BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM
HIJA MBELE YA IMAMA KHOMEINY
Ibada ya hija, ni moja ya masuala ya kiibada na kisiasa ambayo yamefaradhihwa katika dini tukufu ya Kiislamu. Ibada hii muhimu hutekelezwa kila mwaka katika ardhi tukufu ya wahyi, na mamilioni ya watu walio na hamu kubwa, kutoka kila pembe ya dunia, watu ambao kwa hakika huwa ni wa mataifa, jamii, rangi na lugha mbalimbali.
UMUHIMU WA HIJA NA ATHARI ZAKE
Ibada ya hija, ni moja ya masuala ya kiibada na kisiasa ambayo yamefaradhihwa katika dini tukufu ya Kiislamu. Ibada hii muhimu hutekelezwa kila mwaka katika ardhi tukufu ya wahyi, na mamilioni ya watu walio na hamu kubwa, kutoka kila pembe ya dunia, watu ambao kwa hakika huwa ni wa mataifa, jamii, rangi na lugha mbalimbali. Kuna ibada chache kati ya faridha nyingi za Kiislamu iliyopewa uzito na kusisitiziwa Waislamu kama ilivyo hija. Sisitizo la kitabu kitakatifu cha Qur'ani pamoja na nasaha zilizotolewa na viongozi watukufu wa kidini ni nyingi mno na zisizoweza kubainishwa kwa maneno. Abdallah bin Sinaan, anamnukuu Imam Swadiq (as) kwa kusema:
لَو عطّل الناسُ الحجَّ لَوَجَبَ عَلَى الإمام أنْ ?جبرَهم على الحجّ، إنْ شاؤوا و إنْ أبوا؛ فإنّ هذا الب?ت إنّما وضع للحجّ
(Furuu' Kafi j.4 uk 272-Bab Ijbar alal Haj- riwaya ya pili). "Kama watu wataacha kutekeleza hija, kiongozi wa Waislamu (imam) anawajibika kuwalazimisha watekeleza ibada hiyo, wapende wasipende. Hii ni kwa sababu Nyumba hii (al-Kaaba) ilijengwa kwa ajili ya kutekelezwa hija." Umuhimu wa hija ni mkubwa mno kiasi kwamba Imam Swadiq (as) amesema katika sehemu nyingine:
"فإنْ لمْ ?كنْ لَهُم أمْوال، أنفقَ عل?هم مِنْ بَ?ت مال المسلم?ن"
(Furuu' Kafi- Riwaya ya kwanza) "Kama watu hawatakuwa na uwezo wa kugharamia hija, gharama ya safari yao ya hija itatolewa kwenye Beitul Mal (mali ya Waislamu). Mtukufu huyo bado ananukuliwa kupitia sanadi ya kuaminika akisema:
"مَنْ مات وَ لَمْ ?َحج حَجّةَ الإسلام، لم ?منعه من ذلك حاجّة تحجف به أمْ مرض لا ?ط?ق ف?ه الحجّ، أو سُلْطان ?منعه، فل?مت ?هود?اً أوْ نصران?اً"
(Furuu' Kafi- j. 4 uk. 268). "Mtu anayekufa bila kuhiji hija ya Kiislamu, hali ya kuwa hajazuiwa kufanya hivyo kutokana na haja muhimu, maradhi au mtawala (dhalimu), basi na afe kifo cha Yahudi au Mkristo." Kwa kutekeleza ibada ya hija, jamii ya Kiislamu hupata manufaa makubwa ya kijamii, kiutamaduni na kiuchumi pamoja na kufaidika na siri na vilevile thamani nyingi zilizofichika humo. Umoja, mshikamano na udugu wa Kiislamu ni moja ya faida za ibada hiyo muhimu. Imam Khomeini (MA) ambaye ni muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu Iran anasema kuhusiana na suala hilo kama ifuatavyo:
"Hija ni sehemu bora zaidi ya kukutana mataifa ya Kiislamu, ambapo ndugu wa Kiislamu kutoka pembe mbalimbali za dunia huweza kukutana na kujuania hali zaidi. Hii ni nyumba ambayo ni ya jamii zote za Kiislamu na wafuasi wa Nabii Ibrahim (as) aliyewacha dini za upotofu na akashika dini ya haki. Kwa kuweka kando utambulisho wao wa kitaifa, rangi, kabila na kijamii, hurejea katika nyumba yao ya mwanzoni.
Huzingatia maadili ya Kiislamu na kujiweka mbali na mijadala isiyo na maana pamoja na mapambo na hivyo kuwadhihirishia walimwengu udugu wa Kiislamu na dhihirisho halisi la umma wa Kiislamu na wa Mtume Muhammad (saw) (Swahifat Nur j.20 uk.13)."
Historia ya Kiislamu daima imekuwa ikiandamana na juhudi kubwa za kuleta umoja na mshikamano, zilizofanywa na shakhsia pamoja na viongozi mashuhuri wa kielimu na kidini. Sehemu ya juhudi hizo zinazong'ara katika historia ya Kiislamu inadhihiri wazi katika maisha ya Imam Khomeini (MA), shakhsia muhimu katika zama hizi aliyenadi kuwepo umoja na mshikamano miongoni mwa Waislamu. Kuhusiana na suala hilo yeye mwenyewe anasema: "Ni kwa muda wa miaka mingi sasa tokea tuanze kufanya juhudi za kuwaunganisha Waislamu na kuwafanya washirikiane na kuwa kitu kimoja. Hii ni kutokana na ukweli kwamba matatizo yote yanayowakumba Waislamu yanatokana na madola makubwa ya kigeni, madola ambayo yanataka kunufaika na nchi za Kiislamu, kupora utajiri wa Waislamu, kuzidhibiti serikali za Kiislamu na kuzusha migawanyiko miongoni Waislamu (Swahifatu Nur j.13 uk. 164)."
Kufuatia ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran Imam Khomeini (MA) alipata fursa nzuri ya kutumia suhula zilizokuwepo kwa ajili ya kufikia lengo lake kuu la kuwaunganisha Waislamu katika pembe mbalimbali za dunia. Kupitia jumbe zake muhimu za hija alizokuwa akizitoa kwa mahujaji kila mwaka, Imam Khomeini alitumia suhula hizo pamoja na wafuasi wake waaminifu ili kueneza na kufikisha ujumbe wake wa umoja na mshikamano kwa mahujaji, na hivyo kutimiza ndoto yake ya muda mrefu kuhusu jambo hilo.
LENGO LA UMOJA
Wakati suala la umoja linapojadiliwa kati ya madhehebu mbalimbali za Kiislamu, jambo linalopaswa kuwekwa wazi na kuainishwa mwanzo ni iwapo umoja unaokusudiwa ni wa hakika au ni wa kidhahiri tu. Kama umoja unaokusudiwa ni wa kweli na hakika basi, je, ni mbinu na suhula zipi zinazopaswa kutumiwa kama msingi wa kufikiwa lengo hilo? Bila shaka umoja unaokusudiwa hapa ni ima uratibu na muungano wa kweli uliosimama juu ya msingi wa itikadi na tamaduni au malengo na mipango ya pamoja au ni jambo ambalo ni pana zaidi kuliko masuala mawili hayo.
Kabla ya kuendelea na mtazamo wa Imam Khomeini kuhusiana na umoja, tunaashiria hapa baadhi ya aya za Qur'ani na hadithi za Kiislamu ili kulifahamu zaidi suala hili. Qur'ani Tukufu inamtaka Mtume Muhammad (saw) kuwaita Mayahudi na Wakristo katika umoja kwa kumwambia: "Enyi watu mliopewa Kitabu cha Mwenyezi Mungu (Mayahudi na Manasara)! Njooni katika neno lililo sawa baina yetu na baina yenu; ya kwamba tusimwabudu yoyote ila Mwenyezi Mungu, wala tusimshirikishe (Mwenyezi Mungu) na chochote; wala baadhi yetu tusiwafanye baadhi yetu wengine kuwa waungu badala ya Mwenyezi Mungu (au pamoja na Mwenyezi Mungu).
