghi alizaliwa mwaka 1303 Hijria (Machi 1881) katika eneo la Maragha kwenye mkoa wa Sohag nchini Misri. Alihifadhi Qur'ani nzima akiwa bado kijana mdogo na alikuwa miongoni mwa muridi, wafuasi na wanafunzi wa Sheikh Muhammad Abduh. Sheikh Maraghi aliathirika mno na fikra za Sheikh Muhammad Abduh. Sheikh Rashid Ridha ameandika kuhusu mwanazuoni huyo kwamba: Sheikh Muhammad Mustafa Maraghi alikuwa ndugu wa karibu na wenye ikhlasi zaidi kwa Sheikh Muhammad Abduh. Sheikh Maraghi ameandika vitabu vingi katika medani ya Qur'ani na maarifa ya Kiislamu kikiwemo kitabu cha al Auliyaa Walmahjurina na tafsiri ya sura kadhaa za Qur'ani Tukufu. Alifariki dunia mwezi Ramadhani mwaka 1364 Hijria na kuzikwa katika makaburi ya Sayyida Nafisa.

Wanafunzi Wake: 1- Abbas Mahmoud Aqqad
Abbas Mahmoud Aqqad mshairi, mkosoaji na mwandishi mashuhuri wa habari wa Misri alizaliwa mwaka 1311 Hijria (1889 Miladia) katika mkoa wa Aswan. Kazi yake ya asili ilikuwa uandishi habari japokuwa alikuwa hodari mno katika kutunga na kuandika mashairi. Vitabu vyake vingi kama Wahyul Arbain, Hadiyyatul Karawan na Aabiru Sabil vinahusu mashauiri. Aqqad ameandika vitabu kadhaa kuhusu shakhsia adhimu wa Kiislamu kama kile cha Abqariyyatu Muhammad. (Tazama al Munjid fil Aalam) 2- Sheikh Ali Abdul Razzaq

Kuachishwa Kazi al Azhar Sheikh Mustafa Maraghi ambaye alikuwa mwanamageuzi mkubwa alikuwa ameazimia kutekeleza mipango yake ya marekebisho katika chuo cha al Azhar na kwa msingi huo aliwasilisha rasimu ya marekebisho hayo kwa serikali ya Misri. Sheikh Shaltut pia aliandika makala kadhaa katika magazeti akiunga mkono hatua na mipango ya Sheikh Maraghi. Aliutaja mpango huo kuwa ni hatua kubwa katika njia ya koberesha hali ya kiutamaduni na kielimu ya chuo cha al Azhar.

Mahakama iliyokuwa imejaa ufisadi na tegemezi ya Misri ilipinga rasimu hiyo. Baada ya hatua hiyo Sheikh Maraghi alichukua hatua ya kujiuzulu uongozi wa chuo cha al Azhar kama hatua ya kulalamikia uamuzi wa mahakama. Mahakama ya Misri ilikubali kujiuzulu kwa Sheikh Maraghi na ikamteuwa Sheikh Muhammad Dhawahiri kuwa Mkuu wa chuo hicho. Kiongozi huyu mpya wa al Azhar aliamua kuanza kutekeleza mipango na ratiba za mahakama ya Misri lakini alikabiliwa na upinzani mkali wa wanazuoni wenye mwamko. Sheikh Dhawahiri alichukua hatua ya kuwafuta kazi baadhi ya maulamaa waliokuwa safu ya mbele katika upinzani huo akiwemo Ustadh Mahmoud Shaltut hapo mwaka 1353 (17 Septemba 1931).

Baada ya kuachishwa kazi, Sheikh Shaltut hakuketi chini, bali aliingia katika kazi ya uwakili kwenye mahakama za Kiislamu akiwa pamoja na mwanafunzi wake Sheikh Ali Abdul Razzaq huku akiendelea kuandika makala magazetini. Hakulegeza kamba hata kidogo katika misimamo yake ya kimsingi na daima alikuwa kisisitiza juu ya udharura wa kufanyika marekebisho katika chuo cha al Azhar.

Baada ya kupita muda viongozi wa chuo hicho walitambua kwamba kutokuwepo maulamaa wakubwa chuoni hapo kama Ustadh Shaltut kunapunguza heshima na hadhi ya chuo hicho; kwa msingi huo mwaka 1357 Hijria (1935) walimwalika tena kufundisha na kufanya kazi katika chuo cha al Azhar. Sheikh Shaltut alianza kufunza katika kitivo cha sheria cha chuo huo.

Fahari za Kielimu za Sheikh Shaltut Katika kipindi chote cha maisha yake ya kifikra, Sheikh Mahmoud Shaltut alienziwa na kutuzwa mara nyingi kwa sababu ya juhudi na kazi zake kubwa za kielimu na kiutamaduni. Kwa mfano tu, mwaka 1380 Hijria (1958) alitunukiwa shahada ya uzamivu ya Chuo Kikuu cha Chile na mwaka 1382 Hijria (1960) akatunukiwa shahada ya uzamivu pia na Chuo Kikuu cha Jakarta.

