CHINI YA KIVULI CHA MTUME
  • Kichwa: CHINI YA KIVULI CHA MTUME
  • mwandishi: NDUGU ZETU WA KIISLAMU
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 4:49:53 3-11-1403

BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

CHINI YA KIVULI CHA MTUME
Kila tunapoifikia siku ya kuadhmisha kuzaliwa Bw. Mtume Mohammad al Mustafa (S.A.W.W), tunatakiwa tufahamu kuwa: Yeye ni shaksia aliyekuwa ni chanzo na chimbuko la umoja katika vipindi vyote vya historia ya Uislamu. Mtume wa Mwenyezi Mungu SAW ndiye dira ya hisia na itikadi za umma wa Kiislamu.

Kwa hakika Mtume SAW ni nukta ya kukurubiana Waislamu na madhehebu ya Kiislamu. Hakuna shaka kuwa siku kuu yenye baraka ya kuadhimisha kuzaliwa Mtume SAW ndio wakati muhimu zaidi wa kuchukua hatua zenye athari katika kuleta umoja wa Kiislamu. Tunachukua fursa hii kuwapongeza Waislamu wote duniani kwa mnasaba huu muhimu wa Milad Un Nabii na Wiki ya Umoja wa Kiislamu.

Umoja ndio msingi muhimu zaidi ambao unawezesha taifa au umma wowote ule kufikia malengo yake. Ni kwa sababu hii ndio maana moja ya ahadi na mapatano ya Mwenyezi Mungu na Mitume Wake ikawa ni kuleta Umoja na mshikamano katika jamii. Quran Tukufu inakumbusha kuwa wanaadamu wote wameumbwa kwa udongo na wametokana na baba na mama mmoja. Quran Tukufu katika aya yake iliyo wazi kabisa inawataka Waumini wote wajiepushe na mifarakano. Katika aya ya 103 ya Surat Aali Imran, Mwenyezi Mungu anasema: "Na shikamaneni kwa Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yenu: vile mlivyokuwa nyinyi kwa nyinyi maadui naye akaziunganisha nyoyo zenu; kwa neema yake mkawa ndugu…"

Wafasiri wa Quran Tukufu wanaamini kuwa kamba ya Mwenyezi Mungu kabla ya mengine yote ni Quran yenyewe. Mtume SAW katika riwaya aliitaja Quran kuwa kamba ya Mwenyezi Mungu ambayo inaunganisha mbingu na ardhi. Fauka ya hayo Quran inawataka waumini wajiepushe na hitilafu na mifarakano na badala yake warejee kwa Mwenyezi Mungu.

Quran Tukufu inaashiria kuwa mifarakano inatokana na hisia ya kujipenda na chuki miongoni mwa watu. Kitabu hicho kitakatifu kinakumbusha kuwa waliotangulia hawakufikia malengo ya juu waliokusudia kutokana na kuwa na sifa hizo za chuki na kujipenda. Quran Tukufu inataja umoja uliokuwepo huko nyuma miongoni mwa wanaadamu kuwa ni neema kati ya neema za Mwenyezi Mungu na kwamba kutokana na neema hizo wanaadamu waliweza kuongozwa katika maisha yaliyojaa saada na ufanisi.

Katika aya ya 159 ya Surat Aali Imran, Quran tukufu inaashiria kuwepo Mtume SAW pamoja na akhlaqi na tabia njema za mtukufu huyo kuwa mhimili wa umoja na nshikamano miongoni mwa Waislamu. Quran Tukufu inakumbusha kuwa iwapo kutaibuka hitilafu katika suala fulani, basi Waislamu warejee kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake.

Kutokana na kuwa Mtume SAW alikuwa akibainisha wazi maana ya Aya za Quran, basi upatanishi wake katika migongano unaidhinishwa na Quran Tukufu. Mtume SAW kwa kuwa na akhlaqi bora, upendo na urafiki, alifanikisha mkataba wa udugu kati ya Muhajirina na Ansar, ili kuimarisha mshikamano wa Waislamu. Mtukufu huyo pia aliweza kuleta umoja wa Kiislamu na udugu kati ya makundi mawili ya Aus na Khazraj ambayo yalikuwa yakipigana na kuzozana kwa muda mrefu.