" Katika aya hii tukufu, malengo kama vile ya kuepuka udhibiti wa wanadamu wenzetu, kukubali pamoja na kutii moja kwa moja maamrisho ya Mwenyezi Mungu pamoja na kuwa waja Wake, ni jambo ambalo limechukuliwa kuwa muhimili muhimu wa umoja na mshikamano kati ya dini zote za Mwenyezi Mungu. Katika upande wa pili, kuna riwaya na hadithi nyingi zinazosema kuwa lengo la umoja na udugu ni umoja katika malengo na kuwasaidia wanadamu wenzetu katika maisha yao ya kila siku. Imam Swadiq (as) anamnukuu Mtume Mtukufu (saw) akisema: "Waumini ni ndugu wao kwa wao; baadhi yao hukidhi mahitaji ya wenzao (Aamal Mufid uk.150)."
Imam Swadiq vilevile anasema hivi katika hadithi nyingine: "Mtu anayefanya juhudi za kukidhi haja ya ndugu yake muumini, ni sawa na mtu anayefanya sa'i kati ya milima ya Safa na Mar'wa, na mtu anayekidhi haya ya ndugu yake, ni sawa na shahidi aliyeuawa katika vita vya Badr na Uhud kwa njia ya Mwenyezi Mungu (al-Hayaat j.1 uk.233)."
Tunafahamu wazi kutokana na aya na hadithi hizi na nyinginezo nyingi kwamba, makusudio ya umoja katika Uislamu na tafsiri halisi ya neno hilo ni umoja uliosimama juu ya msingi wa tauhidi, utume, thamani za kiutu na malengo ya pamoja. Msingi huu ni ule unaozingatia mahitaji halisi ya kimaumbile ya mwanadamu na masuala yenye udharura katika umma wa Kiislamu bila kuzingatia rangi, kabila, taifa wala madhehebu.
Bila shaka ni wazi kwamba, makusudio ya umoja hapa katika misingi ya itikadi za Kiislamu sio umoja mutlaki unaowataka wafuasi wa madhehebu mbalimbali ya Kiislamu kuachana na mafundisho pamoja na itikadi za madhehebu yao na kufuata fikra moja tu. Kuhusiana na suala hili Imam Khomeini (MA) anasema: "Ndugu zetu wa Kisunni wasidhani kwamba kwenye Uislamu kuna tofauti kati yetu na nyinyi.
Ni sawa kabisa na kama mlivyo na madhehebu manne kwenye usunni na kuwepo tofauti kati ya madhehebu hizo. Licha ya kuwepo tofauti kati ya madhehebu hizo, lakini nyote ni ndugu wala sio maadui. Hii (Ushia) ni madhehebu ya tano pia wala hakuna uadui hapa. Nyote ni ndugu, Waislamu, wafuasi wa Qur'ani na wanaomfuata Mtume mmoja (Swahifatu Nur j.5 uk.246)."
"Masuala haya hayapasi kuzungumzwa katika jamii ambayo watu wake wote wanafanya juhudi za kuuhudumia Uislamu. Sisi sote ni Waislamu na tuko pamoja. La muhimu ni kwamba maulamaa na wanazuoni wenu wametoa fatuwa kuhusiana na jambo moja na nyinyi mkawafuata katika fatuwa hizo na mkawa Mashafi. Kundi moja lilifuata fatuwa za Shafi na kundi jingine likamfuata Imam Jaafar Swadiq (as) na kuwa Washia. Hii haipasi kuwa dalili na chanzo cha hitilafu (Swahifatu Nur j.12 uk.209)." Anasema katika sehemu nyingine:
"Sisi, kwa mujibu wa maamrisho ya Mwenyezi Mungu, Tabaraka wa Taala, tunatangaza udugu wetu kwa Waislamu wote wa ulimwengu, serikali za nchi za Kiislamu na mataifa ya Kiislamu bila kujali madhehebu na nchi zao. Tunawataka Waislamu wote washirikiane na kuwa kitu kimoja. Kila mtu aishi kwa uhuru kamili bila kujali serikali anayoiunga mkono wala madhehebu anayofuata (Sahifatu Nur j.9 uk.202)."
Kwa hakika jambo alilosisitiza Imam Khomeini (MA) katika kipindi chote cha maisha yake ya kisiasa na kimapambano na kuutaka umma wa Kiislamu na hasa mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu kulizingatia, ni umoja na mshikamano kati ya madhehebu yote ya Kiislamu katika misingi thabiti, malengo na maslahi ya pamoja ambayo tutayaashiria katika kurasa zijazo.
MAMBO YALETAYO UMOJA
Katika hotuba na matamshi yake yote aliyotoa katika minasaba mbalimbali na hasa kuhusiana na kutumiwa vyema mkutano mkuu wa hija, Imam Khomeini kabla ya jambo jingine lolote alisisitiza juu ya misingi mitatu muhimu, ili kuimarisha umoja na mshikamano miongoni mwa Waislamu ulimwenguni:
1- UISLAMU
Huku akiashira aya isemayo: "Na shikamaneni kwa kamba (dini) ya Mwenyezi Mungu nyote, wala msiachane…. (3:103)" na kwamba Uislamu ndio ulioweka msingi wa udugu na umoja kati ya Waislamu, Imam Khomeini (as) anasema: "Uislamu umeweka mkataba wa udugu kati ya Waislamu wote na kuwataka wote washikamane na kamba ya Mwenyezi Mungu na kufuata mafundisho ya Kiislamu (Sahifatu Nur j.14 uk.142)." Anaendelea kusema: " Kamba ya Mwenyezi Mungu ni Uislamu, ni njia nyoofu. Kamba iliyoko kati ya Mwenyezi Mungu na viumbe ni Uislamu (Sahifatu Nur j.8 uk.172)."
Kwa kunufaika na mafundisho, sheria za Kiislamu pamoja na ujumbe wa umoja unaopatikana kutokana na hija, Imam Khomeini (MA) anasema kuwa al-Kaaba ni nyumba ya wanadamu na Waislamu wote na wala haihusiani na mtu, kundi wala kabila fulani. Anasema kuwa hakuna kundi lolote linalopasa kudai kwamba lina uwezo na fursa kubwa zaidi ya kudhibiti na kunufaika na Nyumba hiyo ya Mwenyezi Mungu kuliko kundi jingine. Anasema kuwa watu wote ulimwenguni wanalazimika kuwa Waislamu kwanza na kisha kuizuru na kufanya ibada katika nyumba hiyo iliyojengwa kwa ajili ya wanadamu.
Shakhsia na viongozi mbalimbali wa Kiislamu tokea mwanzoni mwa Uislamu wamekuwa wakifanya juhudi kubwa za kuwaunganisha Waislamu na kuwafanya kuwa kitu kimoja katika kukabiliana na maadui wao. Waislamu katika pembe zote za dunia wanapasa kushirikiana na kuelewana, na hilo ni jambo ambalo limesisitizwa na Mwenyezi Mungu katika kitabu kitakatifu cha Qur'an. Mtume Mtukufu (saw), Maimamu watoharifu (as) pamoja na viongozi wengine wa kidini wamekuwa wakifanya juhudi kubwa katika kipindi chote cha historia kwa madhumuni ya kuleta umoja na mshikamano miongoni mwa Waislamu (Sahifatu Nur j.13 uk.163).