Shaltut Ateuliwa Kuongoza al Azhar Mwaka 1359 (1937 Miladia) serikali ya wakati huo ya Misri ilimrejesha Sheikh Maraghi katika uongozi wa chuo cha al Azhar. Ustahiki na kazi nzuri za Sheikh Shaltut vilimfanya Sheikh Maraghi amteuwe kuongoza kitivo cha sheria cha chuo hicho. Mwaka 1379 (1937 Miladia) Sheikh Maraghi alimpandisha cheo Sheikh Shaltut na kumteuwa kuwa Kaimu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha al Azhar. Miaka minne baadaye yaani mwaka 1961, Rais wa wakati huo wa Misri alimteuwa Sheikh Mahmoud Shaltut kuwa mkuu wa chuo cha al Azhar.

Katika kipindi chote cha uongozi wake chuoni hapo Sheikh Shaltut alitoa huduma kubwa mno kwa elimu ya dini ya Kiislamu. Moja ya mipango muhimu ya mwanazuoni huyo katika Chuo Kikuu cha al Azhar ilikuwa ni kufuta hisia za chuki za kimadhehebu. Alipoulizwa na mwandishi wa habari juu ya malengo ya chuo cha al Azhar chini ya uongozi wake, Sheikh Shaltut alijibu: "Miongoni mwa malengo makuu na muhimu ya chuo hiki ni kukabiliana na hisia za chuki za kimadhehebu, kuzidisha uchunguzi na utafiti katika anga ya utulivu na udugu, na kufuata hoja na dalili madhubuti popote itakapokuwa."

Miongoni mwa hatua muhimu za Sheikh Shaltut wakati wa uongozi wake katika chuo cha al Azhar ilikuwa ni kuanza kufundisha fiqhi ya madhehebu ya Shia Imamiyya sambamba na fiqhi ya madhehebu za Ahlusunna. Kazi nyingine muhimu ya Sheikh Shaltut ilikuwa ni kuanzisha shughuli za kukumbuka siku ya Shuraa na vikao vya kuomboleza kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) Imam Hussein (as) katika chuo cha al Azhar. Suala hilo lilionesha mapenzi yake makubwa kwa Ahlyl Bait wa Mtume hususan Imam Hussein (as).

Ustadh Muhammad Wai'dh Zadeh Khurasani anasema: "Katika kipindi cha uongozi wa Sheikh Mahmoud Shaltut kwenye chuo cha al Azhar, shughuli ya kukumbuka siku ya Ashuraa na vikao vya maombolezo ya mauaji ya Bwana wa Mashahidi Imam Hussein (as) vilifanyika katika uwanja wa al Azhar .

Harakati za Kielimu za Shaltut 1- Kuasisi Akademia ya Utafiti wa Kiislamu
Sheikh Mahmoud Shaltut aliasisi akademia hiyo ambayo iliwakutanisha pamoja maulamaa na wanazuoni wa madhehebu mbalimbali. Wawakilishi wa madhehebu zote za Kiislamu walikuwa wakihudhuria katika taasisi hiyo na kujadili masuala mbalimbali ya Kiislamu.
2- Sheikh Shaltut katika Mkutano wa Uholanzi
Mwaka 1937 Sheikh Shaltut aliteuliwa na chuo cha al Azhari kukiwakilisha chuo hicho katika mkutano wa kimataifa uliofanyika nchini Uholanzi. Katika mkutano huo Ustadh Shaltut aliwasilisha makala iliyojadili majukumu ya kiraia na vyombo vya sheria katika sheria ya Kiislamu. Makala hiyo ilichaguliwa kuwa makala bora ya mkutano huo.
3- Mwanachama katika Kamati ya Tafsiri ya Qur'ani ya Redio ya Misri
Kazi ya kamati hiyo ilikuwa ni kusimamia vipindi vya tafsiri ya Qur'ani Tukufu katika Redio ya Misri. Shaltut ambaye alikuwa mwanacha mwenye ushawishi mkubwa katika kamati hiyo alipendekeza kuanzishwe kipindi cha tafsiri ya Qur'ani kabla na baada ya kiraa cha Qur'ani katika Redio Misri.
4- Uanachama katika Kamati ya Fatuwa ya al Azhar
Wadhifa mkuu wa kamati hii ni kutoa fatuwa kuhusiana na masuala mbalimbali ya kifiqhi kwa mujibu wa mahitaji ya jamii. 5- Uanachama katika Jumuiya ya Maulamaa Wakubwa wa Misri

Sheikh Mahmoud Shaltut aliteuliwa kuwa mwanachama katika jumuiya hiyo akiwa mwanazuoni kijana zaidi ya wote. Katika kikao cha kwanza cha jumuiya hiyo, Sheikh Shaltut alitoa mapendekezo muhimu na mwenyekiti wake Sheikh Abdul Majiid Saliim akaamuru iundwe kamati maalumu ya kushughulikia mapendekezo hayo.
6- Mitazamo ya Sheikh Shaltut kuhusu ndoa katika Ujerumani Magharibi
Serikali ya Ujerumani Magharibi ilimuandikia barua Sheikh Shaltut ikimtaka afanye uchunguzi kamili kuhusu suala la ndoa za mitara katika Uislamu na kutuma uchunguzi huo kwa serikali ya nchi hiyo ili utumiwe kutafuta ufumbuzi wa tatizo la ongezeko la idadi ya wanawake nchini humo. Sheikh Mahmoud Shaltut alianza uchunguzi huo na ikapangwa kuwa utarjumiwe kwa lugha tatu za Kiingereza, Kijerumani na Kifaransa. Wakati huo magazeti yaliandika kuwa uchunguzi huo wa Sheikh Shaltut ulikuwa wa kwanza kujadili suala la ndoa za mitara na uongozeko la idadi ya wanawake nchini Ujerumani.