Wenzo mwingine wa Umoja ni kurejea na kuwategemea Ahlul Bayt au Watu wa Nyumba ya Mtume SAW. Quran Tukufu inawataja Maimamu - amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yao - kuwa ni Ulul Amr yaani viongozi au wenye mamlaka na kwamba kuwatii ni sawa na kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake na kwamba maneno yao ni hoja kwa waumini.

Mwenyezi Mungu Katika Quran Tukufu aya ya 59 ya Surat an-Nisaai anasema: "Enyi mlioamini! Mt'iini Mwenyezi Mungu, na mt'iini Mtume na wenye mamlaka katika nyinyi". Hakuna shaka kuwa Watu wa Nyumba ya Mtume SAW ndio waliokuwa karibu zaidi na Mtukufu huyo na ndio wanaoifahamu kwa njia sahihi Quran Tukufu na mafundisho ya dini ya Kiislamu.

Kuwatii wakubwa hao kuna maana ya kumfuata Mtume wa Mwenyezi Mungu na hivyo kufuata mkondo wa haki na saada. Maimamu hao wana nafasi ya kipekee katika kuhuisha Uislamu na kuleta moyo wa umoja miongoni mwa Waislamu.

Baada ya Quran Tukufu kuwataka Waislamu wajiepushe na mifarakano, inawataka waamrishe mema na kukataza mabaya. Quran pia inaonya kuwa Waislamu wasitawanyike kama wafuasi wa dini zilizotangualia ambao waligawanyika na kuwa makundi katika dini zao.

Jambo hili linaonyesha kuwa kuamrisha mema na kukataza mabaya ni suala lenye nafasi ya kipekee katika kuleta umoja na kuzia mifarakano. Fakhr Razi, mfasiri mashuhuri Muislamu anamini kuwa kutawanyika na kujitokeza mifarakano katika dini ima kunatokana na makosa katika kufahamu mafundisho ya dini au kujipenda watu au makundi. Kwa hivyo kuamrisha mema na kukataza mabaya ni kati ya piramidi za nidhamu ambayo inaweza kuzuia kujipenda na mifarakano.

Quran Tukufu inawataja Waumini kuwa ndugu na inatoa wito kwao waheshmiane na kuzingatia haki za upande wa pili. Quran inawataka pia wasichunguzane aibu na pia wasiwe na dhana mbaya miongoni mwao na vile vile wajiepusehe kutupiana tuhuma. Aya za Mwenyezi Mungu zinasema ghiba au usengenyaji ni sawa na kula nyama ya ndugu aliyekufa. Aya hizo tukufu zinatoa wito kwa watu wahurumiane na katika dua zao wawaombee ndugu zao katika dini na pia waombe msamaha na kuondolewa hila katika nyoyo. Aya ya 10 ya Surat al Hashr inasema: " Mola wetu Mlezi! Tughufirie sisi na ndugu zetu waliotutangulia kwa imani, wala usiweke mfundo katika nyoyo zetu kwa walioamini…"

Katika Uislamu, ibada imeratibiwa kwa njia ambayo inamshwishi mtu binafsi na jamii nzima kwa jumla kutekeleza umoja na mshikamano katika jamii. Swala ni nembo ya ibada katika Uislamu na wajibu wa kila Muislamu. Wanaoswali husoma Surat al-Fatiha katika swala zote tano za kila siku. Pamoja na kuwa sura hii husomwa na mtu binafsi katika swala, lakini maneno yenye maana ya wingi hutumiwa na mja anayesimamisha ibada hiyo. Kwa mfano kuna ile aya isemayo, "Wewe tu tunakuabudu, na Wewe tu tunakuomba msaada" .