2- MANUFAA NA MALENGO YA PAMOJA
Jambo la pili linaloleta umoja na mshikamano miongoni mwa Waislamu ulimwenguni ni malengo yao ya pamoja. Kufikia maelewano juu ya malengo ya pamoja si jambo lisilokuwa la kimantiki. Hili ni jambo ambalo limekuwa likifuatiliwa na kutekelezwa na nchi nyingi zilizoendelea duniani. Mfano bora kuhusiana na jambo hilo ni Umoja wa Ulaya ambao baada ya kubuni bunge na soko la pamoja, nchi wanachama wa umoja huo hivi sasa zinafanya juhudi kubwa za kushirikiana na kuleta umoja wa kisiasa na kiuchumi kati yao. Nchi hizo zimefanya juhudi kubwa za kupunguza na kuondoa udhaifu na tofauti zilizopo kati yao na kufikia hatua muhimu ya kuwa na sarafu moja na hata kuondoa mipaka baina yao kwa lengo la kudhamini manufaa na maslahi yao ya pamoja.
Hii leo kwa kuzingatia kuimarika mawasiliano na maendeleo ya kielimu na kiviwanda pamoja na kurahisishwa ubadilishanaji wa masuala ya kiutamaduni kati ya mataifa mbalimbali, uwanja unaofaa umeandaliwa kwa shabaha ya kuimarishwa ushirikiano na mshikamano kati ya Waislamu. Wakati umefika wa kuchukuliwa maamuzi ya pamoja kwa lengo la kudhamini maslahi ya pamoja ya Waislamu. Bila shaka mkutano mkuu wa hija ni fursa bora zaidi ya kuweza kufikiwa lengo hilo. Hii ni fursa nzuri na ya kipekee kwa ajili ya kujadiliwa masuala mbalimbali ya Waislamu na kufikiwa maamuzi ya kuimarisha nukta za pamoja na kuepuka zile zinazoleta mifarakano, fitina na hitilafu miongoni mwa jamii za Kiislamu.
Imam Khomeini anaashiria suala hilo katika mazungumzo yake na mkuu wa ujumbe wa mahujaji wa Iran kwa kusema: "Kwa kuzingatia kuwa faradhi ya hija ni moja ya faradhi muhimu zaidi za kiibada na kisiasa za Kiislamu, na kwa kutilia maanani kwamba mkusanyiko mkuu wa hija ni moja ya mikusanyiko mikubwa zaidi ya dunia, mahujaji waheshimiwa kutoka kila pembe ya dunia wanapasa kukusanyika na kubadilishana mawazo kuhusu maslahi na matatizo yanayowakabili Waislamu na kufanya juhudi za kuyatatua na vilevile kuchukua uamuzi muhimu ya kufikia malengo matukufu ya Kiislamu.
Wanapasa kujadili njia za kuimarisha na kuleta umoja miongoni mwa wafuiasia wa madhehebu mbalimbali ya Kiislamu. Wanapasa kuchukua uamuzi wa pamoja wa kisiasa na kutatua matatizo mengi ambayo Waislamu wa dunia wamezushiwa na maadui sugu wa Uislamu, muhimu zaidi kati ya matatizo hayo likiwa ni la kuleta hitilafu na mifarakano katika safu zao (Sahifatu Nur j.19 uk.191)."
Imam Khomeini anasema katika sehemu nyingine kuhusiana na suala hilo kama ifuatavyo: "Iwapo inshallah, umoja - aliosisitiza na kuukusudia Mwenyezi Mungu na Mtume Wake Mtukufu- utapatikana, serikali za Kiislamu kwa kutegemea uungaji mkono wa wananchi, zinaweza kuunda jeshi la pamoja la ulinzi, jambo linaloweza kuzifanya kuwa nguvu kubwa zaidi duniani. Ni matumaini (ya Waislamu) kwamba serikali za eneo zitapuuza lugha, utaifa na madhehebu na kufikiria tu jinsi ya kutekeleza mpango wa kuwa sote chini ya bendera ya Uislamu (Sahifatu Nur j.18 uk.92)."
Kwa ujumla, katika sehemu kama hii ambayo kwa hakika imejengwa kwa lengo la kuwakutanisha waja wanaompwekesha Mwenyezi Mungu, mipango madhubuti ya kustawishwa umoja kwa msingi wa maslahi na malengo ya pamoja ya mataifa ya Kiislamu inaweza kutekelezwa kirahisi. Hili ni jambo linalowezekana kabisa na ndio maana Imam Khomeini (MA) akalisisitiza katika jumbe zake nyingi kwa mahujaji kwa kusema:
"Ni wajibu kwenu enyi Waislamu ambao mmekusanyika katika ardhi hii ya wahyi kwa lengo la kutekeleza ibada ya hija, kutumia fursa hii na kutafuta ufumbuzi. Fikirieni na kubadilishana mawazo kuhusiana na jinsi ya kutatua matatizo ya Waislamu. Mnapasa kuzingatia kuwa mkusanyiko huu mkubwa ambao hufanyika kila mwaka katika ardhi hii takatifu kutokana na amri ya Mwenyezi Mungu, unakuwajibisheni nyinyi mataifa ya Kiislamu kufanya juhudi kubwa kwa ajili ya kufikia malengo matukufu ya Kiislamu.
Jitihada hizo pia zinapasa kufanyika kwa madhumuni ya kufikia malengo makuu ya sheria takatifu, kunyanyua nafasi ya Waislamu na kuiunganisha jamii ya Kiislamu duniani. Kuweni na umoja na kushirikiana katika kupigania kujitawala na kupambana na kensa ya ukoloni. Sikilizeni kwa makini matatizo ya mataifa ya Kiislamu kutoka kwa wenyeji wa mataifa hayo na kisha mfanye jitihada za kuyatatua bila kuzembea wala kusita. Wazingatieni watu masikini na wanaohitaji msaada katika nchi za Kiislamu (Sahifatu Nur j.1 uk.156)."
3- ADUI WA UMOJA
Hii leo nchi za Kiislamu zinakabiliwa na wimbi kubwa zaidi la hujuma kali na isiyo na huruma kutoka kwa madola ya kibeberu yanayopora utajiri wa mataifa ya dunia. Madola hayo ya kichokozi yamekodolea macho utajiri mkubwa wa nchi za Kiislamu, wala hazisiti kutekeleza kila aina ya jinai na njama kwa ajili ya kupora hazina na akiba kubwa ya maliasili za nchi hizo. Madola hayo hutumia hila, ujanja na mbinu mbalimbali kwa madhumuni ya kudumisha uporaji huo. Huo ni msiba mkubwa ambao Qur'ani Tukufu inawaamrisha Waislamu kukabiliana nao kwa kusema:
وَ اَعِدُّوا لَهُمْ مَا اسْتَطَعْتُمْ مِنْ قُوَّة
Basi waandalieni (wawekeeni tayari) nguvu mziwezazo (silaha)… (8:60). Waislamu wana wajibu wa kutafuta njia za kukabiliana na kuepuka shari ya maadui hao wachokozi kwa kuchukua uamuzi wa pamoja. Mkutano mkubwa wa hija ndiyo fursa nzuri zaidi waliyopewa Waislamu kwa madhumuni ya kufuata mfano wa Mtume Mtukufu (saw) katika kupambana na kufr pamoja na dhulma ya madhalimu. Wanapasa kushauriana na kutafuta njia na mbinu zifaazo kwa ajili ya kupambana na maadui wao wa pamoja.