7- Uanachama katika Kituo cha Lugha ya Kiarabu cha Misri na Misimamo ya Shaltut
Siku sita baada ya tukio la mauaji ya tarehe 5 Juni 1963 na kutiwa mbaroni wanazuoni wa Kiislamu nchini Iran, Sheikh Mahmoud Shaltut alitoa taarifa akiwataka Waislamu wote kuwaunga mkono wanazuoni wa Kiislamu waliotiwa nguvuni nchini Iran kwa kosa la kutetea haki. Katika taarifa hiyo Sheikh Shaltut alikemea mno kitendo cha kutiwa nguvuni wanazuoni hao wa Kiislamu na kuvunjiwa heshima matukufu ya Kiislamu akikitaja kuwa ni aibu kubwa kwa wanadamu. Vilevile alimtumia rasmi telegrafu Shah wa Iran akimtaka asitishe vitendo vya kuwavunjia heshima wanazuoni wa Kiislamu na kuwaachia huru mara moja maulamaa na wananchi waliotiwa nguvuni katika tukio hilo. Matini ya taarifa ya Sheikh Shaltut ni hii ifuatayo: Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehma Mwenye kurehemu.

"Haya ni maelezo yaliyowazi kwa watu.." (Al Imran:138) Katika kipindi cha sasa kunafanyika propaganda chafu na ukandamizaji wa wazi ambao wahanga wake ni maulamaa wa Kiislamu nchini Iran. Rijali ambao wanalingania watu njia ya Mwenyezi Mungu na kulinda dini yake na hawakutenda kosa lolote ghairi ya kutangaza neno la Mungu. Maulamaa wa Uislamu na wanazuoni wa Kiirani wanakandamizwa mara kwa mara na kufungwa jela, huku wakizuiwa kuamrisha mema na kukatazama maovu ambako ni wajibu kwa kila mtu mwenye uwezo. Sehemu nyingine ya taarifa hiyo ya Sheikh Shaltut inasema: Ninawataka Waislamu wote kuwanusuru Waislamu katika nchi zote hususan taifa la Waislamu la Iran na kutumia nguvu zenu zote kwa ajili ya kuwaokoa maulamaa wa Iran kutoka kwenye makucha ya utawala wa kidikteta wa Shah. "Wala msiwategemee wale waliodhulumu usije ukakuguseni moto, na hamtakuwa na walinzi badala ya Mwenyezi Mungu kisha hamtasaidiwa. (Huud:113)

Kutambua Rasmi Israel Kufuatia juhudi za mara kwa mara za Marekani na Uingereza, tarehe 29 Novemba mwaka 1947 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipasisha pendekezo la kuigawa ardhi tukufu ya Palestina katika sehemu mbili za Wayahudi na Waislamu na miezi mitano baadaye serikali ya Israel ikaundwa. Baada ya hapo baadhi ya nchi ziliitambua rasmi Isral. Mfalme Muhammad Reza wa Iran kibaraka wa Marekani na Uingereza ambaye aliona kubakia kwake madarakani kwamba kunafungamana na kuzitii nchi hio mbili, pia aliutambua rasmi utawala huo ghasibu na kufungua ofisi ya ubalozi wa Iran huko Baitul Muqaddas.

Baada ya habari hiyo kosambazwa, wanafikra na maulamaa waliopevuka ndani na nje ya Iran walipinga vikali hatua hiyo. Kiongozi wa kidini wa wakati huo wa Iran Ayatullah Kashani alitoa hotuba kali akilaani vikali hatua hiyo ya Shah. Katika nchi za Kiarabu pia maulamaa wa Kiislamu na wanafikra walilaani vikali kitendo cha Shah wa Iran. Sheikh Shaltut alipinga hatua yoyote ya kuanzisha uhusiano na utawala ghasibu wa Israel na akalaani vikali hatua ya serikali ya wakati huo ya Iran. Sheikh Mahmoud Shaltut alimtumia ujumbe Ayatullah Borujerdi aliyekuwa mjini Qum Iran akisema: Kwa jina la Allah, mwingi wa rehma, Mwenye kurehemu.

Salamu za Mwenyezi Mungu ziwe juu yako na juu ya ndugu zetu, maulamaa wa Iran na watu wote wanaotetea na kulinda umoja na mshikamano wa Waislamu. Bila shaka wewe mheshimiwa na ndugu zetu wote mmesikia habari ya kuhuzunisha katika siku hizi kwamba Shah wa Iran ameitambua rasmi Israel ambayo imevamia ardhi ya Palestina na kuwafanya wakazi wake kuwa wakimbizi na kisha kughusubu haki zao.