Aidha Waislamu wanatakiwa kuelekeza nyuso zao upande wa al Kabaa tukufu wakati wanaposwali. Jambo hili linaonyesha kuwa Quran Tukufu inataka kuleta mshikamano na maelewano katika nyoyo za Waislamu. Quran Tukufu inataja moja ya hekima za hija kuwa ni watu kushuhudia manufaa ya ibada hiyo. Hivi sasa manufaa muhimu zaidi ya hija kwa Waislamu ni kuimarisha mshikamano, udugu na umoja wao na vile vile kuonyesha nguvu na uwezo wao 

Kutekeleza ibada ya hija na Waislamu wote kwa pamoja na katika wakati mmoja huku wakijiepusha kujishughulisha na mijadala isiyo na maana kwenye ibada hiyo tukufu, huondoa tofauti baina ya waumini na kuleta umoja na mashikamano miongoni mwao. Allamah Tabatabai mfasiri maarufu wa Quran anaashiria umoja huu kwa kusema: "Ni lazima tukumbushe hakika hii kuwa hitilafu za makundi mawili ya Shia na Sunni ziko katika matawi ya dini au kwa ibara nyingine furuu din, na wala sio katika misingi yake. Waislamu hawana hitilafu katika masuala ya kimsingi na hata katika matawi ya dini wanaafikiana kuhusu masuala ya dharura katika dini kama vile swala, saumu, hija, jihadi n.k. na wote wanaamini kuwa wana Quran moja na kibla kimoja".

Maulamaa wakubwa wa Kiislamu baada ya jitihada za miaka mingi wametayarisha na kupitisha mkataba au Hati ya Umoja wa Kiislamu. Kwa mujibu wa hati hii ambayo ilitayarishwa kufuatia sisitizo la Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, Ayatullah Ali Khamenei, wasomi na wanafikra wa Kiislamu wameafikiana kuwa watafungamana na mambo yanayoleta umoja na kudhamini heshima na ufanisi wa Waislamu.

Hati hiyo ya umoja inawataka Maulamaa na Wasomi kuongoza harakati za mwamko wa Kiislamu na vile vile kupanga na kuchukua misimamo ya pamoja katika kukabiliana na adui wao wa pamoja. Aidha mkataba huo unawataka wasomi hao wa Kiislamu kuzuia madola ya kigeni kuwa na ushawishi katika nchi za Kiislamu.

Nukta muhimu katika Hati ya Umoja wa Kiislamu ni sisitizo lake kuhusu kujizuia Waislamu kukufurishana na kutovunjiana heshima katika matukufu yao. Hati ya Umoja wa Kiislamu inatoa wito kwa taasisi na serikali kutambua rasmi madhehebu ya Kiislamu na kuwapa wafuasi wa madhehebu hayo haki sawa na raia wengine ili umoja wa kivitendo miongoni mwa Waislamu upatikane.

Ayatullah Khamenei Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu anasema: "Yule ambaye anaamini kuwa Umoja kati ya Masunni na Mashia hauwezekani basi hafahamu lolote kuhusu Uislamu. Leo harakati yoyote ya kuzusha mifarakano katika ulimwengu wa Kiislamu ni dhambi ya Kihistoria. Wale ambao wanayakufurisha makundi makubwa ya Kiislamu kwa sababu zisizo na msingi na kuyavunjia heshima matukufu ya kundi lolote kati ya makundi ya Kiislamu, wawe wanajua au kutojua, wanahesabiwa kuwa ni wahalifu ambao watakumbukwa na vizazi vijavyo kwa chuki na watatajwa kuwa mamluki wa adui".

Sheikh Ashriov, Mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Waisalmu la Russia anasema hivi: "Tunahitaji kuangalia zama za mwanzo wa Uislamu na Mtume Mtukufu wa Uislamu ili tuweze kuhuisha tena umoja wa neno kwa muundo mpya.

Leo tunapaswa kuhakikisha kuwa Masunni na Mashia wanakaa na kushirikiana bega kwa bega. Anaendelea kusema: "Kwa mtazamo wangu, Waislamu walio wengi duniani wanataka sana kuwa na urafiki na mshikamano. Lakini kuna baadhi ya Maulamaa ambao kwa kutoa matamshi ya matusi na utata wanachochea hisia za Waisalmu. Kuwepo Maulamaa kama hawa na baadhi ya wanasiasa ni tatizo kubwa kwa umma wa Kiislamu." Kwa mara nyingine tena tunatoa salamu za heri na fanaka kwa Waislamu wote kwa mnasaba huu muhimu wa Milad un Nabii na Wiki ya Umoja.
MWISHO