Hii ndiyo nukta muhimu aliyokuwa akiisisitiza kila mara Imam Khomeini katika ujumbe wake wa kila mwaka kwa mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu. Alikuwa akisema:
"Ninawaambia kwa unyenyekevu mahujaji na watu wanaozuru Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu, kutoka kila nchi, kaumu na wafuasi wa kila madhehebu kwamba, nyinyi nyote ni taifa moja la Kiislamu na linalomfuata Mtume Mtukufu pamoja na mafundisho ya Qur'ani Tukufu. Mna maadui wasaliti wa pamoja ambao kwa kuzusha hitilafu kupitia vibaraka wao wasiojua lolote, vyombo vya habari na propaganda za mirakano, katika kipindi chote cha historia katika kipindi cha mamia ya miaka iliyopita na hasa katika zama zetu hizi, wamezidhibiti vilivyo serikali na mataifa ya Kiislamu.
Wamepora na wangali wanapora utajiri mkubwa wa nchi zenu na jasho la wadhulumiwa katika nchi hizo. Wanataka kuzifanya serikali mbalimbali za dunia zihudumie maslahi yao kibubusa bila ya hoja yoyote wala kuuliza.
Wanataka kuyatumia kimaslahi mataifa na kuzuia ustawi wa vipawa na viwanda katika nchi masikini kupitia mbinu na njama za kishetani na hivyo kuzifanya nchi hizo ziwe tegemezi zaidi kwa nchi za Magharibi na Mashariki. Maadui hao wameazimia kumnyima kila mtu fikra ya kujitawala na uvumbuzi, na kuzikandamiza vifuani pumzi za kuyaamsha mataifa
Hali ya msiba na masikitiko makubwa mnayoishuhudia hii leo katika nchi za Kiislamu na nchi nyinginezo zinazodhulumiwa, inatokana na njama hizo za maadui wa pamoja wa Waislamu na wadhulumiwa. Kwa maelezo hayo, na kwa kutilia maanani kwamba mmekusanyika katika kituo hiki muhimu cha Uislamu wenye uhai kutoka mataifa na madhehebu mbalimbali, kwa ajili ya kutekeleza maamrisho ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake, fikirieni namna ya kutibu maradhi haya hatari na saratani inayoua.
Mnapasa kujua kwamba ufumbuzi halisi wa tatizo hili unapatikana katika kivuli cha umoja wa Waislamu wote na ushirikiano wao katika kuukata mkono wa madola makubwa katika nchi za Kiislamu (Sahifatu Nur j.19 uk.202)." "Sharti la kufikiwa matarajio ya kimaumbile na malengo ya mwanadamu katika amali na maeneo yote ya hija ni kukusanyika Waislamu wote katika maeneo hayo na kuwa na umoja bila kujali lugha, rangi, kabila, kaumu, nchi wala taasubi za kijahili, pamoja na kuratibu njia za kukabiliana na adui wa pamoja (Sahiftu Nur j.20 uk.19)."
Mwanafikra na mwanafalsafa Shahid Ayatullah Murtadha Muttahari, Mwenyezi Mungu Amrehemu, amezungumzia kwa urefu na kina msingi wa umoja kati ya madhehebu ya Kiislamu, ambapo tunazungumzia hapa kwa ufupi sehemu ya maneneo yake kuhusu suala hilo:
"Waislamu wana mambo mengi ya pamoja ambayo yanaweza kuwa msingi mzuri wa umoja wao. Waislamu wanamwabudu Mwenyezi Mungu mmoja na kuamini utume wa Mtume Muhammad (saw), Kitabu chao wote ni Qur'ani na wana kibla kimoja ambayo ni al-Kaaba. Wao huhiji pamoja na kuwa na masuala yanayofanana katika kuswali, kufunga, kuoa na kuwa na familia, kufanya biashara, kulea watoto na kuzika wafu wao. Wanatofautiana katika sehemu chache mno kuhusiana na mambo hayo.
Waislamu wote wana imani moja kuhusiana na masuala mengi ya ulimwengu na pia kuwa na utamaduni wa pamoja. Wote wanashirikiana katika ustaarabu mkubwa na mkongwe. Umoja kuhusiana na ulimwengu, utamaduni, ustaarabu mkongwe, katika mitazamo na mienendo, imani ya kimadhehebu, ibada na dua, mila na mienendo mizuri ya kijamii ni mambo yanayoweze kutegemewa katika kubuni taifa moja lenye nguvu kubwa ambalo linaweza kuyafanya madola makubwa ya dunia kuliogopa. Na hasa ikitiliwa manani kwamba, suala hilo limesisitizwa sana katika Uislamu. Kwa mujibu wa Qur'ani, Waislamu ni ndugu ambao wanaunganishwa na sheria pamoja na majukumu maalumu (Shish Maqaleh uk.504).
VIKWAZO VYA UMOJA
Kuna mambo na vikwazo vingi vinavyozuia kupatikana umoja miongoni mwa madhehebu na makundi mbalimbali ya Kiislamu, ambapo tunaashiria hapa baadhi ya vikwazo hivyo:
1-UKABILA
Uzingatiaji ukabila, utaifa, mipaka ya rangi, kieneo na taasubi za kujiona kuwa bora kuliko watu wengine ni mambo yanayosababisha vikwazo vingi katika njia ya kuwepo umoja na mshikamano miongoni mwa Waislamu. Kujifakharisha na mambo yasiyo na msingi wala mantiki na yasiyodumu kama inavyoonekana katika baadhi ya jamii, familia, kaumu, nchi na mataifa ni baadhi ya mambo yanayomfanya mwanadamu awe mbali na mafundisho ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu na jambo hilo bila shaka ni tatizo na kikwazo muhimu kinachozuia kupatikana umoja katika jamii ya Kiislamu.
Imam Zeinul Abedeen (as) anasema hivi kuhusiana na suala hilo: "Taasubi inayomfanya mtu kuwa mtenda dhambi ni ile inayomfanya kuwachukulia watenda maovu katika kabila lake kuonekana kuwa bora na wenye thamani kubwa zaidi kuliko watu wema katika kabila jingine. Ni wazi kuwa kuwapenda watu wa karibu katika familia si miongoni mwa taasubi batili, bali kuwasaidia katika kuwadhulumu watu wengine ndiyo taasubi batili (Usul Kafi j.12 uk.308)."
Taasubi kama hiyo huandaa uwanja wa mtengano na kuvuka mipaka ya imani na waumini. Imam Swadiq (as) aamnukuu Mtume Mtukufu (saw) akisema: "Mtu anayefanya taasubi mwenyewe moja kwa moja au kufanyiwa taasubi hiyo na watu wengine, kwa hakika huwa amejivua mkufu wa imani kutoka shingoni (marejeo hayohayo).
Taasubi ina mchango mkubwa usioweza kukanushika katika kuwatenganisha Waislamu. Ni kutokana na ukweli huo ndipo Imam Khomeini (MA) akawataka Waislamu wote na hasa mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu kuzingatia malengo na maslahi makuu ya Uislamu na kujiepusha na moto wa mifarakano, fitina na taasubi zisizo na msingi za ujahili. Anasema:
"Mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu wanawajibika kupaza sauti ya kishindo dhidi ya madhalimu na kutoa mkono wa udugu na urafiki kwa Waislamu wenzao. Wanapasa kujiepusha kusaliti maslahi makuu ya Kiislamu na Waislamu wanaodhulumiwa kwa ajili ya kunufaika na maslahi ya kikabila na kitaifa.