Ni jambo la kusikitisha kuona mfalme ambaye yeye mwenyewe na taifa lake ni la Kiislamu akiwaunga mkono maadui wa Waislamu na kuanzisha uhusiano wa kirafiki na maadui hao. Nimemtumia Shah telegrafu mbili nikimuarifu kuwa hatua hiyo itakuwa kisingizio cha wale wanaotaka kukata uhusiano ambao tumefanya jitihada kubwa kwa ajili ya kuuimarisha. Sina shaka kwamba wewe pia umeathiriwa mno na kitendo hicho cha Shah na utafanya bidii kukilaani vikali. Bila shaka hatua yako itakuwa na taathira kubwa. Ninasubiri kupokea barua yako. Wassalam Alaykum Warahmatullah wabarakatuh.
Ndugu yako Mahmoud Shaltut- Sheikh wa al Azhar

Inasikitisha kwamba wakati telegrafu ya Sheikh Shaltut ilipowasili Qum, Ayatullah Borujerdi alikuwa mgonjwa mahututi katika maradhi ambayo yalihitimisha maisha yake. Hata hivyo Shikh Shaltut hakusitisha harakati zake katika uwanja huo na alichukua hatua ya kumwandikia barua Ayatullah Sayyid Muhsin al Hakim huki Iraq (aliyefariki dunia mwaka 1390 Hijria) akimtaka kuchukua hatua katika uwanja huo. Barua hizo mbili za Sheikh Mahmoud Shaltut zinabainisha masuala kadhaa muhimu: 1- Juhudi na mazingatio yake makubwa kwa suala la kukomboa ardhi tukufu ya Quds.
2- Juhudi zake za kukabiliana na watu wanaoutetea kwa njia yoyote ile utawala haramu wa Israel.
3- Uhusiano wake mzuri na maulamaa wa madhehebu ya Waislamu wa Kishia, suala ambalo linaonekana vyema katika lahani ya barua hizo.
4- Uhusiano wake mkubwa na mawasiliano yake ya mara kwa mara na wanazuoni wa Kishia na kushauriana nao katika masuala muhimu yanayowahusu Waislamu. Baada ya Ayatullah Muhsin al Hakim kupokea barua hiyo huko Iraq, alimtumia telegrafu Ayatullah Behbahani aliyekuwa mjini Tehran na kumtaarifu kadhia hiyo. Ayatullah Behbahani pia alimuarifu Shah kuhusu hasira na upinzani wa maulamaa na wanazuini wakubwa wa kidini dhidi ya uamuzi wake wa kuutambua rasmi utawala ghasibu wa Israel.

Fikra za Umoja Hapana shaka kwamba Sheikh Mahmoud Shaltut alikuwa miongoni mwa wanazuoni wachache wa Kiislamu wa zama hizo ambao walitoa kipaumbele kwa suala la umoja na mshikamano wa Kiislamu. Aliamini kwamba moja ya masuala muhimu ya kuimarisha umoja huo ni kutafuta nukta moja na suala linalowakutanisha wafuasi wa madhehebu zote za Kiislamu. Alifikia uamuzi kwamba jambo hilo ni kitabu cha Mwenyezi Mungu, Qur'ani Tukufu. Kuhusu suala hilo Sheikh Shaltut ameandika kwamba: "Uislamu umewalingania umoja wafuasi wake wote na kuwaainishia nguzo moja ya kushikamana nayo ambayo ni kamba ya Mwenyezi Mungu. Suala hilo limezungumziwa katika aya nyingi za Qur'ani. Wito wa wazi zaidi umetolewa katika aya ya 103 ya suratu Aal Imran inayosema: "Na shikamaneni na kamba ya Mwenyezi Mungu nyote na wala msifarikiane.." Katika aya hii Mwenyazi Mungu amekata aina zote za mifarakano ambazo zinajumuiya mifarakano inayosababishwa na taasubi na chuki za kimadhehebu."

Mwisho wa kunukuu Katika sehemu nyingine Sheikh Shaltut anakitaja Kitabu cha Mwenyezi Mungu Qur'ani na Suna za Mtume wake (SAW) kuwa ndio mambo yanayowakutanisha pamoja wafuasi wa madhehebu zote za Kiislamu. Anasema: "Katazo la mifarakano linajumuisha mifarakano ya kimadhehebu, kwani licha ya kwamba madhehebu na mirengo mbalimbali ya fiqhi ya Kiislamu ilikuwa mingi na mbinu zao zilitofautiana, lakini imetolewa katika misingi ya aina moja iliyomo ndani ya Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Suna za Mtume wake. Hata hivyo na licha ya hitilafu za kimadhehebu katika masuala mengi ya kifiqhi na kuwepo mitazamo tofauti, lakini wote wanakutana katika nukta moja ambayo ni imani ya vyanzo na marejeo asili na matakatifu, yani Qir'ani na Suna za Mtume (SAW)."

Sababu za Umoja kati ya Waislamu 1- Kuacha Taasubi: Mwandishi mmoja wa habari alimuuliza Sheikh Mahmoud Shaltut kwamba ni mambo gani yanayoimarisha zaidi umoja na mshikamano wa Kiislamu? Sheikh alijibu kwamba: "Jambo la kwanza ni kutupilia mbali taasubi na chuki za kimadhehebu na kuchunga insafu na uadilifu. Suala hilo litasaidia katika kufikiwa masharti mengine ikiwa ni pamoja na kutilia maanani utamaduni wa Kiislamu na kufaidika na mitazamo mbalimbali. Vitabu na majarida yanapaswa kuchapishwa na kubadilisha mawazo na fikra, na vyuo vikuu na vituo vya elimu vinapaswa kuwa na mawasiliano ya mara kwa mara na kubadilishana wahadhiri na wanafunzi. Matatizo yote yanapaswa kujadiliwa katika anga ya kidugu. Uhusiano wa kiroho kati ya Waislamu unapaswa kuimarishwa zaidi na kufikia daraja iliyotajwa na Mtume (SAW) katika hadithi isimayo: Iwapo kiungo kimoja cha umma wa Kiislamu kitapatwa na maumivu, basi viungo vingine hukosa usalama na amani."

Sheikh Mahmoud Shaltut alikuwa akitofautisha baina ya hitilafu za kielimu zinazotokea katika taasisi za kielimu kwa upande mmoja na taasubi na chuki za kimadhehebu zinazoshuhudiwa kati ya watu maamuma. Anasema: "Hitilafu za kimitazamo ni jambo la kawaida na dharura ya kijamii ambayo haiwezi kuepukwa, lakini inatofautiana na hitilafu zinazosababisha taasubi za kimadhehebu na fikra finyu. Taasubi inakata misingi ya uhusino wa Waislamu na kupanda mbegu za uhasama na vinyongo katika nyoyo. Hitilafu zinazosababishwa na uchunguzi na utafiti sambamba na kuheshimu mitazamo na fikra za upande wa pili ni jambo la kupongezwa na linalokubaliwa."

Katika sehemu nyingine Sheikh Shaltut anasema: "Mtu yeyote hapaswi kuamini kuwa amefikia ukweli na hakika mutlaki isiyokuwa na shaka ndani yake na kwamba watu wengine wanapaswa kumfuata yeye. Bali mtu yeyote anapaswa kutambua kwamba fikra na mitazamo aliyofikia ni itikadi na matokeo ya juhudi za uchunguzi wake. Asimruhusu mtu kumfuata bila ya msingi na ushahidi wowote, bali afanye jitihada za kujua mashiko yake na atakapopata ushahidi wa kutosha ndipo atakapomuunga mkono."

2- Nafasi na Mchango wa Wanazuoni wa Kidini
Wasomi na wanazuoni wa dini yoyote ile huwa na mchango mkubwa katika kupeleka mbele na kufanikisha malengo ya dini hiyo. Kwa msingi huo iwapo wanazuoni wa Kiislamu watafanya jitihada kubwa za kujenga umoja na mshikamano zaidi na kuuelimisha umma kuhusu hatari za mifarakano na jinsi adui anavyoweza kutumia vibaya hitilafu za Waislamu, hapana shaka kwamba hatua hiyo itaimarisha mshikamano na umoja katika ulimwengu mzima wa Kiislamu mbele ya kambi ya ukafiri na mabeberu. Sheikh Mahmoud Shaltut alikuwa akisisitiza mno juu ya mchango na nafasi ya wasomi na wanazuoni wa Kiislamu katika suala la umoja wa Kiislamu na kuwahimiza kuwa na umoja na mshikamano zaidi. Amesema: "Kwa mara nyingine tena na kwa jina la Mwenyezi Mungu, kitabu kitukufu cha Qur'ani, umoja wa Kiislamu na kamba madhubuti ya Mwenyezi Mungu, ninawalingania maulamaa wa Kishia na Kisuni suala la umoja na mshikamano zaidi."

Njama za Maadui Moja ya njama za wakoloni na mabeberu ni kuzusha hitilafu na mifarakano katika jamii za Waislamu ili waweze kufikia malengo yao ya kishetani na kupora utajiri wa Waislamu chini ya kivuli cha hitilafu hizo. Vilevile tunapaswa kutambua kwamba hakuna mtu anayefurahia zaidi hitilafu na mifarakano ya Waislamu kuliko viongozi wa nchi za kibeberu. Allamah Shaltut alikuwa akitahadharisha mno kuhusu suala hilo na kusema: "Mwenyezi Mungu (SW) ameutaka umma wa Kiislamu kuwa na umoja na mshiakamano na kujiepusha na makundi na migawanyiko inayodhoofisha nguvu na uwezo wao." Wakoloni hawafurahishwi na umoja na mshikamano wa Waislamu kwani wanaelewa kuwa umoja wa Waislamu ni kizingiti na kikwazo muhimu dhidi ya tamaa na mipango yao ya kikoloni na kibeberu. Kwa msingi huo hufanya kila wawezalo kuzuia mipango na harakati za kuwaunganisha Waislamu na kuimarisha umoja na mshikamano wao.

Mchango wa Sheikh Shaltut katika Darul Taqrib Kundi la kukurubisha pamoja madhehebu za Kiislamu liliasisiwa mwaka 1948 mjini Cairo huko Misri kwa shabaha ya kukurubisha pamoja wafuasi wa madhehebu tofauti za Kiislamu. Waasisi wa kundi hilo walikuwa ni: Allamah Muhammad Taqi Qummi, Sheikh Mahmoud Shaltut, Sheikh Muhammad Mustafa Maraghi, Mustafa Abdur Razzaq na Abdul Majiid Saliim. Jumuiya hiyo ilifungwa hapo baadaye. Hata hivyo wanazuoni wa Iran walichukua uamuzi wa kuasisi jumuiya nyingine ya Taasisi ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu kwa lengo hilo hilo. Hadi sasa taasisi hiyo imetoa huduma kubwa katika njia ya kukurubisha pamoja wafusi wa madhehebu mbalimbali za Kiislamu na kuimarisha umoja na mshikamano miongoni mwa wafuasi wa dini hiyo tukufu. Allamah Shaltut alipongeza taasisi hiyo ya kukurubisha pamoja wafuasi wa madhehebu tofauti za Kiislamu akisema: "Taasisi hiyo imezidisha moyo wa udugu na upendo kati ya Waislamu."