Wanawajibika kuwafanya ndugu zao wa Kiislamu kuzingatia zaidi umoja na kuachana na taasubi za kijahili ambazo haziwanufaishi ila mabeberu na vibaraka wao. Hiyo yenyewe ndiyo nusura ya Mwenyezi Mungu (Sahifatul Nur j.20 uk.21)." "Miongoni mwa njama zilizopangwa na maadui wa Uislamu kwa ajili ya kuzusha hitilafu miongoni mwa Waislamu, na kuenezwa na vibaraka wa maadui hao wa kikoloni, ni ukabila na utaifa ambao umezusha chuki na uadui mkubwa miongoni mwao. Hakuna tatizo lolote katika kupenda nchi na taifa, lakini utaifa ambao huleta uadui miongoni mwa Waislamu na kuzusha pengo katika safu zao ni jambo linalokwenda kinyume na Uislamu pamoja na maslahi ya Waislamu (ujumbe kwa mahujaji 24/8/1980)."
"Zingatieni! Enyi Waislamu wenye nguvu! Amkeni, mjitambue na kujitambulisha kwa ulimwengu. Kwa amri ya Mwenyezi Mungu na Qur'ani Tukufu, achaneni na hitilafu za kikabila na kieneo ambazo zimechochewa na madola makubwa na dhalimu duniani pamoja na vibaraka wao waovu kwa lengo la kukuporeni na kuukanyaga utukufu wenu wa kiutu na Kiislamu (Sahifatu Nur j.19 uk.199)."
UPOTOFU NA TAFSIRI MBAYA YA UISLAMU
Moja ya vikwazo vikuu vya kupatikana umoja na mshikamano miongoni mwa Waislamu ni kueleweka vibaya, uchambuzi na tafsiri mbaya na mara nyingine zinazogongana kuhusu Uislamu, tafsiri ambazo hutolewa na watu wasiofaa na wasiofahamu lolote kuhusu mafundisho ya Uislamu. Ni masikitiko makubwa kwamba jambo hilo limepelekea Waislamu kutengana, kuchukiana na hivyo kuwa mbali na mafundisho halisi ya Uislamu. Mwanafikra mashuhuri wa Kiislamu, Shahid Murtadha Muttahari, Mwenyezi Mungu Amrehemu, anasema chini ya anwani, 'Kudhoofika Waislamu katika Zama Hizi', kama ifuatavyo:
"Miongoni mwa nchi za dunia, isipokuwa chache, nchi za Kiislamu ndizo nchi dhaifu (masikini) zaidi. Si katika masuala ya viwanda tu, bali nchi hizi ndizo nchi zilizobaki nyuma zaidi katika masuala yanayohusiana na elimu, akhlaqi, utu na umaanawi. Je, ni kwa nini?.... Ni lazima tukiri kwamba ukakika wa Uislamu kimsingi haupatikani katika fikra wala nyoyo zetu, bali aghalabu fikra hiyo ipo lakini kwa sura ya kufutika.
Fikra yetu ya kidini inapasa kurekebishwa…Fikra yetu kuhusu dini ina makosa. Kabla ya kuwafikiria wenzetu na kutaka kuwafanya wawe Waislamu, tunapasa kujifikiria sisi wenyewe kwanza. Kabla ya jambo lolote lile sisi wenyewe tunahitajia muamko na uhuishaji wa kidini na Kiislamu. Tunahitaji kuhuisha fikra ya kidini na kuwa na harakati ya muamko wa Kiislamu (Dah Goftar uk.144-151)."
Imam Khomeini (MA) anasema kuhusiana na upotovu wa fikra na propaganda mbovu zinazoenezwa ulimwenguni dhidi ya Uislamu na umoja wa Waislamu kwamba, maadui wanatumia mbinu na njama mbalimbali kwa ajili ya kuwahadaa Waislamu na kueneza chuki na uhasama miongoni mwa Waislamu.
Anasema kuwa fikra ya kuwa Wasuni na Washia ni makundi mawili tofauti ya Kiislamu ni fikra potofu na propaganda ambazo zimeenezwa na maadui wa kigeni katika nchi za Kiislamu. Aneendelea kusema kuwa, inasikitisha kuona kwamba malumbano na mivutano hiyo isiyofaa miongoni mwa ndugu wamoja wa Kiislamu inaoonekana wazi kati ya wafuasi wa madhehebu moja ya Shia na vilevile Sunni (Sahifatu Nur j.11 uk.45).
Imam anaendelea kusema: "Kwa masikitiko, falsafa na malengo mengi ya ibada hii muhimu na nyeti (hija) hadi sasa hayafahamiki vyema kutokana na upotovu unaoenezwa na tawala dhalimu katika ulimwengu wa Kiislamu, mashekhe wanaowahudumia wafalme, ufahamu mbaya wa baadhi ya waongozwa pamoja na kutukuzwa kwa baadhi ya watu katika nchi za Kiislamu.
Ufahamu mbaya ambao anawapelekea baadhi ya watu hata kupinga udharura wa kuasisiwa serikali ya Kiislamu, kwa hoja kuwa serikali kama hiyo ni mbaya hata kuliko serikali ya kitaghuti!
Fikra hiyo potovu imepelekea kupoteza maana ibada muhimu ya hija na kufanya udharura wa kubainishwa matatizo yanayowakabili Waislamu na nchi za Kiislamu, kuchukuliwa kuwa kinyume na shria za Mwneyezi Mungu na jambo linalokaribia ukafiri! Vibaraka wa serikali dhalimu, kandamizaji na potovu huyachukulia makelele ya Waislamu wanaodhulumiwa ulimwenguni, wanaokusanyika katika kituo hiki muhimu, kuwa kitendo cha kikafiri na kinachokwenda kinyume na mafundisho ya Kiislamu.
Ili kuwafanya Waslamu waendelee kubaki nyumba na kuwafungulia njia waporaji na mabeberu, waovu hao wameubana Uislamu katika kona za misikiti na maeneo mengine ya ibada na kudai kwamba kushughulikia masuala ya Waislamu ni kinyume na Uislamu, majukumu ya Waislamu na wanasomi wa Kiislamu.
Kwa bahati mbaya, propaganda hizo potovu zimekuwa na zingali zina athari kubwa kiasi kwamba zimewafanya Waislamu wengi kudai kwamba kuingilia kati kila jambo la kijamii na kisiasa katika jamii ya Kiislamu, ni kinyume na majukumu ya wanazuoni na maulamaa wa kidini.
Propaganda hizo zimewapotosha wengi wanaodai kwamba kujishughulisha na masuala ya kisiasa ni dhambi isiyosamehewa. Watu hao wameibadili ibada muhimu ya swala ya Ijumaa kuwa ibada kavu isyokuwa na maana na kudai kwamba kuvuka mipaka hiyo ni kwenda kinyume na Uislamu. Kwa maelezo haya, tunapasa kusema kuwa Uislamu ungali ni mgeni na haujafahamika na wengi. Mataifa ya Kiislamu yamejitenga na kutoufahamu vyema ukweli wa Uislamu (Sahifatu Nur j.19 uk.41)."
3- NJAMA ZA MADOLA YENYE NGUVU
Kama tulivyosema mwanzoni, waporaji wa dunia dama wamekuwa wakifanya njama za kueneza ubeberu wao ulimwenguni na hasa katika nchi zilizo na utajiri mkubwa wa maliasili. Njama hizo hutekelezwa kwa madhumuni ya kupora na kunyonya utajiri wa nchi masikini na nyonge zisizoweza kutetea utajiri wao.
Kutokana na ukweli kuwa madola makubwa huchukulia umoja wa kitaifa kuwa tishio kubwa kwa juhudi zao za uporaji utajiri wa mataifa mengine, madola hayo hufanya jitihada kubwa za kuzusha hitilafu na migawanyiko kati ya wananchi wa mataifa yanayolengwa. Kuchochea hitilafu na tofauti kati ya madhehebu ya Kiislamu ni miongoni mwa njama hizo zinazotumiwa na maadui.