Sheikh Mummad Taqi Qummi ambaye alikuwa miongoni mwa waasisi wa Darul Taqrib mjini Cairo anasema kuhusu mchango mkubwa wa Sheikh Shaltut kwamba: "Katika kipindi cha kuasisiwa na kudhihiri Darul Taqrib, Ustadh Mahmoud Shaltut alikuwa miongoni mwa wanazuoni na wahadhiri wakubwa wa al Azhar. Daima alikuwa akishirikiana na wenzake katika harakati za kuwakurubisha pamoja Waislamu. Katika moja ya vikao vya kundi hilo, Sheikh Shaltut alitoa pendekezo kwamba tunapaswa kuwatambua Mashia na Masuni kuwa ni washirika katika kila kitu kuwatambua wafuasi wa madhehebu hizo kuwa ni wafuasi wa madhehebu za Kiislamu. Hata baada ya kuchaguliwa kuwa Kaimu Mkuu wa Chuo cha al Azhar, Sheikh Shaltut aliendeleza ushirikiano wake na Darul Taqrib."

Katika sehemu nyingine Sheikh Muhammad Taqi Qummi anasema: "Sheikh Shaltut alikuwa mwanachama katika Darul Taqrib kwa kipindi cha miaka 17. Katika miaka mitano ya mwishoni mwa umri wake alichaguliwa kuwa Sheikh wa al Azhar na daima alikuwa akifanya jitihada kubwa za kukurubisha pamoja wafuasi wa madhehebu za Shia na Suni kabla na baada ya kuchaguliwa kuongoza Chuo cha al Azhar."

Wakati alipokuwa shekh wa al Azhar, Sheikh Mahmoud Shaltut alipata fursa ya kutoa fatuwa yake ya kihistoria iliyojuzisha kwa wafuasi wa madhehebu za Kisuni kufuata madhehebu ya Kiislamu ya Shia J'afariya. Fatuwa hiyo muhimu na ya aina yake ya Sheikh Shaltut ilitiwa saini na wanachama wa Darul Taqrib. Fatuwa hiyo wa Sheikh wa al Azhar ilikuwa na mwangwi mkubwa katika nchi za Kiislamu na kuzinawirisha fikra za watu safi na imani kubwa ya kidini za waliokuwa na azma kubwa ya kukurubisha pamoja Waislamu wa madhehebu zote.

Katika upande mwingine kulijitokeza maswali na mijadala ya hapa na pale kuhusu fatua hiyo ya aina yake. Sheikh Shaltut alijibu maswali na mijadala hiyo kwa hoja na dalili za kimantiki.

Mawasiliano ya Sheikh Shaltut na Maulamaa wa Kishia 1- Mawasiliano yake na Ayatullah Borujerdi
Moja ya hatua zilizochukuliwa na Sheikh Mahmoud Shaltut katika njia ya kuimarisha umoja na mshikamano kati ya Waislamu ni kufanya mawasiliano ya mara kwa mara na wanazuoni na maulamaa wa madhehebu nyingine za Kiislamu hususan wanazuoni wa Kishia. Alikuwa akiwaheshimu mno maulamaa wa Kishia hususan Ayatullah Borujerdi na alikuwa akimkirimu na kumuenzi.
2- Swala ya Jamaa kwa Uimamu wa Kashifl Ghitaa
Katika safari yake aliyofanya huko Quds Tukufu kwa shabaha ya kushiriki kwenye mkutano wa Kiislamu kuhusu Palestina akifuatana na wanazuoni wengine kadhaa, Sheikh Shaltut aliswali swala ya jamaa nyuma ya Ayatullah Sheikh Kashiful Ghitaa. Sheikh Shaltut anasifu mandhari hiyo ya kupendeza ya swala ya jamaa iliyowashirikisha maulamaa na wanazuoni wa Kishia na Kisuni akisema: "Ni sura ya kupendeza mno kuona wawakilishi wa Waislamu wanaoshiriki katika mkutano wa Palestina wakikusanyika katika msikiti wa al Aqsa na kuswali kwa pamoja swala ya jamaa nyuma ya mmoja wa wanazuoni wakubwa wa Shia Imamiyya na mwanazuno mwenye hadhi kubwa Shekh Muhammad Hussein Kashiful Ghitaa bila ya kuwepo tofauti kati ya wanaojiita Suni au Shia. Wote wamesimama katika safu moja za ina moja nyuma ya imamu mmoja na kumuomba Mwenye Mungu Mmoja wakielekea kibla kimoja."

Fatuwa ya Kihistoria Hapana shaka yoyote kwamba hatua muhimu zaidi ya Sheikh Mahmoud Shaltut katika kipindi chote cha uhai wake ilikuwa ni fatuwa alitoa akijuzisha kufuata fiqhi za madhehebu zote zinazokubalika za Kiislamu ikiwemo madhehebu ya Shia Imamiyya. Kwa fatuwa hiyo, Sheikh Shaltut alipiga hatua kubwa na muhimu mno katika njia ya kukurubisha pamoja wafuasi wa mashehebu za Kiislamu hususan Shia na Suni.

Historia ya Fatuwa Hiyo Wakati Sheikh Abdulmajid Saliim aliposhika hatamu za kuongoza Chuo Kikuu cha al Azhar, alichukua uamuzi wa kutoa fatuwa inayojuzisha na kuwaruhusu wafuasi wa madhehebu za Suni kufuata madhehebu ya Ahlul Bait, yaani Shia Ithnaasharia. Hata hivyo kabla ya Sheikh Abdulmajid Salim kutoa fatuwa hiyo, vibaraka wa wakoloni na mabeberu walichapicha na kusambaza kitabu kinachovunjia heshima matukufu ya Ahlusunna kati ya wanachama wa Darul Taqrib. Kitabu hicho ambacho kilinasabishwa kwa mwanazuoni mmoja wa Kishia, kilichapishwa bila ya kutajwa jina la mahala kilipochapishiwa na tarehe yake na kusambazwa kati ya wanachama wa Darul Taqrib. Hatua hiyo ilizusha hasira kubwa na mtazamo mbaya kuhusu madhehebu ya Shia.

Hapana shaka kwamba wakoloni walihusika kwa njia moja au nyingine katika njama hiyo ya kichochezi. Sheikh Abdulmajid Saliim ambaye alikabiliwa na njama hiyo hakuweza kutoa fatuwa yake katika mazingira hayo yaliyojaa chuki na uhasama dhidi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia. Kwa msingi huo aliamua kusitisha fatua hiyo na kusubiri fursa nyingine. Hata hivyo takdiri ya Mwenyezi Mungu haikumpa fursa hiyo na Sheikh huyo wa zamani wa al Azhar alifariki dunia kabla ya kufikia lengo lake. Miaka kadhaa baadaye, mwanafunzi wake Sheikh Shaltul alipata fursa ya kutoa fatuwa hiyo. Fatua hiyo ya Sheikh Mahmoud Shaltut ina vipengee vitatu vikuu:
1- Waislamu hawalazimiki kufuata moja ya madhehebu nne za Kisuni (Shafi, Maliki, Hanbali na Hanafi), bali kila Muislamu ana uhuru wa kuchagua moja ya madhehebu ya mifumo ya kifiqhi ya Kiislamu.
2- Inajuzu kuhama kutoka madhehebu moja ya kifiqhi na kufuata madhehebu nyingine.
3- Muislamu yeyote hata Wasuni, anaweza kufuata na kutekeleza ibada zake kwa mujibu wa fiqhi ya Shia Imamiyya.

Matini ya Fatuwa Tarehe 17 Mfunguo Sita Rabiul Awwal mwaka 1378 Hijria na katika siku yenye baraka tele za kuzaliwa Mtume Muhammad (saw) na pia mjukuu wake Imam Ja'far Swaqid (sa), Imam wa sita wa madhehebu ya Shia, Sheikh Mahmoud Shaltut alitoa fatuwa yake mashuhuri na ya kihistoria inayowaruhusu wafuasi wa madhehebu za Suni kufuata madhehebu ya Shia katika hadhara iliyodhuhuriwa na wawakilishi wa madhehebu za Shia Imamiyya, Zaidia, Shafi, Hanbali, Maliki na Hanafi. Fatuwa yenyewe ni hii ifuatayo:
"Madhehebu ya J'afariya maarufu kwa jina la madhehebu ya Shia Ithnaashariya, ni madhehebu ambayo kisheria inajuzu kufuatwa kama zilivyo madhehebu za Kisuni. Kwa msingi huo, ni vyema kwa Waislamu kuelewa ukweli huo na kujiepusha na taasubi (chuki za kimadhehebu) zisizofaa dhidi ya madhehebu makhsusi; kwani dini ya Mwenyezi Mungu na sheria yake haifuati madhehebu wala haiwezi kuhodhiwa na madhehebu makhsusi. Watu wa madhehebu mbalimbali ya Kiislamu wanafanya ijtihadi na kazi yao hiyo itatakabaliwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Watu ambao si mujtahidi (wasiokuwa wasomi wenye uwezo wa kunyambua sheria za fiqhi) wanawezi kukalidi madhehebu yoyote waipendayo na kufuata sheria zake za kifiqhi. Katika suala hili hakuna tofauti baina ya sheria za miamala na za kiibada."

Sheikh Mahmoud Shaltut Fatuwa hii ilipewa mazingatia makubwa katika ulimwengu wa Kiislamu. Wanafikra wengi walilitaja tukio hilo kuwa ni mapinduzi makubwa katika uhusiano wa wafuasi wa madhehebu za Shia na Suni na waliipongeza na kuiunga mkono. Hata hivyo walikuwapo watu wengine wenye fikra finyu na wenye sera za kuzusha hitilafu na mifarakano ambao waliikosoa na kumlaumu Sheikh wa Chuo Kikuu cha al Azhar Sheikh Shaltut kwa kutambua rasmi madhehebu ya Shia.

Sababu za Kutolewa Fatuwa Hiyo Moja kati ya sababu muhimu zilizomfanya Sheikh Mahmoud Shaltut atoe fatuwa hiyo ni kusoma na kutalii vitabu vya fiqhi vya maulamaa wa Kishia na kutadabari na kuhakiki dalili na hoja zao. Sheikh Shaltut alikuwa akiamini kwamba, baadhi ya sheria za kifiqhi za madhehebu ya Shia ni bora zaidi kuliko zile za Suni; kwa msingi huo katika baadhi ya sheria hususan zile zinazohusiana na masuala ya familia kama ndoa, talaka, urithi na kadhalika, mwanazuoni huyu alikuwa akitoa fatuwa zinazofanana na za fiqhi ya madhehebu ya Shia. Nakala ya fatuwa ya kihistoria ya mwanazuoni huyo inahifadhiwa katika jumba la makumbusho la haramu ya Imam Ridha (as) katika mji mtakatifu wa Mash'had, Kaskazini mashariki mwa Iran.