Ima Khomeini anasema hivi kuhusiana na suala hilo:
"Kuzusha hitilafu kati ya madhebeu ya Kiislamu, ni miongoni mwa jinai ambazo zinatekelezwa na watu wenye nguvu ambao hunufaika na hitilafu za Waislamu. Wanaonufaika pia ni vibaraka wao wasiomjua Mwenyezi Mungu wakiwemo mashekhe wa kisultani ambao ni waovu zaidi kuliko hata masultani wa dhulma wanaowahudumia. Kila siku huzidisha njama hizo na kutekeleza nyingine mpya wakiwa na matumaini katika kila hatua kwamba watafanikiwa kuvuruga na kusambaratisha kabisa umoja wa Waislamu (Sahifatu Nur j.20 uk2)."
"Maulama na wanafikra wote duniani na hasa maulama na wanafikra wa dini tukufu ya Kiislamu wanapasa kushirikiana kwa shabaha ya kuiokoa jamii ya mwanadamu inayokandamizwa chini ya ubeberu na dhulma ya kundi hili janja na haini la wachache, ambalo kupitia njama na uhalifu, limeweza kueneza ubeberu wake wa kidhulma ulimwenguni.
Amkeni na kutumia maneno na kalamu zenu katika kuondoa hofu na woga bandia ambao umeenea dhidi ya wadhulumiwa. Viharibuni vitabu hivi ambavyo vimechapishwa na kusambazwa hivi karibuni na wakoloni kwa ushirikiano wa vibaraka wao waovu na hivyo kuchochea hitilafu baina ya madhehebu na makundi mablimbali ya Kiislamu. Ng'oeni mizizi ya hitilafu ambayo ndiyo chanzo cha matatizo yote ya wanyonge na Waislamu (Sahifatu Nur j.19 uk.102)."
4-MATAMANIO YA NAFSI
Miongoni mwa mambo yanayozuia kupatikana umoja na mshikamano miongoni mwa Waislamu ni kupenda nafsi na matamanio ya kinafsi na kimaslahi. Imam Khomeini anaamini kwamba hitilafu na kutengana Waislamu kunatokana na matamanio ya nafsi. Anasema: "Hitilafu daima hutokana na nafsi. Iwapo manabii wote watakusanyika wakati mmoja katika zama hizi hawatakuwa na hitilafu miongoni mwao kwa sababu hawana matamanio ya kinafsi.
Hitilafu hutokea upande mmoja au pande zote mbili zinapokuwa na matamanio ya kinafsi. Fanyeni juhudi za kuhakikisha kwamba matamanio hayo ya kinafsi hayakuathirini na hivyo kuwa chanzo cha ugomvi na hitilafu miongoni mwenu (marejeo hayohayo)." "Mnapasa kutambua kwamba kila mara ugomvi na hitilafu inapotokea miongoni mwenu, basi chanzo chake ni mwanadamu, na kila mara umoja na mshikamano unapopatikana basi chanzo chake ni Mwenyezi Mungu (marejeo hayohayo j.17 uk.147)."
NJIA ZA KULETA UMOJA KATI YA MADHEHEBU
Tulisema katika kurasa zilizopita kwamba, licha ya kuwa kila moja ya madhehebu za Kiislamu ina sifa zake maalumu zinazoitofautisha na madhehebu nyingine za Kiislamu, lakini madhehebu yote yote yana sifa na malengo ya pamoja yanayoyafanana yanayoweza kutumiwa kama chombo na njia bora ya kuyaunganisha. Vilevile tulisema kuwa ibada ya hija ni wakati na sehemu bora zaidi inayoweza kutumiwa na Waislamu kuchukua hatua muhimu za kuimarisha umoja kati yao.
Licha ya hayo, kuna mitazamo tofauti kuhusiana na mipango na hatua za kivitendo zinazopasa kuchukuliwa kwa madhumuni ya kufikia lengo la pamoja la umma wa Kiislamu, ambalo ni kuwaunganisha Waislamu na kuwafanya wawe na msimamo mmoja kuhusu masuala mbalimbali yanayowahusu. Hata hivyo, tunaashiria hapa mitazamo kadhaa ya Imam Khomeini (MA) na jumbe nyingi alizotoa katika msimu wa hija kuhusiana na hatua zinazopasa kuchukuliwa ili kuleta umoja na mshikamano miongoni mwa Waislamu.
1- KUJIEPUSHA NA POROPAGANDA CHAFU
Moja ya njia bora zaidi za kuleta umoja na maelewano miongoni mwa Waislamu ni kuheshimiwa watu. Jamii ya Kiislamu inapasa kutawaliwa na mazingira mazuri ambayo yanamfanya kila mtu au kundi katika jamii hiyo kuhisi kuwa linaheshimiwa na kwamba halidharauliwi wala kukosewa heshima na upande wa pili. Kila mtu katika jamii kama hiyo anapasa kuhisi kuishi kwa uhuru kamili na kutohisi kwamba usalama wake unahatarishwa, hata kama atakuwa ni mfuasi wa madhehebu ya walio wachache.
Kila mtu, bila kujali taifa wala rangi yake, huchukizwa na dharau kutoka kwa wenzake na hivyo kulazimika kutoa radiamali kuhusiana na jambo hilo. Hupenda kuona kwamba anaheshimiwa na wenzake. Kuheshimu watu wengine huleta mapenzi na upendo kwenye jamii hali ya kuwa dharau na udhalilishaji ni chanzo cha chuki, uadui, mifarakano na kutengana. Si bure kwa Mtume Mtukufu (saw) kusema: "Usimdhalilishe yeyote katika Waislamu; kwa sababu hata mdogo wao kiumri ni mkubwa mbele ya Mwenyezi Mungu (Mkusanyiko wa Warram Uk.31)."
Kwa msingi huo hatua ya kwanza ya kuleta umoja na mshikamano katika umma wa Kiislamu ni kujiepusha na dharau na udhalilishaji. Wanazuoni na waandishi kutoka kila madhehebu wanawajibika kujiepusha kusema na kuandika kila jambo linalopelekea Waislamu wengine kuhisi kuwa wamedharauliwa na kukosewa heshima.
Jambo hilo kwa hakika huzusha mifarakano na kuwatenganisha Waislamu. Wasomi na maulamaa wa Kiislamu wanapasa kuwasihi wafuasi wao wajiepushe na masuala yanayozusha utata miongoni mwa Waislamu kama vile kutusi na kuwadhalilisha makhalifa au kukamata na kuwafunga kitaasubi na kiuadui, waumini wanaozuru makaburi au kusoma dua mashuhuri zinazokubalika na Waislamu.
Watu kama hao wanapasa kuzuiwa kutekeleza hatua hizo zenye kuzusha mifarakano miongoni mwa Waislamu. Qur'ani Tukufu inakemea kufanyiwa vitendo kama hivyo vya dharau hata washirikina kwa kusema: "Wala msiwatukane wale ambao wanaowaabudu, kinyume cha Mwenyezi Mungu, wasije wakamtukana Mwenyezi Mungu kwa jeuri yao bila kujua (6:108)."
Imam Khomeini (MA) anasema: "Maulamaa, mahatibu na maimamu wa nchi za Kiislamu na wanafikra wa Kiislamu wanaweza kuidhibiti dunia na kuiweka chini ya mafundisho ya Qur'ani na wakati huohuo kuzuia kuenea ufisadi, kuporwa na kunyanyaswa Waislamu kutokana na majukumu yao mazito ya kuwaungoza watu….
Badala ya kuandika na kutoa matamshi yanayoleta mifarakano miongoni mwa Waislamu, kuwasifu watawala dhalimu, kuchochea uadui dhidi ya wanyonge kupitia Uislamu na kuleta unafiki katika safu za Waislamu, wanazuoni na wasomi hao wa Kiislamu wanapasa kufanya utafiti na kusambaza mafundisho yenye nuru ya Kiislamu katika Umma wa Kiislamu.
Wanapasa kunufaika na vipawa vikubwa vilivyopo katika mataifa ya Kiislamu kwa ajili ya kujiletea wao wenyewe utukufu na vilevile kuimarisha itibari ya umma wa Muhammad (saw) (Sahifatu Nur j.20 uk.126)." Ustadh Shahid Muttahari anasema hivi kuhusiana na suala hilo: "Umoja wa Kiislamu….unawalazimu Waislamu kulinda heshima na hadhi yao ili kuzuia kuenea chuki miongoni mwao. Wanalazimika kujiepusha kutukanana, kutotuhumiana na kutodanganyana. Wanapasa kutotoka nje ya mipaka ya mantiki na hoja na kwa uchache waheshimu kiwango cha chini zaidi ambacho kimewekwa na Uislamu katika kukubaliwa kwenye dini hii wasiokuwa Waislamu;
ادْعُ إِلَى سَبِ?لِ رَبِّكَ بِالْحِكْمَةِ وَالْمَوْعِظَةِ الْحَسَنَةِ وَجَادِلْهُمْ بِالَّتِ? هِ?َ أَحْسَنُ...
(Shish Maqaleh uk.5)."
1- KUJUA VYEMA UISLAMU HALISI NA MASUALA YA PAMOJA YA MADHEHEBU
Kama tulivyosema mwanzoni, kutoujua vyema Uislamu, fikra potofu na maamuzi ya kijahili na ya kitaasubi yanayotolewa na baadhi ya wafuasi wa madhehebu za Kiislamu ni baadhi ya mambo yanayochochea fitina, utengano na migawanyiko kati ya Waislamu. Suala hilo linawalazimu wanazuoni na viongozi wa kidini kufanya juhudi za kila upande ili kuwabainishia wafuasi wao Uislamu halisi pamoja na thamani za kidini za pamoja kati ya madhehebu tofauti za Kiislamu.
Wanawajibika kufanya kila wanaloweza ili kuimarisha maarifa ya kidini na kiwango cha utamaduni wa Kiislamu miongoni mwa Waislamu duniani na hivyo kuondoa dhana mbaya na taasubi zisizo na msingi, na wakati huohuo kuimarisha umoja miongoni mwao.
Kutofahamu vyema wafuasi wa madhehebu ya Kiislamu misingi ya kifikra na kiitikadi ya wenzao ni jambo muhimu linalozusha fitina, tuhuma na chuki kati ya wafuasi wa madhehebu hayo. Kwa hivyo ni wazi kuwa hatari na tatizo hilo linaweza kuondolewa tu kwa kuchunguzwa na kuimarishwa maarifa ya wafuasi wa madhehebu hayo kuhusiana na misingi ya itikadi na imani za wenzao.
Kuhusiana na umuhimu wa kuujua vyema Uislamu na nafasi yake katika kuimarisha umoja miongoni mwa Waislamu Imam Khomeini (MA) anasema:
"Kama nilivyotangulia kusema mara kwa mara, iwapo umma wa Kiislamu hautaamka na kutekeleza vilivyo majukumu yake, iwapo maulamaa wa Kiislamu hawatatekeleza majukumu yao, iwapo Uislamu halisi ambao unaimarisha umoja na kuyahamasisha makundi tofauti ya Kiislamu kusimama dhidi ya wachokozi wa kigeni, Uislamu ambao unayadhaminia saada na kujitawala mataifa na nchi za Kiislamu, utaendelea kudhibitiwa na wakoloni, wageni na vibaraka wao, bila shaka moto wa hitilafu na mgawanyiko utaendelea kuwaka miongoni mwa Waislamu, na hivyo kuiletea jamii ya Kiislamu misiba na mabalaa makubwa zaidi (Sahifatu Nur j.1 uk.343)."
NUKTA!
Mara nyingi, maamuzi na hukumu mbovu pamoja na tuhuma za kimadhehebu zinazotolewa na baadhi ya watu hutokana na kufahamu kwao vibaya mambo yaliyoandikwa kwenye vitabu vya marejeo vya Waislamu wenzao….Kwa msingi huo vitabu na vyanzo vya utafiti na marejeo ya hadithi yanapaswa kuimarishwa kwa kuondolewa humo hadithi zenye utata, bandia, zisizo sahihi na dhaifu. Kuwasilishwa kwa mambo yaliyo wazi na yanayoweza kufahamika na watu wa kawaida katika vitabu na marejeo hayo, ni jambo linaloweza kuzuia kwa kiasi kikubwa hitilafu na migawanyiko isiyofaa katika jamii ya Kiislamu.
KULINDWA HAKI ZA UDUGU
Katika mtazamo mpana wa Kiislamu, Muislamu anachukuliwa kuwa ndugu wa Muislamu mwenzake. Kwa msingi wa udugu huo, kuna haki ambazo Waislamu wamewajibishwa kuzichunga, haki ambazo iwapo zitapuuzwa basi huandaa uwanja wa kudhoofika na kulegalega misingi ya umoja, udugu na mshikamano katika jamii ya Kiislamu. Mtume Mtukufu (saw) anasema:
"مَنْ سَمِعَ رَجُلاً ينادِي: يا لَلْمُسْلِمين! فَلَم يجِبْهُ فَلَيسَ بِمُسلمٍ
Muislamu anayesikia mtu akipaza sauti ya kutaka msaada na kuamua kutomjibu, huyo huwa si Muislamu (Usul Kafi j.3 uk.252)." Mtukufu huyo vilevile amesema:
"مَنْ أصْبَحَ فَلَمْ يَهْتَمّ بِاُمُورِ الْمُسْلِمين فَلَيسَ بِمُسْلِم
Mtu anayeamka asubuhi bila kujali wala kushughulikia masuala ya Waislamu, huwa si Muislamu (Usul Kafi j.3 uk.251)." Katika ujumbe wake kwa mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu, Imam Khomeini alikuwa akiashiria majukumu mazito yanayowakabili Waislamu katika kutatua masaibu na matatizo ya ndugu zao Waislamu katika nchi tofauti. Alikuwa akisisitiza kwamba ibada ya hija ndiyo fursa nzuri zaidi ya Waislamu kukutana na kubadilishana mawazo kuhusianana njia za kushughulikia na kuyatatua matatizo hayo.
Alikuwa akisema:
"Kwa kuwadia msimu wa kuhiji katika Nyumba ya Mwenyezi Mungu, na Waislamu kutoka pembe mbalimbali za dunia kupata fursa ya kuizuru Nyumba hii, mahujaji wanapasa kuzingatia moja ya falsafa muhimu za mjumuiko huu mkubwa katika amali zao za ibada ya hija. Wanawajibika kujadili na kuzingatia hali ya kijamii na kisiasa ya nchi za Kiislamu na kutafuta njia za kutatua matatizo yanayowakabili ndugu zao Waislamu. Wanapasa kulichukulai suala hilo kuwa sehemu ya majukumu yao ya Kiislamu na kiutu. Kushughulikia masuala ya Waislamu ni moja ya faradhi na majukumu muhimu ya Kiislamu (Sahifatu Nur j.2 uk.172)."