Mwanazuoni huyo mashuhuri wa Kiislamu alifanya mambo mengi kwa ajili ya kuwaunganisha Waislamu wa madhehebu za Shia na Suni. Moja ya hatua hizo ni kuanzisha somo la fiqhi linganishi katika Chuo Kikuu cha al Azhar.

Athari na Maandiko ya Sheikh Shaltut Sheikh wa zamani wa Chuo Kikuu cha al Azhar ameandika zaidi ya vitabu 20 na makala za kielimu zilizowasilishwa katika semina na mikutano mbalimbali. Baadhi ya vitabu vyake ni:
1- Tafsiri ya Qur'ani Tukufu. Kitabu hiki ni mkusanyiko wa makala zilizokuwa zikiandikwa na mwanazuoni huyo katika jarida la Risalatul Islam kwa kipindi cha miaka 14. Makala hizo zimekusanywa na kuchapishwa na Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu.
2- Muqaranatul Madhahib fi al Fiqh. Maudhui ya kitabu hiki kama lilivyo jina lake, ni kuhusu juhudi za kukurubisha pamoja madhehebu za kifiqhi za Kiislamu. Katika kitabu hiki Sheikh Shaltut amejadili fiqhi linganishi na mitazamo ya kifiqhi ya madhehebu zote za Kiislamu kuhusu masuala mbalimbali ya kisheria. Mwanazuoni huyo alikuwa akichagua mtazamo wa madhehebu yoyote ambao ulikwenda na wakati na kuambatana na hoja na dalili madhubuti.

3- Min Taujiihatil Islam. Kitabu hiki kilichapishwa mwaka 1959. Katika kitabu hiki, mwandishi anafafanua na kusahihisha baadhi ya masuala ya kidini na kueleza msimamo wa Uislamu kuhusu baadhi ya matatizo ya kijamii.
4- al Fataawa ambacho chapa yake ya 18 ilichapishwa na Darul Shuruq ya Cairo mwaka 1421 Hijria. Kitabu hiki kinakusanya maswali na majibu ya kifiqhi yaliyotolewa na Sheikh Shaltut katika zama za uhai wake. Kitabu hiki ni miongoni mwa athari muhimu sana za Allamah Shaltut katika ulimwengu wa Kiislamu na kinapewa mazingatio maalumu na Ahlusunna katika nchi mbalimbali za Kiislamu.

5- Min Huda al Qur'an, kimechapishwa na Darul Kitabu al Arabi, Cairo. Kitabu hiki kina faslu tano zinazojadili masuala ya Qur'ani na ujenzi wa jamii, Qur'ani na mwanamke, Uislamu na uhusiano wa kimataifa na kadhalika.
6- al Islam Aqidatun Washaria. Hiki pia ni miongoni mwa vitabu muhimu vya Sheikh Mahmoud Shaltut na kimeandikwa katika faslu tatu zinazohusu itikadi, sheria na vyanzo vya sheria.
7- Ilal Qur'anil Karim. Kitabu hiki kinajadili maudhui kuu tatu ambazo ni umuhimu wa itikadi za Kiislamu kwa ajili ya kung'oa mizizi ya ushirikina na kuabudu masanamu, maadili mema na kuitakasa nafsi kwa ajili ya kupeleka juu nafasi ya kiumbe mwanadamu na umuhimu wa kutambua sheria za Kiislamu.
Jua la Cairo Lazama Baada ya kuhudumia dini na umma wa Kiislamu kwa miaka mingi, hatimaye shakhsia mkubwa wa Kiislamu Sheikh Mahmoud Shaltut aliaga dunia tarehe 27 Rajab mwaka 1383 Hijria Qamariya na kuiacha jamii ya Kiislamu katika majonzi makubwa. Maulamaa wakubwa katika nchi mbalimbali za Kiislamu walituma salamu za rambirambi kutokana na kuachwa mkono na shakhsia huyo mkubwa ambaye alifanya jitihada kubwa za kuwakurubisha pamoja Waislamu wa madhehebu za Shia na Suni. Maulamaa wa Iran wakiongozwa na Ayatullahil Udhmaa Borujerdi waliitisha kongamano la kimataifa la kumbumbuka na kumuenzi Sheikh Shaltut katika miji ya Tehran na Qum ambalo lilihudhuriwa na wanazuoni wa Kiislamu kutoka nchi mbalimbali duniani. Ujumbe wa wanazuoni wa Misri katika kongamano hilo lililofanyika tarehe 19 hadi 21 Oktoba 1979, uliongozwa na Kaimu Sheikh wa al Azhar wakati huo Sheikh Mahmoud Abdul Ghani Ashur. Kongamano hilo pia lilihudhuriwa na Mufti Mkuu wa Misri Dakta Nasr Farid Muhammad Wasil. Mwenyezi Mungu aiweke roho ya Sheikh Mahmoud Shaltut mahala pema peponi.

MWISHO