"Waislamu wanalazimika kujadili matatizo muhimu ya Waislamu na kushauriana kuhusu njia za kuyatatua katika mkusanyiko huu adhimu na mtakatifu ambao hakuna nguvu yoyote inayoweza kuuandaa isipokuwa Mwenyezi Mungu (Sahifatu Nur j.15 Uk.123)." "Badilishaneni fikra na mawazo kwa ajili ya kutatua matatizo ya Waislamu…Shirikianeni na kuungana katika njia ya kujitawala na kuondoa donda la kensa na ukoloni! Sikilizeni na kuzingatia matatizo ya kila taifa la Kiislamu kutoka kwa wenyeji wa mataifa hayo na kisha fanyeni kila liwezekanalo kwa ajili ya kuyatatua. Wafikirieni pia watu masikini na wanaohitaji misaada katika nchi za Kiislamu! Fikirieni njia za kuzikomboa ardhi za Kiislamu za Palestina kutoka kwenye makucha ya uzayuni, ambaye ni adui mkubwa wa Uislamu na utu (Sahifatu Nur j.1 uk.156)."
Ni wazi kuwa iwapo Waislamu wote watazingatia na kutekeleza vyema majukumu yao ya kidini, watafanikiwa kutatua matatizo mengi yanayoukabili ulimwengu wa Kiislamu na hivyo kuundalia umma wa Kiislamu mazingira mazuri na ya kuvutia ya maisha. Katika mazingira kama hayo, hakuna Muislamu yoyote atakayemchochea mwenzake kuzusha fitina na mfarakano katika jamii ya Kiislamu na kila mtu atafanya juhudi za kuhifadhi na kulinda heshima ya Muislamu mwenzake.
4- KUTOLEWA FATWA ZA PAMOJA
Miongoni mwa mambo yanayojadiliwa na viongozi wa kidini, ni suala la iwapo inajuzu kwa wafuasi wa madhehebu moja ya Kiislamu kufuata futuwa zinazotolewa na wanazuoni wa madhehebu nyingine ya Kiislamu. Yapata miaka 40 iliyopita, tarehe 17 Rabiul Awwal 1378 na kwa mnasaba wa kuadhimishwa siku ya kuzaliwa Imam Jaffar Swadiq (as), Sheikh Muhmoud Shaltut, mufti wa wakati huo wa Misri na ambaye pia alikuwa mkuu wa chuo kikuu cha kidini cha al-Azhar alitoa fatuwa ifuatayo:
"Dini ya Kiislamu haijamlazimisha mtu yoyote kufuata madhehebu maalumu bali kila Muislamu anaweza kufuata madhehebu yoyote ambayo imepokelewa kwa misingi sahihi na sheria zake kuainishwa vyema katika vitabu vyake maalumu.
Mtu anayefuata moja ya madhehebu haya manne anaweza kubadili madhehebu yake na kufuata madhebu nyingine yoyote kati ya hayo. Madhehebu ya Jaafari, mashuhuri kama madhehebu ya Ithna-Asheri, ni madhehebu ambayo kama yalivyo madhehebu mengine ya Ahlu Sunna, inajuzu kuifuata kisheria.
Kwa msingi huo, ni muhimu kwa Waislamu kulizingatia suala hilo na kujiepusha na taasubi isiyo na msingi waliyonayo kuhusu madhehebu fulani. Dini na sheria za Mwenyezi Mungu hazifuati madhehebu na wala hazitahodhiwa na madhehebu fulani. Viongozi wote wa madhehebu walikuwa mujtahidi na ijtihadi yao inakubaliwa na Mwenyezi Mungu. Kila mtu asiye na utaalamu wa juu wa masuala ya kidini anaruhusiwa kufuata madhehebu yoyote anayovutiwa nayo na kufuata sheria zake za kifikihi. Kuhusiana na suala hilo, hakuna tofauti yoyote kati ya masuala ya kiibada na kimiamala (Khaterat wa Mubarazate Hujjatul Islam Falsafi uk. 310)."
Hatua hiyo ya busara na ya kumridhisha Mwenyezi Mungu iliyochukuliwa na mwanazuoni huyo mashuhuri katika zama hizo kwa madhumuni ya kuwaunganisha Waislamu wa madhehebu tofauti ya Kiislamu inapaswa kufuatiliwa kwa karibu na kutekelezwa na wanazuoni wa madhebu zote za Kiislamu. Wanapasa kuhakikisha kwamba, wamechukua hatua za kivitendo kwa shabaha ya kuimarisha umoja na mshikamano miongoni mwa Waislamu wote wa dunia. Inasikitisha kuona kwamba, badala ya wanazuoni na wanafikra wa Kiislamu kufuatilia kwa karibu suala hilo muhimu, wamelipuuza kabisa na hivyo kudumisha matatizo ya mifarakano na mitengano katika ulimwengu wa Kiislamu.
Hata hivyo, Imam Khomeini (MA) na wanazuoni wengine muhimu wa Kiislamu hawajatosheka tu kwa kutoa jumbe za umoja na mshikamano kati ya Waislamu katika siku za hija, bali wamechukua hatua za kivitendo na za mara kwa mara za kukabiliana na mambo yanayoleta fitina na mifarakano miongoni mwa Waislamu, mifarakano ambayo kwa kawaida huzushwa na wakoloni kupitia vibaraka wao katika nchi za Kiislamu.
Hizi hapa ni baadhi ya fatuwa za umoja za Imam Khomeini (MA):
"Fanyeni tawafu kwa namna ambayo inafahamika na kutekelezwa na mahujaji wote. Jiepusheni na vitendo ambavyo hutekelezwa na majahili, na kamwe msijishughulishe na mambo yanayodhoofisha dini. Katika wukufu mbili (Arafa na Muzdalifa) inajuzu kufuata hukumu na fatuwa za Ahlu Sunna hata kama mtakuwa na yakini kwamba ni makosa (Sahifatu Nur j.9 uk.176)."
"Ndugu wa Kiirani na Washia wa nchi nyingine wanapasa kujiepusha na vitendo vya kijahili ambavyo husababisha mifarakano na udhaifu katika safu za Waislamu. Wanapasa kushiriki katika mikusanyiko ya Ahlu Sunna na kujiepusha kusimamisha swala za jamaa katika nyumba zao na kuweka vipaza sauti vinavyopingana na vya wenzao wa Kisunni.
Wanawajibika kutojiangusha kwenye makaburi matakatifu wala kufanya mambo ambayo mara nyingine yanakinzana na sheria za Mwenyezi Mungu (Sahifatu Nur j.2 uk.13)." "Wakati swala za jamaa zinaposimamishwa kwenye Masjidul Haram na Masjidu Nnabi, waumini wanapasa kuswali swala hizo na wenzao na kutotoka katika misikiti hiyo wakati wa kusimamishwa swala hizo (Manasik Haj uk.257)."
Masuala yafuatayo pia yana athari katika kuleta umoja na mshikamano miongoni mwa Waislamu:
(a) Kuandaliwa vikao vya kila mwaka vya wakuu wa nchi za Kiislamu kwa lengo la kujadili na kubadilishana mawazo kuhusu masuala ya pamoja yanayozihusu nchi hizo.
(b) Kuweka mikataba ya pamoja kwa lengo la kubadilishana masuala ya kiutamaduni, kiuchumi na kijeshi.
(c) Kuanzisha vituo na mashirika makubwa ya habari kwa madhumuni ya kukabiliana na propaganda za kichochezi za maadui wa Uislamu.
(d) Kuanzishwa vyuo na vituo vya kielimu katika nchi mbalimbali za Kiislamu, ambavyo vitawapokea wanafunzi kutoka madhehebu zote za Kiislamu. Wanafunzi hao wanapaswa kufundishwa fikra za kiitikadi na sheria za fikihi za madhehebu zote za Kiislamu na mambo mengineyo
MWISHO